Tumetia maguu katika mkoa wa Kilimanjaro, mkoa ambao unabeba nembo kubwa Tanzania na Afrika nzima kiujumla na sio nyingine ni mlima mrefu wa Kilimanjaro.
Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa ya Tanzania ambayo imepata bahati ya kusimama vizuri katika utamaduni wa Hip Hop kuanzia underground Hip Hop mpaka mainstream Hip Hop.
Tukiwa Kilimanjaro Kumi Nzito za Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki kwenye Micshariki Africa tukapata bahati ya kukutana na mwenyeji wetu, ndugu yetu katika utamaduni, mchizi mwenye maono mengi katika jamii ya wana Hip-hop.
Mwenyeji wetu anakwenda kwa jina la Al Beez. Moja kati ya ma emcee ambaye miaka ya nyuma kidogo alitupa zawadi ya mixtape yake ya Makabrasha Ya Albeez Mixtape free (gusa link hii uipakue album hii bure) kabisa kwa kila shabiki na mfuasi wa Hip hop aweze kupata elimu juu ya kile alichokusudia tukipate.
Mchizi wetu Beez ni mtu chanya sana, katika Kumi Nzito utaweza kumtambua na kumfahamu kiundani kuhusu harakati zake katika Utamaduni wa Hip Hop na harakati yake ya kurudi kijijini.
Oi inakuaje ndugu? Karibu katika Kumi Nzito na Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki kwenye tovuti ya Micshariki Africa. Mimi nakufahamu kama Albeez, sababu ya kukufahamu ni hizi harakati za utamaduni wa Hip Hop na mambo mbalimbali ambayo unafanya. Je kwa mtu asiyekufahamu unaweza kumwambia Albeez ni nani? Na anafanya nini katika underground Hip Hop?
Al beez (Albert Issack) ni mzaliwa wa mkoani Kilimanjaro huko Marangu, aliishi na kusoma Moshi mjini pamoja na mkoani Arusha kwa sasa makazi yake ni Arusha ndipo alipoweka makazi yake ya kudumu japo Tanga, Dar na Mtwara pia ana makazi. Kabila langu mi mchanganyko wa Mngoni na Mchaga japo nimelelewa sana upande wa Wachaga. Kazi yangu kwa sasa ni muhasibu (auditor, cost controller) katika sekta za serikalini pamoja na sekta binafsi.
Katika utamaduni huu wa Hip Hop ninafanya vitu vingi sana na nina malengo makubwa sana ila maono yangu yanasema mimi ni mwanajeshi wa akiba kutokana na kwa sasa muda wangu ni mdogo sana katika kushiriki moja kwa moja na wanautamaduni wengine kutokana na kazi zangu ila nje ya ile mixtape niliyotoa mwaka 2009 (Makabrasha ya Albeez ) zipo nyingine tayari zaidi ya tano pamoja na album tatu lakini pia kuna vitabu zaidi ya saba na short film zisizopungua kumi na tano, ni suala tu la muda ufike ziweze kutoka kuwafikia watu kutokana ninachokiona. Keki ni kubwa na bado haijamegwa kabisa hivyo niliona niweke mambo sawa vizuri kiuchumi ili nitakapokuja, nije kiutofauti.
Lakini pia katika huu utamaduni nina project kubwa inayojulikana kama Turudi Kijijini (Let Us Go Back To The Village Movement) ambapo nilipanga kurudisha vijana katika uzalishaji na usindikaji kwa sababu nina imani biashara kubwa ni ya chakula na nikiwaza mbali zaidi baada ya kugundua ifikapo 2030 uhaba wa ajira Africa kwa vijana itafikia milioni 300 ndio maana nikaona ninunue mashamba mikoa tofauti tofauti kwa ajili ya hiyo harakati na mpaka sasa mkoani Arusha, Tanga na Mtwara ipo active ila soon nitakuwa huru na nitakaribisha watu mbalimbali kushiriki kwa kuwa umoja ni nguvu.
Makabrasha Ya Albeez ni mixtape ambayo ulitoa bure (free) kwa mtu anayetaka, je mapokezi yalikuwaje kwa hiyo bure na raia waliitikia kwa ukubwa gani pindi uliposema hii kitu ni bure? Pia hii mixtape itapatikana lini katika digital platform zote ili ambaye alikosa nafasi ya kupata kwa njia ya WhatsApp apate kuiskia pia?
Makabrasha Ya Albeez nilitoa bure kwa sababu niliamua kufuata kanuni na taratibu za ki mixtape kwa sababu mixtape ni kitu ambacho sio official kwa kuwa unatumia baadhi ya beat ni za watu bila makubaliano nao lakini nilitoa pia bure kwa sababu sijawahi kuwa tayari kusema kwamba kwa sasa na mimi nafanya biashara ya muziki au kwa sasa na mimi nimejikita rasmi katika tasnia ya music. Hapana mimi bado muziki sijauweka kama nafasi ya kwanza, nilifanya vile kwa kuwa kuna watu wangu wananifuatilia toka kitambo hivyo nyimbo nyingi tulizikusanya toka sehemu tofauti tofauti niliporekodia ndio maana ikaitwa “Makabrasha” nikimaanisha vitu mbalimbali vilivyofukuliwa kwenye ghala na dhumuni la bure ni ili nisiwe na deni kwa wahitaji na nashukuru muitikio ulikuwa mkubwa sana, nadhani hii inatokana na kuwa kwenye huu utamaduni kwa kipindi kirefu sasa zaidi ya nusu ya maisha yangu.
Nimekuwa nikiambiwa sana nifungue mitandao ya kuhifadhia nyimbo zangu lakini nimekuwa ni mtu wa kukataa sana na hata mara nyingi nimekuwa mtu wa kukwepa sana video japo ni vitu nikitaka nafanya muda wowote na nimekuwa nikipokea ofa za video lakini nimekuwa mgumu. Hii inatokana na mimi kuamini ni mwanajeshi wa akiba (for future use), siamini kama wote tunatakiwa kusonga mbele mimi nina imani natakiwa kuja na kitu tofauti na siku nikiingia basi niingie rasmi kama mtu mpya na mwenye kitu cha tofauti ambapo hapo nitakuwa na muda wa kutosha popote pale nitakapohitajika.
Japo kwa sasa baada ya kubishana sana na watu juu ya imani zangu nilikubali kupatikana Audiomack tu kama Al beez
Katika Hip Hop kuna nguzo nyingi, kwa nini ulichagua kuwa emcee na sio kufata nguzo nyingine ambazo zipo katika utamaduni? Mwaka gani ulijiona au uliona sasa naweza kuwa mchanaji nikafanya kitu watu wakakipenda na kukusikiliza?
Katika Hip Hop kuna nguzo zaidi ya tano na emcee ameonekana kama ndio nguzo mama. Ni kweli nilichagua kuwa emcee lakini kwa mimi ninafanya nguzo zaidi ya hiyo moja; nipo pia katika nguzo ya afya (health) lakini pia nipo kwenye nguzo ya street fashion lakini pia nipo kwenye nguzo ya ujasiriamali (entrepreneurship), hivi vyote ninavifanya ni suala la muda sahihi ufike wa kutanua hivi vitu. Ukifuatilia huko juu nilishaongelea kwamba kwa sasa nipo chimbo kama mwanajeshi wa akiba ila siku sio nyingi nitakuja lakini kitofauti, ila emcee imekuwa ni nguzo iliyonitambulisha mapema kwa kuwa ni nguzo isiyo na mambo mengi kama nguzo nyingine ambazo lazima uwe na mambo ya vibali na kila aina ya hatua.
Mwaka nilioona hapa naweza kuwa mchanaji ilikuwa ni mwaka 2009 nadhani ilikuwa siku ya Mei Mosi, siku ya wafanyakazi ambapo kulikuwa na watu wengi sana uwanjani sasa wakaitwa wachanaji wapande jukwaani kwani kuna mashindano ya ku rap. Sasa mimi ndo nilikuwa nimetoka zangu shule nikawa nimesimama mahali napimia kinachoendelea basi walipanda watu wengi sana na mimi wana wakasema man hebu nenda kawakalishe. Basi nikapanda na mizuka mingi sana na nakumbuka DJ alikuwa jamaa mmoja anaitwa Dj Manywele nadhani alikuwa huko Dar es Salaam kwenye vituo vikubwa vya habari, basi niliposhika mic nilipita na freestyle jamaa akasema huyu akae pembeni kwanza wakashindanishwa wengine mpaka wakabaki wanne ndo nikaambiwa nipambane nao na nikicheki ni ma bro wakubwa na wenye experience zao, ila siku hiyo ilikuwa kama aibu kwa sababu mistari ilikuwa inanitoka kama natema mate wale jamaa ilibidi wakimbie nikapewa zawadi mbalimbali na kumbe siku hiyo wazazi walikuwepo pamoja na sista zangu kuanzia hapo maza alinipa sana support.
Lakini mwaka mmoja nyuma nadhani 2008 niliwahi mfuata jamaa mmoja anaitwa Mark Denning huyu jamaa ana historia kubwa sana katika sanaa ya kaskazini. Huyu nilimfuata siku moja nipo na jamaa yangu (Sadam) nakumbuka tulikuwa tunatoka club enzi hzo zile club za mchana mwisho saa 12 😀, basi saa moja nafika mtaani nikamuambia twende kwa Mark Den nataka tukamchanie tupate shavu la kuzama studio turekodi, akasema fresh.
Huyu Mark Den alikuwa ni mmiliki wa kundi la Hip Hop hop linaitwa Revolution Army makazi yake yalikuwa Soweto Moshi. Nilivyofika akaniambia sisi studio tulifunga ila hebu nichanie nikusikie, basi pale pale mbele ya jamaa zake niliwapa sana mistari jamaa akaamka akaniambia twende home maana alikuwa na vifaa. Basi palepale akanipa beat na kuniambia niandike maana anahisi naweza fanya nae mambo huku ananiambia, “Man unanifanya nifanye the return of Revolution Army”, na kesho yake tulienda record ngoma yangu ya kwanza. Kile kitu kilinipa sana hope na nikaamini naweza kusonga mbele japo baada ya hapo nilipata sana changamoto mbalimbali (Nadhani hili ni suala linalofanya wengi ndoto zao kuishia njiani, tatizo kubwa kwenye sanaa zetu ukiwa mbunifu jiandae kupingwa na kukatishwa tamaa) ila zilizidi kunijenga na kufanya mambo zaidi na zaidi na kupelekea kukomaa kiakili. Niliendelea kuona matokeo mazuri na makubwa kwa sababu hata mke na ajira nilipata kupitia Hip Hop.
Miaka ya karibuni tumeona kila mtu akishika kinasa baada ya mda mchache anakuja na EP, MIXTAPE au ALBUM. Hii kwa mtazamo wako unachukulia nini, yani namaanisha underground Hip Hop marketing imekua sana mpaka watu kutaka hivyo vitu kwa kila MC ambaye yupo kwenye game au wingi wa studio umechangia hivi vitu kuonekana ni vya kawaida kwa MC? Au watu wanatoa ilimradi kapata nafasi ya kushika kinasa? Ushauri wako juu ya hili ni upi kwa underground Hip Hop?
Kwa upande wangu mimi naona ni ukurupukaji, ujuaji, utoto na kutotaka kujifunza. Nasema hivi kwa sababu moja hii, Hip Hop mambo mengi tunajifunza kutoka kwa wenzetu America lakini ukiachia hilo suala la mixtape, ep na album sio suala la kukurupuka, nikimaanisha naona kwa sasa watu hata mixtape wanaingiza sokoni hapo hapo mtu huyo anasema yeye ni Hip Hop na anatetea haki za watu wasinyonywe wakati yeye mwenyewe tayari kaiba beat ya watu na wala hamlipi huyo prodyuza.
Kingine, mixtape ni sehemu ya kujitangaza. Huwezi toa mixtape, mara EP, tayari album au mtu hata hujulikani tayari album, huu ni upuuzi na ukurupukaji na hii imeanza toka miaka ya 2010 hili game na huu utamaduni kuonekana kituko. Yawezekana ni wingi wa studio sababu ya utandawazi umechangia haya mambo lakini pia wingi wa ukosefu wa ajira na wingi wa ma broo wasiokuwa na fikra yakinifu umechangia kupoteza vijana wengi nikimaanisha mpaka sasa kwa Tanzania hakuna foundation au taasisi au kitivo fulani kinacho deal na haya mambo ya utamaduni wakati wenzetu kwa sasa wanaingia mpaka darasani kisha mtu anarudi mtaani anatoa mixtape kwa ajili ya kujitangaza na kutafuta njia za kupata watu sahihi wa kufanya nae album ili iingie sokoni na hapo waweza kuta kashatoa hata mixtape nane. So kutokana na huu ukurupukaji soko ndo limekufa, watu wameishia kuuziana wenyewe kwa wenyewe na hata hizo album zimekuwa kama ni mixtape kwa sababu album ni kama kitabu, lazima kiwe na mwanzo kati na mwisho. Album lazima iwe na maudhui, lazima ujue umeamua album yako iwe ya kisiasa, kijamii au kibiashara sio unaruka ruka ni lazima mpangilio uwepo.
Ushauri wangu juu ya hili suala ni moja, kwanza hii dhana ya underground Hip Hop tunatakiwa jua sio suala la usela sio suala la kujikatia tamaa ya kimaisha au kutokusikika kwako redioni au mpangilio wako mbovu wa kutafuta mafanikio ya kimuziki basi yakufanye uamini wewe ni underground wengi na asilimia zaidi ya 90 ni upcoming artist (chipukizi), hawana uhusiano wowote na hilo suala, zaidi ya kupotezeana muda na usela usela. Ila mtu huyo huyo akitokea mtu akamchukua na kwenda mpeleka media hawezi kataa na tutamuona kwenye shows na kila panapofaa kuuzia sura.
Underground Hip Hop ni activist, ni mtu anavyoishi utamaduni nje na kufoka foka hata ndani ya jamii yake ana mchango mkubwa kupitia maisha anayoishi. Kwa ushauri wangu tupunguze ujuaji, majukumu yamekuwa makubwa, tujfunze kutofautisha tabia za mtu binafsi, hazihusiani na utamaduni bali tabia binafsi za mtu ndo zitachagua yeye ni mtu wa aina gani katika utamaduni wa Hip Hop.
Kwa kuelewa kwako underground Hip Hop emcee ni yupi? Mainstream emcee ni yupi? Ni kitu gani kinawatenganisha na kujua huyu ni underground emcee na huyu ni mainstream emcee ?
Kwa upande wangu na kwa uelewa wangu kwa muda wote nilioishi katika huu utamaduni zaidi ya nusu ya maisha yangu kiuhalisia kabisa na bila kupepesa macho kwa ulimwengu wa sasa underground emcee hayupo tena na ndio maana hata watu wengi huhusisha underground kwa kuitamka kama upcoming. Ukitaka jua hilo rejea ngoma ya Mtazamo ya Afande Sele kuna mahala Professor Jay anasema ma underground wanafanya rap inang’ara.
Hapa akimaanisha chipukizi, kikubwa na tunapaswa kuelewa miaka ya 1975 huko America pale Hip Hop ilipoingizwa kama sehemu inayoweza ingizia mtu kipato kuna wale walipanga na walisema huu ni muziki wa ukombozi na wakajitenga kabisa lakini walikuja hicho kizaazaa kukosa nguvu na kufutika kutokana na maisha na mifumo yake inavyohitaji, lazima uingie kwenye mifumo ya ki capitalist ili maisha yaende ndo kwa upande wangu nasema hatuna underground ila tuna upcoming pamoja na mainstream artists ambapo huyu upcoming naye anapambana aje kuwa mkondo mkuu na ukitaka jua hilo, ndo maana sanaa yao tayari wanaifanya kibiashara na kama kweli ni handaki mbona hakuna aliyewahi kusema asilimia labda 40 ya haya mapato yataenda saidia jamii juu ya suala fulani? 😃
Kitu cha kuwatenganisha underground na mainstream kiuhalisia na kwa ukweli kabisa ni hakuna kwa sababu hatuna hao underground ila tuna upcoming. Mimi pia niliwahi tamani sana kuishi hayo maisha ya ki underground lakini nikabaini mifumo haitaki tena ni lazima tu kwa vyovyote kafiri atumikiwe ila sasa hapo ndo wewe utachagua uandishi unaotaka ila sio eti kisa unaandika concious basi wewe ndo handaki, hapana hata matozi kibao tu wana mangoma makali na ya hisia.
Una maoni gani juu ya underground Hip Hop ya Tanzania kuanzia kukua kwake na changamoto zake, nini unapendekeza kifanyike ili kuondoa changamoto zilizopo au kupunguza?
Maoni yangu ni moja, watu waachane na kupoteza muda juu ya underground, tufungue mipaka tutafute njia ambazo ni sahihi, huwezi diss mainstream alafu ukiitwa kwenye interview unaenda kama umeamua kuwa na misimamo, hebu ishi kijamii tuone kweli wewe umeamua sio mara uko media mara mtu wa mainstream kaku diss na wewe una jibu. Kwa kifupi ni vyema kumjua adui yetu ni nani, kabla ya kuingia vitani kama adui.
Kwa sasa tupo katika dunia ya digital, yani kupata kazi kwa mashabiki si jambo gumu kama miaka ya nyuma na zaidi kuna platform mbalimbali za kuweka kazi. Je unazungumziaje hizi platform, zina faida kwa sasa kwa msanii au bado tuendelee na mtindo wetu tuliozoea?
Hizi platform ni unyonyaji na watu wengi hujiunga huko lakini manufaa hakuna. Ili sanaa yetu itulipe kabla ya hizi platform tunahitaji haki miliki, tunahitaji elimu ya kibiashara na kiushairi tunahitaji elimu juu kila kitu, juu ya muziki. Kwa sasa hizi platform labda ni kujtangaza tu ila manufaa ya kifedha ni sifuri.
Emcee ni kioo cha jamii, kwa mtazamo wako je ma emcee tulionao katika underground Hip Hop wanafaa kuwa kioo cha jamii au bado kuna sehemu tunapwaya?
Narudia tena hakuna underground Hip Hop pia hayo mawazo tuondoe kwa sababu ndio yamefanya watu wahukumiane kila kukicha. Ni lazima tujue sisi sote ni binadamu, kila mtu ana madhaifu, emcee ni kioo cha jamii kwa kile anachosema ila emcee ni mwanajamii wa kawaida kwa kile anachokwenda kukiishi.
Sehemu tunayo pwaya ni ile kujimilikisha vitu hatuviwezi, unamdiss mwenzio anaimba mapenzi apo apo unasahau na wewe una madhaifu yako kibao. Kile kitendo cha kujiona bora kulko wengine tayari ni kosa tujirekebishe hapo ili kufungua fursa Zaidi. Ni vyema tukavunja mipaka ya kiimani za kuwazika na tukaishi maisha halisi.
Kwa miaka mitano mbele unaweza kuitazamiwa wapi movement yako ya Turudi Kijijini katika underground Hip Hop ya Afrika Mashariki, yani kiukuaji na kiuwekezaji?
Hii ni taasisi kubwa kwa sababu tayari nimeweza fanikiwa kwenye uwekezaji na bado naipambania katika uwekezaji ili hapo baadae taasisi isije yumbishwa na wajuaji. Imani yangu kwa miaka mitano ijayo ni kuwa itakuwa ni taasisi inayozalisha ajira lakini pia kuchangia zaidi pato la taifa kwa sababu ifikapo 2030 Waafrika vijana milion 300 hawatakuwa na ajira hivyo ni muda wetu kuwa wabunifu ili kuja nusuru taifa katika haya majanga
Asante kwa mda wako brother, kwa kumaliza naomba unitajie ma emcee wako 5 bora wa underground Hip Hop na producer bora wa underground Hip Hop. Pia unazungumziaje matabaka yaliyopo katika underground Hip Hop kwa sasa?
Emcee wangu watano bora mpaka sasa kwa Tanzania ni;
- ChindoMan (Umbwa)
- Donnie The Gamble
- Mgosi Mkoloni
- Fredlou
- Kay Wa mapacha
- Albeez
Ma Producer hawa nawaweka kwa heshima kubwa kwa sababu pia ni watu wamewahi kuwa interested kunipa album pasipo kutumia nguvu maana ni wao pia walionyesha upendo
- ChindoMan (Umbwa)
- Prof Ludigo
- Jegala Kondukta Kusini
- Black Ninja
- Patrino
- De La P
- Ambrose (Dunga)
- Paul Loops
- DJ Kushmatic
- Confy Mike
Matabaka ni mazuri sana maana yanaleta kuijtambua, nasisitiza sana utengano, chuki na lawama ili kwa wale wanaojitambua wabadilishe kuwa fursa.