Uchambuzi wa albam: Dreams
Msanii: Lugombo MaKaNTa
Tarehe iliyotoka: 31.08.2021
Nyimbo: 15 + Bonus Track
Waunda Midundo: 10 Wonder, Wise Genius, Burnbob(R.I.P), Oldpaper,
Mixing & Mastering: Nach B & Burnbob, Wise Genius,
Watayarishaji Watendaji: MAKANTA House, AMG Studio, Black Nation

Lugombo MaKaNTa

Biblia husema hivi kuhusu ndoto, “Wazee watapata maono ilhali vijana wataota ndoto” na ndoto ndizo zimebeba maono ya kijana Lugombo MaKaNTa. Mwaka huu emcee huyu alikuwa studio akituandalia mradi wake wa pili ambao aliuita Dreams kwa kimombo au Ndoto.

Baada ya kutuhimiza Upendo Utuongoze kwenye mradi wake wa pili kijana huyu alirudi studio na kutuandalia mradi wake wa pili ambao kusema kweli umekuja kwa wakati mzuri ambapo watu wengi wamepoteza muelekeo kutokana na changamoto za maisha kwa sasa nadhani mradi huu unatusaidia kutukumbusha kuhusu ndoto zetu.

Mradi huu unafunguliwa rasmi na Intro nzuri toka kwa Dotto Maujanja na Siganyota ambao wanatukumbushia kuwa mfumo uliopo duniani kwa sasa ndio unatufanya kukimbilia masomo kuliko kukuza vipaji vyetu au ndoto zetu halisi zilizowekwa ndani yetu na muumba.

Mradi huu ambao umeundwa na producers kadhaa wakiwemo 10th Wonder, Wise Genius, Nach B, pamoja na marehemu Burnbob Wa Kitaa chini ya MaKaNTa House Records umeundwa ki ustadi sana. Lugombo nae anaonesha kuwa japokua yeye ni Maskini Katika Nchi Tajiri (MaKaNTa) yeye ni Tajiri wa mashairi kwenye nchi yenye uhaba huo.

Kwenye wimbo Dreams ambao ndio wimbo uliobeba jina la album ulioundwa na 10th Wonder na Nach B, unaotumia sampuli toka kwa wimbo I’ve Got Dreams To Remember toka kwa Otis Redding Lugombo anatupa historia ya maisha yake akitupa madini kama,

“Haijalishi mfuko baridi wala joto/
Sikimbii umande process ina msoto/
Form 1, Form 2 nikaanza kuota ndoto/
Ku support Hip Hop halina bali kwa vitendo/
Na hili kabla sijawaza kushika vitengo/
Haikamilishi furaha kazi ya mshahara/
Na majukumu ni mengi biashara pia hasara/
Ndoto zinapotimia napuuzia hayo madhara/
Kila mkoa niwe na duka niongoze vikosi/
Nisambaze kazi za wana zaidi ya wadosi/
Nilichukia sana radio zilizoleta ubosi/
Wasiojua utamaduni walituongeza mikosi/
Sikuwaza booth na rap walinichokoza Mkolosae/
Lakini leo popote alipo mwanangu anafurahi/
Sikusahau namwaga matone ya pombe kali/
Naishi ndoto brother niwe au nisiwe na mali/”

Kwenye mradi huu ambao hakuna nyimbo ya kuruka ngoma nilizozipenda ni kama vile Dibaji(Magenge Ya Sae) akiwashirikisha Jadah MaKaNTa, Gwano na Sugu, Imba akiwa na SigaNyota pamoja ya Kay Mapacha wakati huu.

Wise Genius kama ilivyo kawaida yake anatoa midundo mzuka sana kama kwenye Asante Mother Nature akishirikishwa Black Desert, kabla ya 10th Wonder kuua tena na mdundo wenye hisia kwa ajili ya wimbo wenye hisia Kwa Mama, Hip Hop Na Wana. Nash Mc anashirikishwa kwenye wimbo wa Hutoishi Milele akiwa na SigaNyota kwenye mdundo wa Wise Genius tena. Yanatimia Part 1 ulioundwa na Wise Genius pamoja na Yanatimia Part II akiwa na Port Corner ulioundwa na 10th Wonder inaonesha kwa nini ma producer hawa wawili wameshirikishwa kwenye mradi huu. Ni kama walikua wanaambiana we ukimpa Lugombo mdundo mzuri, mie nitampa mdundo mzuri zaidi.

Kwenye Hamjui Nini Bifu  Lugombo anawaonya ma emcee wasimchukulie poa kwenye mdundo baraka sana wa Wise Genius ambao unapiga tarumbeta nzuri sana wakati anatema nyongo kwa wanaoishi maisha ya uigizaji kwenye wimbo ambao hakuna kiitikio kabisa.

Wimbo ambao umeundwa vizuri na Wise G tena Hawatusikilizi akiwa na Wanyamanyafu ni dakika 8 ya madini mwanzo mwisho bila kukuchosha wala kukuboesha. Formula ya mdundo wa Wise G unaendana vizuri na Lugombo kama vile wimbo wa mwisho kwenye mradi huu ulioundwa na Burnbob Wakitaa Endelea Kuchukulia Poa akiwa na Jadah pamoja na kwenye Bonus Track Zao La Jamii akiwa na Natty Brant pamoja na Levis zinapiga vizuri ki boombap mzuka sana.

Nimalizie uchambuzi huu na mistari kutoka kitabu cha Dreams (Lugombo MaKaNTa) sura ya 15. Endelea Kuchukulia Poa beti ya kwanza,

“Lengo kuu ilikua ni furaha kabla ya pesa/
Hizi noti ni matokeo tu usikubali kuwa mateka/
Utajifunza kwa lazima tu baada ya kuteseka/
Walimwengu hawana huruma tu wataishia kukucheka/”

Kwa chochote unachopitia usisahau Dreams zako kama anavyotukumbusha Lugombo MaKaNTa.

Kupata nakala yako ya mradi huu wasiliana na Lugombo kupitia;

Facebook: Lugombo MaKaNTa
Instagram: Lugombo
Twitter: LugomboMaKaNTa
WhatsApp: +255718000522