Lugombo MaKaNTa

Leo tumepata fursa ya kuweza kumtembelea na kupiga gumzo na mwana Hip Hop ambaye pia ni mwanaharakati kutoka Mbeya, Tanzania na pia mmoja wa waasisi wa kundi zima la MaKaNTa (Maskini Katika Nchi Tajiri).

Tumepata fursa ya kuweza kumfahamu yeye na kundi zima la MaKaNTa na pamoja na harakati anazozifanya yeye kama yeye pamoja na kundi hilo.

Karibu sana kaka Lugombo. Kwanza kabisa tuanze kwa kukufahamu, kaka Lugombo majina yako rasmi unaitwaje, unatokea wapi na unajihusisha na nini? Tueleze pia kuhusu elimu yako ulisomea wapi na umefika hadi wapi kimasomo?

Naitwa Frank Andrew Mwakyembe. Mimi asili yetu kwa upande wa dingi au kwa upande wa baba ni Mwakaleli, wilaya ya Rungwe, Tukuyu. Kwa pande za mama zangu mimi ni mwenyeji wa Lugombo, Masoko. Tukuyu.

Kwenye upande wa kujihusisha na kitu gani so far najihusisha na vitu vingi ila kwa haraka haraka mimi ni mining engineer na ni instructor au mkufunzi kwenye chuo cha Sayansi na Teknolojia, Mbeya. Of course hiyo ni kwa upande wa hizi professions ambazo tumeziendea shule.

Na kingine ninachojihusisha nacho ambacho kimetuleta hapa mimi na wewe na tukaanza kuongea ni Hip Hop. Aaah Hip Hop of course ilianza hata kabla ya hizi professions. Kwa hiyo najihusisha na Hip Hop kama mwana utamaduni, a fan first. Sijawai sahau kitu cha kwanza nilicho jihusisha nacho ni shabiki wa utamaduni na ni mwana utamaduni.

Kwenye upande wa elimu huwa  najibu tofauti kwa sababu elimu kama elimu haina kiwango maalum kwamba wewe upo stage gani ya elimu, yaani elimu haijawekwa kwenye stages. Lakini shule kama shule kwenye mfumo rasmi wa elimu ndio umewekwa kwenye hatua kwa hatua. Kwa hiyo so far nina Bachelor Of Science Degree in Mining Engineering kutoka University Of Dar Es Salaam ambayo nilipata 2009.

Currently nafanya Masters hiyo hiyo ya mining engineering lakini nimejikita kwenye Mining Economics. Naisomea pale pale nilipo pata shahada yangu ya kwanza, Dar Es Salaam.

Kwenye upande wa elimu rasmi, aah generally I cannot say niko kwenye level gani as you know kuna elimu rasmi na isiyo rasmi. In general yote ni elimu. When I read books, when I learn kupitia watu wangu wa Hip Hop, tunapo learn kupitia maisha yetu ya mtaani everyday ni hatua kwa hatua; leo wajifunza hichi, kesho unajifunza kingine. Hiyo haina level maalum haijawa classified.

Hongera kwa kuwa mshindi wetu wa kwanza Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards(January 2022). Unajiskiaje kutunikiwa taji hili linalonuia kuwatuza ma emcee kwa ajili ya mashairi na uchanaji wao mzuri? Je huu wimbo wa Gangsta uliokuwezesha wewe kushinda tuzo hili ulikujaje na uliuandikaje na kwa malengo gani?

Aaah nashkuru sana Micshariki Africa kwa kuchukua mda wenu kwanza kwa kuskiliza kwa makini wimbo huo Gangsta na mkanitunukia mimi 2022 January kwamba kama emcee bora wa mwezi huo wa mwaka wetu na nadhani nilikuwa wa kwanza. Nashkuru sana, sana.

Gangsta nimejivalisha systems ambazo watu especially wale ambao tuko naïve kwa kiasi flani tunaitegemea kwamba yenyewe (systems) ndio itatuvusha moja mpaka mbili kumbe ile system ipo na hata ituvushe au isituvushe ipo. Na hiyo system ofcourse katika kila nchi ya dunia hii inaitwa serikali. Haipo kwa manufaa ya watu, watu haswaa wanachokitaka.

Kwa hiyo nimejivalisha ili kuonesha the other side ambayo tunaiona wengi kwa hiyo nikajivalisha viatu halafu mimi nikasema tu mimi ni Gangsta kwa sababu naamini au nimeona serikali nyingi zinazodumu ni Gangsta na viongozi ambao ni wa kweli sana ambao sio ma Gangsta hawawezi kudumu katika huo mfumo. Huo mfumo is about power and money about business. It’s all about that.  Lakini tusioona tunawahi kushabikia kama mpira.

I was trying to show my people kwamba oya, hiyo ni Gangsta

MaKaNTa- Tueleze kuhusu hii harakati. Jina hili lilikujaje na linamaanisha nini na linajihusisha na nini? Tupe historia ya harakati hii. Pia ningependa kujua ni nani wahusika wa kundi hili la MaKaNTa?

Aaah MaKaNTa kama inavyoandikwa hivyo ni kifupi cha Maskini Katikia Nchi Tajiri. Na hiyo

ilitokana na waasisi kuazimia kuwakilisha Africa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Of course Africa nzima kwetu sisi ni nchi moja, lakini kusini mwa jangwa la Sahara tuliona kuna shida hiyo ya umaskini katika nchi tajiri. Nchi zina resources nyingi sana lakini unakuta jamii hazilingani na rasilimali ambazo nchi hizi za kusini mwa jangwa la Sahara zimejaliwa.

Kwa hiyo wananchi hawapati huduma za kijamii wanazostahili kutokana na rasilimali ambazo wanazo. Zaidi zaidi zile rasilimali zimetumika kufaidisha mataifa mengine. Kuna mifano mingi kwa hiyo sitaingia deep hapo. Tukiongelea Congo tunajua Ubelgiji walifanya nini, Tanzania, Mjerumani na Muingereza alifanya nini. Nchi zote, Zimbabwe twende mpaka South Africa, unajua kilichoendelea.  Kwa hiyo tukabaki Maskini Katika Nchi (Zetu) Tajiri. Bado mpaka leo, kuna bibi zetu bado wanafuata maji kilomita kadhaa wakati utajiri wao umefaidisha nchi za watu, utajiri wetu umefaidisha nchi za watu.

Kwa hiyo ndio tulichoazimia kukiimbia, kukisimamia, kukiwasilisha na kukipigania kama MaKaNTa as a family ambayo ilianzishwa mwaka 2011 Mbeya.

Tulianza tu kama watu ambao wote tuna ndoto flani hivi za kusimamisha Mbeya Hip Hop Kulture. Kwamba Mbeya kurudisha heshima yake. Uzuri tulikutana na watu ambao wote ni fans wa Kulture lakini pia ni active. 2011 tulikutana Mkolosae (RIP) ambae alikuwa anawakilisha Mapepo Ya Jangwani kutoka 2000 na alichukua tuzo ya 2003 ya kusini, Nyanda za juu kusini ya Kilimanjaro akiwakilisha Mapepo Ya Jangwani kwenye emceeing. Walikuwa na Latin Ringo na Tovuti. Ofcourse Tovuti, Tata na Mkolosae (RIP), wote wakawa memba wa MaKaNTa, tukajenga kitu kimoja.

Pale alikuwa Adamoe MaKaNTa ambaye alikuwa Dirty South na alikuwa mchizi sana na Geezy Mabovu (RIP) mwanetu. Tutakutana na Siga Nyota (Siga Nyox) 2011 wakati tukifanya collabo nyingi wakati tukifanya hizo harakati yeye alikuwa Kabwela Squad kutoka enzi za shule ya secokandari O Level, Iyunga, Boys.

Na Jadah MaKaNTa, kipindi hicho tukiwa tukipiga nyimbo yeye anakomaa na chorus, lakini talent yake tukaiona ni balaa. Hao nimewataja wote ni waasisi, wale walionzisha.

Lugombo akitokea Gego Boys nilianza kuanzia 2005/6 na tulikuwa na Gego Master  na Echo Flex, tulikuwa na Jitu, tulikuwa na Noody Shujaa, wakati tupo hostel pale. Tumetoka zetu sekondari tumefokafoka tukakutana wote chuo. Nilikuwa Gego Boyz kwa hivyo mimi nilivyopata mitakasi Mbeya basi ikawa ni kutafuta pale ni nani ambao wote wana uchungu kama yule na yule ambao wanataka heshima Mbeya, kusimamisha Hip Hop kama ilivyokuwa mwanzo na isije tu hivi watu wa media ikaja kuchukua watu na kufanya kama inavyotaka. Kwa hiyo tulikutana wote wenye hasira tu.

Ndipo ikazaliwa MaKaNTa lakini tulijipa kazi ya kutafuta tuwakilishe nini kama pamoja kwa sababu individually kila mtu alikuwa anawakilisha maono yake na experience yake kwenye Hip Hop Kulture lakini mpaka MaKaNTa inazaliwa November 2011 ni kwamba tulipeana kazi tuwakilishe swala lipi la kijamii, swala lipi ambalo linasumbua ambalo au ni jema au lazima tusimamie swala chanya kwa jamii yetu. We cannot be rapping kama wengine kwamba tu una grab the microphone lakini sina ambacho nakisimamia, sina ninachokipigania. Tukasema sisi ni watu wazima, tumechana huko nyuma kwa hiyo itabidi tufanye kitu na tuweke kitu sensitive iwe mada kuu. Ndipo tukaja na hiyo harakati ya Maskini Katika Nchi Tajiri na slogan ikiwa hatutaki umaskini katika nchi tajiri. Aah nadhani nimeeleweka. Blessings.

So far members ni wengi, tulivyoendelea katika harakati, mwaka mmoja tu miwili baadae tukakutana na Stamico Stimela, harakati zile zile, ana hasira zile zile, tuka join. Kabla tu ya hapo tukakutana na wadogo zetu of course hamuwezi tu mkawa ma brother mnafanya, kuna wadogo zenu they got talent ya rap. Tukasema yes, kwa sababu sasa tukiandika mda wote tukiandika mada, mnakuta labda hamuandiki sawa na wadogo zenu, basi tukasema kuwe na MaKaNTa seniors na MaKaNTa juniors. Sasa MaKaNTa juniors ni wale wa kukiwasha.

Of course kwa sasa remember it’s more than 10 years ago, sasa hivi ni watu wazima, topics wanazijua zote yaani. Sasa hivi kama tunataka kuwatafuta MaKaNTa wengine ambao wawe juniors ni kazi ya wale ambao walikua juniors ku recruit wengine ambao watakuwa kwenye same page ambao wanaelewa kwamba these brothers are like this. Kwa hiyo now wamekuwa seniors sasa hatuwezi kusema they are juniors anymore. Wamekua, wamekua watu wazima wana ndoa zao, wana watoto sasa hivi yaani that’s it you get the pictue. Blessings, tuko wengi kuna Ezdon MaKaNTa kuna watu they don’t even touch a microphone. Wapo yaani kwenye family so, it’s quite a huge family kwa ajili ya harakati kuhakikisha inaenda.

Hadi sasa Lugombo umetoa miradi mingapi, ilitoka lini na inaitwaje? Je kwa upande wa MaKaNTa hadi sasa mmeshatoa miradi mingapi, lini na inaitwaje?

2016 Lugombo MaKaNTa of course niliachia mixtape inaitwa Made In Green City, alafu 2018 nikaachia album inaitwa Upendo Utuongoze na nashakuru kwa jinsi handaki au Hip Hop family wameipokea na wimbo ule ambao unaitwa Upendo Utuongoze ukawa ni slogan kubwa sana katika Hip Hop family, Hip Hop community ya wanaofuatilia katika Hip Hop Kulture kwa hapa kwetu.

2021 niliachia album nyingine inaitwa Dreams nimeachia mwezi August tarehe 31 ambayo sisi kama MaKaNTa tunaadhimisha kama siku ya hayati Mkolosae. Mkolosae ndiye aliye play part kubwa ya kutukutanisha sisi pale Mbeya mpaka ikazaliwa familia ya MaKaNTa. Alitukutanisha mmoja baada ya mwingine yaani mimi nilikutana naye sababu hii, mara akakutana na wengine sababu hii, wengine wana historia mara hivi hivi, yaani yeye ndiye aliyefanya tuungane na tukaanzisha hiyo familia kwa hiyo niliachia Dreams the album kwa sababu ya ndoto zangu lakini pia aliyefanya sasa hizo ndoto zitimie under the umbrella of MaKaNTa ndiye hayati Mkolosae. Kwa hiyo familia ikafanyika kwa kuunganishwa na Mkolosae na ndio maana nikaachia Dreams ambayo ilikuwa ndoto zangu nyingi nimezisema mle ambayo nikaachia tarehe aliyoyutoka Mkolosae tarehe 31.08.2021. Yeye alitutoka miaka mitatu kabla ya hiyo tarehe niliyoachia.

MaKaNTa  kama MaKaNTa mradi tuliotoa 2015 tulikuwa tushamaliza mradi unaoitwa Maskini Katika Nchi Tajiri Vol. 1 ndio ikafuata hiyo Made In Greencity  ya Lugombo, lakini kabla ya hapo Adamoe MaKaNTa 2014 alitoa Uhuru Haupo Huru Mixtape.

2017 ikatoka album ya MoMuMo inaitwa MoMuMo. Ndio maana 2018 nikaachia kama nilivyosema Upendo Utuongoze kwa hivyo tulikuwa na mfululizo flani. Wakati huo huo mwanzoni 2018 Adamoe akatoa album inayoitwa Nje Ya Mtaala. 2018 hiyo hiyo tukaachia compilation album December ya Mkolosae inaitwa Life Of Mkolosae, tuna project nyingi sana. Hii Life Of Mkolosae is a compilation of projects kutoka kipindi anafanya na akina Complex (R.I.P), Mapepo Ya Jangwani hapa Dar Es Salaam, amefanya na akina Suma Lee projects zipo zote kwenye compilation hiyo called Life Of Mkolosae. 2020 Momumo aliachia project nyingine inaitwa Hisia album. Kwa hivyo tuna projects nyingi. Hivi sasa tupo currently kuachia Maskini Katika Nchi Tajiri Vol. 2 ambayo tumeshaanza na tutafanya na producers wawili; Double (Dodoma) na pia tutafanya na official producer wa MaKaNTa ambaye pia ni member of the family Oldpaper MaKaNTa ambaye ni mdogo wa damu kabisa wa Mkolosae na ndio producer wetu mkubwa ambaye tumeanza naye na ni sehemu ya MaKaNTa juniors na we can’t call them juniors anymore maana sasa ndio wanachukua majukumu, harakati katika familia ya MaKaNTa.

Kusema kweli project hii ya MaKaNTa Vol. 2 ina hasira zaidi kuliko ile ya kwanza kwa sababu tulipofanya ile Vol. 1 tulikuwa hatujajihami vizuri na ufahamu, kuongeza ujuzi, kuongeza maarifa hapa na pale, kwa hiyo tumeongeza experience na tunajieleza vizuri zaidi kila iitwayo leo. Mawazo ya 2015 hayawezi kuwa mawazo ya 2021. Blessings na of course pia 2022 haipiti bila album ya queen Jadah MaKaNTa. Kwa hiyo project zote hizo zinakuja na pia watu wanarekodi daily. Ila zitakazotoka rasmi mwaka huu ni MaKaNTa Vol. 2 na album ya Queen Kong ila jina la album Jadah kaniomba nisilitaje kwanza. Atleast MaKaNTa Vol. sio rahisi mtu kuchkua jina aseme atafanya album ya MaKaNTa ila album ya Jadah MaKaNTa ni rahisi kutaja jina mtu mwingine akasema wacha alitumie kwenye album yake. Blessings.

Pia tueleze kidogo kuhusu hii MaKaNTa House Records na Machata House, huku mnajihusisha na nini?

Aah, MaKaNTa Africa ni jina la familia, ni jina la kikundi la sanaa, of course sipendi kuliita kikundi kwa sababu tunavyoishi ni zaidi ya kikundi cha sanaa. Mother Nature katusaidia sana tuishi kama family, kuelewana, strength, weaknesses, yaani siwezi kusema kikundi na of course huwa hatutumii kikundi, ni family. Hiyo ndiyo MaKaNTa Africa, sio kampuni wala nini, ni family.

Sasa ukija kwa MaKaNTa House (Records) hiyo ni kampuni, ukija kwenye Machata House hiyo ni kampuni. MaKaNTa House ni kampuni inayo deal na music business, especially Hip Hop kwa hiyo inaweza ikarekodi, inaweza ikafanya kazi na msanii yoyote ambaye anaweza aidha akasimamiwa na MaKaNTa House au akajirekodi na akajisimamia mwenyewe ndio maana ukiona kazi utaona “MaKaNTa House Presents”

Pia unaweza ukaona “MaKaNTa Africa Presents”… ujue hiyo kazi haijasimamiwa na MaKaNTa House kama kampuni bali imesimamiwa na familia tu member mmoja wa familia kafanya kile kitu sio under the company.

Machata House ni kampuni ambayo ina deal na fashion, kwa sababu katika Hip Hop tuna street fashion, kwa hiyo ni kampuni kwa ajili ya street fashion, ambayo pia ni zao la MaKaNTa as a family. So Machata House ndio kazi yake hiyo. Nafkiri hapo tumeona tofauti ya MaKaNTa Africa, MaKaNTa House and Machata House. Machata House ni anybody ambaye ana nafasi anaweza akawekeza, of course priority ni MaKaNTa Africa wao ndio kwanza wanaanza alafu wengine ambao wanaweza kuwekeza wao wanakaribishwa.

Of course tuna affiliate mmoja mkubwa sana wa MaKaNTa anaitwa Ben Mbuya ni mmoja wa waasisi wa Machata House, kwa hiyo sio lazima uwe pale ndani, hapana, mtu yoyote ambaye anasema we have to invest in street fashion anaweza aka invest akija MaKaNTa ata invest under Machata House kwenye stree fashion. Ambaye anasema I need to invest kwenye music na MaKaNTa Africa ata invest under MaKaNTa House Music (Records) even though the business name is MaKaNTa House. Blessings, nafkiri imekaa vizuri hiyo.

P.A.N.D.E – Push Art Not Drugs Exhibitors. Tueleze kuhusu hii harakati, tupe historia kidogo kuhusu harakati hii na utueleze mnajihusisha na nini. Pia tueleze kidogo kuhusu mwendazake Mokiwa, mahusiano yenu yalikuaje na mchango wa huyu mwana kwa Hip Hop na sanaa ya bongo kiujumla ni yapi?

Push Art Not Drugs (Exhibitors) rasmi ilikua mwaka 2016, ndio hizo idea zilikuwepo tangu wakati yuko Sinza Darajani ofisi kwa dada yake Martin (Mokiwa) mwenyewe alikuwa ana frame (duka) ya carwash, tangu wakati tunakutana kwa mazingira yake kujadili movement, lilikuwa wazo lipo la kuunganisha wanaharakati na na emcees tofauti tofauti katika kuhamasisha jamii hasa vijana wakaweza kutoka kwenye matumizi ya madawa wakaweza kutumia vipawa vyao kama sanaa ya kuchora, kama sanaa ya kuandika, kama sanaa ya ushairi au ya Hip Hop na kadhalika. Sanaa yoyote ambayo inaleta matokeo chanya kwa jamii ili watu waweze kutoka vijiweni kwenye madawa ya kulevyi wakaja kutumia vipaji vyao walivyobarikiwa na Mungu, sanaa katika kuendesha maisha yao. Hilo ndio lilikuwa wazo kuu ambalo Mokiwa alikuwa nalo.

Kwa hiyo wakati muda ukienda kitu ambacho kilikuwa kinatusumbua ni ofisi rasmi ya hii taasisi na hatua zikaanza za kuunganisha nguvu ya mmoja kwa mmoja mpaka time ilikuwa ni 2017 ndio mimi nilikuwa nimeamua kutafuta ile ofisi Tabata baada ya kuona kwa mda mrefu tunahangaika tuifanya wapi na wapi  tukaona ile frame (mlango wa duka) tunaweza tukaifanya ofisi ikabidi niiteke. Baada ya kuiteka ikabidi nimpigie mwanajeshi Mokiwa, hapo ni 2017 mwishoni.

Kwa hiyo baada ya hapo sasa ndio kujiandaa kwenda kufanya hatua za kuhama, kumuaga sister kwa sababu ndio alikuwa anasimamia mazingira ya pale na kusogea Tabata na kuanza kuiweka rasmi kama P.A.N.D.E, makao makuu yakawa Tabata. Hapa hatua zikaanza rasmi kusogea. Mpango ulianza 2015 mwisho 2016 pale idea ilikuwa imechachamaa na alikuwa anachora na ndio safari nazo pia zilikuwa nyingi kwenda Botswana, Malawi na South Africa zote kuwakilisha sanaa. Kwa hiyo kipindi kile akili yake ilikuwa inawaza kua kuna jambo lazima lifanyike. Kwa hiyo kwenye yale maono nilipoona huyu mbishi ana maono ndio ile sasa nikaona nisichelewe, tuwe na ofisi kwa hiyo mimi nikafanya haraka tukapata ofisi tukahamia na hatua zikaanza na comrade ndio nguvu zikaanza kutengeneza taasisi na hiyo nguvu ndio ambayo tulikuwa tunakusanya maoni yetu pamoja kutokana na maono ya comrade Mokiwa.

Lakini katika mambo ya uchoraji na harakati za movement ni kuwa jamaa alianza kuchora tangu akiwa Dodoma, kipawa hichi ni cha mda mrefu kutoka Utawala Na Ukoo. Na Dodoma alifanikiwa kufanya exhibition waliyoiita Sokoni Exhibition, na ndio ilikuwa vision kubwa kuwa tuje kuwa na exhibition yetu inayohusiana na sanaa tukaita watu tofauti tofauti ndio maana ikawa Push Art Not Drugs Exhibition, hii exhibition kwamba hii exhibition yetu sasa inahusu sanaa zote na kuhamasisha vijana kutoka kwenye madawa basi kwenda kuuza na kuskuma sanaa mtaani.

Huu umoja wa P.A.N.D.E kama taasisi bado upo na ina nyanja zote za taasisi kama mwenyekiti, makamu mwenyekiti, Katibu, makamu katibu, muweka Hazina, mtu wa nidhamu na kadhalika pamoja na wajumbe wengineo

Martin Africa Mokiwa of course mimi kwanza nilimwambia kwenye signature zake nilimwambia kila art unayofanya weka signature Africa Mokiwa, I loved the name! Martin Africa Mokiwa ni kitu kikubwa sana kwake, lakini ndiye mtu pekee katika underground Hip Hop yetu kwa hapa bongo kwa sababu underground Hip Hop is world wide, kwa hapa bongo yeye ndio alivusha sanaa kwani alikuwa ana uwezo wa kuchora na kwenye street fashion yeye ndiye alituvusha mipaka kama nilivyokutajia hapo mwanzo. Yeye ametufanya tuipe thamani sana street fashion, jamaa akienda South Africa watu wamevaa P.A.N.D.E kwenye majukwaa ya fashion, wamevaa Sanaa Africa kwenye majukwaa ya fashion, Zimbabwe wamevaa, Botswana wamevaa, Malawi wanavaa, mambo mengi sana amefanya Martin Africa Mokiwa al maarufu kama Jedikouga. That’s how jamaa amechangia kwa harakati za Hip Hop hapa Tanzania, we appreciate him, we love. Huwa tunasema big log ila kwa sababu hatujui the other dimension the loss could be vice versa, lakini Mkolosae MaKaNTa, Martin Africa Mokiwa ni mapengo ambayo tunaishi nayo katika harakati yetu ya Handaki

Pia kuna mwana tulimpoteza mwaka jana kama sijakosea Burnbob Wa Kitaa. Naona naye pia alikuwa na mchango mkubwa kwenye hizi harakati za Hip Hop sio tu kwa MaKaNTa bali hata kwa Mbeya na Tanzania kiujumla. Ni urithi aliotuachia sisi mashabiki mwendazake Burnbob Wa Kitaa?

Hagai Mwairunga aka Burnbob, kama kawaida yetu pale Mbeya MaKaNTa sio ati tulikuwa tunafanya kazi MaKaNTa House Records tu au MaKaNTa House Music tu, tulikuwa tunaingia studio tofauti tofauti kwa sababu ladha ni tofauti tofauti kutokana na producer flani. Yeye tulikutana naye kwenye studio ya ndugu yetu mmoja wetu anaitwa Last Born, ilikua inaitwa Quality Records, hapo tunaongelea 2014/2015. Alikuwa anafanya pale so tulikuwa tunaenda sana kwa sababu kama MaKaNTa tulikuwa tunakubali alichokuwa anakifanya, lakini mwishowe baada ya mda Last Born alitaka kufungua studio yake kwa ajili ya maboresho na huo ndio mda Burnbob akaona nyumbani ni MaKaNTa House na mwisho wa siku akawa anashinda pale na tutakubaliana kufanya kazi pamoja baada ya kuandikishana mkataba na moja kwa moja akawa member wa MaKaNTa House. Burnbob alikuwa familia.

Wakati nilipokuwa naandaa album ya Upendo Utuongoze nilimkabidhi title za ngoma zangu na kusema kweli alitumia hisia sana kuniandalia midundo mzuka sana kama ukiskia kwenye ngoma Upendo Utuongoze, If I Die Young, Kesho Yetu na kazi nyingine kibao kwa album yetu hii. Ukicheki cover ya Upendo Utuongoze utaona imeandikwa Lugombo & Burnbob, kwa sababu ana asilimia zake mle. Of course MaKaNTa House ina royalties zake pale ila mimi na Burnbob pia tuna royalties zetu.

Producer hawezi kuishia ile unayomlipa studio kwa ajili ya kazi, producer anatakiwa aishi kutokana na royalties zinazotokana na ile album aliyo produce, kwa sababu beat alipotengeneza hatukununua haki miliki, ma producer wa MaKaNTa House akiwemo Old Paper House analijua hili.

Kwa hiyo burnbob amebaki katika legacy ya MaKaNTa House, legacy ya MaKaNTa Africa kwa sababu amehusika kwenye miradi yetu kadhaa kama vile Upendo Utuongoze na Dreams. Hata familia yake mpaka leo wanafurahia kuwa bado wanapata chochote kwenye shughuli zetu. R.I.P Hagai Mwairunga aka Burnbob.

Mkoa wa Mbeya umebobea kwa kutupatia sio tu viazi kwa wingi bali hata ma emcee, watayarishaji pamoja na waigizaji wenye uwezo mkubwa. Mmefanikiwa vipi kwenye haya maswala ya sanaa? Nini siri ya mafanikio ya Mbeya ambayo wengine wanaweza kujifunza kutoka kwenu na wakafanikiwa pia?

Kuongelea attitude ya watu wa Mbeya, kuongelea mafanikio ya watu wa Mbeya katika sanaa kiujumla katika urban culture, katika Hip Hop, bongo fleva kiujumla urban music hilo litatakiwa turudi kwenye general behaviours, attitudes za watu wa Mbeya. 

Sababu kubwa ya mimi kuandika Made In Greencity ilikuwa ni kwamba urban culture wengi ambao walikuwa wanatamba wamelelewa au wamepitia mkoa wa Mbeya. Mbeya has a lot to do with this urban culture. Hilo swali lilichangia sana kukutana kwa MaKaNTa. Kwa hiyo mafanikio ni watu aina flani, ambao wapo maeneo flani ambao asili yao ni aina flani, ofcourse hata vyama vya upinzani utakuta Mbeya wapo fasta kupinga mfumo. Mbeya ni watu ambao hawako reluctant na status quo na watu pia ambao wanakaribia ni watu wa Arusha. Blessings brother.

Matukio na matamasha pamoja na vinasa ni muhimu sana kwa wana Hip Hop. Nimeona pia unahusika kwa kuandaa cyphers kadhaa kule Mbeya zikiwemo Afrika Huru Cyphers pamoja na Kinasa Wazi Cyphers. Nini kiliwasukuma kuandaa haya majukwaa, malengo ni nini na walengwa ni akina nani? Nani anaruhusiwa kuhudhuria na kushiriki cypher hizi?

Kwenye cyphers aah, kama ambavyo ni misingi mikubwa peace, love, unity and having fun lakini badi bado inapokuja wahudhuriaji ni yoyote yule anayependa utamaduni huu. Tunakutana pale ili kuweze kuziba gap la kutengwa na vyombo vingine vya habari. Pale tunaelekezana lyricism, jamii yetu inahitaji kuskia nini.

Asilimia kubwa ya wanaokuja pale ni mashabiki wa Hip Hop lakini kila mtu anakaribishwa kama vile waimbaji wa RnB bora kinachowasilishwa pale ni kile tumekubaliana. As a fan yoyote anaweza kuhudhuria ila kupanda jukwaani kuna limit. Cypher zote za Mbeya yani Kinasa Wazi, African Huru Street Cypher kuna limit ya nani anaweza kuchana pale. Kwanza unatakiwa kuwa mwana Hip Hop alafu unatuonesha zile Hip Hop elements ila kwa ajili ya burudani tunawakaribisha wana RnB, waimbaji, ma emcee pia upande wa graffiti pia. Tumeona talanta kibao kutoka kwa cypher hizi na bado tunawekeza kwa mambo haya kwani talanta zipo nyingi sana. Blessings.

Ni nini kinachokufanya wewe ujivunie kuwa mwana Hip Hop wa handakini? Je kinachomtofautisha mwana Hip Hop aliye handakini na aliye mkondo mkuu (mainstream) ni nini? Je mwanahandaki ina maana hapaswi kwenda au kuskika mainstream?

Aah, najivunia kuwa handaki kwa sababu hapo ndio nipo huru. Ukiangalia systems hazitaki fikra huru zinataka fikra zinazo favour systems ina favour status quo, tunataka nyimbo za namna hii. Unakuta sana sana huenda na kile serikali kinataka kuskia na waliojaribu kuwa tofauti kwenye mainstream media au systems au industry wamejidhulumu nafsi zao, wengi sana. Na wengi wanaingia kwenye utamaduni bila kujua, they think its rap music, its money, its good life its enjoyment. Yaani wao wanaingia kwa ajili ya rap and money. Rap is one product of the culture, kwa hiyo wengi wanaingia wakiona Tv zina influence their lifestyle kuwa jamaa wamemcheki kwa TV kuwa wana hela ila wanakuja kujitambua baadaye.

Nitakwambia mistari mmoja ili ujue kwa nini mimi ni proud kuwa underground artist. KRS One 1995/96 alisema you cannot be Hip Hop if you ain’t got no side hustle . You have to have a side hustle and you really have to learn the principles of the Kulture. Ni kwa sababu umeingia kwa rap utapelekeshwa utasahau hata maana kwani maana niku express yourself through art. Ikifika point you cannot express yourself though art unajinyima, unadhulumu nafsi yako mwenyewe. Hata ukijaribu kurudi baadaye the real Hip Hop fans wanapata tabu kuwaelewa watu kama hao, kwa sababu hawakuingia utamaduni kwa ajili ya self expression ila waliingia pale kwa ajili ya pesa.

Nakupa mfano mmoja Nelly aliwahi kutoa line kum diss KRS ONE kwa kusema “I’m tired of Niggaz judging whats real Hip Hop/Half the time be the niggaz who’s album flopped” lakini leo hii KRS ONE anatoa album kisha anakwambia “They ain’t got nothing to say”.Mentality ya mainstream media ni kwamba inamdumaza mtu hadi anafkiri kwamba maisha yatakua vile foerever kumbe pale unapewa spotlight tu ambayo zile contents ulizokuwa unatoa pale hazikuwa na hisia zako, hukukuzwa na hisia hizo, ukaaacha society nyuma ukawa mtu wa corporates. Hawajui kama hawatakuwa hapo forever na kama hawatowekeza itakula kwao.

Mimi siwezi kuwaambia wadogo zangu pale Mbeya kuwa fanya muziki, peleka redioni subiri matokeo. Hua nawaambia fanya muziki ila unafanya nini ukisubiria kama walivyotuhimiza wazee wetu kua masomo kwanza kisha muziki baadaye. Mimi huwa namwambia mtu anayeuza mtu akomae sana asije akachukua mtaji wake wa mtumba na kuupeleka kwenye muziki au redioni, utaendeshwa, utakua frustrated kwa sababu hii industry haitaki free thinkers, haitaki kujua na if you are Hip it means to know na wewe unachojifanya mjinga kwa sababu unajua kwa sababu umeshaikataa system hivyo utaishia kwenye frustration.

Ndio maana underground Hip Hop ilizaliwa baada ya watu kuanza kupotosha culture. Kulture ya Hip Hop ina International Declaration of Peace ambayo utamaduni wa Hip Hop imetambuliwa na UN kama International Kulture Of Peace & Prosperity na government zetu nyingi hazijui hili swala ila zipo UN.

Mtu mwingine anaona kama ukienda mainstream ni kuwa umetenda dhambi, no man! Unapokwenda mainstream huendi wewe, unapeleka bidhaa yako kama unaona kuna umuhimu wa kuitangaza, wewe ujue a reason why you are doing that. Kwa mfano unataka hii bidhaa yangu ambayo ni rap music au rap music album niitangaze basi nitaenda redioni na kama modern media haitoshi nitaenda kwenye traditional media naitangaza na sitabishana nao wanaposema lipia hiki na hiki kwa sababu najua naenda kwa chombo cha mtu.

Mbona Instagram tunaweka tangazo ya bidhaa yetu tunalipia dollar 5 au kumi? Ni kwa sababu natangaza bidhaa yangu. Pia DJ anaweza kusema lazima nae umchane kitu ili aweze kucheza muziki wako. Hivyo uwe tayari, usiwe mjinga kwamba unaenda kumwambia akuchezee muziki na hujui biashara yake. Tumekataza hilo, blaming game ni game of the failures na tumekataza hilo. Kama hutaki kufuata masharti ya wamiliki redio subiri wakutafute wenyewe. Sisi wakati mwingine tunatafutwa kwani mwandishi wa habari ameona kuna content atauza kwa wateja wake ndio maana kanitafuta. Watu lazima waelewe hili.

Blaming ni udhaifu mkubwa na kama mwana Hip Hop kama unalaumu inamaanisha hujajifunza bado. Blessings brother.

Lugombo nimekuona upo active sana inapokuja kwa maswala ya mitandao ya kijamii. Nguvu ya mitandao hii kwa mwana Hip Hop aliepo handakini ipo wapi? Mbona basi sijakuona ukikumbatia hizi Digital Music Apps kwa ajili ya kusambaza muziki wako kwa mashabiki?

Social netoworks, mitandao ya kijamii inaruhusu kila mmoja aitumie kwa manufaa yake. Sasa mimi nimekuwa active sana kwa sababu naamini kwamba platform niliyonayo Instagram, Twitter, Facebook na YouTube ndio channel yangu, TV au radio yangu ya kuwafikia walengwa na ndio maana niko very active. Kama nilivyokwambia hapo mwanzo kuna modern na traditional media. Hasa hizi social platforms ndio modern media. Kwa hiyo ndio sehemu pekee ambayo apart from majukwaa ya mtaani hiyo ndio platform mbadala za kuwafikia ambao hawapo mitaani.

Tukiongelea kwenye zile website za mauzo ni kwamba MaKaNTa tumefanya tathmini ya kwamba nikitoa album leo baada ya miezi sita feedback napata kubwa nikitumia njia gani; social platform zetu au zangu Lugombo MaKaNTa au za MaKaNTa Africa au za Watunza Misingi au nitumie hizo social platform za kuuza muziki ambao ni rasmi?

Kwa uzoefu wetu tumegundua kwamba hizi feedbacks tunazipata vizuri kwa kutumia hizi social platform zetu na ndio maana tunaweka/kuachia nyimbo kwenye hizo platform especially ambazo hazina maswala ya kulipana labda YouTube, labda SoundCloud, Audimack kidogo na zingine kama hizo kuliko zile za mikataba ambazo tunaweka kazi kisha tunalipana kwa sababu kila kitu kina foundation zake. SoundCloud hutegemei kulipwa kwani una promote kazi zako, YouTube unaanza kulipwa ukifikia vigezo flani, najua kama sijafikisha vigezo vyao nilipwe kuliko wale ambao nitaweka ambao wananipa expectation flani, mategemeo flani kwa hiyo tunatangaza hizo platform kunadi kazi zetu tulizoachia tu. Feedback tunayopata ni kubwa kwa uelewa wangu hapa kuliko kwa streaming apps.

Mimi nikiachia album nikapata watu 125 wanaonunua album yangu kwa elfu kumi, naona ni kubwa kupata milioni moja na point kuliko ambapo niiweke ambapo siiuzi mimi kama mimi, wanauza website flani, napewa asilimia flani ila kwa miezi ile mitano/mi sita sipati hata laki mbili au laki tatu. Lengo ni watu gani na wangapi unawafikia ili waamini kwa harakati zako. Sisi bado hatujaamini fully kwa hiyo mitandao mingine inayo uza kazi zetu. Na kuna mfano wa website moja kuturushia elfu ishirini na tano zetu tulipigwa danadana si mchezo na ikafikia hatua tutoe kazi zetu pale, walichokiweka hawakukisimamia na wakati huo huo tunasubiria kile tushauza karibu milioni kwa wateja wetu kupitia mitandao yetu, radio zetu, tv zetu ambazo ni hizi social media accounts.

Ila tusisahau kuwa lengo kuu ni utamaduni na wala sio pesa. Uki focus na pesa sana utakuwa frustrated sana maana pesa katu haitowahi kukutosha. Usisahua ulianza huu utamaduni kwa kuupenda na baadae ukaanza kushiriki kwa zile elements. Hivyo unaweza kuamu kukaa na kufurahia utamaduni au kushiriki kutoa zile bidhaa za utamaduni pia.

Tutarajie nini toka kwako na kundi zima la MaKaNTa hivi karibuni?

MaKaNTa mwaka huu tupo kwenye harakati za kuandaa Maskini Katika Nchi Tajiri Vol. 2 na album ya Jadah MaKaNTa na ofcourse singles nyingi sana zitaingia YouTube. Kwa mfano mwaka huu Micshariki Africa wamenipa tuzo ya heshima ya Micshariki Africa Emcee Of the Month Mwezi January 2022 kwa wimbo Gangsta, baada ya hapo nikatoa wimbo mwingine Fuck Off, pia kutoka album nilioachia ya Dreams nimeachia single nyingine inaitwa Kissing You Better, tutazidi kuachia kazi kwenye channel za YouTube za Lugombo MaKaNTa, Jadah MaKaNTa, MaKaNTa Africa na za Momumo pia.

Emcee Momumo pia kaachia album zake pale Booomplay, nendeni mkaskilize miradi hiyo,

Tueleze kidogo kuhusu baadhi ya machata yenu mnayomiliki. Je yanapatikana wapi na kwa shilingi ngapi?

Machata House so far tunatolea bidhaa nyingi Mbeya Mjini. Kwa muda huu ambao tunaongea na wewe machata ambayo tuna authority moja kwa moja ni yenye logo ya Maskini Katika Nchi Tajiri (MaKaNTa) ni chata la Lugombo, Queen Kong, Watunza Misingi, Adam Shule Kongwe, Wasadikaya, Akili 100 Asili 100. Kila bidhaa ina garama yake; kofia gharama yake, begi gharama yake, tshirt garama yake. Fulana ya MaKaNTa Africa 25,000 Tshs, fulana ya Adam Shule Kongwe 25,000 Tshs, fulana ya Akili 100 Asili 100 50,000Tshs, begi Asili 100 Akili 100, 80,000Tshs, MaKaNTa Africa begi 70,000 Tshs, kofia Akili 100 Asili 100 bei ni 50,000 Tshs, kofia MaKaNTa Africa 40,000.00, umenisoma? Mizula Asili 100 Akili 100 40,000Tshs, unaona vile zinatofautiana?

Kwa hiyo kwa yoyote anaona thamani ya kile tunachokifanya ana nunua. Ni yeye aone value kwani hatuuzi bidhaa, sisi tunauza zile chata na anayethamini anapata ile logo anachangia, kwamba mimi ni mmoja wao, nimeelewa harakati za hawa ndugu zangu. Bidhaaa anayonunua mtu ndio kuchangia kwenyewe kwa hizi harakati zetu anapoagiza hizi bidhaa mteja wetu.

Album zetu pia zinaenda kwa bei tofauti; Maskini Katika Nchi Tajiri (MaKaNTa) Vol. 1 10,000Tshs, Upendo Utuongoze 10,000Tshs Hisia ya Momumo 5,000Tsh, Momumo the album 5,000Tshs, Nje Ya Mtaala ya Adamoe 10,000Tshs, Uhuru Haupo Huru Mixtape 5,000Tshs, Dreams the album 10,000Tshs. Tunaandaa album nyingine inaitwa MaKaNTa Vol 2. 10,000Tsh, Jadah album yake inakuja (jina nimelificha kwa sasa) album itakua 10,000Tshs.

Mtu anaweza kuagiza kwenye social media account zetu au nicheki mimi kupitia namba yangu ya simu (+255) 0718 000 522 au akamcheki Siga Nyota (+255) 0714 481 423.

Hip Hop nimeona ikija kwa upande wa akina na dada ina changamoto kukubalika. MaKaNTa kama sijakosea kwenye kundi hili lote dada aliye frontline ni Jadah MaKaNTa. Ni nini kinachosababisha Hip Hop kupata support ndogo toka kwao na nyie kama MaKaNTa mna mikakati gani kuweza kuskika kwao na pengine kuongeza akina dada wengine kwenye kundi lenu MaKaNTa?

Aisee umeongea point muhimu sana kuhusu ushiriki wa dada zetu katika Hip Hop Kulture hapa Tanzania niseme. Kwa wenzetu kule Marekani tunaona walivyo active, yupo Queen Bee, Remmy Ma na wengine ma role model kama akina Lauryn Hill, akina Sa Roc, Rapsody wanaishi utamaduni. Ukija kwetu socially hii kitu imekuwa changamoto hapa kwetu hata huwa tunamuuliza Jadah mbona haja recruit mwenzake akaingia kwenye utamaduni huu.

Mbeya tuna akina Phina pia kuna Z-Flow, tunafanya jitihada tuwe nao ila majukumu huwa yanawazidi. Pia tunaangilia vile wanaweza kuwa influence wengine wawe pale. Kwa upande wa bongo fleva wametuzidi kwa kuwa na akina dada wengi bado utakutana na migongano kibao ambayo wenye vipaji wanaachwa pembeni lakini wale Malaya wa mjini wanapewa chance kubwa ya ku shine hata kama ile talent haipo. Sisi tunatambua kuna choo na kuna kioo, na sisi tunapoona choo kinapewa nafasi kubwa kuliko kioo cha jamii basi tunajua kabisa huko sio pa kwenda na hatuwezi kabisa kuwashauri dada zetu. Kwa hiyo its either wabaki wachache kwenye uchanya ambapo wengi watabaki na watatumia akili sana ili kuweza kujisimamisha kuliko kutumia migongo ya umalaya na uchoo wao kujulikana ili wawe wasanii wanaojulikana.

Kuna changamoto kubwa sana na nafkiri ndugu yangu wa Micshariki Africa unalifahamu hili. Hizi changamoto tuzi address pamoja ili kuweza kupata more talents kwenye Hip Hop Kulture lakini ambazo zina value knowledge and self understanding kuliko kupelekeshwa na soko. Challenge ni kubwa na wanao survive wamebahatika kupita kwenye mikono salama.

Mwisho kabisa, ni kipi ambacho sijakuuliza ambacho ungependa

Kitu ambacho ningependa kuongeza kwenye mahojiano yetu ya leo ndugu yangu; wasanii hii haina mipaka haijalishi yupo kwenye utamaduni wa Hip Hop, yupo kwenye bongo fleva,yupo kwenye singeli, yupo kwenye taarabu, ni msanii kuelewa kabla ya kufanya anachokifanya kuingia na kuanza kuwa active kujishughulisha na sanaa aelewe kwa nini anaingia kwenye ile sanaa. Wengine wanawaza wapate umaarufu, wengine hela au nipate hiki ila kabla hawajawaza yote hivi wajifunze na wasome historia ya waliopita katika hizi sanaa. Huweze kwenda bila kujifunza kwa waliopita kwa sababu waliopita yaliyowakuta yanajirudia hakuna kipya. Kipya ni mabadiliko ya teknolojia tu ila mzunguko wa maisha ni ule ule tu kwani hata waliokuwa nyuma yetu walikua na teknolojia iliyokua ime advance kuliko ya wale waliokua nyuma yao lakini mfumo ni ule ule tunarudia.

Wajifunze why tunafanya watajifunza changamoto zitakazokuja watazitatua vipi ili wasiishie kwenye msongo wa mawazo, masikitiko na kupotea njia na kupoteza dira kama yanayowakuta wenzetu waliopo kwenye shirikisho.

Chamsingi zaidi nakielekeza kwa wanangu waliopo kwenye utamaduni wa Hip Hop waingia kwenye utamaduni wakijua changamoto walizopitia kaka zao nyuma. Na hizo changamoto watakuta tumezielezea tayari, tumeziimba, tumeziongelea kwenye majukwaa huru. Tafadhali wajue wanapoingia wajue kama changamoto zile zile wanazozikimbia sehemu zingine zipo, kwa sababu changamoto zipo kila sehemu.

Huwa nawaambia kwani kuna darasa la kwanza mpaka la saba miaka, form 1 mpaka form 4, miaka mi nne jumlisha 11,five mpaka 6 jumlisha 13 chuo miaka minne miaka 17 lakini unakuja kuanza kazi unapata mshahara laki 3. Kwa hiyo umekaa miaka 17 shule uje kupata mshahara wa laki tatu. Sasa wewe ambaye umeanza muziki leo unataka mwakani uwe maarufu upate ma milioni na milioni, una kichaa? Umewekeza mda, umewekeza nguvu (energy), umewekeza pesa gani kwa sababu kila kitu ni kuwekeza. Kwa sababu kila kitu ni kuwekeza time, energy and money au uwekeze hela moja kwa moja ila muda ni pesa kwa hiyo watu wajitambue kwamba unapowataka kuwekeza kitu lazima kuwe na mda ili kitu kiweze kukua.

Mtu amewekeza wimbo mmoja leo anataka awe superstar aitwe kwenye show alipwe ma milioni, wataishia kwenye frustrations. Waogope sana maisha ya kuigiza. Wanayoyaona kwenye ma TV sio maisha halisi. Wasanii wetu especially Hip Hop iwe ni breakdancer au emcee lazima uwekeze pesa energy na muda. Waelewe hizo basics za investments. Ukiwa emcee ukijielewa hautapata shida kama anayopata aliye kwenye bongo fleva ambaye kwa sababu walimpa jina redio flani anaogopa kwenda kununua chips na mshikaki kwenye kibanda flani anaagiza yeye aletewe ndani na hapo hana shilingi buku. Anaona shida kukaa sehemu flani kula barabarani kula mihogo barabarani kwa sababu kafunikwa na lile wingu la branding.

Hip Hop sisi ndio kioo cha jamii, kwamba this is who we are. Waache ulimbukeni. Nawapenda sana na sio ati nimeanza kusema hivi leo. Maisha halisi sio maigizo. Anza kwa jamii yako kujifunza changamoto ya pahala unapotokea, mwana Hip Hop ndio dira.

Blessings Micshariki Africa. Mnachofanya nyie ni kikubwa sana sana. We need to have independent sources of media, independent sources of news, independent sources of Hip Hop like Micshariki Africa. Na appreciate mnachofanya.

Nawashauri wote ambao tunatafuta independence, realness in the Kulture, Micshariki Africa imethubutu na inaendelea kufanya hiki kitu. Basi kwa mda huu effort zetu kila mmoja anae feel kwamba Kulture iende mbele achangie mawazo kwenye Micshariki Africa, aisee Micshariki Africa ongezeni graffiti zinazofanywa East Africa. Uganda kuna matukio ya mtaani ya graffiti, Dar es Salaam kuna Wachata tunaomba muwalete kwenye website yenu, kuna cyphers mikoa mingi ya Mbeya zenye theme na slogans. Micshariki tuleteeni taarifa za mashinani ili taarifa ziletwe na watu ambao ni wetu, Hip Hop inakuwa in control inakuwa na nguvu zaidi pale inapoweka vipengele kuwa wanaoandika kuhusu utamaduni ni wale ambao moja kwa moja wanahusika na Kulture.

Tuwaambie pia watu kuwa Umoja Wa Mataifa umeshatambua kuwa Utamaduni wa Hip Hop ni International Kulture of Peace and Prosperity. Kama UN imetambua basi nchi zote chini ya umoja huu zinatakiwa zitambue hili. Kwa hiyo sio swala la kutuweka kwenye shirikisho tu ila inatakiwa watuweke kwenye utamaduni ili wanaojua Hip is to know wasiseme Hip Hop ina wajuaji. We will not say yes to bullshit. Blessings.

Shukran sana kaka Lugombo MaKaNTa kwa muda wako, tumejifunza mengi na natumai waskilizaji na wasomaji wamejifunza kitu toka kwako.Tunashkuru sana kwa mda wenu hadi hapo tutakapokutana tena, kwaherini.