Micshariki Africa na mzee wa Kumi Nzito, Beberu La Mbegu leo tupo jiji la Dar es Salaam. Kama kawaida ya Kumi Nzito na Micshariki Africa ni kukupa habari mbalimbali za wadau wa utamaduni wa Hip Hop hasa handaki au underground Hip Hop.
Nia kuu ni kusaidia mashabiki na wafuasi wa utamaduni wa Hip Hop kuweza kuwafahamu kiundani juu ya kazi mbalimbali wanazozifanya kwenye huu utamaduni wa Hip Hop.
Wiki hii tupo na mwandishi/mtunzi na mchambuzi wa muziki Muddyb Mwanaharakati toka ndani ya jiji la Dar es Salaam mitaa ya Chanika.
Muddyb Mwanaharakati ni mtunzi, mwandishi, mhariri pia ni mchambuzi wa makala mbalimbali za muziki na filamu. Pia makala zake za muziki na mambo mbalimbali zinapatikana Wikipedia.
Moja ya sababu kubwa ya Kumi Nzito kumtafuta Muddyb Mwanaharakati ni kutaka kufahamu harakati zake kuhusu muziki na mtazamo wake kuhusu muziki wa underground Hip Hop ulivyo kwa miaka ya sasa.
Karibu uweze kumfahamu japo kidogo mdau huyu wa underground Hip Hop upate katika yale kumi usiyoyafahamu toka kwake na mitazamo yake kuhusu game.
Mambo vipi ndugu? Karibu katika Kumi Nzito na Beberu La Mbegu. Naomba kwanza kufahamu majina yako na historia yako kwa kifupi. Muddyb Mwanaharakati ni nani na anafanya nini?
Muddyb Mwanaharakati ni mwandishi wa riwaya na hadithi za watoto. Muda mwingine huandika makala za Hip Hop na muziki mzuri wowote ule. Lakini zaidi ni Hip Hop. Ni baba, mume, na rafiki wa watu wengi. Pia ni mfanyakazi katika kampuni ya maji ya Uhai Bakhresa.
Kitu gani kilikusukuma au kukuvutia (kukushawishi) kuingia kwenye huu utamaduni wa Hip Hop na sio kufuata tamaduni za muziki tofauti na Hip Hop?
Msukumo kutoka kwa watu walionizunguka. Hasa makaka wa kitaa ambapo miaka ya ‘90 tulikuwa tukiishi pamoja. Mabraza hao tuliishi maisha fulani amazing sana. Hapo kijiweni palikuwa na radio ya Panasonic Double Deck halafu muziki unahamishwa kwenda katika speaker moja kali sana, ilikuwa ikiitwa KENWOOD, kiwete imepinda mgongo.
Tulisikiliza zaidi muziki wa Hip Hop kutoka USA. Zaidi Naughty by Nature, Kriss Kross, Dr. Dre, Da Luniz, Tupac, Snoop na wale wote waliochana tambara la ‘90. Kutokana na kijiwe hiki, sikuweza tena kuhamia upande mwingine hadi nakuwa mtu mzima.
Maana miaka ya 90 kuwa emcee ni kitu kikubwa kwa vijana wengi na sio kuwa mwandishi wa makala kama ulivyo wewe. Kitu gani kilikusukuma kuwa mwandishi wa makala za Hip Hop na sio kua mchanaji (mchenguaji) au producer wa Hip Hop?
Mimi nilipenda kuwa mpashaji ama DJ tangu miaka ya awali ya upendaji wa hip hop. Mwaka wa 2002 nilikuwa na radio yangu iliyokuwa ikisikika Kiwalani yote iliitwa Mafuvu FM. Kutoka jina la zamani Scientific FM. Upendo huu nimeendelea nao hadi sasa. Sikuona nafasi yangu katika kuchana licha ya kuwa na uwezo wa kuandika mashairi butu na kadhalika.
Katika watu wenye ufahamu mkubwa wa muziki wewe ni mmoja wapo. Nini kilikukwamisha mpaka ukafunga redio yako na kuamua kuingia katika uandishi wa makala za muziki na uandishi wa riwaya ikiwa unajua watanzania wengi ni wavivu wa kusoma na wepesi wa kusikia?
HOFU! Ilikuwa hofu ya kibali cha radio wakati huo. Pia ilikuwa radio ya mtaani tu si kama redio rasmi. Muda! Ni kama sasa tu siko kamili mazima kutokana na kazi kuwa nyingi.
Naona kwa sasa unaandika sana vitabu vya riwaya je kuna siku umewaza kuja kuandika vitabu kuhusu historia ya Hip Hop Tanzania?
Ni kweli kabisa. Ninao huo mpango wa kuandika historia ya Hip Hop Tanzania. Nina madini mengi nimeyahifadhi. Ninatarajia siku moja niyakusanye sehemu moja na kuunda kitabu.
Nimekuwa kwenye mawasiliano na wana mabreka wa miaka ya 80 na 90 mwanzoni. Pia nimepata kuongea na majagina wengi na makuhani wa muziki wetu.
Juzi kati nilipata wazo la kuandika hizo mada katika mtindo wa kipekee sana. Nitatumia jina la "SOGA ZA HIP HOP YA TANZANIA."
Ili niweze kuweka mawazo yao kama yalivyo bila kutia mbwembwe. Ninayo katika posti yangu ya 2017
Kwa ufahamu wako unaweza kunitofautishia underground emcee na mainstream emcee? Underground emcee ni yupi? na mainstream emcee ni yupi?
Zamani tulitafsiri wale waliobahatika kusikika mara kwa mara kwenye vyombo vya habari tuliwaita watu maarufu. Wale waliosikika mara chache tuliwaita underground.
Siku hizi jambo limechukua kona tofauti.
Emcee kama Nash anayepata hata mialiko Ulaya na Amerika, hujihesabia kama underground emcee kisa tu hataki kupiga magoti kwa wenye redio zao.
Kumekuwa na visa na mikasa mingi iliyopelekea kuanzishwa kwa harakati za handaki.
Kuhitimisha kuhusu utofauti wao kwa muktadha wa kileo, mainstream ni wale wanaokubali kufanya vyovyote na wenye redio ama TV zao halafu underground ni wale wasiotaka kupangiwa nini cha kufanya.
Naomba kama utapenda ututajie makala zako 5 bora za muziki ulizoandika, emcees wako wa 5 bora toka afrika mashariki, bila kusahau producers wako wa 5 bora toka Afrika Mashariki.
Emcees
- Ngwair
- Nash MC
- Jay Moe
- Professor Jay
- One The Incredible
Producers
- Miikka Mwamba
- P Funk
- Bonny Luv
- Marco Chali
- Q
Makala
Kwa sasa tupo katika dunia ya digital yaani kufikisha kazi kwa mashabiki si jambo gumu kama miaka ya nyuma na zaidi kuna platform mbalimbali za kuweka kazi. Je unazungumziaje hizi platform, zina faida kwa sasa kwa msanii au bado tuendelee na mtindo wetu tuliozoea?
Platform zina faida sana. Ule muundo wa zamani ulikuwa unatengeneza miungu watu wengi sana. Ulikuwa mfumo wa kinyonyaji unaotia simanzi na misongo ya mawazo. Sasa ni nguvu yako kuposti na kurejea mara kwa mara kuposti kile ulichokitoa.
Pamoja na hayo, bado wengi hawafahamu sanaa ya Online. Sanaa hii inataka uwajibikaji wa hali ya juu. Kila wakati, kila nukta, kila sekunde kuposti na kutangaza tena katika platform zingine. Kutumia mifumo ya platform husika kujitangaza. Mfano katika YouTube, kuna YouTube ads ambayo yenyewe unalipia kiasi fulani kisha matangazo yanajiroll katika video nyingine. Hii husaidia sana kukuza channel na mengine. Kama nilivyosema, usiache platform yako ijitangaze. Tumia Instagram, Facebook, Tik Tok na nyinginezo kutangaza kazi zako mara kwa mara.
Inapokuja kwenye maswala ya kama kuna faida au la sina maneno mengi. Hizo ni mambo ni sehemu ya muziki. Wacha uendelee!
Asante sana brother kwa mda wako, kwa kumalizia unaweza kutoa ushauri gani katika underground Hip-Hop ya Tanzania na muziki wa kizazi kipya kiujumla yani nini kifanyike ili kuongeza thamani kwa wasanii wetu na muziki wetu?
Ili tufike tunapotaka, tunahitaji juhudi na nia ya kutimiza malengo yetu. Tuache kufikiria sana katika mawanda ya kindani bali pia tuwaze nje ya hapa. Si lazima kubadili lugha. Leo hii muziki wa India unapaa duniani kote lakini wanaimba kikwao. Tujichanganye, tuchangamkie fursa. Hata kama itakuwa na faida kiasi lakini muhimu kutoka nje ili tupate kufahamika kimataifa. Hii itasaidia muziki na lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Bidii, kusimamia tunachokifanya kwa asilimia 100, kujaribu nje ili kujitangaza.
Unaweza kuwasiliana na MuddyB Mwanaharakati kupitia mitandao ya kijamii;
Facebook: Muddyb Mwanaharakati
Instagram: muddyb_mwanaharakati