Ni msimu wa tuzo na iwapo umekuwa ukiishi chini ya mwamba au unapanga kuangalia baadhi ya matukio yajayo na pengine kuhudhuria basi tuzo za Unkut Hennessy Hip-Hop Awards zimewasili.

Wametoka kutangaza walioteuliwa na kwa kweli kutokana na mwonekano wa mambo, mwaka wa 2021 ni mkubwa zaidi na bora zaidi kwani  kuna wasanii kama vile Kitu Sewer, Khaligraph Jones, Juliani, Scar Mkadinali na wengine zaidi wakijumuishwa.

Tulizungumza na Ruby V, mwanzilishi wa Unkut Africa na Unkut Hip-Hop Awards ili kupata machache kuhusu jinsi safari imekuwa kama, nini kimebadilika tangu aanze tuzo hizi na nini cha kutarajia mnamo 18 Desemba 2021.

Ruby V

Karibu sana Micshariki Africa Ruby V. Kwa wale wasiofahamu Tuzo za Unkut Hip Hop, tafadhali wape historia fupi ya lini tuzo za Unkut hip-hop zilianza.

Tuzo za Unkut hip-hop zilianza rasmi mwaka wa 2019. Tulikuwa na tukio Sands Club, Life Plaza kule Kilimani na ilikuwa ni uzoefu mzuri, lakini kabla ya hapo tulikuwa tumetoa tuzo za Hip-Hop mtandaoni mwaka wa 2018. Nadhani watu hawakuzitilia maanani tuzo hizi lakini taarifa zake zilisambaa kama mlipuko na nadhani hiyo ndiyo iliyonihimiza kufanya tukio halisi mnamo 2019.

Tuzo za Unkut Hennessy Hip-Hop ni tuzo za kwanza na pekee za Hip-Hop tulizonazo nchini Kenya, na wewe ni miongoni mwa wanachama waanzilishi, ni wanachama gani wengine ambao wameshiriki katika safari hii ambao ungependa kuwatambua?

Marekebisho, mimi si miongoni mwa wanachama waanzilishi, mimi ni mwanzilishi. Niite ipasavyo (akicheka), ndiyo kweli, mimi ndiye mwanzilishi na tuna jopo ambalo kwa kawaida huchagua orodha ya mwisho ya walioteuliwa. Jopo la mwaka huu tunaye Jinx, ambaye ni mwanahabari (Homeboyz Radio, Kiss Fm), tunaye Ondu Street Lawyer ambaye ni mwanzilishi wa 254 Battle Rap League na pia mmiliki wa Back 2 Basics Podcast, Nimoh Futuristic mwanzilishi wa Sauti Za Mabinti, Curtis, mtangazaji wa redio, Ghetto Radio mwenye kipindi chake Hip-Hop Republik.

Bila kumsahau Tela Wangeci, mwandishi wa habari za muziki katika magazeti ya Tangaza na Beda.

Kwa hivyo naamini tunalo jopo lenye uwezo kabisa.

Je, binafsi ina maana gani kwako kuandaa tuzo ya kusherehekea na kuwatunuku wasanii wa Hip-Hop toka Kenya pamoja na wadau wengine wanaotendea haki utamaduni huu?

Unajua ni kuangazia talanta, kuna talanta nyingi hapa ambazo zinahitaji kusherehekewa, zinahitaji mahala pa kuonekana na ndio sababu tuna onesho la tuzo za hip-hop kuadhimisha wabunifu wa hip-hop wa Kenya.

Kufuatia majibu chanya kwa Unkut Hennessy Hip-Hop Awards 2020, je, umeona tukio/onesho lolote la tuzo la Hip Hop kama hili?

Ndio niliona mtu alianzisha Tuzo za Hip-Hop za Kenya. Nadhani hicho ndicho kitu pekee ambacho nimekiona.

Mada ya 2021 ni 'Kubadilisha simulizi', ni msukumo gani nyuma yake?

Naam, ilianza siku za nyuma, hip-hop kimataifa imekuwa ikichorwa na taswira mbaya kama hii; kuwa imetoka geto au kitaa na kuwa ni chafu na kuwa wasanii wa hip-hop ni wakorofi. Kwa hiyo toka enzi hizo hata ukiangalia kwa mtazamo wa wakenya enzi zile ilikuwa ni kama “Wanaochana ni watu waliotoka ma ghetto yanayo ongea lugha ya Kiswahili.” Lakini baada ya muda tumeona mabadiliko ya simulizi na hip-hop imekuwa zaidi ya muziki wa porojo na vurugu.  Pia tuna watu/wadau wa utamaduni wanaosukuma mazungumzo kuhusu hip-hop kama vile afya ya akili. na hiyo ni poa kweli. Kwa hivyo sisi kama Unkut Africa tumekuwa sehemu ya kubadilisha simulizi.

Mwaka jana (2020), kulikuwa na Hennessy akija kama washirika; una mashirika mengine yanayotaka kuunga mkono tukio la mwaka huu?

Ndiyo, tuna mashirika mengine yanayotaka kutusaidia. Kwanza nitoe shukrani za dhati kwa Mike Rabar (wa Homeboyz Entertainment), alitupandisha daraja mwaka jana. Alituwezesha kupiga hatua nzuri na ilikuwa ya kushangaza sana. Mwaka huu tuna UN Habitat, wamekuja kutuunga mkono. Pia tuna Trace Radio kama mshirika wetu rasmi wa vyombo vya habari na tunashukuru sana kwa hilo. Tunayo Little Cab, Create 2030, bila kusahau Psychwell Foundation ambayo inahusu ufahamu wa kiakili kwa wabunifu. Ninawashukuru wote kwa wakati mzuri kwa kuja na kutuunga mkono na ninatarajia kuwa na washirika zaidi watakaotuunga mkono pia.

Na bila shaka tuna Mike Rabar, HB entertainment kama washirika wetu wa kiufundi.

Je, una maoni gani kuhusu hali ya sasa ya KE Hip-hop?

Watu wanafanya mambo yao kusema kweli, wanajaribu wawezavyo kuifanya mziki mzuri.

Je, kuanzishwa kwa kipengele cha East Africa kunaashiria mipango yoyote ya baadaye ya kuwa na Unkut Hip-hop Awards East Africa?

Kwa kweli sitaki kuzungumzia hilo, tusubiri tuone mustakabali wetu.

Hip Hop ikiwa ni fani inayotawaliwa na wanaume sio tu nchini Kenya bali hata duniani, ni maneno gani ya ushauri unaweza kuwapa akina dada wanaojaribu kutoka katika anga za hip hop iwe ni kama emcee, Dj, blogger au hata  kama mratibu wa matukio ya Hip Hop kama unavyofanya wewe mwenyewe?

Ulimwengu ni wako, usiruhusu jinsia yako ikuzuie wewe kuuonesha ukuu wako ulimwenguni kote. Hakika kama mwanadada unapaswa kujaribu, hip-hop inahitaji wanawake zaidi, na tunakuhitaji. Ikiwa unaogopa, fanya kile kinachokuogopesha. Hatimaye dunia itavutiwa na unachokifanya mwisho wa siku.

Je, wewe binafsi umekumbana na changamoto zipi katika mchakato wa kuanzisha tuzo hii?

Changamoto ni nyingi sana. Hapo mwanzo ilinibidi kufadhili tukio kwa hela zangu mwenyewe, na unapofadhili tukio peke yako mara nyingi inakuwa ngumu kwa sababu huna ridhaa kwa hivyo kutumia bajeti yangu inakuwa ngumu zaidi.

Pili, wale wavunja moyo katika Hip-Hop ya Kenya, hawakufurahishwa na ninachofanya, kitu ambacho  kwani ni kitu ambacho walitamani kufanya lakini hawakufanya na bila shaka hilo liliniathiri kiafya na ki akili. Lakini  kama unavyojua bado tuko uwanja, bado tunasukuma letu.

Tuambie kidogo kuhusu mapenzi yako ya hip hop kwa wale wasioijua. Yalianzaje?

Yalianza mwaka wa 2014, nilipokuwa mfanyakazi wa ndani(intern) pale Homeboyz Radio. Nilienda kwenye Hip-Hop Hook-Up, mpango wa hip-hop ambao uliandaliwa na kusimamiwa na Smallz Lethal kwenye jumba la Sarakasi Dome na Dj Final Kut aliniona hapo na akahisi tunaweza kufanya kitu, kwa hivyo akaniuliza niongee na John. Rabar na kumwambia nataka kuwa sehemu ya utamaduni wa hip-hop, na ndivyo nilifanya hasa. Ilinichukua muda kidogo kwenda kwake kwa sababu nilikuwa mwanafunzi wa ndani (intern) tu lakini niliingia humo. Sikujua mengi kuhusu tamaduni ya hip-hop ya Kenya wakati huo lakini nilitumia mda wangu kuutafiti, kujfunza juu yake na ndiyo nikawa nguvu kwenye maeneo haya.

Kando na kuwa mhusika wa media na mwandalizi wa hafla, je, unachana pia?

Hapana sichani.

Tuzo za Unkut Hennessy Hip-Hop ni tukio la kila mwaka, kando na tuzo, ni nini kingine ambacho jukwaa la Unkut Africa hufanya?

Nadhani hili ni jambo unaweza kuangalia katika majukwaa yetu ya mitandao ya kijamii na kweli kupata kuona.

Tunasukuma ufahamu wa afya ya akili; kuna laini ya mavazi, Unkut Fit ambayo ndiyo imeanza. Kwa kweli nina mipango mingine mikuu ila ni vyema kama tutaweza kua na gumzo tena mwaka ujao na kuona jinsi  mambo yanavyoendelea.

Kuna matukio mengine tunaandaa, kwa sababu tu nimekuwa kimya kwa mwaka mzima nikizingatia kuandaa Tuzo za Unkut Hip-Hop haimaanishi kuwa hatuna mambo mengine tunayofanya.

Unkut Sound Check ilikuwa ikifanyika kila mwezi kabla ya kufungwa na inaonekana kwenye mitandao yetu ya kijamii.

Tupitishe mchakato wa kuwapata washindi, inakuwaje kuanzia uteuzi hadi utoaji wa mwisho wa tuzo. Je, timu yako imefanya nini ili kuhakikisha haki inakuwepo na kwamba walio bora zaidi wanashinda ili kuepuka kushutumia kuhusu upendeleo?

Watu watanyoosha vidole vya lawama kila wakati kuhusu upendeleo lakini kama nilivyosema kuna jopo ambalo huchagua wateuliwa wa mwisho na jopo hili kwa kawaida hukagua sarafu ya utamaduni wao na athari ambayo wamekuwa nayo. Pia tunaangalia jinsi mtu huyu / mbunifu / podikasti / media ya mtandaoni imekuwa katika jumuiya ya utamaduni wa hip-hop, na inapokuja suala la kuchagua washindi hatuwachagui, mashabiki huamua kwa kupiga kura.

Khaligraph Jones na Ruby V

Je, kuna mipango ya siku za usoni ya kuandaa onesho hilo katika kaunti/majimbo mengine nchini Kenya kusaidia katika kukuza sio tu tuzo bali pia utamaduni wa hip hop?

Sijafikiria kuandaa hafla hiyo katika kaunti zingine lakini tunajumuisha wasanii bila kujali unatoka wapi, iwe unatoka Kisumu au Mombasa. Nadhani hatuwezi kufanya kitu kama tuzo za Kisumu Hip-hop, nadhani tunawaangazia wasanii wanaofanya kitu katika mikoa hiyo na kuwaingiza kwenye tuzo za hip-hop kwa sababu tena Nairobi ni mji mkuu hivyo tunatarajia mambo mengine kufanyika huku lakini ni pamoja na wale wasanii wote kutoka mikoa mingine kuhakikisha wanahusishwa.

Ni nini motisha na lengo lako ulipoamua kuanzisha tuzo hizi? Je, unakaribia kutimiza lengo lililokusudiwa?

Motisha ...

Hapo awali, Hip-hop ya Kenya iliwakilishwa tu kama kitengo kimoja katika maonesho yote ya tuzo ilhali kuna watu wengi wanaowakilisha hip-hop nchini Kenya, kwa hivyo nilitaka kuangazia hilo.

Tumefanikisha kusudi na tunaendelea kila mwaka. Tunapata wasanii wapya wanaojiunga na orodha, wakiwa wamewaunganisha wachuuzi na kuona jinsi ukuaji wao unavyoendelea kwa wakati. Nina furaha sana kwamba Unkut ni sehemu ya mazungumzo haya, mapinduzi ya KE hip-hop.

Inapendeza sana kuona tumetoka wapi, wasanii ambao tulianza nao 2016 na kuona wadau wengine wakiingia na kuwa sehemu ya harakati na ndio tunakua pamoja. Inashangaza sana.

Asante kwa muda wako Ruby V. Tunakutakia kila la kheri wakati wa utoaji wa tuzo.

Asante sana Micshariki Africa kwa kunirabisha.