Emsa Msanii Mkubwa

Dar DSM sema Dar Es Salaam moja kati ya nyimbo za mkongwe wa muziki wa Hip Hop Tanzania Sugu akizungumzia kuhusu Dar Es Salaam.

Nimenukuu kipande kidogo cha wimbo huo kwa sababu kubwa moja ya kutaka ufahamu ndugu msomaji wiki hii tupo ndani ya jiji la Dar Es Saalam.

Unaweza sema Bongo kama mtu mzima Prof Jay alivyotamka kwenye wimbo wake wa Bongo Dar eS Salaam. Wakongwe waliona mengi katika jiji la Dar.

Lakini Beberu wiki hii nimemuona Emsa Msanii Mkubwa moja kati ya vipaji vikubwa katika underground Hip Hop ya Tanzania na Afrika mashariki kwa baadae.

Jina "Msanii Mkubwa" alipata kutoka kwa mashabiki wake baada ya kuvutiwa na kile alichokuwa anakifanya juu ya jukwaa pindi kinasa kikiwa mkononi kwake.

Kumi Nzito na Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki kwenye Micshariki Africa ikaona sio mbaya kupiga nae story mbili tatu na kuzileta kwenu wasomaji mpate kumfahamu kiundani Emsa Msanii Mkubwa ni nani na anafanya nini katika underground Hip Hop.

Ungana nami katika kufatilia Kumi Nzito na Emsa Msanii Mkubwa ndani ya Micshariki Afrika.

Mambo vipi ndugu? Karibu katika Kumi nzito Na Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki hapa Micshariki Africa. Mimi nakufahamu kama Emsa Msanii Mkubwa. Je kwa mtu asiyekufahamu unaweza kumwambia Emsa ni nani? Na anafanya nini katika underground Hip-hop?

Mambo ni poa sana. Asante kwa kunikaribisha katika Kumi Nzito. Naitwa Emsa na najihusisha na muziki wa Hip Hop hapa Tanzania pia nimekuwa nikijihusisha na mambo mbali mbali yanayohusu underground Hip Hop toka mwaka 2012 kama ku perform majukwaani (Kilinge, Bure, Kinasa n.k) pamoja na kuuza bidhaa kama vile flana za machata na santuri zangu mwenyewe.

Hivyo kwa ufupi naweza nikasema Emsa ni mmoja kati ya wasanii wanaofanya na kuwakilisha underground Hip Hop Tanzania.

Katika Hip Hop kuna nguzo nyingi. Kwa nini ulichagua kuwa Emcee na sio kufuata nguzo nyingine ambazo zipo katika utamaduni? Mwaka gani ulijiona au uliona sasa naweza kuwa mchanaji nikafanya kitu watu wakakipenda na kunisikiliza?

Nimechagua kuwa emcee maana ndio nguzo ambayo naweza kuitumia vyema na kuwasilisha nilichonacho na kikaeleweka katika jamii. Yaani ndio kitu ninachokiweza, nikisema nitumie na nguzo nyingine nitakuwa nafosi.

Kiukweli kabisa kuanzia mwaka (2020) ndipo niliona sasa nimekuwa imara na naweza kufanya kitu kitakachokubalika na kueleweka. Ukiangalia nyimbo kama 1. Machache 2. Aliniambia 3. Mafanikio utaona utofauti kati ya Emsa wa 2012 na huyu wa sasa.

KIRUA ni EP yako ya kwanza kutoka kama sikosei, mafanikio ya hii EP kwenye game yako yakoje? Je imekufikisha ulipokusudia au ulikuwa unajitambulisha kwanza kwa mashabiki waweze kukufahamu?

Ni Kweli kabisa KIRUA ni Extended Play (EP) yangu ya kwanza. Nakumbuka kipindi natoa hii Ep target yangu ilikuwa ni kusogeza mashabiki wangu na wasio mashabiki wangu karibu, yani nilitoa namba ya WhatsApp na nilikuwa naituma WhatsApp tu tena mimi mwenyewe kwa hiyo wote waliokuwa wananitafuta kutaka EP nilisevu namba zao na mpaka leo ni watu wangu wa karibu na wamekuwa wakiwa watu wa kwanza kupata update zangu zote za muziki. Ndio maana hata muda mwingine nimekuwa mvivu na hizi social networks (FB &IG) maana watu ambao Ninawa target wengi ninao WhatsApp. Ninapohitaji watu wapya au kazi ifike kwa wengi zaidi huwaga ndo nawekeza nguvu katika social networks na blogs. Hivyo kwa lengo la kuwa na mashabiki wangu karibu KIRUA EP ilifanikisha hilo.

Mafanikio mengine KIRUA EP ilinikutanisha na wazawa wa KIRUA maana ni jina la kijiji kilichopo mkoani Kilimanjaro. Yaani naweza nikasema hii EP ilinitambulisha na kunikutanisha na watu. EP ilianza kurushwa WhatsApp baada ya idadi lengwa kufikia ndipo nilii upload Audiomack na YouTube.

Tukitoa KIRUA EP je kuna mradi mwingine ambao ulifanikiwa kuingia sokoni? Je mtu akitaka miradi yako anaweza kupata kwa njia gani?

Tukitoa KIRUA EP mradi mwengine ulioingia sokoni ni album yangu Uwezo By Nature iliyotoka 2018. Kupata miradi hii, KIRUA EP ipo Audiomack pamoja na YouTube lakini Uwezo By Nature ni mpaka unicheki mwenyewe. Mradi unapatikana kwa njia ya soft copy na hard copy.

Kwa sasa tupo katika dunia ya digital yani kupata kazi kwa mashabiki si jambo gumu kama miaka ya nyuma na zaidi kuna platform mbalimbali za kuweka kazi. Je unazungumziaje hizi platform, zina faida kwa sasa kwa msanii au bado tuendelee na mtindo wetu tuliozoea?

Kuna kauli mbili nazishikilia sana #1 "Hustle hard, in this life nobody sees what you get from what you dreaming". Kiukweli hizi platforms kwa wasanii wachanga hazilipi na nilithibitisha hili niliposikiaga mdundo.com inalipa aisee niliweka mangoma yote mpaka album, sambaza sana link kila kukicha mimi na link, downloads zikaongezeka na rank yangu ikapanda. Kuna watu wakaona napiga mpunga mrefu kumbe kiliingia kiasi kidogo sana na nilipo request mpunga wangu account ikaonesha nimeshapokea pesa na sikupokea. Hivyo kama ni msanii mchanga anafanya muziki ili apate faida ni vyema akamiliki soko lake mwenyewe na akaendelea kuuza kwa njia iliyozoeleka ila kwa hawa wa management wenye uhakika wa streams kuanzia 100,000 hizo platforms nahisi zinawalipa ila sijafanya tafiti.

"Don't make someones opinion be your reality"

Wasanii wengi walio mkondo mkuu huaminisha watu kwamba hizo platforms zinalipa vizuri na wanapiga mpunga wa kutosha na maisha yao ni mazuri kupitia muziki lakini kiuhalisia wengi wao hawapo kama tunavyohisi, maisha yao ni kama yetu tu  na pengine tumewazidi ila wao walichotuzidi ni hizo photoshoot na kupiga picha maeneo mazuri. Hivyo basi naweza nikasema kila mtu aamini katika njia anazotumia kusambaza kazi zake as long as zikiwa zinamlipa au kumpa atakachotaka na endapo akapokea ushauri kuhusu hizi digital platforms asiufanye huo ushauri kuwa uhalisia pasipo kufanya uchunguzi wa kwanza.

Miaka ya karibuni tumeona kila mtu akishika kinasa itachukua mda kidogo anakuja na EP, Mixtape au Album hii kwa mtazamo wako unachukulia nini yani namaanisha underground Hip Hop marketing imekua sana mpaka watu kutaka hivyo vitu kwa kila emcee ambaye yupo kwenye game au wingi wa studio umechangia hivi vitu kuonekana ni vya kawaida kwa emcee? Au watu wanatoa ili mradi kapata nafasi ya kushika kinasa? Ushauri wako juu ya hili ni upi kwa underground Hip Hop?

Hii wasanii wengi kuja na EP inatokana na gharama za kurekodi kuwa ndogo, studio pia kuwa nyingi pamoja na producers wengi kufanya kazi kishkaji na wasanii mpaka watu waliokuwa mashabiki wa Underground Hip Hop nao wakaanza kutoa mangoma na Eps.

Wengi hawajui maana ya Ep na album pia hawafahamu kwamba hivi vitu ndo vinavyoleta heshima. Hii inapelekea wanafanya kazi mbovu kuanzia production mpaka maudhui na kuuwa soko, "Wanatoa toa tu Ep na album ili na wao waonekane wamefanya" Wengine wanarekodi mangoma mengi wakishaona hayawezi kwenda wanayakusanya na kuita EP au album.

Ushauri wangu ni kwamba "TUZIPE KAZI ZETU ZA SANAA THAMANI" hii inaendana na uwekezaji {Tuwekeze pesa na muda wa kutosha katika kazi zetu} ili kazi inapotoka iwe bora kuanzia kwenye production na maudhui.

Kwa miaka mitano mbele unajitazama wapi katika underground Hip Hop ya Afrika Mashariki yani kiukuaji na kiuwekezaji?

Kiukweli game yangu kwa sasa inachangamoto kiasi kana kwamba nashindwa hata ku predict ndani ya miaka mitano mbele nitakuwa level ipi.  Iko hivi, kazi ninayofanya kwa sasa inakula muda mwingi sana pia haiendani na muziki "kazi yangu na muziki ni vitu viwili tofauti". Hata business partners wangu wa kazi hawapaswi kujua kama nafanya muziki. Mwaka huu panapo majaaliwa nitaachia album ambayo itabeba sanaa yangu yote kisha nita stick kwenye kazi, baada ya kufikia mafanikio ninayoyahitaji kupitia kazi ndipo nitakaporejea tena kwenye game.

Una maoni gani juu ya underground Hip Hop ya Tanzania, kuanzia kukua kwake na changamoto zake. Nini unapendekeza kifanyike ili kuondoa changamoto zilizopo au kupunguza?

Underground Hip Hop ya Tanzania kuna muda inakuwa na kuna muda inafifia kutokana na wasanii kutokupendana wenyewe kwa wenyewe na kuwa wabinafsi. Kingine kumekuwa na matabaka. Kuna watu wanaigawa underground Hip Hop na kujimilikisha pia kuna watu ambao wana criticize kila jambo haijalishi ni linajenga au linabomoa kitu ambacho kinafanya harakati nyingi zinazoanzishwa kukuza underground Hip Hop zinaibuka na kupotea. Hapo hapo pia kuna watu wana chuki dhidi ya mafanikio ya watu kupitia muziki.

Kuondoa Changamoto hizi ama kupunguza mi naona ni tuache matabaka, ubinafsi, roho za kwanini kisha tuwe kitu kimoja na kusaidiana anapoteleza mtu aelekezwe kwa njia stahiki sio kwa kukishusha thamani alichofanya au anachofanya.

Kwa uelewa wako underground Hip Hop emcee ni yupi? Mainstream emcee ni yupi? Ni kitu gani kinawatenganisha na kujua huyu ni underground emcee na huyu ni mainstream emcee?

Kwa uelewa wangu under group Hip Hop emcee ni msanii wa Hip Hop ambaye;

  1. Anafanya muziki pasipo kutegemea airtime za media wala kiki
  2. Mashairi yake yanagusa maisha ya mtaa

Mainstream emcee ni msanii ambaye;

  1. Anafanya muziki kwa kutegemea airtime za media
  2. Ana fake maisha "Wenyewe wanasema kujibrand" unakuta mtu anatumia pesa nyingi ili kuaminisha watu kwamba anaishi maisha mazuri au kufanikiwa,
  3. Anategemea management ije kumfanyia kila kitu.

Kiufupi mainstream wengi wanaishi katika mifumo tegemezi.

Asante kwa mda wako brother, kwa kumaliza naomba nitajie emcee wako 5 bora wa underground Hip-Hop pamoja na producer bora wa underground Hip Hop. Pia unazungumziaje matabaka yaliyopo katika underground Hip Hop kwa sasa?

Asante pia.

Kiujumla ni ma emcee wengi sana wa underground kwangu ni bora nikisema niwataje watano itachukua muda kuchuja. Producers bora pia wa underground Hip Hop kwangu wapo wengi, nikisema nimtaje mmoja moyoni nitabaki na kinyongo kwamba kuna wengine sijawatendea haki.

Matabaka hayajengi ni vyema tukatatua tofauti zetu na kuwa kitu kimoja.

Mcheki Emsa kwenye mitandao ya kijamii;

Facebook: Emsa Msaniimkubwa (Emsa Msaniimkubwa)
Instagram: Emsa Msaniimkubwa