Mackapizo

Kuna msemo wanasema wahenga wa sasa pale Mwanza; “Ukitoa yale mawe, Ziwa na Rock City Mall wanabaki na nini?”

Mimi leo kwenye kumi nzito nawapa jibu wanabaki na Hip Hop. Rudia kusema kimoyo moyo hapo ulipo Mwanza itabaki na Hip Hop.

Kumi nzito za Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki kwenye Micshariki Africa na leo tupo jiji la miamba Mwanza.

Ndani ya jiji la miamba tunapokelewa na Mackapizo MC Sayuni. Mgeni wetu wa leo atatujuza mengi tusiyoyajua kuhusu yeye na nini anafanya katika utamaduni wa Hip Hop.

Kama ilivyo kawaida ndugu msomaji wa sasa na wa zamani katika Micshariki Africa nakujuza leo utaweza kumfahamu kiundani Mackapizo na harakati zake katika underground Hip Hop.

Mambo vipi ndugu? Karibu katika kumi nzito na Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki kwenye Micshariki. Mimi nakufahamu kama Mackapizo kisha ikafuata Mackapizo MC Sayuni sababu tunafahamiana kitambo sana. Je kwa mtu asiyekufahamu unaweza kumwambia Mackapizo ni nani? Na anafanya nini katika underground Hip Hop na MC Sayuni lilitoka wapi?

Mackapizzo ni jina lililotokana na kuvunja vunja majina yangu mawili Makarius Mzampola. Mwanzo nilikuwa nahusudu sana gangsta rap. Ila baada ya kuokoka na kurudi kwa muumba kiimani mwaka 2016 jina likaongezeka Mc Sayuni. Kuna story kidogo nifie mabatani 2015 sikufa japo nilibebwa na ambulance. Nikiwa hospitali malaika wakaniijia wakaniambia okoka na hata kama ikitokea ukaendelea na Hip Hop ila iwe Gospel Hip Hop. Fundisha jamii na sisitiza kutenda mema. Ndio maana nina ngoma inaitwa Nitafufuka Siku Ya Tatu inaongelea imani sana.

Mackapizzo anatokea Mwanza na kwa sasa Mc Sayuni anajihusisha pia na kuimba kwaya ya Mt. Gozanga Kimara. Japo katika utamaduni wa Hip Hop yupo pia.

Katika Hip Hop kuna nguzo nyingi kwa nini ulichagua kuwa emcemcee na sio kufuata nguzo nyingine ambazo zipo katika utamaduni? Mwaka gani ulijiona au uliona sasa naweza kuwa mchanaji nikafanya kitu watu wakakipenda na kunisikiliza?

Nilichagua uchanaji sababu nilijikuta nafanya hivyo ilikuwa inborn. Uchanaji nilianza rasimi 2004. Japo mwanzo brother ambaye namfuata mara 3 alikuwa anachana pia akawa ananifundisha uchanaji. Bidii zangu pia kununua tape za instrumentals za mbele na kuzichania. Nikiwa shule ya msingi mpaka sekondari hakuna ambaye alikuwa hanijui shule na pia mtaani nilikuwa na washikaji zangu walikuwa watu wazima na wanachana kitendo ambacho mzee wangu alikuwa anaamini sipendi shule.

Wimbo wa kwanza ulifanya lini kwenye studio gani na unaitwaje ? Pia ulijisikiaje ulipofanikiwa kuachia huo wimbo? Toka umeanza mpaka sasa una kazi ngapi, namaanisha Ep, Mixtape, Album unazo ngapi?

Wimbo wa kwanza nilifanya 2007 kwa producer Master P, Mwanza, huo wimbo ulifanikiwa kupigwa Passion Fm pale na baadae 2009 nilikuwa nafanya freestyle sana kiasi cha kualikwa na Ezden De Rocker Kiss Fm kwenye Kiss Collabo Mix Show.

Ngoma nime record zaidi ya 20 hadi nyingine sina. Sina EP, Album, Mixtape nadhani hicho ndo kilio/failure yangu kwenye huu utamaduni 😄😄

Wimbo wangu pendwa toka kwako ni Shika Kipaza Kwa Adabu wazo la wimbo huu lilikuwa ni nini? Pia inasemekana kuna mtu mmoja aliomba kufuta ubeti wake kutokana na mtindo wa kiitikio mliochagua je kuna ukweli juu ya hili jambo?

Lengo la huo wimbo lilikuwa ni kuhamasisha wachenguaji kuwa katika misingi na kuchana vitu sensitive. Japo pia ulikuwa wa kuelezea maisha halisi tu ya mtaani. Mwanzo nilitamani iwe movement kabisa na Kama kuna mtu hashiki kinasa kwa adabu apigwe. Wimbo ulirecordiwa na Abby MP mitaa ya Kariakoo studio Chata Noga.

Kipindi hicho nilikuwa nafurahi kuchukua ma Mcee tu twende nao studio wa burst. Wazo lilianza na wimbo wa Ulimwengu Shujaa Remix beat la Tongwe ila tuli record niliweka ma emcee kama 8 wimbo uligeuka cypher. Ila baadae nikawaza Raf, Bassat, Maarifa maana wanangu hawa. Na Meddy Samurai ambaye kwangu ndio alikuwa emcee Bora kuliko wote ali record ila aliomba verse ifutwe. Alitaka wimbo uitwe Mwendokasi nikakataa. Pili verse ilikuwa laini. Baada ya kusikia verse zetu mmmh zilikuwa mauaji sema hayo yalishaisha. Kwangu Meddy Samurai atabaki kuwa emcee bora nchini asilimia 90 Meddy anachana maisha halisi.

Kipindi upo chuo ulikuwa na mizuka sana ya kutoa nyimbo yani namaanisha kabla ya kutoka MackApizo Mc kuja MackApizo Mc sayuni. Huyu Mc Sayuni mda mwingi amekuwa mtu wa kuandika na kushauri sana kuhusu mambo mbalimbali. Swali langu, je gospel Hip Hop bado ni uhuni kwenye jamii ya imani zetu au wewe ndio umekuwa muoga kutoka na watu wa imani yako waliokuzunguka?

Jamii ya watu wa dini inaamini kurap tu uhuni tosha. Ila Kuna namna navyofanya sasa ninaamini watapenda.

Miaka ya karibuni tumeona kila mtu akishika kipaza itachukua mda kidogo anakuja na Ep, Mixtape Au Album hii kwa mtazamo wako unaichukuliaje yani namaanisha underground Hip Hop marketing imekua sana mpaka watu kutaka hivyo vitu kwa kila Mc? Au watu wanatoa ili mradi kapata nafasi ya kushika kinasa. Ushauri wako juu ya hili ni upi kwa underground Hip Hop?

Kwa mtazamo wangu EP, Mixtape na Album ni heshima kwa emcee. Kwangu navyoona Hip Hop marketing haijakua hata kidogo. Hata hela zinazolipwa huko online mfano mdundo.com bado sio hela ya kumsaidia emcee kuishi vizuri. Wengi wanatoa sasa EP na album kushika kinasa tu ile burudani. Cha ajabu hizo album nyimbo nyingi hazina madini kuna ambazo hazina vina kabisa, kuna ambao album nzima mtu hajui kuchana.

Nashauri kwanza, emcee kabla hujatoa Ep, Album, Mixtape uwe kuna kitu una focus kwenye huo ujumbe unaotuuzia, pia emcee weka mipango ya kuuza nyimbo mifumo yote hard and soft copy. Mwisho tujue mziki wetu huu bado haujawa industry ndio maana mapato yanategemea shows na kuuza online nje ya hapo emcee anakufa hivyo tujihusishe na ujasiriamali tupate kitu kidogo.

Kwa sasa tupo katika dunia ya digital yani kupata kazi kwa washabiki si jambo gumu kama miaka ya nyuma na zaidi kuna platform mbalimbali za kuweka kazi je unazungumziaje hizi platform zina faida kwa sasa kwa msanii au bado tuendelee na mtindo wetu tuliozoea?

Kuuza kwa digital sasa kweli kumerahisisha sana japo bado kwa kweli EP, Album, Mixtape ambazo ma ma emcee wametoa wakauza kupitia hizi platform. Hata wao unagundua bado hazijawalipa kihivyo kiasi cha kulipa kodi na kuweka misosi mezani.

Hela inayopatikana huko mara nyingi hata hairudishi gharama za utayarishaji studio na nk. Kwa kifupi digital ni nzuri Ila tungeangalia namna nzuri ya kufikisha taarifa kwa wadau wa mziki ndipo tuanze kuuza huo mziki wetu.

Una maoni gani juu ya underground Hip Hop ya Tanzania kuanzia kukua kwake na changamoto zake, nini unapendekeza kifanyike ili kuondoa changamoto zilizopo au kupunguza?

Underground Hip Hop inazidi kukua maana matamasha ya wazi yameongezeka. Changamoto ninayo iona: hii underground kuna watu wanataka kujimilikisha, hawataki mawazo mapya, pia namna ya ku generate income bado ni tatizo kwenye soko la underground Hip Hop yetu.

Una mipango au mpango gani juu ya wazee kuweza kutoa nafasi kwa Mc kutumbuiza Hip Hop Gospel kwenye makanisa?

Taratibu tunaendelea kuwaelewesha naamini wataelewa.

Katika utamaduni wa Hip Hop kuna nguzo zake ambazo zinajulikana, lakini wengi wa watu wamejikita katika nguzo moja ya emcee ambayo inaonekana ni nyepesi kwa wengi wao je nikisema na wewe umechagua kuwa emcee sababu ni nguzo pekee ambayo kila mtu anatamani kuwa emcee? Pia kama hutojali unaweza kutuelezea emcee ni nani katika Hip Hop?

Nilichagua kuwa emcee sababu kuna ujumbe nilikuwa nataka kuupeleka kwa jamii na njia hii nilipokuwa katika ukuaji nilikuwa napenda watu wanavyoghani. Sijui kuchora graffiti, Dj najua kuchana. Kwangu mimi emcee wa Hip Hop, ni mtu mwenye stadi za kughani ambaye kwa ustadi mkubwa huwa amepanga mashairi yake yenye maudhui flani kwa jamii anayokusudia.

Emcee ni kioo cha jamii kwa mtazamo wako je ma emcee tulionao katika underground Hip Hop wanafaa kuwa kioo cha jamii au bado kuna sehemu tunapwaya?

Bado tunapwaya sana, bado watu wanahamasisha asilimia 90 pombe, ngono na weed. Ilipaswa tuzitumie asilimia 70 kuielekeza jamii.

Asante kwa mda wako brother, kwa kumaliza naomba nitajie ma emcee wako 5 bora wa underground Hip Hop na pia producer wako bora wa underground Hip Hop. Pia unazungumziaje matabaka yaliyopo katika underground Hip-hop kwa sasa?

Emcees wangu bora,

  1. Hashim Dogo
  2. One The Incredible
  3. Rado Kiraka
  4. Salu T
  5. Adam Shule Kongwe

Producer Bora: ABBY MP

Kuhusu matabaka: sio poa, sipendi baadhi ya watu kujiona wanaimiliki Hip Hop na wanajua sana, kwa kweli hapo hatutakubaliana. Mwisho nawakubali sana wanaowaelekeza ukweli 😄😄😄😄👏🏼👏🏼

Facebook: Mackapizzo Mc Sayuni