Uchambuzi Wa Albam: KiswaHealing
Msanii: Kitu Sewer x Maovete
Tarehe iliyotoka: 20.01.2021
Nyimbo: 14
Mtayarishaji: Gitonga Mukira
Mtayarishaji Mtendaji: I.M. Brima Rainman
Mchanganya Sauti na Midundo: Gitonga Mukira
Studio: Siepna Inc

Gitonga Mukira - Kitu Sewer - I.M. Brima Rainman

Dunia imepitia mambo kibao ndani ya miaka miwili au mitatu iliyopita ambayo si ya kawaida na ambayo kusema kweli yametuacha na makovu kibao sio tu kiafya bali pia kimawazo, ki mahusiano, kiuchumi, kisaikolojia na kimazingira.

Ni ndani ya wakati huu mgumu sisi kama binadamu hutafuta njia ya kuweza kujitibu majeraha haya na ndipo mwaka huu kundi la Maovete(Gitonga Mukira na I.M. Brima Rainman) wakishirikiana na gwiji wa Hip Hop toka Kenya waliamua kuingia studio na kugeuka waganga. Wakati madaktari bingwa duniani walikua wakihangaika kutafuta chanjo ya Uviko pamoja na dawa ya nzige waliokua wamefurika ardhi ya Africa Mashariki na kusababisha hasara  isiyohesabika vijana hawa waliamua kutafiti tiba mbadala.

Ilipofika tarehe ishirini mwezi wa kwanza mwaka huu wasanii hawa waliitoa tiba yao rasmi na kuiweka sokoni tayari kwa matumizi. Tiba hiyo ilitambulika kwa jina KiswaHealing.

KiswaHealing inaanza na utangulizi wa maagizo toka kwa daktari bingwa wa michano ambaye ameanza kubobea hivi karibuni kwa maswala ya uchanaji Brima. Brima anatuorodheshea changamoto tunazozipitia duniani kwa sasa na kisha kutuambia kua wao wanatuletea tiba mbadala.

Tiba hii ambayo imepikwa chini ya usimamizi wa mtaalam wa maabara mziki Sienpa Inc imenuia kututibu kwa kutumia njia nne tofauti; lugha ya Kiswahili, Mashairi, midundo inayotumia sampuli toka kwa nyimbo za kitambo na kughani.

Mradi huu ambao kusema kweli hauna nyimbo ya kuruka unaanza na singo iliyobeba albam hii Kun Faya Kun ambao ni wimbo unaongelea mtu kusafiri ki mawazo na kwenda mbali na ili kuweza kujichunguza na kujitibu vilivyo. Kitu Sewer anaweka msingi mzuri sana na pamoja na kaka Brima wakitupatia nondo zinazotusaidia kujihoji ilhali Gitango akisaidia kwenye kiitikio. Kitu Sewer anaanza kwa kusema,

“Nilienda far na me nikapoteza network ya God/
Kumbe anataka tuwe sote mind body and soul/
Na hakuna shortcut ni tuwe ndani yahii baro/
Na ku pay attention hata kama si doo/
Nilidhani ni hallucination ni kama nachizi jo/
Kumbe ni echo za mind yangu zina bounce kwa wall/
Kuna msee ananicheki kumbe ni me kwa kioo/
Siri ni yetu watatu ni wa ku poison sinia/
Hakuna kitu valuable kama kimya kwa hii dunia/…”

Wimbo chanya sana wa kukutia moyo ambapo Kitu Sewer pamoja na Brima wanasema kuwa uwezo wa kujitibu uko mikononi mwako;

Brima:

“Niskize vizuri me ni brain kwa akili yako/
Me ndio memory za utotoni mwako/
Life yako ina revolve around me/
Know thyself we jijue jiamini/
Hauhitaji psychologist au ku seek medical advice/
Device plan ya personal fulfilment na ui actualise/”

Kitu Sewer nae pia anasisitiza hili akisema kwa ucheshi,

“Huskii huyu psychologist amenifanyisha PE/
Ati niangalie sura yangu kwa mkojo nime pee/”

Wimbo ni madini mwanzo mwisho.

Utunzi huu mzuri unaendelea kwenye nyimbo zinazofuatia kama vile Utakwenda Wapi? wakiwa na JayHillz. Wimbo mzuka sana ambapo Kitu Sewer anatueleza hata vile changamoto za kimaisha kidogo zimsababishe Johnny Vigeti kujiua. Wimbo mzuka sana ambapo kuna lead gita flani freshi sana pamoja na sauti ya Gitonga kwenye kiitikio.

Endelezi ambao ni wimbo wa nne kwenye mradi huu unaendelea vizuri na vile vigezo vinne vinavyo wezesha mradi kunawiri. Kila mmoja kwenye wimbo huu anasimama vizuri kwenye zamu yake; sio tu Siepna anayewapatia vijana hawa mdundo mzuka sana bali hata kwa upande wa mashairi ambapo mkongwe wa Hip Hop toka kundi la Kalamashaka Robah anatuonesha kua penseli yake bado ina makali.

Mradi unaendelea kwa mtindo huu kwenye wimbo unaongelea mahusiano Committee Ya Maovete wakiwa na JayHill ilhali kwenye wimbo wa Drunken Master(Barua) wanaongelea sekta ya mziki na changamoto zake kwenye mdundo ambao umetumia sampuli ya Charoni Ni Wasi toka kwa Habel Kifoto & Maroon Commandos. Mimi kama mtaita nasema kongole kwa kuutumia vizuri na pia kuendelea kuenzi vilivyotulea.

Pandemic(Remix) pamoja na Pandemic Pt (Bonus) wakiwa na Blackskillz ni nyimbo zinazozungumzia changamoto zilizopo duniani kama vile Uviko 19 (Brima anaiita changamoto hii Coronization) ila pia wanakutia moyo na kukuambia kuwa wewe haupo peke yako katika hili hata kama mambo ni magumu vipi.

Nyimbo nyingine ambazo zimenivutia japokua mradi wote kiujumla ni moto ni kama vile Weh Ongea, Haina Makelele, Cheki Number na Nayo Nayo. Kwa ufupi mradi wote ni mzuka sana na mimi binafsi nisingeweza kuruka wimbo hata mmoja wakati nilipokua nauskiliza. Wanasema mziki ni tiba na dawa bora iliyowahi kutoka mwaka huu imekuja kwa muundo wa muziki toka kwa maabara za Siepna Inc toka Nairobi. Kama una dukuduku kuhusu chanjo, tiba mbadala ipo. Pata makala yako ya KiswaHealing ujitibu taratibu. Mradi sahihi kwa mda sahihi.

Wafuate Maovete na Kitu Sewer kwenye mitandao ya kijamii:

Instagram: kitusewer_swafi
Instagram: maovete