Uchambuzi Wa Albam: Boy Wa Daggo
Msanii: Liquid Flowz
Tarehe iliyotoka: 03.07.2021
Nyimbo: 15
Midundo/Watayarishaji: W4nj4u, G-BvG, Iam, A-Z
Watayarishaji Watendaji: W4nj4u, Lee Mshindi
Mixing & Mastering: W4nj4u
Studio: Glitch Records

Liquid Flowz

Mwaka wa 2021 ulikuwa ni mwaka ambao nilibahatika sio tu kuskia miradi kibao ya ma emcee toka Africa Mashariki bali pia kuweza kuskia ma emcee ambao sikuwafahamu hapo awali. Mmoja wa emcee hawa ni Liquid Flowz ambaye nilinong’onezwa kuhusu mradi wake Boy Wa Daggo kwenye kundi moja la mziki kule WhatsApp.

Kama kawa cha kwanza kukitia machoni nilipopata mradi huu ulikuwa ni mchoro wa jalada ambalo linaonesha kichwa cha Liquid Flowz kama jitu flani nililoliona kwenye sinema moja iitwayo The Terminator ya Arnold Schwarzenegger pengine kututahadharisha kuwa yaliyo ndani si ya kitoto.

Liquid Flowz ni emcee anayetokea Nairobi Kenya. Hivyo basi unajua moja kwa moja kuwa mradi utachanwa kwa lugha tatu; Kiswahili, Kingereza na Sheng. Na hili unaliona wazi kwa jina la album tu Boy Wa Daggo; yaani ni kijana anayewakilisha mitaa anayotokea na pengine alipozaliwa Dagoretti Corner.

Mradi huu ambao umeundwa asilimia 95 na W4nj4u (inasomwa Wanjau) umetumia midundo tofauti kama vile boombap na drill kiasi na emcee Flowz kazibariki na mashairi yake yanayomiminika ki Liquid. Liquid Flowz anatukaribisha kwenye mradi huu na maombi kwenye Prayer Service kabla ya mradi huu kuanza rasmi akisema,

“Skia hii prayer Sir Jah, Whoever You Are/
As we speak niko juu ya jaba kitu nimekosa ni maziwa/
Hii Safari ni refu na sijui kama nitafika/
Reject kwa society , school dropout na drug trafficker/
Onesha hii raia njia wakuwe ready kwa kile niko about kuwapatia/
Watahija hekima tele juu hii si ili kitu walikua wanatarajia/
From being written off to being case ya kutajika/
Boy Wa Daggo mi ndio ule msee uliambiwa/”…

Mistari inayodondoshwa kwenye wimbo huu wa maombi yanaweka bayana nini ukitarajie toka kwenye mradi huu; mistari yake ya kiujanja, ucheshi, kutojali maoni ya watu wasiomtakia mema pamoja na uwezo wake wa kuhoji nafsi yake.

Mradi huu ambao midundo mingi inapiga taratibu inaanza vizuri na ina ngoma zenye mada tofauti kama, ujasiriamali, changamoto za maisha, utafutaji, mahusiano, ulaji wa bata, imani na hata utumiaji wa mihadarati.

Nyimbo ambazo mimi binafsi nilivutiwa nazo ni kama Siezi Show akiwa na Elli akiongelea umuhimu wa kuficha hisia zako ila kuwa mtu wa kusema ukweli kwa aliyekukosea, Baadaye, akiongelea vile yupo busy na utafutaji na kama wewe umekuja na kabobo zako basi mkutane baadae, mzuka sana. Pia hali hii ya utafutaji ameiongelea kwenye Momma Knows.

Sumbuana pia ni wimbo mzuka sana wa mahusiano ambapo Flowz anaweka bayana kuhusu mahusiano na binti flani “Shory ameweza/Kama si Vera maybe ni Huddah” juu ya vinanda flani mzuka sana akiongelea uzuri wa mahusiano, kupatana, kukosana, kufanya mapenzi, umbo lake, uvaaji wake lakini hata baada ya haya yote mahusiano yake yana changamoto kama mahusiano yoyote yale. Kuna dada kauwa kwenye kiitikio akiwa na Flowz. Natamani ungekua na beti ya pili.

Nyimbo nyingine nilizozipenda ni kama No Cap akiwa na emcee/mtayarishaji HR The Messenger pamoja na Eli akisema Flowz kwa ucheshi “Yesu ndio ana save mi nazi spend, Sportpesa” kiitiko kikisema,

“Arif bana si uniashie ki vela/
Juu kuna venye niko chini/
Hizi shida za mtaa siezi hepa/
So me na try kucheza chini/
Daily msee hu dedi mtaa juu ya paper/
Ma youth wamejiami na mpini/
Huku una genya ama una end up jela/
Uki snitch unaingia mitini/”

Maisha mtaani ni magumu na ukitoboa ni kitu cha kumshukuru maulana kwani vijana wanaishi kwenye mazingira magumu sana yenye changamoto kibao kama madawa ya kulevya. Kumalizia nyimbo nyingine nilizo zipenda ni kama Anyday Anytime, 0420HRS, No Retreat na Eazeh akitema mistari kama, “Ndoto yangu kwa mwingine labda jinanimizi” au “Mi ndio the shit na bado sinuki mafi”.

Mradi mzuka sana ambao umetoka moyoni mwa Liquid Flowz, una uhalisia sana, unamtibu, unatutibu. Liquid Flowz, Boy Wa Daggo kawasili rasmi Micshariki Africa na tumempokea vizuri.

Kuwasiliana na Liquid Flowz mcheki kupitia;

Facebook: Liquid Flowz
Instagram: Liquid Flowz