Msanii: Kay Wa Mapacha
Album: Street Entrepreneur
Tarehe iliyotoka: 15.12.2019
Nyimbo: 9 Plus 1 Bonus track
Producers: Sigga – Paradise Apple Studios, Professor Ludigo, 10th Wonder, Bano Styles, AMOC, Freddy Saganda

Levison Kasulwa kama anavyojulikana rasmi Kay wa Mapacha/Kay Mapacha ni emcee aliyezaliwa mwanzoni wa miaka ya themanini. Kay Mapacha alizaliwa Dar es Salaam na pacha wake aitwaye Dotto Mapacha ambae pia ni emcee, kabla ya wote kuhamia Arusha ambapo historia yao kimuziki ilipoanza.

Kulwa na Dotto walianza mziki 1994. Enzi hizo baada ya kupewa video cassatte za hip hop na mshikaji wao mmoja walivutiwa na muziki aina ya hip hop pamoja na R & B iliyokuwemo humo. Ma emcee waliowapa motisha enzi hizo ni akina Eric Sermon, Dr. Dre, Snoop Dogg, Redman, Method Man, Keith Murray, Busta Rhymes na wengineo. Walipoanza kidato cha kwanza kule Kenya walianza kujifunza kuandika mistari na pia kuchana. Hadi walipofika kidato cha nne walikuwa na uwezo wa kuingia studio ili kujaribu kurekodi wimbo wao wa kwanza ambapo walikutana na Proffessor Ludigo aliyewakubali na kuwaweka chini yake. Waliendelea hadi 2005 ambapo kwa kushirikiana na wengine walianzisha lebo yao iitwayo Pasu kwa Pasu.

Baada ya miaka mitatu Kulwa na Doto ambao enzi hizo walikua wanajiita Mapacha 50-50(Pasu kwa Pasu) walianza kujiita Maujanja Saplyaz baada ya lebo hiyo (Pasu kwa Pasu) kusambaratika. Maujanja Saplayaz ikaanza miradi ambayo mojawapo ilikuwa uuzaji wa t-shirt kando na uchanaji kutokea mwaka 2007 hadi sasa. Kando na t-shirt mapacha hawa wana bidhaa yao ya pilipili.

Album ya Street Entrepreneur ni mradi wa kwanza rasmi wa Kay Mapacha ambao aliufanya bila ya kumshirikisha pacha Dotto. Kabla ya mradi huu Kay alikua ameshafanya miradi kadhaa hapo nyuma akiwa na Dotto ikiwemo album yao ya kwanza Ghetto Love kisha ikafuatia Magenge in Green (Mixtape), Happiness 24/7 na pia 369 Mixtape.

Baada ya kuona changamoto wanazopitia vijana wengi kuhusu maswala ya ajira na ujasiriamali Kay aliamua kutumia uzoefu wake wa biashara na kuunda album aliyoiita Street Entreprenuer ambayo utafsiri wake kwa lugha ya Kiswahili ni “Mjasiriamali Mtaani”.Aliamua kuchambua mambo muhimu kuhusu ujasiriamali na kuyaweka kwenye nyimbo ili kumuhamasisha mskilizaji na taarifa zitakazomuwezesha kuanzisha biashara yake mwenyewe.

Nyimbo zote za albam hii zinamfafanulia msikilizaji vitu ambavyo anatakiwa kujua ili kuanza na kukuza biashara yake. Mafunzo ya album hii ambayo ni kama “course” ndogo ya ujasiriamali ambapo mtu anaweza kuhitimu na cheti cha ujasiriamali bila hata ya kuhudhuria darasa.

Album hii imefanyiwa utafiti wa hali ya juu kando na kutumia ujuzi wa biashara kwenye maisha yake Kay. Kukwama na kuanguka kibiashara zake kumemuwezesha yeye kuunda album iliyokwenda shule hata kwa msikilizaji ambaye hajawahi kuuona mlango wa shule.

Album hii iliyoundwa Paradise Apple chini ya usimamizi mkuu wa producer Sigga inaanza kwa utangulizi unaotolewa na Gego Master wa “Asili Mia, Akili Mia” kabla ya album kuanza na somo la kwanza liitwalo “Plan” iliyoandaliwa na AMOC. Kwenye wimbo huu Kay anaanza kwa kusisitiza umuhimu wa kuwa na mpango kwa ajili ya biashara yako. Kay anasema kwenye vesi ya kwanza kuwa

“Kila plan inaanzia akilini/
Na ramani nzima unaifanya ki mahiri/
Hakikisha unasimamia misingi/
Plan yenye michoro yakuleta dili/”
Vesi ya pili pia anaanza na madini haya,
“Plani nzuri ndio mahesabu mazuri/
Sababu siku nzuri huanza asubuhi/
Kazi nzuri huleta wawekezaji/
Sajili mchongo kuwakwepa wababaishaji/
Plan mahesabu, inafata mitaji/
Kama muwekezaji hichi ndio kitanzi”

Kwenye nyimbo ya Mchongo akiwa na Monster, Kay anaongea kuhusu umuhimu wa rafiki zake kumuunganisha na michongo ya hela kuliko kumpa hela yaani bora apate rafiki amfunzae kuvua samaki kuliko rafiki anayempa samaki tu. Album inaendelea kutupa madini kwenye nyimbo za Fursa, Business na Promotion. Promotion inaongelea umuhimu wa kunadi biashara yako akisema Kay “kizuri kinajitembeza/ hiyo ilikua zamani!” ilhali Gego Master haachwi nyuma anapotoa mfano wa kuji promote/kujinadi akisema, “Tangaza kimataifa/Si unaona Sankofa/Ukinunua T-shirt album ni bure kabisa!”

Pia kwa kuwa watu wengi wanaogopa hasara kwenye biashara, Kay anasema kwenye wimbo Hasara akiwa na Ado Tembo kuwa,

“Hasara ni sehemu ya biashara/
Hata ma benki makubwa nayo hupata hasara/
Unaweza ingia mkenge hadi unatoka kipara/
Na bado unakomaa mwanangu kama Digala”

Album hii ipo matawi ya juu ki maudhui na imetimiza lengo la Kay la kuhakikisha kuwa mafunzo yaliyotolewa ni rahisi kuelewa na kukariri. Wimbo kama Business unaweza kufanya uhisi unachelewa kuanza biashara yako pale anapoimba Whymen Muddy kua,

“Ukiamua kufanya business, wewe fanya/
Unatakiwa uwe serious.”

Somo la mwisho kwenye course ni wimbo uliobeba jina la album Street Entreprenuer. Chamsingi album hii inakupatia maarifa na mawazo yatakayokuwezesha kufanikiwa kibiashara. Kila wimbo, kila mstari ulioandikwa kwenye album hii ni jiwe le msingi la kukuwezesha kujenga biashara ya aina yoyote kama anapomalizia Kay kwenye wimbo wa mwisho akisema,

“Huwezi nipata mtaa bila dili la kufanya/
Ukinikuta idle nitawauzia hata nyanya!”

Shabiki yoyote, emcee na mtu yoyote mwenye mawazo ya kufungua biashara yake hapaswi kukosa nakala hii kwenye collection yake ya hip hop. Album hii yenye nyimbo 9 ni fupi, tamu na inalenga hoja za ujasiriamali moja kwa moja. Pata nakala yako.