Jumatatu jioni (31.07.2023) ilikuwa siku ngumu mno, taarifa za kifo cha DJ Steve B ziliumiza nyoyo zetu.
Hakika, ni pigo kubwa katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya kwa kumpoteza DJ Skills.
Steve B alianza kufahamika enzi hizo akiwa rapper. Steve B, Mbaraka na Immam Abbas waliunda kundi na kujiita 'Underground Souls". Lao lilikuwa ni kundi lililong'ara sana kwa kurap kwa kiingereza.
Siku zilivyokwenda Steve akajitafuta na kujipata kwenye U'DJ na akaanza kufahamika akiwa East Africa Radio kisha akasogea pale Clouds FM na kilichofata baada ya hapo ni historia.
Tunamkumbuka Steve B Kwa umahiri wake akiwa mitamboni; alichagiza sana makuzi ya jina la 'Bongo Flava'.
Steve B alikuwa na familia ya DJ, wakijiita Nyuki DJ's, enzi hizo ushindani wao na Kwafujo DJ's ulichangamsha sana game, pia ulitupa burudani na fani ya U'DJ ilipata hadhi yake.
Steve B alikuwa na sikio la muziki, aliposikia kwa mara ya kwanza wimbo wa Ahadi Za Bosi alivutiwa zaidi na verse ya Ngwea. Ikumbukwe enzi hizo marehemu Mangwea hakuwa ameachia wimbo hata mmoja.
Alianza kusikika kwa wimbo huo wa Bad Brain.
Steve B alitafuta mawasiliano ya Ngwea na kisha akamleta Ngwea Dar kutoka Dodoma na akawa msanii wake na kuanza kum' manage. Walifanikiwa kutoa single mpaka albamu yake A.K.A Mimi"
So Ngwea hakuwahi kuwa na label pale Bongo Records bali alikuwa akifanya kazi kama msanii wa Steve B.
Idadi ya wasanii waliopita kwenye mikono ya Steve B ni kubwa mno, kwani Steve alikuwa kama mlezi kwa wasanii na ma DJ's waliofatia baada yake.
Itoshe kusema kwamba mchango wa Steve B kwa industry ya muziki ni mkubwa sana.
Steve alianza kusumbuliwa na maradhi ya figo kuanzia mwaka 2019, kwa miaka yote hiyo alikuwa akipambania afya yake mpaka tarehe 31 July 2023 presha ilipokuja kuhitimisha safari yake hapa Dunia.
Mola amlaze mahala pema peponi Steve B, DJ Skills.