Tulipotoka:

Kwa uelewa wangu kuhusiana na uuzaji na usambazaji wa kazi, hususani za muziki wa Rap na Bongo Fleva kama tunavyopenda kuiita, miaka ya mwanzoni mwa 2000 (kama sijakosea) hadi miaka ya baadae jukumu la uuzaji na usambazaji wa kazi za muziki alikua nalo mdosi kwa jina maarufu Mamu. Kwa nilivyoskia na kufahamu Mamu ilikua pia ni store ya uuzaji wa kazi za muziki iliyokuwepo Kariakoo. Mdosi alichofanya alikua akiwapa deal wasanii mbalimbali kwamba unatengeneza album halafu ye anakulipa kwa kununua master ya album yako halafu anaendelea kuiuza.

Alichokua anafanya anakupa deal na kukwambia kiasi atakachokupa kutokana na popularity uliyonayo kwa kipindi hicho. Inasemekana alikua anatoa hela nzuri japo changamoto ilikua ni kwamba anaichukua master na huwezi kuendelea tena kupata (chochote kutoka kwa kazi ile) ye akishachukua master na ku duplicate kuuza nakala.

Tulipo:

Mfumo wa kumwachia mdosi au kugonga copy kwake ulifika mwisho miaka ya baadae (nashindwa kutaja mwaka exactly) na hii ni baada ya kuaminika kuwa soko la album halipo tena.

Wasanii wakahamia kwenye kutoa singles na kutegemea shows zitakazo tokana na hizo singles, naweza kusema ni kama walikatia tamaa mfumo huo wa uachiaji wa kazi. Wasanii wenye majina makubwa na media waliaminisha kuwa album hazina tena soko hivyo wasanii wakajikita kufanya singles tu na kupiga hela za show.

Wasanii wa Rap/Hiphop hawakukata tamaa waliendelea na mfumo wa kutoa album sambamba na mixtapes na baadae EP. Movements tofauti zikawa chachu katika mfumo mpya wa uuzaji na usambazaji wa kazi.

Ni katika kipindi hiki ambapo wasanii walikuja na mfumo wa kuuza kazi zao wenyewe mkononi au kwa mifumo mingine.  Kutoka Arusha, Watengwa ni kati ya watu waliofanya utaratibu wa kuuza wao wenyewe, Tamaduni Muzik, Vinega kama sikosei hata pia movement ya Okoa Hip Hop.

Ukawa ni utaratibu wa kuuza wenyewe maana mambo ya mdosi hayapo tena, kwa hiyo wana wanatengeneza miradi na kuuza wao wenyewe. Mifumo ya CD na mingine baadae ikatumika na ujio wa dijitali ukawa umefika.

Kwa uelewa na uzoefu wangu ni kwamba mfumo ambao ulitumika hapa ni huo wa kuuza CD na baadae ukaja mfumo wa nakala laini (soft copies) kupitia WhatsApp, Email Au Telegram. Wasanii kama Nash MC, DDC, Tamaduni na wengine wakatumia huu mfumo kupush na kuuza kazi zao.

Ujio wa dijitali nao ukawa sio haba na mifumo ya DSPs (Digital Streaming Platforms) nayo ikabisha hodi. Kwa uzoefu wangu kwa wasanii wa Rap mfumo wa kuuza mwenyewe kwa shabiki au mtu anaehitaji kazi yako (album, ep au mixtape) ni mzuri zaidi kuliko huu wa kuuza kwa dijitali (DSPs) kwani kuuza mwenyewe msanii anaiona hela yake moja kwa moja tofauti na dijitali ambapo tayari kunakua na mtu wa katikati au kwa jina lingine third party.

Bongo Fleva wakaja wakashtuka kwamba album zina umuhimu kwa hiyo nao wakarudi kuanza kutoa albums, eps lakini ma emcee wao ilikua ni utaratibu hata ilipoaminika album haziuzi tena waliendelea kutoa miradi. Kwa Hip Hop ilikua ni mwendelezo tu ila wenzetu ni kama walianza upya.

Kwa wao (Bong Fleva) mfumo ambao wamekua wakiutumia ni wa DSPs na zamani CD ambapo msanii kama Vee Money aliwahi kuweka kwenye DSPs na kutoa CD.

Miaka inavyoenda CD hazitumiki sana au tena hivyo wasanii wa Rap/Hiphop ni muhimu wakakomaa na soft copies (WhatsApp au email qua Telegram). Hard copy kama CD zitolewe kwa baadhi ya mashabiki wanaohitaji lakini pia flash zinaweza kuwa mbadala wa CD.

Kuchanganya mifumo hii miwili (kuuza mwenyewe na kuweka kwenye DSPs) kuna hasara yake kwa sababu unaweza kukosa balance katika mauzo yako kwa sababu bado hakuna weledi wa kutosha kuhusu matumizi ya hizo DSPs kwa nchi yetu. Niliona hili kwenye album yangu ya kwanza niliyoitoa mwaka 2018 Fikra ni Vazi la Rap ambapo niliiweka kwenye platform ya Boomplay na kuuza mwenyewe, kwa kweli nilipata mauzo kwa kuuza mwenyewe lakini Boomplay ikawa hola.

Tunapoelekea:

Ulaji wa muziki umebadilika kutoka matumizi ya tapes, CDs mpaka sasa tupo dijitali. Duniani watu wengi kwa sasa wana consume muziki kwa njia ya DSPs ambapo hata wenzetu tumekua tukiona wanatoa miradi kwanza kwenye hizo DSPs kisha hard copies kama CDs, Vinyls ndio zinatoka.

Kwetu bado kuna changamoto kwenye ulaji huu wa muziki kwa sababu Watanzania wengi bado kwao hizi huduma sio rafiki. Mfano platforms kama Apple Music, Spotify zimekuja miaka ya karibuni tu hapa hivyo bado wengi hawajazizoea na ndio platforms ambazo zina malipo mazuri. Huku kwetu tumezoea na kuamini YouTube tu wakati katika ulipaji yenyewe iko chini sana, hii nadhani ni kutokana na jinsi media na wasanii maarufu wamekua wakiaminisha kuhusiana na platform hiyo.

Kwa wenzetu wa kuimba nadhani hizi DSPs zinawafaa kwa mtazamo wa namba maana ili ufaidike nazo unahitaji numbers za kutosha. Namba wanazo na zinaweza kuwasaidia kupata manufaa zaidi.

Kwa watu wa Rap/Hiphop nadhani ni muhimu zaidi wakijikite katika kuuza wenyewe mpaka pale watakapoona mfumo unawa favor wao kufanya hivyo (kuweka kwenye DSPs).

Imeandikwa na Fivara

©️ REKUSA