Mantik Barz

Karibuni sana Micshariki Africa Jukwaa la Hip Hop, jukwaa linaloangazia taarifa zinazoendana na utamaduni wa Hip Hop kutoka Afrika Mashariki. Leo tumepata fursa ya kuweza kupiga gumzo na kaka yetu kwenye utamaduni. Kaka Mantik Barz ili tuweze kufahamu harakati zake, shughuli zake na mchango wake kwenye utamaduni huu wa Hip Hop.

Taarifa: Kama ungependa kuskia Podcast ya gumzo hili nenda moja kwa moja hadi mwishoni mwa makala haya.

Kwanza kabisa tuanze kwa kukufahamu jina lako rasmi.

Aah jina langu kamili ninaitwa Jerry Leobenus Muganda. Hilo ndilo jina halisi linalopatikana kwenye kitambulisho cha taifa na vyeti.

Mantiki Barz unatokea wapi na unapatika wapi kwa sasa?

Aah mimi ninatokea Dar es Salaam ndiyo mji ambao nimekulia ijapokuwa sikuzaliwa Dar es Salaam ila nimekulia Dar na nimeisha huku kwa muda mrefu. Sasa hivi pia napatikana Dar Wilaya ya Ilala katika kata ya Pugu. Hapo ndipo ninapopatikana kwa sasa.

Tueleze kidogo kuhusu historia yako ya muziki ulivyoanza hadi ulipo fika kwa sasa.

Kwa kweli katika muziki mimi binafsi nilianza kama shabiki, yaani, ni mtu ambaye anapenda kuskiliza muziki wa aina zote. Maeneo ambayo tulikuwa tunaishi kulikuwa kuna muziki. Nyumbani hata mama alikuwa anapenda muziki. Nakumbuka siku za nyuma kidogo tulikuwa tunakwenda mpaka kuwatazama wale DDC Milimani Park Ochestra Kariakoo pale na mama. So nyumbani watu walikuwa wanapenda muziki. Mimi hata baba yangu pia alikuwa mtu anayependa muziki sana. Alikuwa na kanda nyingi pale, vilikuwepo vitu vingi ambavyo vilikuwa vinashawishi mtu kusikia muziki kama ma radio, maspika makubwa mzee alikuwa navyo.

Kwa hiyo tuliiishi hivyo. Muziki ulikuwa sehemu kubwa ya maisha yetu ya kila siku. Kwa hiyo mimi nilianza kuwa shabiki baadaye, nikaja nikajigundua kuwa nina uwezo wa kufuatisha nyimbo. Watu kama akina Juma Nature kipindi wana rap, wakina Solo Thang lakini kubwa zaidi alikuwepo mtu mmoja mtaani kwetu ninapoishi Mbagala, mtu wa Sapatapa. Sapatapa alikuwa anakaa mtaani kwetu na ni mmoja kati watu wa mwanzo kabisa kuwahi kurekodi. Kwa hio tulikuwa tukipita kama watoto wao walikuwa wakubwa tunawaona wanafanya michano akiwa na washikaji zake.

Kwa hiyo pale nikapenda kuwa kama mshikaji lakini kutokana na harakati za shule na nini nilichelewa kidogo. Wakini ulikuwa ukishika daftari langu nyuma lazima ukute michano, mtu ameandikaandika nyimbo na vitu kama hivyo. Kwa hiyo ilikuwa lazima utanikuta katika mazingira hayo ya kimuziki. Baada ya hapo sasa kufikia kidato cha pili, nikaanza kuandika. Halafu nikawa sasa natukuma kuandika nyimbo za shule kama kuna graduation tunabadilisha nyimbo ambazo zina fahamika zile za bongo flava ambazo zinafahamika mimi nitie maneno ambayo ni maudhui ya kuwaaga watu na ikawa hivyo na nafanya vizuri watu wanapongeza na kufika miaka 2010 – 2011 nikawa naskiliza sana watu wa Tamaduni Muzik na pale nikajifunza skills za ku rap lakini nikajifunza namna ya ufanyaji biashara hiyo ya muziki kupitia rap nikaanza kuandika.

Kwa mara ya kwanza nilianza kurekodi mwaka 2014 lakini mpaka sasa hivi nishafanya kazi nyingi na hapa nilipotokea mpaka nilipo fikia.

Mimi binafsi nimeanza kukufahamu kama Mantik Barz ila baadae nilipopata miradi ya DDC (Dom Down Click) kama vile Fasihi Simulizi niliskia ngoma ya jamaa anaeitwa Logic, nika connect ni wewe. Hivi haya majina mawili yalikujaje na mbona uliamua kuacha kutumia jina Logic na kuanza kutumia jina Mantik Barz?

Aah, nakumbuka wakati nipo mwaka wa pili Chuo Kikuu Cha Dodoma, rafiki yangu mmoja anaitwa Justine Kakoko almaarufu GSP The Conscious alikuwa mchanaji mwenzangu. Lakini pia mtu wangu wa karibu na ni mtu ambaye alikuwa amenitangulia kwenye mambo ya Sanaa. Kwa hiyo kuna siku moja kulikuwa na wimbo niliufanya pale BM Records papo hapo Dodoma. Alienda akauskiliza. Akatokea kuupenda sana akaniambia, “Unajua wewe unapangilia vitu kwa mtiririko mzuri sana yani jinsi unavyo organize hayo mawazo. Yaani hayampi mtu shida kuelewa yana mantik lakini jina nikupe uitwe Logic. Logic utaligawa katiwa zile herufi manake kila herufi moja ina maanisha neno moja yaani manake Leaving On Greatness Innovations and Consciousness.”

Halafu mimi nilikuwa nachukua Shahada Ya Falsafa Na Sayansi Ya Siasa. Sasa Logic pia ilikuwa sehemu ya kozi yangu kwa hiyo ilikuwa naishi katika mazingira hayo ya falsafa na vitu vingine. Kwa hiyo kimsingi ikawa imekuwa kubwa sana katika mtindo huo na kuniwekea kwamba ina relate na yale maisha ninayoishi na kitu ninacho soma na mambo mengine yote ambayo kila siku yananifika katika maisha.

Baadaye nilikuja kuskia kwamba kuna mchanaji mmoja kutoka California anaitwa Logic. Nikamtafuta, nikaangalia kazi zake ni mchanaji mzuri na nini, sasa nikaona kwa nini hili jina la Logic nisiliwache na kisha nikamchemki Maalim Nash ambae ni mwanaharakati wa Kiswahili na alikua hapendi kuniita kwa jina na la kingereza akawa anasema, “Wee Mantiki bana, Logic, Logic nini, mbona unapenda uzungu? Wee ni Mantik…” Nikakubali na kutoka hapo nikaanza kujiita Mantiki kwasababu ilikua inabaki Kiswahili lakini pia hakuna mfanano tena na lile jina la Logic.

Kwa hivyo hapo ndio majina yalipo toka lakini ni vitu ambavyo vina maana sawa ila ni swala la lugha. Logic na Mantik ni yule yule na vitu vilivyo nifanya niwe hivyo na ndio naendelea kuviwasilisha mpaka leo.

Mpaka sasa una miradi mingapi kaka Mantiki na inaitwaje na ilitoka lini?

Miradi yangu ambayo ipo official kabisa ni mitano;

  1. Tii Misingi Bila Shuruti (TMBS) – Album – 2017 – Ilifanyika chini ya studio ya 255 ya Ngwesa, Dar es Salaam, Kijitho Nyama
  2. Jifunze Kutoka Kwa Mzee Baba – EP – Ilikua na nyimbo tano
  3. 21st Of November – EP – ilikua na nyimbo takriban 4

2018 kidogo nilikua kwenye mapumziko

  1. Shahada Ya Mtaa – Album - 2019 – Moja kati ya album nzuri sana kuwai kufanyika
  2. Uzito Wa Juu – Album – 2021. Hii ilikua album kama zilivyokua Shahada Ya Mtaa na TMBS.

Kwa hiyo jumla nina miradi mitano.

Shahada Ya Mtaa ulikua mradi classic sana. Ni mmoja ya miradi iliyonipa hamasa ya kuanzisha tovuti ya Micshariki Africa ambayo hapo awali ilikua inaitwa Hip Hop Africa Mashariki. Tueleze kidogo kuhusu mradi huu, kwanini uliamua kuunda, kwanini uliuita Shahada Ya Mtaa na mbona kwa upande wangu naona unulikua mradi personal sana kwani mambo mengi uliyo yaongelea kwenye nyimbo kadhaa ni vitu ambavyo wewe binafsi ulipitia?

Aaah kwanza asante sana sana kama ni kweli, Shahada Ya Mtaa ilikuwa kati ya moja ya album kali za muda wote ambazo hata na wewe pia ili weza kukushawishi kuwasilisha kitu hichi ambacho unafanya sasa hivi. Asante sana, nashkuru na inanipa nguvu hiyo.

Lakini ukweli ni kwamba Shahada Ya Mtaa unaweza ukahisi kwamba mimi nimejizungumzia mwenyewe lakini nimereflect mambo ambayo yanawagusa watu wengi sana, yani kinacho nikuta mimi pengine kinamkuta na mtu mwingine. Na si pengine, hebu jaribu kufanya research. Mfano haya malalamiko ya ubovu wa mfumo wa elimu ya Tanzanai yameathiri watu wengi sana sio mimi peke yangu. Kwa hiyo mimi kama kioo naonekana kama njia ya watu wengine waweze kujithathmini na kujitafuta hapo. Imekuwa hivyo kwasababu watu wengi wanakumbwa na hayo lakini wengine sio wachanaji, sio wasanii, yaani hawana namna nyingine yakuwasilisha hizo kero zao au halisi iliyokuwepo au kusema sasa tunachukua hatua hii kulingana na hiki na hiki wakaskika. Wanaweza wakawa wamechukua hatua zao pembeni huko walipo kwasababu si wasanii, sio watu ambao wana platform wanaweza wakaskika kama mimi kama mnavyoweza kuniskia na ndio maana unakuta ni nguma kujua kwamba hawa watu ni wengi kiaski hiki au hivi vitu alijizungumzia mwenyewe.

Vitu vingi sana huwa watu wanafanya au wachanaji wakichana  wanachana kutokana na hisia zao. Yaani huwezi kuchukua hisia za mtu mwingine lakini kama kitu ni cha ukweli na kina exist kwa upana automatically kitawagusa tu watu wengi.. Kwa hiyo sio kuwa mimi binafsi nimepitia, wamepitia watu weni hivyo vitu lakini mimi tu nimekua speaker wao.

Kwa ajili ya kukagua ya kukagua mradi wako mpya Uzito Wa Juu. Tueleze kidogo kuhusu mradi huu; mradi ulitoka lini (tarehe, mwezi mwaka), pia mradi huu ni nani walihusika kama ma producer ua waunda midundo, na mixing alifanya nani? Mbona nna chemistry nzuri sana na De La Funky na Abby MP?

Mradi huu ulitoka tarehe 05.02.2021. Ulifanyika chini ya maproducer wawili; Abby MP na De La Funky katika upande wa beats lakini katika mixing and mastering amefanya Abby MP. Studio ni Digg Down Records, Sinza Da es Salaam.

Huu mradi nilifanya kwanza wimbo wa Uzito Wa Juu. Ila huu wimbo niliweza kuu break nakuona kwamba kila kinachokuja hapo ni heavy. Yaani kwamba kila mada iliyozungumzwa katika kila wimbo ilikuwa na hoja za msingi. Ilikuwa si rahisi kila mtu kufanya ngoma zenye mada ya namna hiyo. Kwa hiyo mwisho wa siku kwa ujumla wake nyimbo zote hizo ni mambo ya kiufundi. Wale jamaa wanajielewa wanajua kupiga muziki wa Hip Hop na wanapenda muziki wa Hip Hop.

Kwa hiyo chemistry inakuja pale unakuta mimi niko real kwenye Hip Hop na wao wapo real sana katika upigaji wa midundo ya Hip Hop. Wao wenyewe wale ni wana Hip Hop sio kwamba mtu anakuja kukupigia mdundo kwasababu anajua ku cheza na vyombo, hapana. Wale wenyewe wanaishi Hip Hop, wanajua ladha za Hip Hop.. Wanakuwa wanaweka akili yao, moyo wao, katika kila wanachokifanya. Ndiyo maana mimi na wao tunakuwa tunashikana sana. Lakini licha ya hivyo pia ni maelewano, unawaelewa na mimi nakuwa muelewa kwao. Kwa hiyo nje ya music production, tuna ushkaji mwingine pia. Kimsingi tunajadili vitu vingine. Maisha na kadhalika. Na ndio sababu hiyo tukifanya kazi inakua poa sana.

Tutarajie nini kutoka kwako hivi karibuni?

Najiandaa kufanya album tatu. Hazitotoka kwa mda mmoja lakini nitazirekodi zote nitaachia moja. Nitaipa gap, nitaachia nyingine, nitaipa gap nitaachia nyingine kwasababu huu mda wa hapa katikati vitu vingine natakiwa kufanya. Kwa hiyo nitastop kidogo masuala ya muziki kwa maana ya kuandika na kupata muda wa kurekodi. Lakini vitu vingine tutakuwa tunafanya kwa hiyo hilo ndilo kubwa zaidi.

Mantiki najua wewe pia ni muhitimu na una shahada ya chuo. Umesomea chuo gani na umehitimu na shahada la somo gani? Mbona uliamua kuendelea na muziki na wewe ni msomi ilhali wanadai kua muziki wa Hip Hop ni wa kihuni? Wewe ni muhuni pia? Unalizungumziaje hili swala la watu kusema kua Hip Hop ni uhuni?

Binafsi naweza nikasema kwamba mimi ni muhitimu wa Shahada Ya Falsafa Na Sayansi Ya Siasa, chuo kikuu cha Dodoma na nilihitimu 2016. Kuhusu kwamba kwanini niliamua kuendelea na muziki na mimi ni msomi? Muziki ni maisha yangu ya kila siku. Yaani pengine hakuna huo usomi unaouzungumzia bila muziki wangu na huwezi amini ile kozi nilio soma inanisaidia sana katika muziki au huu utamaduni wa Hip Hop kwasababu ukisoma falsafa unakuwa mzuri sana katika research. Lakini pia ukisoma political science unakuwa deep katika mambo mengi ya kisiasa ambayo kila siku yakitokea na sisi pia tunatakiwa ku ya address kwasababu siasa ni mambo yetu ya kila siku na human being ndio political animal yaani ndio binadamu pekee ambae anafanya siasa.

Bado naitumia elimu yangu ya darasani ya mambo ya chuo katika ishu za muziki. Lakini pia mambo ya social interractions ukiyasoma unajua vizuri jinsi ya kukutana na watu na kuweza kuchangamana nao. Kufanya biashara ya muziki. Sometimes mtu anaweza akakucheki hapa akakwambia bana mimi nina alfu tatu nataka album ilhali album nauza alfu kumi. Hapo inahitaji busara kidogo katika namna unaweza kumjibu ili usiweze kupoteza wateja. Japokuwa jamaa ana pesa kidogo lakini kweli ni kuwa ni muziki wangu anauskiliza. Kuna namna lazima umtreat ili uweze kumbakisha hata siku akija kuwa na hela nyingi hawezi kununua kazi zako.

Kwa hiyo nikisema labda watu wanategemea naenda kufanya white collar jobs, hizo nilifanya ila nikaona kwamba mtu hawezi kua tajiri kwa kutumiza ndoto za mtu mwingine aliekuajiri. Ila unaenda kutimiza ndoto zake. Halafu mimi spendi sana kujielezea elezea sana kwa mtu eti imefika asubuhu aniulize kwanini hiki, sasa hivi na nini. Mimi napenda sana kuwa huru na uhuru ndiyo umenifanya mimi ku deal sana na mambo yangu kuliko kutafutia wengine ndoto zao. Kuzifikia kwa kunitumia mimi kama daraja la mafanikio yao, kwa malipo kidogo ambapo mengi huingia kwa nauli na chakula. Kwa hiyo sikuona kama itakuwa sawa.

Kuhusu kwamba usomi, ki ukweli ni kwamba mimi sio msomi mimi ni muhitimu. Bado sijafanya tafiti zile wanazofanya wale ma PhD holders na watu wengine wanaofanya tafiti kubwa kubwa ambazo zimeleta matokeo chanya katika jamii zao.

Na suala la kusema Hip Hop ni uhuni, binafsi mimi sio muhuni, kabisa si muhuni. Na uhuni ni tabia ya mtu binafsi na haihusiani na Hip Hop. Hip Hop ni Hip Hop na uhuni ni uhuni, ila mtu anaweza akawa yuko katika utamaduni wa Hip Hop lakini yeye muhuni lakini hiyo isiutukanishe utamaduni wote. Asemekani kwamba mtu flani yeye ni muhuni, lakini sio kusema kwamba yule mwana Hip Hop ni muhuni. Hapo utautukanisha utamaduni bila sababu za msingi. Kwasababu kuna mtu mwingine utamkuta ana tabia hizo hizo ambazo tunazisema kua huyo mtu ni muhuni lakini hata hajui hata Hip Hop ni nini wala hajawai kujishughulisha nayo na chochote. Kwa hiyo tu ni tabia ya mtu kwahiyo tujifunze tu kutofautisha kati ya Hip Hop na tabia binafsi za mtu.

Changamoto unazo kabiliana nazo kwenye hizi shughuli zako za muziki ni zipi?

Changamoto kubwa ninazopitia katika shughuli zangu za muziki ni ufinyu wa muda. Kwa kweli na kosa muda wa kutosha kutokana na majukumu mengine ya kifamilia na majukumu mingine. Mii siangaliagi sijui huyu hapigi muziki sijui nini, mimi ndio maana sipelekagi muziki huko. Kitu kingine ambacho naweza kukiona kama changamoto ni kuchukulia poa mambo ambayo watu tuna invest time na gharama nyingi kuyafanya hivi ambavyo wao wanayaona waokuyabeba kwa wepesi. Mtu anaweza kuja anataka album kwa shillingi alfu tatu bila kujua imegharamiwa vipi hadi kufiki ilipo fika.

Je umepata manufaa gani tangu uanze muziki?

Manufaa ni mengi, fedha lakini pia nimeweza kutengeneza mtaji wa watu yaani social capital. Nina watu wengi ambao tunaweza tukasaidia katika ishu zingine za kimaisha tofauti na maswala ya muziki. Lakini manufaa mingine nadhani ni urathi. Sahii unaweza ukakutana na kijana anaechana akakwambia mimi namkubali Mantik Barz ndio akafanya nipende kuchana. Kwahiyo urathi huo tuliouacha pia ni manufaa lakini katika mauzo Allahamdhulilai si haba tunauza. Kila siku mimi nauza, kutoka hizo kazi za 2017 mpaka kesho mtu akija anaweza akakucheki. Na kila siku tunaongeza watu wapya lakini kikubwa pia ni heshima. Unakutana na watu wanakuthamini wanatupa heshima sana. Haya ndio manufaa makubwa zaidi.

Tuelezee kidogo kuhusu kundi lenu Ngome Ya Chuma.

Ngome Ya Chuma sio kundi, ila ulikua wimbo ambao tulifanya mimi, Fivara na Rabi James lakini tuliona baadae kama ule umoja wa watu watatu tunaweza tukafanya miradi mingi sana japokua kuna changamoto ya muda na umbali wa watu kukaa maana Fivara nae yuko Mwanza, Rabi na mimi tupo Dar kwa hiyo kidogo ikawa imeshindikana lakini sio kundi. Yaani huwezi kusema kwamba ni kundi la wachanaji ila ilikua ni wimbo ambao tulikua tunaamanisha tu kwamba Hip Hop na vitu kama hivyo.

Athari za Hip Hop kwa lugha ya Kiswahili ni Hip Hop. Je Hip Hop kwa Kiswahili inakuza lugha au inaharibu lugha?

Athari za utamaduni wa Hip Hop kwenye upande wa Kiswahili zipo katika pande mbili. Kuna athari ambazo ni chanya lakini kuna zingine sio chanya lakini katika maswala mazima ya kukuza au kudidimiza lugha kwa wale ambao wana skiliza hizi Hip Hop ambazo ni za wale watu ambao ni wenyewe kabisa wana Hip Hop kwa kweli inakuza. Wengi wetu ambao tunafanya muziki huu tunatumia Kiswahili fasaha ambao sisi ndio tuko upande ule ambao tunatakiwa. Tunatumia Kiswahili fasaha kwa maana inawafikia watu wengi na tunaweza kutumia misaimiati mingi ya lugha ya Kiswahili. 

Lakini kuna upande mwingine watu wanatumia lugha wanayo iita Swanglish, sijui Kiswahili kilichochanganywa na Kingereza na kiukweli hio ndio athari ambayo inakua ni hasi inamaana Kiswahili kinakua hakiendi mbele.

Lakini leo hii ukinikuta mtu kama mimi ninavyo rap au Maalim Nash amefika mpaka Ujerumani ana rap katika lugha ya Kiswahili unaona kabisa lugha inafika mbali na watu wanapenda kujifunza na kiukweli hata kuna dada ambae nishawai kuwasiliana nae yuko nchini Marekani aliwai kuniambia mimi napenda sana hiyo lugha unayotumia katika kuchana. Siielewi lakini najikuta ninaipende kwasababu ina rhythm nzuri sana. Na Kiswahili kwa kweli katika uchanaji au hata katika kuimba kinaskika vizuri sana, kina mtiririko mzuri kwa hivyo kinapelekea kukua kwa lugha ya Kiswahili, vizuri kabisa kwa wale ambao wanatumia vizuri. Kwahiyo hata mimi nawasihi wengi waendelee kutumia Kiswahili katika mashairi yao kwani tunaweza tukapata vitu vingi sana kupitia lugha hiyo na tunaweza tukawaunganisha watu wengi zaidi hasa hapa East Africa, Kiswahili kinazungumzwa sana, barani Africa kinazungumzwa hata Ulaya kwenye baadhi ya nchi.

Kwahiyo waeza ukafanya kitu kikaonekana bado sio kigeni kwasababu hata Kiingereza chenyewe sisi hatukijui vizuri basi tu rap katika hii lugha ambayo tunaijua vizuri maana tutawakilisha mada zetu kwa ufasaha zaidi.

Ni kipi ambacho sijakuuliza ambacho ungependa kutuambia? Pia unapatika wapi kwenye mitandao ya kijamii?

Kitu ambacho haujaniuliza ni labda kwamba kwanini sipendi sana kufanya mahojiano, kwanini hua nafanya mahojiano na kituo kimoja tu cha radio ambacho ni EFM katika kipindi cha Jabir Saleh. Kiukweli ni kwamba tunakosa watu wakufanya mahojiano ya Hip Hop kwasababu wao kwanza sio sehemu ya utamaduni, hawajui nini wanatakiwa kufanya katika kumhoji mtu wa utamadhuni huo alafu wanashindwa kufanya research walao ndogo kulingana na utamaduni na huyo mtu wanae enda kumhoji anaejihusisha na utamaduni huo.

Yaani kwa mfano unaweza kwenda katika kituo kimoja cha radio ukashangaa mtangazaji anakuomba umuandikie maswali, si vibaya lakini inasikitisha kwasababu unategemea yule mtua anaekuja kufanya kitu na wewe yani ana uelewa kidogo kuhusiana na kitu ambacho unajishughulisha nacho. Kusema wewe umuandikie maswali maanake hakujiandaa na wewe maanake wewe ni kama unaenda kujiuliza mwenyewe na kujijibu mwenyewe. Kwa hiyo kidogo nadhani hilo ndio haukuniuliza kwanini mimi sifanyi mahojiano sana, yaani nafanya mahojiano mara moja tu kwa mwaka. Kama mwaka huu sijafanya kabisa mahojiano na haya kwa mwaka huu yatakua pengine mpaka nitoe mradi kwani mimi sio mimi sio mpenzi wakuenda tu kwa vituo na kuzungumza zungumza tu hata kama sina kitu cha kuzungumza.

Mitandao yangu ya kijamii

Instagram: mantikibarz_
Facebook: Mantik Barz
WhatsApp: +255 0685 878 289

Shukran sana Mantiki Barz tumejifunza mengi na natumai wasomaji na waskilizaji wetu watapata madini kutoka kwa gumzo letu. Shukran sana hadi hapo tutakapo kutana tena, asanteni.