Albam: Mahat Mabangi – The Untold Story
Wasanii: Magode na Dabliu
Tarehe iliyotoka: 12.12.2016
Nyimbo: 15
Wapiga midundo na ma producer: Samora GKV Mwamba, Ndocha
Mixing & Mastering: Samora GKV Mwamba
Studio: Chuo Records, Ziki Safi, Higherlinxx

Kama vile New York, Nairobi pia wana msemo usemao kuwa, “Kama unaweza kuishi Nairobi basi una uwezo wa kuishi popote pale duniani” mie naongeza “Kama waeza kuishi Eastlands, Nairobi basi waweza kuishi popote duniani”.

Kabla ya Nairobi kuwa jiji lenye msongamano kama ilivyo leo, ubaguzi ulitawala kiasi kwamba kulikuwa na matabaka matatu ya watu. Makundi matatu tofauti, ambayo yalikuwepo wakati wa ukoloni, yalikuwa Wazungu, Waarabu na Waafrika.

Waafrika waliruhusiwa tu kukaa katika Mashariki ya barabara kuu ya Uhuru inayojulikana kama Eastlands. Makazi ya watu weusi yalikuwa maeneo ya Pumwani ambapo kulikuwa na mifereji ya maji, vyoo vya jamii na maeneo ya kufulia.

Nyumba zilizoko Bahati, Kaloleni na Jericho zilifanywa ndogo kwa makusudi ili kuwakatisha tamaa Waafrika kutembelewa na jamaa zao.

Ukweli mwingine wa kupendeza juu ya maeneo yaliyokusudiwa Waafrika ni kwamba makazi katika maeneo kama Muthurwa yalijengwa karibu na mji ili wafanyakazi watembee kwenda na kurudi kazini na pia nyumba za bei rahisi ilikuwa njia ya kuhakikisha kuwa hakuna mahitaji ya nyongeza ya mshahara.

Kwenye haya mazingira ya historia ya ubaguzi dhidi ya mtu mweusi ndio walipozaliwa vijana Magode na Dabliu (W). Walipozidi kukua walipitia na kuona changamoto tofauti tofauti maishani mwao zikiwemo utumiaji wa madawa ya kulevya, kushuhudia vifo vya mabeshte zao waliouawa baada ya kuingia kwenye maisha ya ujambazi pamoja na unyanyasaji wa polisi ndipo walipoamua kuandika story kuhusu maisha haya.

Magode na Dabliu walijitosa rasmi kwenye ulingo wa mziki mwaka 2012 na baada ya mashabiki kukubali kazi zao waliamua kubaki na Hip Hop hadi sasa. Waliendelea baadae kutoa miradi yao wakiwa na kundi lililoitwa  PCL(Punchlines & Crazy Lines) na wakafanikiwa kutoa singles kabla ya wawili hawa kuamua kutoa albam yao ya kwanza 2016 Mahat Mabangi – The Untold Story.

Kwenye kitu chochote unacho kifanya introduction au utangulizi ni kitu muhimu sana. Hivyo basi mradi huu ni utangulizi mzuri wa kuonesha uwezo wa kundi hili na pia utangulizi wa mradi huu umeonesha moja kwa moja lengo la mradi huu. Intro inawapata ma emcee hawa wakiwa mtaani na washkaji zao wakijadili ni wangependa kuskia albam ya aina gani. Mazungumzo yanamalizika kwa mmoja wao akisema, “Mi napenda albam yenye story….”

Na hapo moja kwa moja tunaona kuwa mradi huu unahusu hadithi za maisha, mitaa, mahusiano, mapenzi na changamoto kiujumla wanazozipitia sio tu vijana hawa bali pia vijana wengi Africa.

Wazazi ni watu muhimu sana maishani mwetu, hivyo basi albam hii kwenye nyimbo kadhaa zikiwemo mbili za awali zinaonesha upendo walionao kwa wazazi wao. Kwenye nyimbo kama Mama, Like Father na Heavens Doo upendo kwa wazazi wao unaoneshwa dhahiri na wachanaji hawa. Kwenye Mama akiwemo Magode tu akishirikiana na Rosy, mama anakumbukwa kwa wema na nidhamu alizomfunza emcee Magode. Pia dada Rosy anatendea haki mdundo akiimba kwa sauti murua sana wakati emcee Magode akitusimulia hadithi juu ya vitu alivyofanya mamake ili kuweza kumlea toka utotoni hadi ukubwani.

Baba nae hakuachwa nyuma pale Magode na Dabliu wakiwa na Shaquay- Li wanapomkumbuka baba mzazi kwenye Like Father. Mdundo, mashairi pamoja na kiitikio vyote vimechanganywa vizuri kutupatia ngoma murua sana.

Nyimbo za kutia watu moyo pia zipo kama vile Misimu Zangu wakiwa na Ndocha pamoja na Inami-Misi. Mashairi ni hadithi nzuri ya kukutia moyo yanayo chanwa juu ya vinanda vinavyopiga taratibu. Kwenye wimbo huu kiitikio kikisema,

“I’m a winner/
(Sometimes we up sometimes we down)/
Sita give up/
(But all the time we’ll make it work)/”

Mapenzi pia ni moja ya mada zilizoguswa kwenye mradi huu kwenye nyimbo kama I’m in love, Someday na Too Late. Someday na I’m Love zote ni nyimbo kali sana.

Too Late unamkuta Dabliu akiwa na Cafu The Truth pamoja na Brax wakimwambia ex wao kuwa kashachelewa, wao washasonga mbele. Ma emcee wote walisimama vizuri kwenye wimbo huu wenye mdundo makini sana.

Nyimbo za bata pia zinapatikana kwenye mradi huu kwenye nyimbo kama Me na Mabeshte wakiwa na PCL Army pamoja na Niko freshi.

Huruma ni wimbo ambao unamkuta Magode akitoa shoutout kwa mitaa yake iliyopo Eastlands of Nairobi ukiwemo Huruma alipokulia. Magode anafunguka changamoto alizopitia alipokua akikaa mitaa ya Huruma, Jericho, Kayole, Bahati,Dandora na Majengo.

“Wengine wetu wamefanya security kuwa law/
Ibiwa nangos unapigwa koto mpaka home/
Ma boi kibao wamefanyiwa home justice/
Wale mang’aa wamejifanya ku rob masses/
Hoping to get rich alafu wahame slum/
Lakini wanatoka wakiwa maiti kwa hearse/
Ma boi ni ma playa mademu wao wana ball/
Ma school dropout ni wengi, wengi hawana goals/
Mtoto ako na mtoto kwao hawezi rudi/
Inabidi come-we-stay kwao hana budi/
Vituko na cinema zina go mbele na nyuma/
Nimejionea mengi juu nimelelewa Huruma!/”

Ndani ya mradi huu pia yupo gwiji wa spoken word Teardrops akitupatia shairi poa sana liitwalo Huku Mtaani.

Pia muunda jaladio la albamu nae hakuachwa nyuma kwani alichora vizuri kilichonuiwa kuwasilishwa na wachanaji hawa; mchoro unaonesha muuza gazeti akisoma gazeti mojawapo anayoyauza – huyu ni mtu anayeona na aliyeona mengi kitaa hicho anapofanyia biashara na jambo likitendeka halimpiti, liwe ni habari rasmi kwenye magazeti au habari za kitaa . Nyuma yake tunaona changudoa flani  aki negotiate na mtu aliyeko ndani ya gari la afisa – hili nalo linaeleweka. Kwa kupitia picha hiyo tunaona vile ufisadi umepenya kila pembe ya nchi yao. Hapo kando ya muuza magazeti kuna ndege huitwa Kaloli, Marabou Stock au Bwana Afya aliyejikita juu ya pipa la takataka akiashiria ule uozo uliopo ndani ya jamii yetu kwani nedge huyu hula uchafu ulioachwa na watu .

Kama vile Mahatma Gandhi alivyokua na uwezo wa kutetea haki za wanyonge nchini South Africa na India bila ya kutumia vita basi vijana hawa wawili pia kwa kutumia mziki wa Hip Hop wameweza kupaza sauti na kuweka bayana changamoto za mitaa ya walala hoi wengi wanaoishi Mashariki mwa Nairobi bila ya kuzua rabsha. Wametumia vizuri kinasa, kick na snare, vinanda, gita na msaada kutoka kwa ma emcee na waimbaji wengine kufanikisha hili. Ila kulingana na changamoto zao jina la Mahtama Gandhi lilibadilishwa kidogo na kuwa Mahat Mabangi – The Untold Story, kuonesha kuwa japokua mtindo wao umehamasishwa pakubwa na Gandhi wao wanatumia mbinu tofauti kuelezea yanayowakera. Kwa hili wamefanikiwa pakubwa kwani mradi huu ni real, ni story ya vijana wengi wa Nairobi, Kenya na hata Africa Mashariki. Stori zao zipo hewani sasa kwa yoyote anayetaka kuziskia. Mradi huu utadumu kwani mimi nimepata fursa ya kuuskia 2021 ilhali ulitoka 2016.

Ohh, kamusi ya lugha ya sheng inahusika hapa kwani maneno ya sheng kibao lazma yatakupita ila albam itadumu!

Wasiliana na Dabliu na Magode kupitia:

Facebook: Alfred Magode
Instagram:ma_gode