Leo tumetimba Nakuru, Kenya ili kuweza kukutana na kufanya maongezi na mtayarishaji mzoefu kutoka handakini ambaye kwa majina anafahamika kama Level Next. Level Next amefanya kazi kibao na ma emcee wa Kenya wakiwemo Veryl Mkali Wao, Romi Swahili, Shahidi The X-Calibur, Kalimani The MC, Trabolee na wengine wengi. Hivyo leo tumeona ni vyema tuweze kukaa naye tupige gumzo tumfahamu na tufahamu shughuli zake nzima za utayarishaji na natumai tutajifunza kitu kutoka kwake
Kwa hivyo karibuni sana kwenye mahojiano yetu na producer Level Next kutoka Nakuru.
NB: Kama ungependa kuskia Podcast ya gumzo hili nenda moja kwa moja hadi mwishoni mwa makala haya utaikuta.
Karibu sana Micshariki Africa kaka Level Next. Kwanza kabisa tuanze kwa kukufahamu, unaitwaje, unatokea wapi au unawakilisha Hip Hop kutokea maeneo gani hapa Africa Mashariki?
Mimi naitwa Charles Arigi, nimetokea NAX (Nakuru), kila siku nimezaliwa na kukulia pale na ninaiwakilisha 1183
Level Next, jina lilitoka wapi na linamaanisha nini?
Kusema kweli mimi nilifanya kubatizwa hili jina, ni story ndefu kidogo. Mtu aliyenipa jina hili ni Genetic Disorder (mchanaji), ndio alienipa jina hilo. Alikuja studio akanipata nikiandaa mlo wa midundo na hapo hapo akaanza kusema , “Yo midundo yako ipo Level zingine, ziko Level Next”. Mie nikamshukuru kwa hili na nikaaamua kulitumia kama jina langu la kazi.
Jina linaonesha vile ninavyojiona, yaani mimi huwa nafanya kitu ili kuzidi kujinoa zaidi ili niweze kwenda hatua ya juu zaidi.
Tueleze kidogo kuhusu historia yako ya kuwa producer, safari ilianzaje, lini na wapi hadi kufika ulipofikia mahali ulipo kwa sasa?
Kama mtayarishaji safari ilianza mwaka 2006 na hapo ndipo nilipoweza kuona mara ya kwanza nilipata fursa ya kuweza kutumia studio ya kidigitali ambayo wengi wanaifahamu kama FL (Fruity Loops). 2006/2007 nilikuwa najifunza, miaka saba baadaye 2014 hapo ndipo nikaandaa album yangu ya kwanza The Rift. Hapo ndipo nilipotokea ila katikati hapo nilifanya production kwa album ya kwanza ya Trabolee, tulirekodi nyimbo kadhaa ila yote tisa kumi ni kuwa safari imekuwa ndefu na imekuwa na panda shuka zake yaani imekuwa learning curve kwangu. Nimejifunza mengi na nazidi kujifunza, si ati nimejifunza kusoma.
Kwa hiyo nilianza hivyo mambo yakazidi kuwa vizuri nikakutana na watu kadhaa ambao walinoa kipaji changu na ikatokea kama ilivyotokea na sasa tuko hapa.
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/LevelNExt.jpg)
Nimeskia sana kuhusu 1183, hebu nieleze kidogo kuhusu kundi hili?
1183 ni kundi ambalo tulisema hapo awali liwe la wachanaji wa Nakuru kwanza. 1183 ndio sababu kuu ya mimi kuandaa album yangu ya kwanza The Rift kwa sababu ilikuwa kama jukwaa kwa ajili yetu. Mahali sisi tumetoka kuna jamaa flani kwenye group yetu anaitwa Bishop Toka Nduki.
Bishop alikuwa anatusimulia hadithi mbaya mbaya kuhusu sekta ya muziki nchini Kenya, kuhusu mchezo mzima vile watu watakunyima majukwaa ya kuonesha talanta yako kisa na maana eti umetokea Nakuru na si Nairobi na mimi nikasema kama hawataki kutupatia majukwaa yao basi tutengeneze majukwaa yetu na tukafanya hivyo kupitia album hii na jambo hili likafanikiwa. Kwa hiyo kupitia album hiyo watu waliweza kuwafahamu ma emcee kama vile Trabolee, Romi (Swahili), Bishop Tokanduki na Genetic Disorder. Kwa hiyo kundi lipo bado lipo imara na bado tunasukuma gurudumu. Aah na lipo hapa kwa ajili ya kukupa sauti halisia, sauti safi ya Hip Hop, hicho ndio kitu tunachojaribu kufanya. Tunajaribu kufikisha ujumbe kuwa sio lazima ukubaliane na hizi ghilba zao. Unaweza kufanya Sanaa yako vile unavyotaka na watu wataipenda vile ilivyo na sio lazima ubadili sanaa yako kama wanavyotaka wao. Huo ndio uzuri wa kundi letu, sio lazima ushushe viwango vyako kabisa. Sisi ni kama tulivyo tunafanya muziki tulioupenda na bado tunaupenda na jinsi tulivyo upenda na bado tunafanya kama tunavyotaka kuufanya na hio ndio 1183.
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/LevelNext-Main-1.jpg)
Level Next, unafanya production ya muziki wa aina gani?
Level Next ni mtayarishaji wa muziki wa Hip Hop. Nimejikita kwa sauti za Boombap. Hivi karibuni nimejaribu kufanya muziki wa RnB ila sanasana nimejikita kwa mdundo wa Boompab. Sababu ya hili ni kuwa mimi nimezingatia sana kundi langu na kwa kundi langu muziki tunaoundaa ni Boombap.
Kwa ufupi hapo ndipo nilipojikita kama mtayarishaji ila hili halimaanishi kuwa unaweza kuniweka ndani ya boksi bado natatifiti kuhusu sauti nyingine lakini kile kilicho karibu na moyo wangu ni Boombap.
Nieleze kidogo kuhusu changamoto za kuwa producer na producer aliejikita kule Nakuru, Kenya. Hujawahi kuwaza kuhamia Nairobi kama njia mojawapo ya kuzidi kuonekana?
Changamoto za kuwa mtayarishaji sana sana wa muziki wa Boombap ni kuwa wakati mwingine watu hawaelewi vile ni ngumu kutengeneza hiyo midundo ya Boombap na hivyo wengine wanaweza kuchukulia poa kazi zako. Unajikuta unataja bei flani nao wanataja bei flani ambayo mara nyingi ni bei ya chini iwezekanavyo (akicheka), uchizi kabisa.
Aah watu wengine hufikiria kama mtayarishaji changamoto nyingine kwangu ni kama watu wengine huja na matarajio kuwa mimi kama mtayarishaji ndio nitafanya kila kitu. Kwao wanachokitaka ni kuchana tu na wewe ufanye vingine. Wakati mwingine msanii anatakiwa alete kitu mezani ili arahisishe kazi ya mtayarishaji sio rahisi bali iweze kuwa bora zaidi. Kwa hiyo hizi ndio changamoto kuu kama mtayarishaji wa Hip Hop.
Kwangu mimi kuishi Nakuru, naipenda Nakuru, nilizaliwa Nakuru, nimezaliwa na kukulia huku na sijawahi kuwaza kamwe kuhusu kwenda Nairobi kwa sababu , sijui nini ni ila sioni kama Nairobi itaelewa sauti ya muziki wangu. Nafkiri nikiwa Nakuru huwa sina presha, huwa nanoa kipaji na sanaa yangu na sauti yangu tofauti na Nairobi ambapo wasanii watakuja kibao na kuanza kunishawishi nibadili mtindo wangu.
Nikiwa Nakuru nafanya kazi na 1183 na ni wachache na hawanisumbui kuhusu mtindo wa sauti yangu ya muziki. Ukiipenda unaipenda na ukiichukia unaichukia na hivyo ndivyo ninavyopenda
Level Next, wewe unamiliki studio yako binanfsi au umeajiriwa? Je hawa ma emcee unaofanya nao kazi sanasana 1183 wapo kwenye mkataba na studio yako au huwa mnafanyaje?
Nina mpangilio wangu, kama kundi tuna mpangilio wetu. Kwa hiyo tuna mpangilio wa aina mbili, nime andaa studio kejani(nyumbani) kwangu ilhali kundi tumeandaa studio eneo jingine. Kwa hiyo kama kazi ni za kundi na hawataki kuingilia ratiba zangu au nafasi yangu huwa tunafanya kazi kwa lile eneo jingine.
Kwangu mimi 1183 ni kama familia, unajua hawa ni kama kaka na dada zangu. Siwaangalii kama wateja ila ni ukweli kuwa mahusiano yetu ni kama mtu na kaka zake. Hivyo ndio sisi hufanya kazi na nafkiri na huo mpangilio hatujawahi kuwa na ishu zozote kwani mfumo tulionao unatufanyia kazi na kama linafanya kazi basi mimi sirekebishi chochote.
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/Rift.jpeg)
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/Veryl.jpg)
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/Bishop.jpg)
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/Blaque.jpeg)
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/Occult.jpeg)
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/EE.jpeg)
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/RomiSwahili.jpeg)
Kaka tueleze kidogo kuhusu jinsi unavyofanya kazi, mteja akija kwako mnaanzaje toka afike na wazo lake hadi ukamilishaji wa mradi wake iwe ni wimbo mmoja au hata albam?
Mimi hufanya kazi kwa njia mbili; nichukue vocals vizuri na pengine ichanganywe na iwe mastered chini ya paa letu. Mteja anaweza kuja na mdundo wake na tutakubaliana bei na hili linakuwa na unafuu kwake. Kama yeye atakuja kwangu na anataka tuuunde mdundo kutoka mwanzo mimi hupenda kwanza tuelewane na msanii ili nielewe anavyofikiria, anachokipenda na anachokichukia, tukipiga story. Mimi siamini kuingia studio kama kwa mfano nimetoka kupiga kazi na Veryl Mkali Wao kisha wewe Kefa unafuata. Staki niingie studio na wewe na mawazo na akili ile ile niliyokuwa nayo na Veryl na pia nifanye na wewe hivyo hivyo.
Lazima nibadili na ilinichukua mda mrefu kujifunza na kuelewa hili. Kwa hiyo lazima tutapiga story na kusema kweli niko na mzigo wa midundo zaidi ya 1000(elfu moja) na sio hata najisifia, niko na midundo zaidi ya 1000 na kama najua mteja anapenda nini basi najua moja kwa moja nitaenda wapi nimtolee midundo flani ambayo ipo tayari ila asipopenda tunaweza unda midundo toka mwanzo. Kwa hiyo hili nalo lina bei tofauti.
Mixing and mastering huwa tuna mhandisi(wa sauti) chini ya paa letu anaitwa Edd The Beat Smith na yeye ndio humaliza mzozo inapokuja kwa kazi zetu hivyo mimi humpa yeye na hivyo ni msururu. Nachukia kufanya kila kitu peke yangu kwa sababu huwa inamnyonya mtu na inamaliza nguvu za ubunifu wake tu.
Teknolojia imekusaidia vipi wewe kama producer au imekupa manufaa gani?
Imesaidia kusawazisha uwanja wa uchezaji. Ndio maana nilikwambia sitaki kwenda Nairobi, shukran kwa teknolojia. Naweza skuma kazi zangu kupitia Instagram, Facebook, Twitter kwani hapo ndio napatikana sana aah pia YouTube. Kwangu mimi teknolojia imenisaidia sana.
Kitu kingine ni kukutana na watu. Na kukutana wa watu tofauti kila siku kama sio kila wiki ambao wanataka kufanya kazi na mimi na wakati mwingine wako mbali. Nimepata ofa ya kufanya kazi na watu flani kutoka Tanzania. Walihisi tunapiga kazi nzuri sana huku. Niliitiwa kazi flani nafkiri ilikuwa Veryl alikuwa anafanya kazi na mtu na mdundo huo mimi ndio nilipaswa kuandaa na ngoma yenyewe ilikuwa anashirikiana na msanii kutoka Denver, Marekani. Kwa hiyo hili ni jambo zuri kwani teknolojia imefanya dunia imekuwa kijiji, watu wanaweza nitafuta mimi naweza watafuta kwa urahisi, pia tunaweza piga kazi kwa kupitia njia ya mtandao. Wewe una record kisha unanitumia sauti kisha naifanyia mixing huku ili nyimbo ziundwe freshi zaidi. Hivyo basi teknolojia ina mambo mengi mazuri sana.
Je kazi ya u producer inakulipa, umepata mafanikio gani toka kwa fani hii?
Bado haijanilipa kifedha, najua ndio unachomaanisha. Kifedha bado. Inanilipa kwa njia tofauti kama vile kuona wasanii wanakua. Nitakupa mfano mzuri Veryl naweza sema najivunia kuona safari ya ukuaji wake. Kwa hiyo kwangu hayo ni malipo pia. Kitu kimoja ambacho nilijiambia wakati nikianza hii sanaa hapo awali, hela haikuwa ishu kwangu kwani nina uwezo wa kuzipata senti kwa njia tofauti. Ninafanya hili kwa ajili ya utimilifu wangu mwenyewe. Kama italeta hela nitafurahi na sitakataa ila kama haitaleta hela mimi niko poa kwani nina mishe kibao ninazozipiga. Kwa hiyo kila kitu kiko poa. Inaweza kuwa poa muziki ikilipa kwani itaniongezea kipato ila hadi sasa mambo bado.
![](https://micshariki.africa/wp-content/uploads/2022/09/LN.jpg)
Wewe hutumia vifaa gani pamoja na software gani kwa shughuli zako za utayarishaji ? Na je unapiga vyombo gani vya mziki ?
Sasa hivi kama mtayarishaji ninafurahia kutumia Ripper, pia nafurahia kutumia Q-base, Serato Studio,MPC studio ila kati ya zote hizi ninayoipenda sana ni FL Studio. Nimekuwa nikitumia FL Studio kutoka mwaka 2007. Kwa hiyo mimi naifahamu FL, nimeridhika nayo ila hili halimaanishi kwamba siwezi kutafuta vitu vipya. Pia napenda Ebritone ambayo pia ni nzuri sana. Pia napenda Reason. Kwa hiyo inategemea na hisia zangu na nini ninachokifanya ila kwa mara nyingi huwa natumia FL Studio.
Inapokuja kwenye ala mimi ni mmoja wa wale watayarishaji ambao hawapigi chombo chochote cha muziki. Kwa sababu mbinu yangu na sauti yangu ni mtindo wa kutumia sampuli. Ninafahamu sampuli na nina uwezo wa kukwambia sauti nzuri ni ipi. Nina hilo skio, nimefunza maskio yangu kuskia hilo, ila kwa upande wa vyombo vya muziki sipigi chochote, pole.
Je unahisi kuwa mashabiki wanawapatia ma producer na waunda midundo heshima wanayostahili ?
Jibu langu la ukweli ni hapana. Watayarishaji ni wale wanaochekiwa mwisho. Ila ni sawa wakati mwingine mimi hupewa pongezi juu kazi yangu ni noma balaa na nashkuru kwa hilo. Ila mashabiki wengi huwa hawajali kaka, bora wimbo ni mzuri wanachokijali ni msanii ni kitu cha ajabu sana.
Je kando na kuunda midundo je wewe unachana?
Ndio hauwezi kuwa 1183 kama hauchani ndio kigezo cha kwanza. Kwa hiyo ninaandaa album yangu mpya na watu wataniskia vizuri kwenye album yangu binafsi kwani kwenye album yangu ya kwanza sikuchana kwani nilikuwa kama mtayarishaji tu. Wakati huu narudi kama mtayarishaji na mchanaji kwa hiyo itakuwa poa sana ila nikwambie tu kuwa 1183 huwezi ingia kama hujui kuchana. Haiwezekani kabisa!
Gharama za kazi zako zipoje?
Bei ni nzuri tu juu ni huduma kwa hiyo hakuna bei maalum. Mimi ndio naweka bei kwani mimi ndio najua kazi itakayofanyika ila hatuwezi kosana na mtu. Sijawahi pata malalamiko mtu anasema bei yangu ni ghali sana kuwa ni bei ya hasara sana, bei yangu ni ya haki kabisa
Kipi ambacho sijakuuliza ungependa kutuambia?
Aah kitu kingine ambacho nimesahau kukwambia ni wapi ninapotoa mskumo wangu. Ninapata msukumo wangu kutoka maisha yetu ya kila siku, vitu ninavyopitia, vitu ambayo mashabiki pamoja na familia yangu wanavipitia. Inapokuja kwa vitu vinavyonipa mskumo orodha ni ndefu. Pia mtayarishaji wangu pendwa ni The Reason Audon. Pia Dr. Dre yupo hapo pamoja na Pete Rock, 9th Wonder. Pia 9th Wonder ndio alinifanya nikabadili sauti yangu baadaye wakati wa kazi yangu ya muziki. Na wa mwisho ni DJ Premier, Ed The Beatsmith, Tedd Josiah na Musyoks.
Level Next mtu akihitaji huduma zako anakupata wapi? Tupe anwani za mitandao ya kijamii unayotumia.
Unaweza kunipata;
Facebook: Level Next Music (The Dope Beat Specialist)
Instagram: Level Next Beats
Twitter: LevelNext1183
Facebook kuna namba yangu ya simu, pia unaweza ni call, unaweza nitumia
Email: levelnext1183@gmail.com
Shukran sana kwa kukubali kufanya mahojiano nasi na kila la heri kwenye mishe zako.
Shukran shukran ni mi nafaa nikupatia mzee. Na wacha nikupatie maua yako leo Kefa unapiga kazi nzuri sana. Mwenyezi Mungu akubariki kaka, kazi nzuri sana kaka, kila siku!