A Town, A City, Chuga ukipenda tamka Arusha. Kumi nzito za Beberu La Mbegu zimetua moja ya majiji makubwa ya Hip Hop kwa Tanzania. Arusha inapata respect kubwa katika Hip Hop sababu ni sehemu ambayo imetoa ma emcee wengi katika utamaduni.
Ndani ya Arusha nakutana na mwenyeji wangu memba toka kundi la RPG, Jay Yank Rpg ni mmoja kati ya wachanaji wakali na wenye ujumbe wa kutosha kimashairi. Mtindo wa uchanaji wake nao ni kivutio tosha katika masikio ya msikilizaji yoyote yule wa Hip Hop.
Kumi nzito zinakudondoshea maswali kumi mazito ambayo yamejibiwa kiufasaha sana na ndugu Jay Yank Rpg. Ndani ya maswali utapata nafasi ya kumfahamu vizuri Jay Yank Rpg kuhusu mziki wake na harakati zake. Ungana nami katika kunisoma na umsome Jay Yank Rpg.
Mambo vipi ndugu? Karibu katika kumi nzito na Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki kwenye mtandao wa Micshariki Africa. Mimi nakufahamu kama J Yank Rpg sababu tunafahamiana kitambo sana, je kwa mtu asiyekufahamu unaweza kumwambia J Yank Rpg ni nani? Na anafanya nini katika underground Hip Hop?
Safi Kaka na shukrani sana kwa kunikaribisha katika hiki kipindi. Mimi kwa majina halisi ninaitwa Joseph Msechu ila kwa jina ambalo ninafahamika katika Utamaduni huu wa Hip Hop ninajulikana kama J Yank RPG na huku handaki ninafanya harakati za muziki wa Hip Hop.
RPG inasimama badala ya nini au tuseme inawakilisha nini katika kile unachokifanya kwenye Hip Hop? Kama inawezekana ututajie kiundani zaidi tuweze kufahamu
RPG hili ni Jina la kundi letu ambalo tunatumia kutuwakilisha katika huu utamaduni wa Hip Hop, ambapo kwa kirefu ikinyumbuliwa ina maana ya Rap Poetic Grenades. Na ndani yake RPGs inasimamiwa na kuongozwa na wahusika watatu pekee ambao kwa majina ni J Yank RPG (Mimi), Slaiyank RPG, na JoeMic_RPG.
Nje ya RPG, J Yank kama J Yank kuna mradi gani ambao upo sokoni umeuachia ambao raia wanaweza kuupata?
Mpaka sasa bado sina mradi wangu binafsi zaidi ya kazi kibao ambazo nimeshiriki na kundi langu la RPGs na nyinginezo ambazo nimeshirikishwa na washkaji wengine kibao tu. Ingawaje tulikuwa tumejikita katika kazi za kundi sana sana, lakini karibuni tunatanguliza mradi wa Slaiyank ambao tutawajuza watu tunauachia lini na pia vilevile kwa sasa tupo katika maandalizi ya mradi wetu sisi wawili, mimi na member mwenzangu Joe Mic ambao pia tutawajulisha watu utatoka lini pia.
RPG mipango yake ya baadae ni ipi katika underground Hip Hop. Je mshatazama mpango wa kufanya kazi na ma emcee wa nje ya Tanzania ili kuongeza idadi ya wafuasi wenu wapya?
Mipango yetu ya baadae ni kwamba RPG tumejipanga kuwaletea kazi bora zaidi na za kiwango pia. Wafuasi watarajie kuona videos maana ni muda kidogo hatujafanya hivyo. Na kuhusu kufanya kazi na emcees wa nje katika kuusafirisha huu muziki ni moja kati ya mpango kazi uliopo, hivyo mengi mazuri tuyategemee kutoka hapa.

Kundi la RPGs - (Kutoka kushoto) - Joe Mic - J Yank - Slai Yank
Mtu akitaka kazi zako au za kundi lako anaweza kupata kwa njia zipi au platform zipi? Kama ni tofauti na platform zilizopo anazipata vipi?
Katika suala la kuzipata kazi zetu mtu anaweza kufanya mawasiliano na sisi moja kwa moja iwe katika mitandao ya kijamii ama mawasiliano ya namba za simu ili kuweza kupata kazi zetu kwa sababu bado hatujaziweka kazi zetu katika baadhi ya mifumo tofauti na YouTube pekee. Ila kwa uhitaji wa albums na mixtape tunachekiana tu kisha utapata nakala na kuendelea ku'support kazi zetu zaidi
Mwaka 2021 nilikuona katika Festival ya Hip Hop Asili kama mshiriki wa shindano la kusaka mchanaji bora kama sikosei kwa bahati mbaya ushindi ukaenda kwa mchizi mwingine. Kwa ushiriki wako katika Hip Hop Asili Festival umejifunza nini kama emcee juu ya shindano lile?
Hakika nilikuwa mmoja kati ya washiriki katika event hiyo ya Hip Hop Asili Festival na nilishiriki vyema kama ilivyostahili uwepo wangu katika vipindi na matukio kadha wa kadha kulingana na mpangilio wa tukio lilivyokuwa limepangiliwa. Na pia nilijifunza mambo kadhaa na kujiongezea maarifa zaidi kupitia kaka zetu waliotutangulia katika huu utamaduni kupitia madarasa tuliyokuwa tumepangiwa na kuhudhuria. Na pia niliweza kupata uzoefu wa namna na jinsi ya kuweza kufanya kazi zangu/zetu kiufanisi zaidi na kuweza kufikia matarajio tunayojiwekea sisi kama kundi na hata mimi binafsi pia, hivyo kwa ujumla niseme nilipata mtazamo chanya katika hii tasnia yetu.
Kwa sasa tupo katika dunia ya digital yani kupata kazi kwa washabiki si jambo gumu kama miaka ya nyuma na zaidi kuna platform mbalimbali za kuweka kazi je unazungumziaje hizi platform, zina faida kwa sasa kwa msanii au bado tuendelee na mtindo wetu tuliozoea?
Ni kweli usemacho kuhusu upatikanaji wa kazi za wasanii kwa hivi sasa ni rahisi sana kulingana na mifumo iliyopo na pia kwa nielewavyo mimi kila jambo lina faida yake na hasara pia. Hivyo hata hii mifumo naamini wapo ambao wamenufaika nayo na ikawasaidia sana tu na pia wapo ambao bado haijawanufaisha na huenda wanaendelea kukomaa pia, siwashauri kukata tamaa kwa hao ambao bado haijawanufaisha kikubwa waendelee kupambania kile wanachoamini na cha zaidi wafanye kazi zao kwa viwango stahiki watafikia wanapotizamia
Kwa kuelewa kwako underground Hip Hop emcee ni yupi? Mainstream emcee ni yupi? Ni kitu gani kinawatenganisha na kujua huyu ni underground emcee na huyu ni Mainstream emcee?
Emcee wa handaki ni mshairi aliye na dhamira ya kufundisha/kuwafahamisha vijana kwa mtazamo chanya kupitia miundo bunifu ya sauti na kumaanisha mada ya kufurahisha. Emcee husoma aina yake ya sanaa aliyoichagua kwa kutafiti na kujifunza kutoka kwa wataalamu waliomtangulia, kupata ujuzi na pia kuelewa wajibu alionao kama. Emcee.
Na Rapa wa mkondo mkuu ni mtu ambaye hachukulii aina hii ya sanaa kwa uzito, huchukua njia za mkato hadi mwisho na hajali uadilifu wa kisanii wa utungo. Mtu huyu anadharau chombo hiki cha mawasiliano ili kunyamazisha hadhira, kuunda hisia za uongo za kustahiki na kuwadharau kaka na dada zao. Na pia huyu rapper wa mainstream lengo kuu ni kupata hela tu bila kujali kuwa anapoteza maadili ama La!
Na kinachowatofautisha hawa watu pia ni namna ya uuzaji wa Kazi zao kwa sababu mainstream mara nyingi huwa ni label kubwa zinasimamia msanii mfano: TDE na kina Kendrick. Ila underground huwa ni label ndogo ndogo (Indie) na msanii binafsi mwenyewe kimpango wake.
Tukizungumzia underground Hip Hop ya Tanzania kwa mtazamo wako je imesogea sehemu nzuri katika jamii yetu tuliyokusudia watufahamu au bado tuna safari ndefu kufikia jamii yetu?
Handaki ya Tanzania kiukweli tumesogea pazuri mpaka sasa japokuwa bado tunakwenda pole pole kwa kiasi fulani. Ni kama safari ya matumaini. Wasanii wa underground wameanza kupenya na kuifikia mitaa kwa msaada wa mtandao, ukijaribu kuangalia kwa sasa mpaka na wao wameanza kualikwa na mainstream media kuonesha uwezo wao. Kwa hiyo hapo kazi kubwa iwe kwa wasanii wenyewe kutengeneza nyimbo nzuri (production na maudhui pia) hii itawasogeza zaidi na mitaa ambayo ndio chimbuko lao kwa maana ya wanapotokea.
Asante kwa mda wako brother, kwa kumalizia unaweza nitajia emcees wako wa 5 bora wa mda wote bila kusahau producer wa 5 bora kwa mda wote. Pia unazungumziaje matabaka yaliyopo katika underground Hip Hop je yana tija kwenye utamaduni au tuyapotezee yanadumaza utamaduni?
Shukrani sana pia kaka, tuko pamoja...Kwa Emcees wangu watano bora wa muda wote hapo wapo wengi ninaowakubali lakini kulingana na idadi elekezi hapo kuna hawa hapa ambao ni Johnny Vigeti, Hashim Dogo, JCB, Nash Mc, na Adam Shule Kongwe. Ingawaje wapo wana kibao ninawaaminia na wao kwa nafasi ya upendeleo ninawajumuisha kwa nafasi ya sita hapo (Wana Wote Wa Handaki).
Producers wangu watano wa muda wote kuna Chizan Brain, Duke Tachez, P-Funk Majani, Palla, na Dr. Luis.
Kuhusu suala la matabaka katika underground Hip Hop mimi sioni tija kwa uwepo na mtawanyiko baina yetu nikiamini kwa ule msemo wa "Umoja Ni Nguvu" hivyo ni vyema zaidi tukashikamana kwa Umoja na Upendo pia tukasaidiana kuzisogeza harakati zetu mbele ili zifike mbali zaidi na zaidi naamini tukishikamana inawezekana.
Mcheki J Yank kupitia mitandao ya kijamii;
Facebook: J Yank Rpg
Instagram: j_yank_rpg