Uchambuzi Wa Album: Invisible Currency
Emcee: Khaligraph Jones
Tarehe iliyotoka: 07.03.2022
Nyimbo: 17
Watayarishaji: Vince On The Beat na watayarishaji wengine
Mixing & Mastering: Ares 66
Studio: Blu Inc Corp

Nyimbo Nilizozipenda: Rada Safi, Ikechukwu, Ateri Dala, Maombi Ya Mama, Wanguvu, Tsunami, How We Do, Bad Dreams, Flee, Hiroshima, The Khali Chronicles, All I Need

Khaligraph Jones

Khaligraph Jones amekuwa ndani ya hili game la Hip Hop kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Ndani ya miaka hii The OG kama anavyopenda kujiita amefanikisha kuachia kazi kibao kali sana kama vile Embesha, We Run Dem, Natesa, Yego, Mazishi, Yes Bana, Micasa Sucasa, Omollo na nyingine kibao. Pia wakati huo huo ameweza kutumia ubunifu wake na kuandaa msururu wa Khali Cartel (Cyphers) ambazo zimewapa fursa wasanii wengine kupiga kazi nae.

Msanii huyu ambaye alianza kwa kujijengea jina kama mmoja wa wachanaji bora wa mitindohuru (freestyles) kutokea nchini Kenya aliachia album yake ya kwanza Testimony 1990 mwaka 2018 ilipokelewa vizuri na mashabiki wake na kumuwezesha Omollo kujiwekea msingi mzuri inapokuja kwenye miradi. Baada ya miaka miwili na chenji Papa Jones alirudi tena na mradi wake wa pili ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na gamu Invisible Currency.

Mradi huu unafunguliwa kwa utangulizi mzuri na wimbo uliobeba jina la mradi Invisible Currency ambapo anaongelea historia ya wapi alipoanzia na wapi alipo na ndoto zake zinavyoweza kufanikishwa kutokana na yeye kujituma kwenye mziki wa Hip Hop akikwambia,

“Can’t even say how long I’ve been in this city/
You might assume that everything in the beginning was pretty/
Who’d ever thought I’d make it big in the city/
From eating crumbs to getting state house invitations like I’m Jimmy Wanjigi/”

Baada ya hapa emcee huyu anatupeleka kwenye ibada kwanza ili aweze kumshukuru muumba wake kwenye All I Need. OG haogopi kuonesha kuwa imani yake imekuwa moja ya nguzo iliyomuwezesha yeye kushinda changamoto alizozipitia. Hili unaliona wazi pia kwenye Maombi Ya Mama akiwa na Adasa ambao pia ulikua singo ya pili kutoka kwenye mradi huu.

Kwenye wimbo huu pia kando na maswala ya imani emcee huyu anatufungulia pazia ya moyo wake ili tuweze kuona maisha yake ya nyuma yalikuwaje na vile mama yake alivyokuwa mtu muhimu kwenye vitaa hii ya maisha. Ngoma chanya sana hizi za kukuinua na kukupatia mtazamo chanya wa maisha. 

Ikechukwu pia kwa namna moja au nyingine inaendeleza mada ya imani bado kwani neno kwa kabila la wa Igbo kule Nigeria linamaanisha nguvu ya Mungu na pia ni jina analoweza kuitwa kijana wa kiume. Hivyo basi OG anajibatiza jina hili kuonesha vile yeye ni muujiza kutoka kwa mwenyezi bado. Pia wimbo Am On The Move akiwa na Blackway pia maudhui ni ya imani bado.

Mada inabadilika na emcee huyu anatuonesha vile Rada Safi kwa sasa ambapo mambo yamebadilika sio kidogo kutoka aingie kwenye hili game. Anakwambia yeye bado ni mtu wa kawaida hata kama amefanikiwa kimaisha akisema,

“Rada safi rada safi
Omollo dong an generous hapana ngati/
Doh nimekafunga siwezi mind panda basi/
Naishi vile nataka nataka kitu siwezi ni kubamba umati/
Don Pablo proof kandarasi/
I make a living na kalamu na karatasi/
An entertainer tho sipendi sarakasi/
Kiki na izi kasheshe za media na paparazzi/”

Kwenye Ateri Dala akimshirikisha muimbaji Prince Indah emcee Jones ana “imba” flani mzuka sana wa mapenzi. Kiitiko kinaimbwa na lugha ya kijaluo au Luo kwenye mdundo flani wa ki utu uzima unaoambatana na ile nyama ya ulimi inayomnawisha mwanamke. Neno Ateri Dala linamaanisha nikupeleke nyumbani. Zile gita pale mwishoni safi sana. Maudhui ya mahusiano pia unayaona kwenye Ride For You akiwa na Rudeboy.

Baada ya hapa Jones anatupeleka sherehe kidogo kwenye ngoma mbili tofauti; Kamnyweso akiwa na mzee wa ma tumbler Mejja kwenye mgoma flani unaotumia mdundo flani wa ki Zouk hivi na baadae anashirikiana na muimbaji mkongwe wa bongo flava Ali Kiba kutoka kwenye Wanguvu.

Inner Peace akiwa na Kev The Topic kutoka Ghana ni wimbo chanya sana ambao ni wa kukutia moyo sana na kwenye kiitio Kev anakuinua na sauti yake tamu kabla ya kuchana freshi madini sawia na Khaligraph. Usijali wanayosema watu we jiamini, piga kazi yako kama anavyoimba Kev kwenye kiitikio…

“Don't you let up on yourself or nobody don't you fall
Watch your steps when you move coz they want you to lose control
Why you letting them in why you letting them change your soul
If you dig deep inside of yourself then you will find gold, gold”

Jones nae anaimba sio kitoto, sauti yake inapanda na kubadili ili kukutia moyo kama Papa wa Vatican! Omollo anachana na kuimba sio mchezo.

Kwenye Tsumani akiwa na Scar Mkadinali Omollo anajikuta akiingia uwanja wa ndondi ki mistari na mmoja wa wachanaji wazuri kutokea Kenya na kundi la Wakadinali. Ubeti wa tatu unawakuta wawili hawa wakibadilishana kinasa vizuri sana baada ya kila mmoja wao kujitegemea kwenye ubeti wa kwanza na wa pili.

Moja ya ngoma zangu pendwa kwenye mradi huu ilikua ni How We Do akishirikiana na muimbaji Xenia Manasseh. Mdundo wa ngoma umenikumbusha enzi hizo West Coast  na Jones anazidi kuonesha umahiri wake wa uchanaji na unataji wa mdundo. Pia anakukumbusha kuhusu Notorious B.I.G akikwambia , “Relax and take notes…”Nani kama sisi… anamalizia da’ Xenia. Flee pia unamkuta Jones akikwambia wewe ongea sana ila mwisho wa siku utajikuta ukisepa ili kutopata mabomu ya emcee Jones.

Uwezo wa Kaligraph Jones wa kuchana hadithi ya kubuni unaonekana kwenye Bad Dreams ambao unakuwa kama filamu flani nzuri sana.

Hiroshima ambao ndio singo ya pili toka kwa mradi huu inamkuta Omollo akirusha nondo ki Yego hadi mamtoni America wakati akishirikiana na Dax. Wimbo huu unawakuta wawili hawa wakilipuka nondo kama bomu la atomic lilioangushwa kule Hiroshima na Nagasaki ambapo kila mmoja anataka kuonesha uwezo wake wa kurap akisema Jones,

“Man I’m always gonna rap like this every day but ain’t no rapper gon match up/
Its quick but they never like that/
Ain’t met a nigga who could out track me on a record when I’m in the right back/”

The Khali Chronicles ni wimbo unaotufungia mradi huu ambao Jones anatumia fursa hii kuongelea historia ya maisha yake na ya muziki. Hapa ndio unaona vile kuwa kila hatua dua na watu hutoka mbali. Papa Jones anasoma historia yake na anawapa maua pia wale wote waliochangia kumsukuma iwe kwa uzuri au ubaya na kumwezesha afike alipo.

Nilichokipendea mradi huu ni vile emcee huyu amekuwa jasiri na kutufungulia maisha yake. Naona mradi huu ni personal sana toka kwa Papa Jones. Khaligraph karudi tena na bado ana njaa ya kuchana kama aliyokuwa nayo miaka 15 iliyopita wakati akianza kuandika na kuchana kwenye vitongoji vya Nairobi. Invisible Currency ambayo ina ashiria imani yaki inaonesha kuwa The OG anataka heshima yake na hato achia kinasa sauti kabla hamjampa!

Mfuatilie Khaligraph Jones kwenye mitandao ya kijamii kupitia;

Facebook: Brian Ouko Omollo
Instagram: Khaligraph Jones
Twitter: Khaligraph Jones