PapaFau60

Micshariki Africa na mzee wa Kumi Nzito, Beberu La Mbegu leo tupo jiji la Dar es Salaam. Kama kawaida ya kumi nzito na Micshariki Africa ni kukupa habari mbalimbali za wadau wa utamaduni wa Hip Hop hasa handaki au underground Hip Hop.

Nia kuu ni kusaidia mashabiki na wafuasi wa utamaduni wa Hip Hop kuweza kuwafahamu kiundani wadau wa utamaduni huu juu ya kazi mbalimbali wanazozifanya kwenye huu utamaduni wa Hip Hop.

Wiki hii tupo na emcee Papa Fau60 toka ndani ya jiji la Dar Es Salaam. Miongoni mwa mambo yanayotazamiwa kuwa ni ya ajabu kwa vijana wengi ni pale ambapo vijana wanapomuona kijana mwenzao akidili kwa sana na mambo ya kumtumikia Mungu.

Vijana wengi wanaamini wanaopaswa kumtumikia Mungu ni mzee au mtu mwenye matatizo flani. Kwa mtu mzima Papa Fau60 ni tofauti kabisa na vijana wengine wengi. Yeye kachagua kumtumikia Mungu kwa njia ya kuimba (kuchana).

Papa Fau60 ni miongoni mwa ma emcee wachache sana hapa nyumbani Tanzania ambao wanafanya Gospel Hip Hop. Kwa umri wake na anachokifanya lazima ubaki na maswali ya kutaka kujua au kufahamu kwa nini anafanya Gospel Hip Hop na sio kingine.

Kumi nzito za Beberu La Mbegu inamleta kwako Papa Fau60 ili umsome na kumfahamu japo kwa kifupi kuhusu kazi zake na harakati zake mpaka kuamua kuzama katika Hip Hop Gospel.

Soma kumi nzito ndani ya Micshariki Africa uweze kumsoma Papa Fau60.

Mambo vipi ndugu? Karibu katika Kumi Nzito na Beberu La Mbegu ambazo zinapatikana kila wiki hapa Micshariki Africa. Mimi nakufahamu kama Papa Fau60 je kwa mtu asiyekufahamu unaweza kumwambia Papa Fau60 ni nani? Na anafanya nini katika underground Hip Hop? Hii 60 katika Papa Fau60 inasimama kuwakilisha kitu gani?

Papa Fau60 ni underground emcee ambaye amejikita kwenye utamaduni wa Hip Hop kwenye maudhui ya Injili known as Gospel Hip Hop. Kama ilivyo nguzo kuu ya Hip Hop kusambaza elimu kwa jamii, Papa Fau60 aliamua kuhudumu kwenye upande huu akitumia nyenzo na kanuni za utamaduni wa Hip Hop kwenye kuwasilisha habari za neno la Mungu kwa jamii.

60 ina simama kama umri wa miaka. Kipindi nimeplan kuingia kwenye game ya gospel rap mama yangu alikua katimiza miaka 60 ya kuzaliwa kwake.

Labda nikurejeshe nyuma kidogo ili upate concept. Hapo awali nilikuwa nikifanya secular music, mama yangu alikuwa akinipinga na hakuvutiwa kabisa na chaguo hili katika maisha yangu. Alikuwa akinishawishi sana nirudi kwenye upande wa muziki wa Injili ambapo ilikuwa ni njia yake toka akiwa binti mdogo paka leo hii.

Mama yangu alikua akiimba kwaya na alitamani sana nijiunge na kwaya ya vijana ila mimi upande huo haukuwahi kunivutia toka nilipokuwa mdogo nilishavutiwa na wachanaji na wachenguaji hodari kama kina Mr Cheeks na wengine.

Mvutano huo uliendelea kiasi mzee wangu hakuwa tayari kunipa baraka juu ya nilichokifanya kitu ambacho kilinivunja moyo nikaamua kuachana na muziki kabisa mpaka mwaka 2020 janga la Corona lilipoitikisa dunia ndipo nilipopata wazo la kurudi kwenye muziki.

Nikiwa na mtazamo wa kufanya Gospel rap, nilipozungumza naye (mama yangu) na kumweleza uamuzi huo hakuwa na pingamizi na alinipa baraka zote na kuniambia kama nimeamua kuifanya kwa ajili ya Mungu niifanye na kubarikiwa na hapo ilikua ni kipindi ambacho alikuwa anakaribia kuadhimisha kumbukizi ya miaka 60.

So nikabeba 60 kama kumbukumbu ya upatanisho wa idea yangu ya kuifanya rap kwenye maudhui ya gospel na kumbukizi ya miaka 60 ya umri wake mama na hii ni kama zawadi yangu kwake.

Nini kilikusukuma mpaka ukachagua kuwa wewe utafanya Gospel Hip Hop na sio mziki mwingine ikiwa sehemu kubwa ya vijana wengi wapo mbali sana na mambo ya dini?

Mazingira niliyokulia toka nikiwa mdogo yamekuwa na mchango mkubwa sana wa mimi kusimama hapa nilipo, kuanzia malezi ya wazazi na jamii iliyokuwa ikinizunguka. Nilikulia mazingira ya missionaries muda mwingi nilikuwa nikiona watu wakijihusisha na maswala ya ibada muda mwingi pia wakihubiri habar za kuchochea matendo mema, taratibu na mimi niliendelea kuishi kwenye njia hiyo japo kwenye ukuaji tunakutana na mambo mengi ila kuna kitu kilibaki ndani yangu ambacho kimekuwa chachu ya mimi kua hapa leo hii.

Real Talk ni Ep yako ya ngapi toka uanze kufanya mziki? Je mapokeo kwenye nyumba za ibada yapoje juu ya mtindo wako wa kuabudu yani viongozi wa dini na wazee wanakuchukuliaje?

Real talk ni mradi wangu wa kwanza kabisa toka niamue rasmi kuzama kwenye tasnia hii. Ni mradi uliotoka mwishoni mwa mwaka jana, December13, 2021 ukijumuisha track 5. Mapokezi kwa jumuiya ya watu wanaonizunguka naweza sema yamekua mazuri sana. Comment nyingi zimekuwa zikitanabaisha kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakitumia jumbe zilizomo kwenye mradi huu kuwaasa vijana wao kiurahisi kutokana na aina ya uwasilishaji wa maudhui uliotumika ni uwasilishaji ambao unaweza kuwafikia vijana kwa urahisi tofauti na Gospel songs za kawaida.

Kiujumla mapokezi ni mazuri, kuanzia family mpaka streets, watu wengi wamekua inspired na kitu ninachokifanya kwa sababu mara nyingi muziki wa Hip Hop umekuwa ukitafsiriwa kuwa ni mziki wa wahuni/fujofujo matusi nk… kwa ujio wa Ep ya Real Talk kumeleta mtazamo mpya kwa wanajamii hasa ambao wameisikiliza na wadau wengine ambao wamekuwa wakifuatilia muziki kwa ukaribu wengi ambao wamepata nafasi ya kuisikia wamekuwa wakinipongeza na kunitia moyo niendeleze harakati hizi kwenye upande huu niliouchagua.

Baada ya hii EP tutegemee kitu gani kipya kutoka kwako?

Baada ya Real Talk kuna single track zitafuata lakini kubwa kabisa ni maandalizi ya ujio wa mixtape yangu ya kwanza kabla ya kusogea kwenye album kwa sababu hiki ninachokifanya ni kitu kigeni kwa upande mmoja kwa hapa nyumbani tofauti na nchi ya America so wadau wa muziki wa Hip Hop wawe tayari kupokea maudhui ya gospel Hip-hop.

Gospel Hip Hop kwa Tanzania unaona watu wanaipokea vipi au bado kuna changamoto kwa watu kuelewa kile unachokikusudia?

Kwa hapa Tanzania kuna changamoto kidogo kama ilivyo kwenye mambo kadha wa kadha hata kwenye hili pia kuna changamoto zake japo kwa kiasi kikubwa baadhi ya watu wanapopatiwa elimu au ufahamu juu ya hii wamekua wakielewa... Ila wengi wao mwanzo huwa wanahisi kama tunafanya dhihaka kwenye maswala ya dini kutokana na aina ya mirindimo inayotumika na style nzima ya uwasilishaji.

Ni emcee gani alikuvutia au kukushawishi kufanya unachokifanya sasa?

Emcee aliyenivutia sana kufanya hiki ninacho kifanya ni Derek Minor kutoka Middle Tennessee...wapo ma emcees wengi ila huyu ndiye emcee aliyenivutia zaidi.

Una maoni gani juu ya handaki ya Tanzania kuanzia mafanikio na changamoto zake, nini unapendekeza kifanyike kuondoa changamoto zilizopo?

Handaki ya hapa Tanzania, inafanya vizuri sana lakini kitu kinacho turudisha nyuma always ni umimi. Kama tutaondoa umimi na kukazia mshikamano tunaweza kusimama na kufikia malengo tunayoyapanga. Pia ni lazima watu kukubali kujifunza kwanza kwa sababu Hip Hop basic ina stand kwenye knowledge, kama tutakimbilia kufanya msingi pasipo kuwa fit kichwani bado itakuwa ngumu kuikomboa mitaa na hata kujikwamua wenyewe kiuchumi na kuondokana na umaskini. Hivyo ni muhimu sana kuwepo au kuanzishwa clinic za Hip hop walau hata mara moja kwa mwaka kuwapatia emcees basics za Hip Hop, nadhani itachangia sana kutengeneza watu makini wa kutoka handakini.

Kwa kuelewa wako underground Hip Hop emcee ni yupi? Mainstream emcee ni yupi? Ni kitu gani kina watenganisha ili kujua huyu ni underground emcees na huyu ni mainstream emcee?

Underground Hip Hop emcee ni self-made artist ambaye hutumia skills zake personal kujikwamua kwa kutumia utamaduni wa Hip Hop kwa mfano mtu kama Nash Emcee, Mantik Barz or  XP Experience. Hawa wote hawategemei media ili kujipatia vipato vyao. Wanatumia knowledge na skills zao personal kujitengenezea kipato chao binafsi kwa mfano kuandaa miradi mbalimbali, uuzaji wa machata yao pamoja na santuri zao.

Ukija kwa mainstream emcee huyu ni emcee ambaye hupata kipato kupitia connection za media stations kwa mfano matamasha mbalimbali yanayoandaliwa na radio/tv stations mbali mbali  mfano Fid q, Joh Makini na wengineo. Vipaumbele vya moja kwa moja kwenye vyombo vya habari ndicho kinachowatenganisha mainstream emcees na underground emcees.

Mtu akitaka kazi zako anaweza kupata kwa njia zipi au platform zipi? Kama ni tofauti au nje ya platform zilizopo anazipata vipi?

Ep ya Real Talk inapatikana kwenye digital platform zote. Kuanzia Boomplay, Audiomack, YouTube, Amazon n.k. Kwa kufuata kiunga kilichopo kwenye ukurasa wangu wa Instagram: @papafau60worldwide. Pia kwa mtu anayehitaji kuipata direct kutoka kwangu anaweza kunicheki kupitia  email yangu Faustinefrancis45@gmail.com

Au kugusa link

Audiomack: papafau60worldwide
YouTube: papafau60worldwide

Asante kwa mda wako brother, kwa kumalizia unaweza nitajia emcees wako wa 5 bora. Pia unazungumziaje matabaka yaliyopo katika underground Hip Hop je yana tija kwenye utamaduni au tuyapotezee yanadumaza utamaduni?

Emcees wangu wa 5 wa muda wote ni

  1. Hasheem dogo
  2. Salu T
  3. Adili chapakazi
  4. Nash Emcee
  5. Jay Moe

Issue za matabaka kwa nyakati hizi hazina tija, tunahitaji kufanya mambo kwa mshikamano ili tuzidi kukua na kudumisha nguzo ya upendo umoja na amani.