Jimmy Al Jabbar

Tanga bado kulala kwa fani, moja kati ya neno toka kwa mkongwe Mr Ebbo (apumzike kwa amani) alipenda kulitumia kumaanisha Tanga ipo macho katika fani.

Micshariki Africa na mzee wa Kumi Nzito, Beberu La Mbegu tupo ndani ya Jiji la Tanga, ni miongoni mwa majiji  ambayo yana watu wenye uwezo mkubwa sana katika kufanya mambo makubwa kwenye game japo wadau kuna namna wameamua kufumbia macho.

Kwa kuona hilo Micshariki Africa ikaona sio kesi kufika mpaka Tanga, tukapokelewa na mwanetu kabisa mtu ambaye yuko poa na kila mtu na mtu ambaye ukienda kiujuaji utatulizwa kwa kuelimishwa ukatulia.

Wiki hii tuko na Jimmy Al Jabbar, ambaye ni spiritual seeker, activist, actor, emcee, songs writer na script writer pia. Jimmy bila kusahau pia ndio muasisi wa kundi zima la Waasi Fulani.

Nia ya Kumi Nzito ni kukupa elimu kidogo juu ya kile usichokifahamu au kama unakifahamu inakukumbusha kupitia wadau mbalimbali ambao inakutana nao na kupiga story kuhusu underground Hip Hop.

Ungana nami katika maswali na majibu toka kwa Jimmy Al Jabbar upate kuyajua mengi kuhusu yeye na Waasi Fulani bila kusahau underground Hip Hop.

Inakuaje ndugu? Karibu katika kumi nzito na Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki kwenye website ya Micshariki Africa. Mimi nakufahamu kitambo kidogo kama Jimmy, Sokwe Mkongwe na Dizonga sababu ni nini mpaka unabadilisha a.k.a sana? Je kwa mtu asiyekufahamu unaweza kumwambia Jimmy ni nani? Na anafanya nini katika underground Hip Hop?

Ebana fresh tu asante sana nimeshakaribia ndugu. Ni kweli Kabisa ila kwa mtazamo wangu nickname zangu zinatokana na ukuaji wa kifikra pamoja na watu ambao wananizunguka.

Kwa mfano kipindi najiunga Facebook nilikuwa natumia nickname ya Jimmy Msauzi ila kipindi kile watu wengi walikuwa wanatumia hiyo Msauzi ndipo mwanangu mmoja kwa jina Bravo Buku Jero akawa ananiita Dizonga akiwa na maana ya Msauzi Ili kujitofautisha na wengine ikabidi nibadilishe hivyo nikajulikana kama Dizonga.

Msauzi lenyewe lilipatikana chuo kutokana na kuwa msimuliaji mkubwa wa stori za mabaharia kuzamia nchi ya Afrika Kusini kujitafutia malisho ya kijani kwa hiyo hapo likazaliwa jina la Msauzi. Hiyo Sokwe Mkongwe lilitokana na mimi mwenyewe kutafuta maarifa huru katika ukuaji wangu wa kiroho likiwa na maana ya Spiritual Operate Knowledge Wisdom and Education (S.O.K.W.E) na hiyo Mkongwe ni mapito yangu katika kutafuta Ukweli.

Zikapita nicknames nyingi na sasa najulikana kama Jimmy Al Jabbar au Zadafi Allah na hii imetokana na ushawishi wa Maarifa ya kundi huru katika Spiritual awakening linalojulikana kama Five Percent au NGE (Nation of Gods and Earth) kwa hiyo ndivyo ilivyo katika ushawishi wa kujitafuta na watu wanaonizunguka.

Kwanza Jimmy ni jina langu halisia katika vyeti vya serikali, majina kamili naitwa Jimmy John Mkombozi na ni uzao wa mwisho katika uzao wa Mzee John Daniel Mkombozi (Marehemu) nikitanguliwa na dada zangu wanne.

Mimi ni mwenyeji wa Mkoa wa Tanga wilaya ya Korogwe kabila langu ni Mzigua. Kwa Sasa naishi Mkoa wa Geita katika wilaya ya Chato nikihudumu Katika Idara ya Elimu. Pia Mimi ni baba wa watoto wanne wa kiume ni watatu wa kike mmoja. Nje ya hayo Mimi ni emcee/ rapper/ ghostwriter, spiritual seeker, actor.

Katika usahihi hapo mimi sio underground Hip Hop bali ni local Underground Hip Hop kutokana na underground Hip Hop yenyewe kuwa corrupted katika upande wa bongo. Katika upande huo mimi ni mwalimu ,mchenguaji ,mhubiri, mwandishi ,mburudishaji, mjasiriamali kwa kifupi nipo katika nguzo (Elements) za Hip hop moja kwa moja na pasipo moja kwa moja.

Katika utamaduni wa Hip Hop kuna nguzo zake ambazo zinajulikana, lakini wengi wa watu wamejikita katika nguzo moja ya Emcee ambayo inaonekana ni nyepesi kwa wengi wao. Je nikisema na wewe umechagua kuwa emcees sababu ni nguzo pekee ambayo kila mtu anatamani kuwa utasemaje? Pia kama hutojali unaweza kutuelezea MC ni nani katika Hip Hop?

Sio kweli katika utamaduni huu wa Hip Hop hakuna nguzo ambayo ni nyepesi nguzo zote ziko sawa sababu yote ni mazao ya thoughts anachokiwakilisha DJ ni sawa na anachokiwakilisha mchata, anachokiwakilisha mvunjaji (break dancer) vyote vinatumia Knowledge and Understanding.

Mtu anakuwa anavyokuwa kulingana na mazingira yanayomzunguka, mfano mtoto akikulia mtaa wa Panya Road au ukahaba na yeye atakuwa katika mazingira hayo hayo ndivyo ilivyo hivyo hivyo. Mimi nimekuwa katika mazingira ya Emcees na mimi nimejikuta ni emcee sio kama kuwa emcee ni kitu rahisi, wanaofanya kuwa emcee ni kitu rahisi ni wale wanaorahisisha hizi nguzo rahisi kwa tungo nyepesi kwa kuwa wanarap vitu ambavyo ni vyepesi na hawazingatii dhana ya kuwa emcee.

Bila shaka kaka emcee inatokana na nguzo inayoitwa Emceeing kwa maana ya Rapping kwa hiyo anayewakilisha hii nguzo anaitwa Emcee au Rapper. Emcee ni yule mwanafunzi wa utamaduni wa Hip Hop ambaye ana njaa na kiu ya maarifa japokuwa anayo kichwani lakini pia bado anayo njaa ya kuyasaka zaidi kupitia njia mbali mbali ikiwemo kusoma vitabu na kufanya tafiti katika mambo yaliyopita, yaliyopo na yanayokuja.

Pia anaweka jitihada zake zote katika uandishi ili kuifikia jamii yake katika nyanja zote kwa mfano kijamii, kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kijamii. Vile vile kunyanyua umati kwa kile anachowakilisha kwa kuwa kile anachowakilisha kinagusa kila moyo wa yule aliyehudhuria tamasha lake ukumbini.

Ukiachana na hayo Emcee pia anatakiwa kuzingatia haya yafuatayo;

Kwanza awe na uelewa wa mambo yaliyopita, yaliyopo na yanayokuja kwa usahihi. Afanye research ya kina kabla ya kuandika, wakati wa kuandika na pia wakati wa kuwasilisha kazi zake kwa hadhira. Ukiachana na hilo katika kazi zake awe na ujuzi wa kuzingatia aina za uandishi na zana zote za uwasilishaji wa kazi zake mfano Metaphor, similes, Vocabulary na Street Language(Sitiari, tashibiha, Msamiati na Lugha ya Mtaani) hayo ni mavazi ya mashairi. Mengineyo awe mwanafunzi katika sanaa yake kila inapoitwa leo na pia ajue freestyle (mitindo huru) na freestyle battle kupitia freestyle.

Kundi la RPGs - (Kutoka kushoto) - Joe Mic - J Yank - Slai Yank

Kwa uelewa wako underground Hip Hop emcee ni yupi na mainstream emcee ni yupi? Ni kitu gani kinawatenganisha hawa wawili na mtu atajuaje kuwa huyu ni underground emcee na huyu ni mainstream emcee?

Underground emcee;

Kama nilivyotangulia kusema kuwa emcee ni zao la Element ya emceeing hivyo huyu ni Mwanafunzi Wa Utamaduni ambaye ana njaa ya Maarifa na kila siku anajifunza kitu kipya/vitu vipya. Kupitia Skills alizonazo ataifikia jamii yake katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kidini, kijamii na kuishape jamii katika muelekeo sahihi. Pia anakuwa yuko aware na kile anachotaka kuwakilisha kwa hiyo huyu ni mtu wa kufanya research kila anapotaka kuandika kuhusu jambo fulani.

Pia katika uandishi wake lazima mashairi yake ayavishe mavazi au atumie zana za uwasilishaji kwa usahihi mfano metaphor, similes, vocabulary na Street Language (Codes). Na pia yuko makini katika uchaguzi wa beats kulingana na topic/content anayotaka kuwakilisha.

Mainstream kuna rappers wengi kuliko emcees. Hapa kwa matakwa ya kibiashara mara nyingi hawa sio wanafunzi wazuri wa Utamaduni, wanafanya vitu kwa maslahi yao binafsi. Tungo zao mara nyingi ni za kupotosha jamii, sio kujenga na mashairi yao asilimia kubwa yako uchi sana. Hawako aware na kile wanachokiwakilisha kwa maana hawafanyi research hivyo wanajikuta kwenye migogoro na baadhi ya jamii za watu fulani fulani. Hawa pia mara nyingi wanapita na beat yoyote kutokana na vibe yake ila sio content. 😀

Vitu vinavyowatenganisha hawa ukicross vizuri wakati naelezea hawa jamaa utaunganisha dots na kujua tofauti zao.

Miaka ya karibuni tumeona kila mtu akishika kinasa inapita mda kidogo anakuja na EP, Mixtape au Album hii kwa mtazamo wako unachukulia ki vipi, yani namaanisha underground Hip Hop marketing imekua sana mpaka watu kutaka hivyo vitu kwa kila MC ambaye yupo kwenye game au wingi wa studio umechangia hivi vitu kuonekana ni vya kawaida kwa MC? Au watu wanatoa ili mradi kapata nafasi ya kushika kinasa? Ushauri wako juu ya hili ni upi kwa underground Hip Hop?

Yap ni kweli kabisa nowadays kumekuwa na mlipuko mkubwa sana wa wachanaji na sio kitu kibaya ila UBAYA unakuja pale mtu anashika kinasa huku akiwa hana sub-elements za u-emcee, no content, uwasilishaji mbovu, no Rhythm, no Poetry ili mradi anayo ngabobo ya kulipia studio na pesa ya kukusanya wapambe watakao mpa back up.

Kwa upande mwingine pia haya ni madhara hasi ya teknolojia kama ulivyotangulia kusema sio kwamba market ya Underground imekuwa kubwa sana ni vurugu tu kila mmoja anaitaka hii miliki, kazi kuwa nyingi sio mbaya, je hizo kazi zina viwango vinavyokidhi sikio la mlaji! Mi napenda kazi ziwe nyingi sokoni ila zenye viwango yaani ukisikiliza unasema yes huu ni muziki, ila siku hizi album, mixtape na EP asilimia 90 ni mbovu sana mpaka tunanunua kwa machale 😂

Hapa katika ushauri wangu kila kitu kina wakati wake tusiforce au kusubiri ukomalie kwenye game unachoresha huu mkondo wa Handaki, jipe muda, jijenge kwa maarifa muda ukifika utaonekana tu kila kitu kitakuwa wazi kama vazi la kahaba kuliko kuforce kinasa wakati kichwani ni mtupu.

Kwa sasa tupo katika dunia ya digital yani kupata kazi kwa mashabiki si jambo gumu kama miaka ya nyuma na zaidi kuna platform mbalimbali za kuweka kazi je unazungumziaje hizi platform zina faida kwa sasa kwa msanii au bado tuendelee na mtindo wetu tuliozoea?

Hii ya Digital Platforms ni zao la globalization, means dunia sio KIJIJI tena Dunia imekuwa ghetto, kwa hiyo hii imerahisisha upatikanaji wa bidhaa nyingi kwa urahisi kuliko zamani hususan hii ya muziki. Zamani kupata album ilikuwa mpaka usafiri mkoa kwa mkoa ila nowadays unawasha data unaingia sehemu unakwarua zaga.

Kwa upande wa faida sina uhakika Kwa sababu sijui malipo yao yako vipi ila kwa ushauri wangu kabla ya kupeleka kazi zako katika platforms inabidi kwanza ucheck condition zao, sio unaingia kama nyumbu tu na pia kingine watu wasitake faida kwa haraka kila kitu kina hatua zake. Huwezi kuweka wimbo kwenye platform leo kesho ukakulipa na pia ubunifu katika kazi unahitajika kama watu wanahitaji faida kubwa. Hatuwezi kupingana na mabadiliko ya teknolojia ila tubadilike nayo huku kichwani tukiwa timamu, namaanisha soma terms and conditions kabla haujaweka kazi zako katika platforms fulani. Huu muda sio wa kuuza kazi mkononi peke yake.

Tukizungumzia underground Hip Hop ya Tanzania kwa mtazamo wako je imesogea sehemu nzuri katika jamii yetu tuliyokusudia watufahamu au bado tuna safari ndefu kufikia jamii yetu?

Kwanza kabla sijajibu swali lako naomba nitoe ufafanuzi kuhusu Underground Hip hop ambayo ni zao ambalo limetokana na ambako utamaduni huu ulipoasisiwa, hii ni baada ya nguzo ya Emceeing kupata mafanikio ya kutosha, nguzo nyingine zilitengwa na watu wajanja hivyo walichukuliwa emcees wakali ili kufanikisha biashara za watu hivyo kikazaliwa kitu kinaitwa Mainstream (Mkondo Mkuu) Wakirap kuhusu ngono na mambo ambayo yako kinyume na dhumuni la kuasisiwa kwa huu utamaduni.

Sasa wale waliotengwa wakaja na hii kitu inaitwa Underground (Handaki) wakajumuisha nguzo zile zilizotengwa katika Mkondo Mkuu baadae tena wajanja wenye resources kwa maana ya pesa nao wakateka hizi harakati napo kuna wana wakaona sio kweli nao wakajitenga wakaanzisha Local Underground Hip Hop kwa kuingiza nguzo zote katika uwasilishaji wa Rap.

Sasa nikujibu swali lako kuwa Underground Hip hop Bado iko katika hatua hizi na bado safari yetu ni ndefu sana sababu tuko katika hatua ya kwanza.

Una maoni gani juu ya underground Hip Hop ya Tanzania kuanzia kukua kwake na changamoto zake, nini unapendekeza kifanyike ili kuondoa changamoto zilizopo au kupunguza?

Changamoto za Underground Hip Hop ni zile zile za miaka nenda miaka rudi, utegemezi katika ufanyikaji wa miradi mbali mbali ikiwemo albums, mixtapes na matamasha, kingine ujuaji mwingi na kukatishana tamaa.

Changamoto hizi zitaondoka endapo watu watakua huru kiuchumi, pia kufanya kazi kama team na tuambiane ukweli pale ambapo tunazingua.

Emcee ni kioo cha jamii kwa mtazamo wako je emcees tulionao katika underground Hip Hop wanafaa kuwa kioo cha jamii au bado kuna sehemu tunapwaya?

Mimi sio muumini mzuri wa hili neno “kioo cha jamii”, sisi watu wa open minded tunaamini yule mtu unayemuona kwenye kioo ndio wewe sasa hauwezi kutumia taswira ya mwingine kama mwongozo wako. Ukweli ni kuwa kuna kitu kinaitwa Know Thyself yaani uijuie nafsi yako kwanza mengine ndio yafuate.

Labda hapo kidogo swali lako nilihamishie katika maudhui asilimia kumi ya content zinazowakilishwa katika handaki zinafaa kulisha jamii na asilimia 90 hazifai kuwa Food for Thoughts kwa jamii. Katika majumuisho hapo bado tunapwaya katika contents kama wanaolisha pure ni asilimia kumi tu hizi 90 ndio zinatakiwa ziilishe jamii yaliyo mema sio kufanya trash.

Mpaka sasa kuna kazi ngapi ambazo umeziachia wewe kama wewe (solo project)? Pia tuzungumze kuhusu Waasi Fulani, naomba kufahamu zaidi kundi hili, nani wamo katika kundi hili kina na harakati zao ni zipi katika huu utamaduni wa underground Hip Hop? Pia tutegemee kitu gani kikubwa kutoka kwa Waasi Fulani?

Kutokana na mwingiliano wa majukumu ila kwa sasa nipo karibu na studio tofauti na zamani katika mzingira yangu ila muda sio mrefu nitaingiza bidhaa mtaani.

Waasi Fulani ni Open Minded people katika taswira ya kuogopesha kwa maana ya Uasi ila tukija katika Supreme Mathematics inakaa hivi

Waasi

6+1+1+3+1=12=1+2=3

Fulani

8+6+3+1+5+1=24=2+4=6

Waasi 3 + Fulani 6= 9

9 katika Supreme Mathematics inawakilisha Born means to bring into existence (Mental birth of Self) or to be reborn into the Knowledge of Self.

So Waasi Fulani ni all Free Thinkers ambao wako nje ya mifumo inayotunyonya kama vile dini na siasa.

Sisi katika hii tunnel ya underground ni walimu, wajasiriamali, wahubiri, wajenzi huru wa maarifa kupitia nguzo ya Emceeing .

Watu wasitegemee kitu kikubwa sana kutoka kwa Waasi Fulani ila ukubwa wa kile kidogo tutakacho wakilisha kikaishi kati yao na kujikomboa kimaarifa.

Pia kuna kazi ya Waasi inaitwa Dakika Za Mwisho inapatikana katika tovuti ya Micshariki Africa pale wanaweza kuisikiliza na pia kuna miradi mingine bado iko studio, soon iitakuwa mtaani.

Kwa miaka mitano mbele unaweza kuitazamiwa wapi Waasi Fulani katika underground Hip Hop ya Afrika Mashariki yani kiukuaji na kiuwekezaji?

Sisi kama Waasi Fulani tunazo short and long plans. Katika short plans ni kuhakikisha tunaifikia jamii yote ya Hip Hop kwa maana ya products zetu ambazo ni muziki na logo na makala pia za kuelimisha zinatokana na mashairi tunayoandika.

Long term plans ni kuwafikia/kuifikia jamii yetu kwa ukaribu kwa maana ya matamasha ambayo tutakuwa tunayaandaa kwa kutumia materials na resources zetu wenyewe na pia kingine sisi ni wajasiriamali hivyo malengo yetu ya mbele ni kuwa wajasiriamali wakubwa ili kuiondoa ile dhana ya utegemezi kwa wanaoitwa washika dau. Kwa vision hizo ndizo tunazojitazamia huko mbeleni.

Asante kwa mda wako brother, kwa kumaliza naomba nitajie emcees wako 5 bora wa underground Hip Hop pamoja na producers bora wa underground Hip-Hop. Pia unazungumziaje matabaka yaliyopo katika underground Hip Hop kwa sasa?

Inapokuja kwa underground Hip hop emcees ni;

  1. Adam Shule Kongwe
  2. Flyin Sousa
  3. Magazijuto
  4. Neno wa Kwanza
  5. Mapacha

Producer bora wa underground Hip Hop

Black Ninja

Matabaka yapo na sio mazuri kikubwa tuvunje matabaka tuyaunganishe kama chain ambayo itasukuma gurudumu letu na kulifikisha sehemu sahihi. Mambo ya ukanda, ushikaji, ukabila na ubrother hauna maana yoyote katika Karne ya 21.

Instagram: therealsokwemkongwe
Twitter: @KnowledgeBorn99
Facebook: Jimmy Al Jabbar (Zadafi Allah)

Clubhouse: @SokweMkongwe

Kwa upande wa Waasi Fulani

Instagram: waasifulani
Facebook: Waasi Fulani