Ni siku nyingine tena ya kupata maswali kumi mazito toka kwa ndugu Beberu La Mbegu. Kama kawaida kumi nzito inadili na watu wa utamaduni wa Hip-Hop, ma Emcee, Producers, Dj's na wadau mbalimbali katika utamaduni.
Yote katika kusaidia kufikisha japo kwa kidogo kwa wasomaji na wadau wa Hip Hop waweze kuwajua au kuwafahamu kiundani emcees, producer na Dj's wao ambao wanawapenda.
Kwa juma la leo kumi nzito tupo na emcee kutoka mkoa wa Geita kwenye mji wa Ushirombo ukipenda sema "mji wa madini" ambapo tunakutana na ndugu yetu Emmanuel Peter Sahani jina la taifa ilo jina la kazi muite Plate Mdaijasho.
Plate Mdaijasho ataweza kutujibu kwa usahihi mzuri maswali yetu kumi kuhusu kazi zake na movement zake mbalimbali anazopiga hapo Ushirombo. Unataka kumfahamu Mdaijasho ni nani shuka chini apo tuanze pamoja.
- Beberu La Mbegu
kufahamu majina yako na historia yako kwa kifupi. Plate Mdaijasho ni nani na anafanya nini?
Jina langu kamili ni Emmanuel Peter Sahani. Nilizaliwa mkoani Kigoma na kusomea shule ya msingi mkoani humo. Asili yangu ni Msukuma wa Bariadi Ntuzu na kwa sasa naishi Ushirombo, Bukombe Mkoani Geita.
Plate MdaiJasho ni msanii wa muziki wa Hip Hop aliyeamua kuelimisha jamii yake na kuhamasisha ijitambue kifikra kwa kujua haki(Jasho) zao na njia ya kudai haki hizo.
Swali 2; AHM (Agro Hip-Hop Movement) kwa kifupi ni harakati zinazohusu kitu gani katika utamaduni je ni break dance, Dj's, emcees, graffiti? Pia kuna muingiliano gani kati ya AHM na Chimbo Letu Kahama ya pale Kahama?
AHM ni vuguvugu la uhamasishaji wa kutumia kilimo kwa manufaa katika sanaa. Lengo kuu ni kusaidia shughuli za utamaduni wa Hip Hop kiuchumi ili emcee, break dancer, DJ na mpiga machata wawe huru katika maamuzi.
AHM ina ukaribu sana na Chimbo Letu Kahama. Mimi ni muasisi wa vuguvugu hilo na ni mshiriki pia wa CLK. AHM ni moja ya wadhamini wa matukio yanayoandaliwa na CLK.
Swali 3; Mpaka sasa unazo Ep tatu zipo katika mfumo wa tamthilia yani toleo la kwanza mpaka la tatu nini kilifanya Ep yako itoke kwa mpangilio huo?
Kikubwa kabisa ni maudhui yanayopatikana katika Ep hizo. Unajua kujenga taifa ni tamthilia isiyo na mwisho, hivyo hata Ep hizi zitaendelea kutoka kwa mtindo huo na zitakuwa zinapatikana bure kabisa ambapo mtu akitaka kusikiliza anaweza kutembelea kwenye account yangu ya YouTube kwa kugusa kiunganishi humo atapata nyimbo zangu zote.






Swali 4; Baada ya hizi EP zako za TuTaLeTa (Tulijenge Taifa Letu Tanzania) tutegemee album itatoka lini? Je mapokezi kwa wadau na mashabiki wako unayaonaje mashabiki wameongezeka au wamepungua?
Jibu; Kwa kweli tangu nitoe Ep za Tujenge Taifa Letu Tanzania (TuTaLeTa) mashabiki na watu wanaosikiliza muziki wangu wameongezeka sana. Lengo la kutoa Ep hizi ni kuonesha uwezo na kuwaweka tayari watu na ujio wa album yangu ambayo bado naiandaa. Siwezi nikasema itatoka lini ila Ep za TuTaLeTa zitaendelea kutoka. Mwisho wa mwaka huu itatoka TuTaLeTa Ep Vol.4. Mungu akipenda nasisitiza kama bado hujasikiliza Ep zangu fuata hii YouTube link uweze kusikiliza.
Swali 5; DKC (Door Knockers Cyphers) nimekuona katika toleo la tatu ukiwa na wachenguaji mbalimbali toka Afrika Mashariki. Je ni kitu gani unaamini kiliweza kuwashawishi waandaji wakakupa nafasi na wewe kuonesha uwezo wako? Je Door Knockers Cypher kuna sehemu imekupa mafanikio au bado unajiona upo vile vile?
Sijui ni kitu gani kiliwashawishi waandaaji ila naamini ni kudra za Mungu tu zilifanya waandaaji wakanipa nafasi hiyo. DKC imeniongezea fan base kubwa sana nje ya Tanzania.
Swali 6; Kwa ufahamu wako unaweza kunitofautishia underground emcee na mainstream. Underground emcee ni yupi? na mainstream emcee ni yupi?
Underground emcee ni emcee ambaye yuko huru katika ufanyaji wake wa kazi. Hana lebo na hata kama akipata label, hiyo label lazima iwe huru na impe uhuru emcee wa kufanya kile ambacho ni sahihi. Ujumbe wake katika kughani huwa umeegemea zaidi kufungua fikra za watu na kuwapatia maudhui yalicho chanya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Mara nyingi maudhui haya yamekuwa sio rafiki kwa baadhi ya wafanya biashara wa muziki wanaomiliki label kubwa za biashara ya muziki, wanawamiliki wasanii wanaowapa ujumbe na mahadhi watakayo wao ili biashara zao ziende. Wasanii hao wamilikiwa na label hizo kubwa zisizo huru wanaitwa mainstream emcees.

Plate Mdaijasho
Swali 7; Mikoa ya kanda ya ziwa miaka ya nyuma ilifanya vizuri sana kwenye muziki wa kizazi kipya mpaka Hip Hop tofauti na sasa. Je nini kinakwamisha kwa emcees na wasanii wa sasa kutofika walipofika wale waliowatangulia?
Kanda ya ziwa inafanya vizuri na itaendelea kufanya vizuri tu katika tasnia ya muziki. Sababu huku kuna vipaji sana japo changamoto zilizopo Mwanza ndio changamoto zilizopo mikoa mingine pia. Ila kwa sasa hivi kanda ya ziwa ina studio nyingi zaidi kuliko kipindi cha awali, ina vyombo vya habari vingi kuliko awali na kuna wasanii wengi underground na mainstream kama ilivyo mikoa mingine.
Swali 8; Ukiwa kama mpigania haki na msemaji wa watu wa maisha ya chini kama unavyotuambia kwenye nyimbo zako je kwa mtazamo unawaona wapi watanzania wa maisha ya chini kwa miaka ya mbeleni kuanzia elimu, afya mpaka chakula?
Kama mfumo utaendelea kuwa hivi, naona idadi ya watu wa kima cha chini wakiongezeka na gap la mwenye nacho na asiyenacho litazidi kukuwa. Hivyo naona kabisa mahitaji muhimu yatazidi kuwa magumu kwao maana mfumo wa ubepari haujawahi kuwa rafiki na maskini.
Swali 9; Kwa mtazamo wako hapo mtaani kwako je unaamini Hip Hop imeikomboa jamii yako au jamii yako ndio imeikomboa Hip Hop ili isipotee?
Hip Hop inakomboa mtaa wangu. Vijana wengi wanapata elimu ya mtaani ambayo haifundishwi darasani kupitia Hip Hop. Wanaamka kifikra kupitia Hip Hop. Wana msemo wao hapa mtaani kwangu Tujenge Taifa Letu Tanzania (TuTaLeTa). Na kweli kupitia harakati za Agro Hip Hop Movement wamefanikiwa kujikimu kiuchumi na wana matumaini ya kutoka katika ujasiriamali na kuelekea kwenye uzalishaji.
Swali 10; Nisaidie kunitajia hii kitu kwa upande wako. Emcees wako wa 5 bora toka Afrika Mashariki bila kusahau producers wako wa 5 bora toka Afrika Mashariki. Pia tumalize kwa hii nini kifanyike kuondoa mgawanyo uliopo katika utamaduni wa Hip hop?
Emcees
- Salu Tee
- Bad Ngundo
- Experience
- Pizzo Madawa
- Kitu Sewer
Producers
- Stim Master
- Kunta (Official Beats)
- Evano Ke
- Mwamba Mgumu
- Black Ninja
Msingi ni Upendo. Na Upendo haina maana tufanane mawazo na tusitofautiane kifikra. Tuuishi Upendo maana hata hasi ina chanya ndani yake.
Huyo ndio mgeni wetu wa leo ndugu Plate Mdaijasho kwa kazi zake mpya pitia kwenye account yake ya YouTube bonyeza subscribe pia weka alarm ili kukupa kumbusho kwa wakati pindi wimbo mpya ukipandishwa. Pita na hii channel yake ya YouTube utapata kusikia na kutazama kazi zote za Plate Mdaijasho.
Pia wasiliana na Plate Mdaijasho kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii;
Facebook: Plate Mdaijasho Sahani
Instagram: Plate Mdaijasho Sahani
Twitter: plate_mdaijasho