Wakati nilipokuwa nikifanya mahojiano na Rado pamoja na Nyeke Da Nyiki kwa muda tofauti, nilifurahia sana mahojiano yetu na jinsi walivyokuwa wepesi kunijibu chochote kile nilichowauliza kuhusu Ku.Tu. Rado Kiraka alinijibu maswali yangu kwa njia ya voice notes za WhatsApp ambapo kwa nyuma ilikua ikipiga midundo mizuri ya Hip Hop kama vile Slippin’ ya marehemu DMX, Hot Damn ya The Clipse. Ungelidhania tulikuwa tunafanya mahojiano studio.
Rado Kiraka
Nyeke Da Nyiki naye tulifanya mahojiano ya simu moja kwa moja ambapo nilipata elimu ya awali kuhusu Ku.Tu kwa kirefu kabla ya yeye kuniunganisha na Rado Kiraka ambaye ali refresh alichonipa Nyeke na kuniongezea zaidi. Karibu Micshariki Africa ili ulifahahamu kwa undani tukio la Ku.Tu.
Karibuni sana Micshariki Rado Kiraka na Nyeke Da Nyiki.
Heshima sana Micshariki Africa na mwanzilishi wake Kefa. Salute sana kaka, kwa sababu wazo ulilosimama nalo ni wazo kubwa. Tunaweza sema ni mawazo ambayo yapo lakini ulichotumia ni uthubutu. Kwa hiyo napenda kuheshimu sana na kutambua ulichoamua kukifanya.
Najua vikwazo na changamoto ni vingi pale watu wanapojaribu kuona kwamba hichi kitu kakianza mtu flani na mawazo mengine huwa yanakua kwenye maslahi. Yaani huyu mtu kaanzisha jambo basi litakua kwa ajili ya maslahi yake,. Kwa hiyo hapo bahati Mbaya sana nguvu huwa inapungua kwani baadhi ya watu hua wanaanza kujiweka pembeni kwa sababu wanaona watakua wamechangia moja kwa moja kwenye maslahi ya muhusika wakati unakuta wazo limeanzishwa ni ya maslahi ya pamoja.
Lakini hapo nilikua napenda nigusie upande wa misingi ni kwamba za ki sasa za kiroho za watu zinabadilika sana. hebu fikiria nini ni kibaya hapo kwa mtu kuchangia maslahi yako wewe tofauti na akiwa amekaa tu, maana yake atakuwa amekuongezea kitu. Lakini hebu angalia kwamba hata wazo lenyewe linakuwa sio la maslahi yako ni la maslahi ya wote lakini kwa uwoga mtu anakaa pembeni kwa kuona itakuwa kwa maslahi yako
Kwa hiyo ki misingi kwanza tumekwisha tambua kuwa kuna roho flani ya utengano ambayo inatutenganisha. Na Kwa upande wa Ku.Tu nadhani ndio sababu imefanya tumegundua hili tukio maana yake watu wengi wamekua wakifanya mambo binafsi binafsi. Sasa tumeona tuje kuwa na mfumo wa pamoja ambao kila mmoja atakua ni sehemu na tunasema nafasi ya mtu katika Ku.Tu ni kujitoa kwako katika majukumu. Basi kila hatua utakayo jiweka ndio itakua sehemu yako katika Ku.Tu. Yaani maanake Ku.Tu ni Free Nation, ni taifa huru la kila mmoja ili kusimamia misingi, malengo, nguzo za H.I.P H.O.P kwani tunaamini huko kuna knowledge and movement na hicho ndicho tunachohitaji kuendeleza maktaba zetu yaani maana yake kuwa tutaishi nacho na kuwarithisha hao wajao. Chem Chem sana Kefa.
Maana ya Ku.Tu ni nini na jina lilitoka wapi? Tupe historia ya nyuma ya Ku.Tu, mlianzaje? Je malengo au nia ya Ku.Tu ni nini?
Maana yake ni Kuna Tukio. Tunasema Ku.Tu Kutwa Kuchwa mpaka Kucha au tunasema Ku.Tu ni maji ya bendera si unajua watu wanywe maji ya bendera. Isiwe ni kitu kinachotawaliwa na mambo ya maslahi na kusababisha mambo kukwama na tunajitahidi kusiwe na chochote cha kukwamisha hili. Ni jambo la lazima kama vile kupumua.
Jina likitokea kama wazo na likawakilishwa kwa wana waliopo karibu na familia ya Watunza Misingi kama Wanaboma, Viraka, MaKaNTa, Akili 100 Asili 100, Mapacha na familia zingine mbali mbali ndani yake.
Ku.Tu ilizaliwa baada ya kuona kwamba movement au harakati nyingi zinazofanyika mwishoni zinahitaji kuwa na uwakilishi. Sasa tumejikuta harakati zinafanyika lakini hazina majukwaa ya uwakilishi. Harakati hizo zinazofanyika ni kama ma emcee kama emcee wanafanya mazoezi yaku perform lakini hawapati majukwaa wakati wakisubiri yale majukwaa ya ki maslahi hivyo watu wanapoteza umakini na u sharp wao kwa sababu wanakosa maeneo ya kujinoa.
Pia inafanyika miradi mingi kama albams, mixtapes, ep’s singles lakini zinakuwa zinapita kwa sababu huwa hakuna uhimizaji, hakuna ukumbushanaji na vitu vinakua kama vimemwagwa tu. Kwa hiyo Ku.Tu imekuja sasa kama wazo la kuwakutanisha kwa sababu tunasema kutu lengo lake ni kuunganisha na kuimarisha mtandao wa handaki dunia nzima! Kwa sababu tupo hapa tulipo (Dar na Tz) tunaanzia hapa tulipo ila nafasi zifike kokote watu walipo kwamba Ku.Tu ni wazo la kutuunganisha na kujiimarisha kwa kupitia huku huku handakini.
Tutajiunganisha na kujiimarisha vipi? Ku.Tu inavipengele katika tukio. Tukio la Ku.Tu lilivyoandaliwa limewekwa kuwa na vipengele vi nne;
- Vitabuni
Kwenye kipenge hicho atakuwepo DJ pale na kupitia ile playlist atakayokuwa anaipiga pale ya ambayo imeletwa mahususi baada ya watu kutambua kuna tukio la Ku.Tu basi wale ma emcee watatakiwa kutanguliza ngoma zao tokea popote walipo hata kama ni Mwanza iwe ni albam, ep’s mixtapes au hata singles. Sisi tutaziweka katika ile playlist. Kwa hiyo DJ kitu atakachofanya siku ya tukio toka mwanzo hadi mwisho wa hiyo session ya kitabuni basi itakua ni kucheza hizo ngoma mbali mbali za hao wadau wa handaki. Kwa hiyo atakayekuwepo tu ndio kazi zake zipapigwa pale.
Pia kwenye kipengele hichi tutakua tunashirikisha baadhi ya watu wenye elimu mbali mbali na ambao wako tayari ku share kwenye hii maktaba kubwa ili kuangalia tufanye vipi. Pia kupitia hapa watu wanaweza kuskuma kazi kwa kushirikiana kufanya kazi pamoja Baadhi ya watu ambao tumewahi kushirikiana nao ni JuLaWaTa( Jukwaa La Wajamaa Tanzania).
Mbinu Kwa Mbinu
Mbinu kwa mbinu ni kila aliyefika pale anapata nafasi ya jukwaa na anaonesha alicho nacho pamoja na mwenye mashairi anayakariri, una single, unaweza kui launch pale pia zinafanyika video wakati tukio linaendelea. Kule Kiwalani kuna familia iliunda video wakati wa tukio na video yenyewe tatari ipo online pale YouTube.
- Mihuri Kazi
Mihuri lazima iwakilishwe. Tunapoongelea Hip Hop culture huwa tunaongelea mihuri kwa mfano wa Wu Tang Clan (W). Vitu kama vile sio vidogo, ile ni industry, watu wameishi kupitia muhuri ule na imekua soko kubwa. Kwa hiyo tunahamasishana pia tuweze kufanya vitu kama hivyo. Kila mwenye muhuri atapewa nafasi na kuelezea muhuri wake una maana gani, unahamasisha nini, anaweza akatuonesha kazi ambazo amezifanya ili kuweza kuamsha hicho kiwanda. Shughuli hii ya mihuri hua tunaifanya mara moja kila mwezi.
- Magenge
Kwenye magenge hapa tunahimiza kutambuana, kufahamiana kwa wote tuliofika pale manake mtandao na ukoo wetu unakua. Kadri matukio ya Ku.Tu yatakavyofanyika mtandao utazidi kupanuka pia. Kwa hiyo tuishi katika spirit ya kukua na kila mtu anaalikwa. Nafurahi kuwa na ushirika na Micshariki Africa kwa sababu mimi naona ni kiungo kikubwa muhimu sana na naamini ndani ya mda nayo itakua kwani malengo ni mtandao. Tuendelee kushirikishana ili kusogeza huu mtandao.
Kingine ni kuwa Ku.Tu nyumbani kwake ni pale Msasani Club, Dar kila ijumaa ya mwisho wa mwezi lakini kama moja ya magenge yoyote yatajitoa kuialika Ku.Tu maeneo yao basi Ku.Tu itafanya hivyo ila lazma washafanya upembuzi wa kujua hilo tukio litafanyikaje mtaani kwao kwa upande wa organization. Tayari watu wa Bagamoyo, Baobab wameweza kujitoa na kutushirikisha na tumefanya tukio pale. Kwenye tukio namba nne kule Kiwalani ilionesha sura ya uunganishi maanake hata wasanii wa kitambo sana walijitokeza pale. Mtu kama Luten Kalama alikuweko, Nala Mc alikuepo, FBC Camp alikuwepo, Big Black Gorilla nae alikuepo pamoja na Suma G na ma emcee wengine kibao. Ni sura kama hiyo ambayo tunahimiza au tunatoa wito twende nalo ili tuweze kuunganisha na kuunganisha… Chem Chem sana Micshariki.
Ku.Tu mnajishughulisha na nini?
Ku.Tu tunachojishughulisha zaidi ni kusimamia uzalendo. Tunajishughulisha na kazi za sanaa za Hip Hop kwa sababu imetuongoza katika knowledge and movement ufahamu na maendeleo) ya kila siku. Huwa kuna vitu tunashirikishana hata kama kila mtu ana ishu zake kama vile kuandaa wimbo pamoja. Pia tunajiangalia tusije tukatekwa na kujisahau kwenye upande wa burudani au meza ya karamu kwani wengi sana wanailazimisha iwe ni burudani.
Je nyie mnajisimamia kwenye hizi shughuli zenu au mna wafadhili? Mnawezaje kuandaa matamasha haya?
Shughuli za Ku.Tu kwa sasa kila mtu anafanyia alipo kwani ndio tumeanza na hatuna mdhamini wala mfadhili. Mdhamini wetu ni Mungu Mkuu na mioyo inayojitolea kwani tunaamini wengine wengi wangeweza kufanya hivyo lakini uthubutu, utayari, roho ya kuunganisha, mapenzi ya mkuu mwenyewe ili watu waweze kufanya hivyo…haya ndio ndio yameweza kuwa wadhamini wetu na wafadhili wetu. Ku.Tu pia tuna group la familia la pamoja la members pale WhatsApp ambapo pale kila mshiriki anaona kinachoendelea, tunapeana ratiba na pia uhamasishaji wa michango kwani huwa kuna bajeti. Kwa hiyo tunamuhimiza mtu yoyote anaweza kuona namba zetu akajitoa kadri awezavyo.
Kwa sasa tunalipia vitu vingi, vichache ndio tumeweza kumiliki kama vyetu. Sound system huwa tunakodi na kulipia na kadhalika. Nina imani hivyo vyote tutakuja kuvimiliki kutokana na umoja wetu ambao ni nguvu yetu.
Ku.Tu inaongozaje au kuratibu vipi shughuli zake? Mna viongozi na katiba?
Ku.Tu inaongoza na kuratibu shughuli zake kama hivyo, tunaambiana, tunaitikiana. Na sisi tunasema ni maamuzi ya lazima kwa hiari. Kwa hiyo halazimishwi mtu, hafungwi mtu na katiba yoyote. Tunaendeshwa na ufahamu wetu kwamba wote tumejitambua, kila mtu anaweza kujua kipi ni kulia, kipi ni kushoto, kipi ni ndio, kipi ni sio, kisicho husika tunaulizana, tanachangia mawazo ya pamoja. Hatujajifunga na mambo ya katiba au kiongozi ni nani, hapana. Kama tulivyosema ni kujitoa kwa majukumu.
Kwa hiyo kifupi Ku.Tu inajisimamia yenyewe kwenye shughuli zake na uandaaji wa tamasha yake kwa watu kujitolea. Na nataka ni kwambie kuwa roho ya kujitoa ni kubwa sana kwani kama isingekuwepo hiyo roho ya kujitolea basi mara moja mtandao mzima una uwezo ungevunjika.
Lakini tunamshkuru mkuu ametuunganisha katika roho ya kujitoa kwani tuna tukio bila kuwa na insurance lakini yana uwezo ya kuwa na uhakika.
Mnapokutana siku ya tukio, shughuli zinazofanyika ni zipi na tamasha lenyewe huwa ni la siku ngapi?
Kwanza ningependa kusema ni vizuri au hamasa likiitwa tamasha ila sisi tunatambua likiitwa tukio, maana yake baada ya matukio kadhaa tunatamani au tunafikiria kuwa na tamasha. Kwa sasa Ku.Tu ni tukio la masaa yasiyozidi nane mpaka kumi kwa sababu tukio huwa linakua ni la siku moja na hufanyika Ijumaa au Jumamosi ya mwisho wa mwezi ila ikiwa imealikwa inakuwa Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuanzia saa kumi jioni mpaka saa 6 usiku na kwa tamasha huu mda hautoshi. Tunatamani kuwa na matamasha ila kwa sasa tuna tukio la Ku.Tu.
Shughuli nzima inakuja na mgawanyo wa majukumu kati yetu kama vile Dj anayecheza playlist ambayo ni kipengele cha kwanza cha Ku.Tu, MC anayeongoza ratba nzima, watu wanaofanya shughuli za mapokezi na kuandikisha majina ya waliohudhuria tukio, mawasiliano kabla na wakati wa tukio kwa njia tofauti ikiwemo kusambaza mabango/posters, uhamishaji michango na kadhalika. Pia siku ya tukio lenyewe huwa kuna mtu anawahi kabla ya tukio kuhakikisha mitambo inawekwa na kujaribiwa kabla. wahusika wote wapo kwenye uhai wa tukio.
Ku.Tu huunganisha na kuimarisha mtandao wa handaki kuchwa mpaka kucha, Chem Chem sana.
Je walengwa wa tamasha hili ni akina nani?
Walengwa wa tukio kama maudhui ya Ku.Tu ni kuunganisha na kuimarisha mtandao wa handaki Tanzania kwa hiyo walengwa wa tukio ni wote walio katika mtandao wa handaki. Na aliye katika mtandao wa handaki ni nani? Ni yeyote, popote. Kwa hiyo Ku.Tu ni tukio la wote kwa maudhui ya knowledge and movement(ufahamu na harakati). Awe anafanya Hip Hop, awe anafanya mziki wa kimila ila yenye maudhui ya knowledge & movement au pia underground emcees na kadhalika.
Miaka mitano au kumi mbele mnaona Ku.Tu itafika wapi?
Ninachoweza kusema katika tafakari ni kuwa Mkuu ndio anayeona wapi itakapofika lakini pia sisi pia tuna maono au mawazo ya kuendelea kuwa na uimara kwenye handaki ambavyo ni vyanzo vya uendelezo wa utamaduni walipozaliwa warithi. Pia tunatarajia matunda toka hapo ambayo ni umoja, kujitoa, uthubutu, uzalendo na utambulisho.
Pia tunaamini kutazaliwa kiwanda ambacho kinaweza kuwa kina kambi ya maudhui na uzalishaji na hapo yatatokea masomo ya nini kimefanyika mpaka tumefika hapa. Masomo haya yanaweza ya kawa ni sehemu kubwa ya utengenezaji wa zana na sanaa zinazoendelea. Tunaweza kusema ni maudhui dhidi ya maslahi.
Mwishoni ninachoweza kusema ni kua tunatarajia uhuru wa moja kwa moja yani utambulisho/identity. Usijikute unafanya kitu kwa ajili ya maslahi yako kwani pale utambulisho wako hautakuwepo. Pia tunatarajia kuwa na uwezo wa kumudu pia. Pia tunatarajia kuwepo uwezo wa kudumu. Ukiweza kuwa na hivi vitatu; utambulisho, uwezo wa kumudu na uwezo wa kumudu huo unakuwa ni uhuru kamili. Chem, Chem!
Je tangu muanze tamasha hili mapokezi hadi sasa yamekuaje?
Tunamshukuru Mungu mapokezi yamekua mazuri na tumeongeza familia kadhaa ambayo ni hayo magenge tuliyoyaongelea hapo awali. Mapokezi pamoja na idadi ya ushiriki yameenda yakiongezeka.
Wasanii wanaotumbuiza kwenye tukio wanapatikana au kuchaguliwa ki vipi?
Tukio hilo huwa kama chujio na hivyo basi mtu anahitaji kufika pale na kushiriki. Mtu akifika pale na kushuhudia performance tayari ataona uelekeo wa tukio zima na moja kwa moja ataona kuwa kushiriki pale ni rahisi bila hata maelekezo yoyote.
Kwa wale ambao sio wasanii ila wanasimamia misingi ya Hip Hop kama vile graffiti/sanaa, Djing, Bboying, je wanapata fursa ya kuonesha vipaji vyao pia na kwa njia ipi?
Ndio, hiyo iko hivyo. Ndio nguzo zote zinakaribishwa pale kama vile ma DJ wanaowakilisha Hip Hop vizuri kama vile Dj Onejast toka Baobab, Bagamoyo, Dj Jegalla Old Garage(OG) na pia Dj Black Ninja toka B.B.C(Boom Bap Clinic), (wote vile vile ni ma producer wa handaki). Hivyo nguzo zingine za Hip Hop zinapata fursa kwenye tukio na tunawaalika wengine wote wafike kama walikuwa hawalitambui hili.
Nini cha mwisho ungependa kuwaambia wasomaji watu ambacho sijakuuliza?
Napenda kukumbusha au kukupa tahadhari kwamba hichi tunachokifanyana ni zaidi ya tunachokiona. Haya maswala ya mziki au sanaa yako katika sehemu kuu mbili; kimwili na kiroho na upande wa kiroho ni upande mkubwa sana tofauti na nafasi ambayo umepewa. Kwa hivyo ninachopenda kukuhimiza ni kwamba anza kuingia kwenye madarasa na kuanza kutambua sanaa kwenye upande wa kiroho na hapo utagundua ubunifu mwingi sana.
Kama ungependa kujua zaidi kuhusu Ku.Tu au ungependa kuhudhuria tujio hili wasiliana na
Facebook: Nyeke da Nyiki
Facebook: Radoph Adoph
Au jiunge moja kwa moja kwenye group la WhatsApp la wana Ku.Tu;
WhatsApp: Ku.Tu 2021