Micshariki Africa na mzee wa Kumi nzito tumetua pande za Kaunti ya Kisii, Kenya. Kama ilivyo kawaida ya kumi nzito ni kuwapa habari mbalimbali za wadau wa utamaduni wa Hip-hop hasa handaki au underground Hip-hop.
Nia kuu ni kutaka kusaidia mashabiki na wafuasi wa utamaduni wa Hip-hop kuweza kuwafahamu watu ambao wanasukuma gurudumu la underground Hip-hop kwa aina mbalimbali ya sapoti yao katika utamaduni.
Tukiwa Kisii County tunapokelewa na mwenyeji wetu ambaye ni Musiq Jared. Kupitia kumi nzito tutaweza kumsoma na kumfahamu kwa undani zaidi ndugu Musiq Jared na movement zake katika underground Hip-hop.
Musiq Jared ameweza kutujibu maswali yetu vizuri na kutupa ufahamu kwa kile ambacho tulikuwa tumeshindwa kukifahamu kutoka kwake.

Mambo vipi kaka? Karibu kwenye Kumi nzito Za Beberu La Mbegu . Ningependa kujua kwanza jina lako na historia yako kwa ufupi.
Jina langu ni Jared Osallo .Nlizaliwa na kukulia Busia, Kenya lakini kwa sasa ninaishi Kaunti ya Kisii. Hiyo ndiyo ninaweza kusema juu yangu kwa kifupi! (Akicheka).
Musiq Jared ni nani? Na anafanya nini kwa ajili ya utamaduni wa Hip-Hop ?
Musiq Jared ni mjuzi wa muziki, mtangazaji wa muziki, mwanzilishi mwenza wa Door Knockers Cyphers, mjasiriamali wa vyombo vya habari na pia mwanablogu. Ninaangazia sana Hip Hop kwa kuwa hiyo ndiyo aina ya muziki ninayoipenda tangu nikiwa mdogo. Kwa sasa ninafanya kazi na Kefa Mkombola wa Micshariki Africa kwa lengo la kuwa daraja la wana Hip hop kati ya Kenya na Tanzania na pamoja na Afrika Mashariki. Hadi sasa tupo pahala pazuri kwani tunafikia malengo tuliyokusudia.
Nimeona sehemu wewe ndiye founder wa door Knockers Cyphers nini kilifanya ukaja na hii kitu katika Hip hop?
Wazo hilo lilikuja mwaka jana Desemba, 2021. Nilihisi wasanii wetu, hasa wale wa handaki hawapati majukwaa ya kuonesha uwezo wao. Kuja na cypher ilikuwa njia moja ya kuwaunga mkono. Mbali na kuwapa wasanii jukwaa pia ilikuwa njia ya kufanya kitu kwa ajili ya utamaduni wa Hip Hop.
Niliwasiliana na Brima wa Maovete , nikamshirikisha wazo na alikuwa tayari sawia na Peter Mutisya wa P-Mani Records, Evano (64 Hip Hop) ambaye ndiye mtayarishaji wetu mkuu, na Kefa Mkombola (Micshariki Africa). Tumefanikiwa kufanya cyphers 4 ihali ya 5 itatoka kabla ya mwisho wa mwaka huu. Tunabisha hodi tu na wapenzi wa Afrika Mashariki watuazime masikio na kusikiliza tunachotoa. Hakuna kingine ila muziki bora zaidi wa Hip Hop kutoka Afrika Mashariki.

Lengo kuu la DKC ni nini katika huu utamaduni wa Hip Hop?
Kuwapa rappers wa Afrika Mashariki (pamoja na walio ughaibuni) jukwaa la kupanua wigo wa mashabiki wao. Kuziba pengo hilo kati ya mkondo wa kawaida na wa handaki. Mwisho wa siku ni kuhusu Hip Hop.
Underground Hip-Hop kwa Kenya ipo vipi kwa miaka ya sasa hivi imekua au bado ipo kama miaka ya zamani iliyokuwa inaanza kuingia Kenya?
Hali ya Hip Hop nchini Kenya sasa ni nzuri sana. Hip Hop inazidi kuimarika. Watu wanaongezeka, wanakubali na wanaunga Hip Hop yetu. Angalia chati za muziki. Utapata kama nyimbo 3-4 za Kenya zitaangaziwa hapo. Tuko kwenye njia sahihi ikilinganishwa na miaka 10 au 20 iliyopita.
Wachanaji wa kike nchini Kenya si wengi kama wenzao wa kiume. Je, ni vizuizi gani vinavyowazuia wanawake kutoshika vinasa sauti na kuwa ma emcee?
Si kweli. Kwa sasa tuna wanawake wengi wanaokuja kwa kasi ikilinganishwa na siku za nyuma. Tuna watu kama Femi One, MC Sharon, Monski, Veryl Mkali Wao, Ulrykah Benard. Wanawake wote hawa wanafanya vizuri sana. Nataka kumshukuru Nimoh Futuristic wa Sauti Za Mabinti kwa kutoa jukwaa kwa ajili ya wanawake wetu ili wasikike. Kwa hivyo wanawake wanawakimbiza ma emcee wa kiume si kidogo.
Pia nini kifanyike kuweza kuongeza female emcees katika underground Hip-Hop?
Tunahitaji kuwaunga mkono wanawake wetu. Watayarishaji, watu mashuhuri kwenye vyombo vya habari na wanaotengeneza rekodi wanapaswa kuacha kuwatumia vibaya na kuwanyanyasa wanawake wetu. Hebu tuwaunge mkono wa dhati inayotoka mioyoni mwetu. Hili litatuwezesha kuwa na wachanaji wa kike wenye vipaji na ujuzi zaidi kwenye tasnia hii.
Je door Knockers Cyphers toka ilipoanza imefanikiwa kufikia malengo iliyojiwekea au bado ndio safari inaanza?
Ndio bila shaka tumefanikisha mambo kibao. Kuweza kuwakutanisha wasanii kutoka nyanja tofauti za maisha na tamaduni sio jambo rahisi, lakini tumeweza kufanya hivyo. Hayo ni mafanikio makubwa.
Ni utaratibu upi unatumika kumpata emcee atakaye shiriki kwenye Door Knockers Cyphers?
Kwa mwaka huu tulikuwa tunamcheki msanii tunayetaka kupiga nae kazi ya yeye mwenyewe akiafiki tunalianzisha. Lakini mwakani tutakuwa na utaratibu tofauti na mzuri wa kuchagua washiriki.
Je, kwa ufahamu wako ni nani emcee wa Hip Hop wa handaki?
Emcee ni mshairi aliye na dhamira ya kufundisha/kuwafahamisha vijana kwa mtazamo chanya kupitia miundo bunifu ya sauti na kumaanisha mada ya kufurahisha. Emcee husoma aina yake ya sanaa aliyoichagua kwa kutafiti na kujifunza kutoka kwa wataalamu waliomtangulia, kupata ujuzi na pia kuelewa wajibu alionao kama MC.
Rapa wa mkondo mkuu ni yupi?
Rapa ni mtu ambaye hachukulii aina hii ya sanaa kwa uzito, huchukua njia za mkato hadi mwisho na hajali uadilifu wa kisanii wa utungo. Mtu huyu anadharau chombo hiki cha mawasiliano ili kunyamazisha hadhira, kuunda hisia za uwongo za kustahiki na kuwadharau kaka na dada zao.

Naomba kama utapenda ututajie makala zako 5 bora toka Micshiriki Africa
- Gumzo langu na Nimoh Futuristic
- Uchambuzi wa album The Mwananchi Initiative ya Kayvo Kforce
- Mahojiano yangu na Smallz Lethal
- Gumzo langu na Ruby V wa Unkut Hip Hop Awards
- Mahojiano yangu na Ulrykah Benard
Emcees wako wa 5 bora toka Afrika Mashariki.
- Nikki Mbishi
- Kitu Sewer
- Johnny Vigeti
- Navio
- Nash MC
Bila kusahau producer wako wa 5 bora toka Afrika Mashariki
- HR The Messenger
- Sela Ninja
- Evano 64
- Biko Beats
- Ares 66
Ni lini Door Knockers Cyphers itawaunganisha kwenye Cyphers moja emcees toka Uganda, Tanzania na Kenya katika track moja?
Huo ndio mpango tulionao kwa sasa na mwakani tutakuwa na vijana kutoka Uganda wakipamba DKC. Pia tuna mipango ya kuleta wachanaji kutoka Rwanda na hata DRC.
Cha mwisho cha kumalizia je Door Knockers Cyphers ina mpango wa kuja na Ep, Mixtape au album kwa siku za baadae au ndio itaishia kutoa tracks na emcees mbalimbali?
Kwa sasa hatuna mipango yoyote ya Ep, mixtape au albamu lakini tutakusanya vipindi vilivyotolewa kuwa mradi wa pamoja. Ninachoweza kusema kwa sasa. Wacha tungojee na tuone wakati ujao nini kitajiri.
Mfuate:
Facebook: Musiq Jared
Instagram: @musiq_jared
YouTube: Door Knockers Cyphers