Mambo vipi ndugu? Karibu katika Kumi Nzito Za Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki kwenye Micshariki Africa. Kwa kuanza naomba kufahamu majina yako na historia yako kwa kifupi kuhusu mziki wako ulipotoka mpaka ulipo sasa?
Kwa majina naitwa Ibrahim Twaha Ibrahim ni mtoto wa kwanza kwa mzee Twaha Ibrahim Juma ambaye alikuwa mchezaji wa mpira, na pia alikuwa msikilizaji wa mziki aina ya Reggae na ndio naona kama kishawishi kikubwa cha mimi kuwa mwanamziki. Mimi ni mzawa wa Mwanza ila kabila langu ni Mhaya wa kutokea Kagera maeneo ya Kanyigo.
Muziki rasmi niliuanza toka mwaka 2000 nikiwa darasa la tano japo haikuwa kivile mwaka 2003 ndio nilianza mziki rasmi nikiwa kama solo artist mwaka 2007 nilikutana na Mad Brown pamoja na Kashankala ndio ukawa mwanzo wa Wavuja Jasho na hapo tulifanikiwa kurekodi nyimbo kadhaa ambazo hazikufanya vizuri kutokana na production kutokuwa nzuri. Ila ilipofika mwaka 2008 nilikuwa nafanya track pembeni kama solo artist na nilifanikiwa kufanya track zisizopungua 14 ambazo hazikuwa na kiwango kizuri. Mpaka kufikia kuachia mixtape ya Fasihi Za Mtaa niko chini ya Wavuja Jasho japo ukipanga na Mungu anapanga, kwa bahati mbaya mwaka 2020 mwanachama wa Wavuja Jasho, Mad Brown alifariki na tukawa tumebaki mimi na Kashankala ila kwa sasa tuko watano.
Baba alikuwa anapenda Reggae na pia alikuwa anacheza mpira, ni kitu gani uliona ni kibaya kwenye vitu viwili alivyokuwa anapenda baba mpaka wewe ukaamua kuwa na chaguo lako la kupenda Hip Hop na kuwa mchanaji?
Baba alikuwa anapenda sana muziki japo na mpira alikuwa anaucheza naona kupenda kwake muziki ndio ikawa chachu kwangu kuwa mwana wa michano.
Kuna utofauti gani unauona wakati upo solo artist mpaka ukaamua kujiunga na wenzako na kuanzisha crew ya Wavuja Jasho. Lengo lilikuwa ni kupata nini ambacho ulikosa wakati upo mwenyewe?
Tofauti ipo maana japo kichwa kimoja hujitosheleza ila sio kikamilifu niliona kuwa na Wavuja Jasho ni moja ya mafunzo au darasa maana kila mtu huwa ana kitu anachojifunza kwa mwenzie. Japo nilikuwa najiweza mwenyewe kuna vitu vimenifanya nijiamini, bila Wavuja Jasho isingekuwa rahisi. Kiufupi Wavuja Jasho ndio wamenifanya niwe hivi nilivyo sasa.
Wimbo wa kwanza ulifanya lini, kwenye studio gani na unaitwaje? Pia ulijisikiaje ulipofanikiwa kuachia huo wimbo?
Wimbo wa kwanza niliachia mwaka 2005 na jina la wimbo ni Ubishi niliufanya Material Records na producer Dr Side na nilimshirikisha Medani. Nilijisikia furaha ya kurekodi. Hela ya kurekodi alinipa mama yangu japo alifanya kazi ngumu kwa wahindi na ndio maana ya kuuita huo wimbo Ubishi maana sikuwa na hela ila mama aliniwezesha kama mwanae baada ya kuamini mimi naweza ila kipato ndo kinachoniangusha.
Baada ya hii EP kutoka mashabiki zako wategemee kitu gani kutoka kwako kwa siku za mbeleni?
Wategemee vitu vizuri zaidi maana vipo vingi na vizuri zaidi yaani wategemee ngoma kali zinazosimamia misingi na tamaduni za Hip Hop maana ndo kama nimeanza kutoa Fasihi Za Mtaa ya B balance. Wategemee kufatia na Ep ya Wavuja Jasho na baadhi ya video ambazo zitakua nyingi kutokana na kipato ila baada ya hii Ep itafuatia Ep yangu ambayo itakua nimechana Kihaya na lugha nyingine.
Kuna upotoshaji mkubwa sana katika underground Hip Hop, wewe umejipanga vipi ili kukabiliana nao?
Ndio, hayo mambo yapo hata kwenye maisha ya kawaida ila mimi nishajipanga maana kila mtu anavyokuja ndivyo unavyompokea ila hapa linabaki chaguo lako kwenye akili yako kukubali au kukataa.
Emcee ni kioo cha jamii. Je mfumo wa muziki wako ni wa kujenga jamii au kubomoa jamii?
Mfumo wangu ni kwa ajili ya kuijenga jamii maana ndio iliyonizunguka. Naishi nayo, naona yanayotendeka kwenye jamii na ndio maana nakuwa kama muwakilishi wa kuwakilisha matatizo yao.
Tuzungumzie kuhusu Wavuja Jasho na malengo yenu ya mbeleni katika underground Hip Hop, mnajiona wapi kwa miaka miwili mbeleni, je mtakuwa mmefikia malengo yenu au ndio safari itakuwa inaanza?
Hasa malengo ya Wavuja Jasho ni kuendelea kutoa elimu kupitia mfumo wa burudani japo lengo kubwa katika maisha ni kutafuta pesa ili familia ziishi vizuri. Kwa sasa ndio tunaandaa kwanza Ep yetu na ikishakamilika ndio yatajulikana yanayofuata kikubwa watu wawe na subra juu ya Wavuja Jasho.
Mfuate B Balance kwenye mitandao ya kijamii upitia;
Facebook: Jasho Mvuja B Balance
Instagram: bbal.ncemvujajasho