Mchoraji Yohan Mudibo akiwa ofisini kwake.

Yonah Mudibo ni mchoraji ambae nilitambulishwa kwake kwakupitia kazi yake moja aliofanya kwenye albam ya Fikrah Teule iitwayo  Azania Na Wanawe. Maongezi  yetu yalifanyika kwa njia za kisasa, WhatsApp, kulingana na umbali uliopo kati yetu.

Yonah Wanjala Mudio ambae ni mshindi wa tuzo za sanaa za Sondeka Awards ni mzaliwa toka Mombasa, Kenya anaeongelea hivi sanaa yake, “Mimi ni msanii mzuri ninayetumia njia mbali mbali kuelezea sanaa yangu. Hizi ni pamoja na uchoraji wa mafuta, rangi ya maji, kuchora penseli, sanaa ya mwili, sanaa ya kamba, kati ya zingine. Ninazingatia sanaa ya kamba kwa sasa, na kazi zangu zimejikita katika hadithi ambazo zimeelezea historia ya watu weusi na zile ambazo zimeathiri jamii. Baadhi ya kazi zilizokamilishwa ni pamoja na zile za Fela Kuti na Nina Simone, na zingine zikiendelea.”

Sanaa ya Yohan imepata fursa kuonekana na wenyeji wa Mombasa pale soko la Markititi, maeneo ya kitu cha reli cha Mombasa na pia kwenye barabara kuu za mji huo. Kwa sasa Mudibo anapatika studio za BelaBela kule Bamburi Mombasa akiendeleza harakazi zake za sanaa. Ni furaha yangu kumshirikisha katika mahojiano haya ambayo ni sehemu ya safu tuliyoipa jina “Sanaa na Hip Hop.”

Historia yako ni ipi? Jina na unajishughulisha na nini kimaisha?

Mimi ni mzaliwa wa Mombasa, Kenya ila nimekaa maeneo tofauti tofauti nchi Kenya. Kando na usanii wa uchoraji, upakaji rangi na kuunda vifaa, body art(uchoraji mwili) na string art mimi pia ni seremala baada ya kuanza kujifunza majuzi wakati dunia ikipia janga la Corona.

Kazi tofauti za Yonah Mudibo

[Click image to enlarge]

Niambie kidogo kuhusu Yonah, umetokea wapi, ulikulia wapi and utoto wako ulikuaje, umesomea wapi?

Nilianza shule mbili tofauti za msingi kule Mombasa; St. Lwanga Magongo pamoja na Mikindani Primary kabla ya kuhitumu na kwenda  shule ya upili St. Peter’s Mumias Boys kule Mumias. Nimemhitimu toka chuo kikuu cha Technical University Mombasa nilipo somea kua mwalimu wa Kingereza na Fasihi.

Utoto wangu ulikua mzuri maana nilikua na vipaji vingi tofauti kama kucheza mpira wa miguu,kucheza mpira wa mikono pamoja na mpira wa kikapu, mpira wa magongo(hockey)na michezo mingine tofauti ilhali kimasomo pia nilijitahidi. Pia nilipata fursa ya kucheza mpira wa kulipwa! Mitaa ya Mikinda na Jomvu ndio ilinikuza na ndio iliyonifanya nijitambue sana sana kupitia marafiki zangu walio kua na ushawishi chanya maishani mwangu.

Mbona uliamua kua mchoraji?

Mie nimezaliwa kwenye familia ambayo uchoraji ni kitu cha kawaida nanilikua napenda kuchora nikiwa mtoto. Kando na baba yangu, binamu zangu, wajomba zangu pamoja na shangazi zangu walikua wachoraji. Baba yangu alianza kunichorea vitu tofauti ambavyo nilijitahidi kuvichora pia. Pia nikiwa darasani nilijikuta nikishindana na marafiki zangu kuchora watua au mwalimu wetu hadi kipaji change kikakua na kuniwezesha kushinda tuzo kadhaa.

Kwenye shughuli hii ya uchoraji ni mtindo gani uliokuvutia sana?

Kwasasa nimejikita kwenye mtindo wa uchoraji wa String Art (uchoraji wa kutumia uzi na misumari) kwasababu hii mitindo mingine kaka uchoraji wa kutumia penseli pamoja na rangi na vinafanywa na watu wengi na mie nilitaka niwe tofauti na wakipekee na watu wengi wanahifahamu kwa hili.

Mchoro wa hayati mshindi wa tuzo la Nobel Professor Wangari Maathai

Kazi yako hunuia kusema nini?

Kazi yangu inahamisha mtu mweusi kujikubali na kujithamini kwani uwezo anao wakufanya jambo na likafanikiwa. Kwenye kazi zangu yangu ya sting art hua napenda kuenzi watu wanaojulikana kwasababu moja au nyingine au ambao pia wamesahaulika kama vile Fela Kuti, Nina Simone, Anas Aremeyaw Anas, Lucky Dube pamoja na Wangari Maathai. Hawa ni watu ambao wametuonesha njia yakufuata kama waafrika ili tuweze kusonga mbele bila husahau tamaduni zetu.

Mchoro wa hayati Luck Dube. Umechorwa kwa kutumia kamba na misumari.

Kazi yako inatoa maoni gani juu ya maswala ya sasa ya kijamii au kisiasa?

Kazi yangu sanasana huongelea kuhusu maendelea kisiasa na kimawazo na pia kujitambua tunapotokea kihistoria, tamaduni zetu chanya na shule zetu asili ambazo kama tungezifuata hakungekuwa na haja na kufuata mila za wageni pamoja na mifumo yao ya masomo.

Je ni nani alikuvutia pa kubwa ki uchoraji na kukupa hamasa ya uchoraji? Pia ni nini hukupa hamasa na motisha ya kuchora?

Baba yangu Anthony Mudibo ndie alienivutia sana kua mchoraji japo kua hakua mtaalamu wa uchoraji. Alikua mwalimu alienifundisha kuchoraji kwa kutumia penseli toka nikiwa mdogo. Kinacho nipatia motisha ya kuchora ni kua naweza kutumia kipaji changu kutoa ujumbe kuhamasisha watu kujikubali, wapendane wawe na umoja ila wasijisahau kama waafrika.

Umekuzaje kipaji hiki hadi vile kimekupa ajira?

Nikiwa mdogo nilikua na chora sana na nilipotaka kuingia shule ya upili niliomba kupelekwa kwenye shule ambayo inamasomo ya uchoraji na uundaji vitu na ndio maaana nikaenda St. Peter’s Mumias Boys. Pia nikajiendeleza zaidi baada ya kumaliza shule ya upili kabla ya kukutana na wachoraji wengine walioniongezea ujuzi wa ziada kama vile Robert(Bob) alienifundisha kuchora rangi za mafuta na hapo nikaanza kuuza kazi zangu. Pia nikaanza uchoraji wa mwili pamoja na string art na kujaribu kubuni vitu tofauti tofauti. Siri ya msanii ni kujaribu(kitu kipya) kila wakati ili kuweza kunufaika na sanaa hii.

Je unatafutaje fursa za kazi?

Mie hupatika kwenye studio za BelaBela kule Bamburi ambayo ina wasanii tofauti ambao wanajulikana katika nyanja tofauti na kwakupitia mahusiano yetu ya kikazi ndipo wateja wetu hupatikana. Wateja wangu pia hunisaidia kutangazana bidhaa zangu sawia na mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Instagram. Pia nauza kazi zangu kwa gallery au nyumba za sanaa

Kazi zako kupatikana kwa bei gani?

Kazi za uchoraji mwili zinaweza kugharimu kati ya Kes 500 hadi Kes 2000 kulingana na ugumu wa kazi yenyewe ilhali kwa kazi ya string art inagharimu kimo cha chini sana cha Kes  50000 ilhali picha za mchoro zinategemea ukubwa na maelezo ya mchoro na ugharimu kati ya Kes 1500 hadi Kes 2000, ila ikiwa zaidi itapendeza sana!

Ilikuaje ukafanya kazi na mwana hip hop Fikrah Teule?

Tumefahamiana na Fikrah Teule toka zamani baada ya kukutana nae Alliance Francais Mombasa kwa mara ya kwanza. Tuliendana nae kimawazo na hivyo basi ikawa rahisi kufanya nae kazi.

Mchoro wa jalada la albam ya Azania Na Wanawe wa emcee Fikrah Teule

Mchoro wa jalada la albam la Azania Na Wanawe uliliundaje? Ulipataje wazo kutoka mwanzo hadi mchoro kukamilika? Shughuli hii ili kuchukua mda kiasi gani?

Niliuunda baada ya maongezi yangu na Fikrah ambapo aliniambia alitaka kukumbushia tamaduni zetu ikiwepo tamaduni ya kusimulia hadithi na ndio maana niliamua kumchora bibi akiwahadithia wajukuu wake. Pia kwa mchoro hua kuna vitu flani nilivyo vificha ambavyo mnatakiwa mvigundue nyie wenyewe!

Kando na kazi hii ya FT je ulishawai kumchorea msanii mwingine yoyote jalada la albamu?

Nimeshafanya kazi pia na muimbaji Larota Africa toka Mombasa. Nilimfanyia kazi ya body art au mchoro wa mwili kwa ajili ya jalada la albamu yake iitwayo Rhythm of Love.

Mchoro wa mwili uliotumika kwenye jalada la albam ya Larota Africa

[Click image to enlarge]

Wewe huskia mziki unapochora ? Hua unapenda kuskia nini kama jibu la la swali la kwanza ni ndio?

Ndio, mie hupenda kuskiza mziki ninapo chora na mziki hunipa motisha na huamsha ubunifu wangu. Mie huskia mziki wa Lingala, Bongo Flava, Hip Hop kiujumla, miziki ya wa Sauzi pamoja na miziki toka nchi ya Nigeria na Rock vilevile. Mie huskia chochote kilicho undwa kwa ubunifu.

Siku yako huanzaje?

Siku yangu japo kua sio kila siku huanza na mazoezi saa kumi na moja unusu hadi kumi na mbili unusu asubuhi kabla ya kuoga kujiandaa kwa ajili ya siku yangu. Kisha huelekea studio zetu za BelaBela na kuzifungua saa mbili. Kisha umalizia kazi yoyote ambayo ni kiporo au kaunza kazi mpya.

Wewe unapenda nini sana kuhusu kua mchoraji ?

Ninachopenda kuhusu kua mchoraji ni kua siku yangu inaweza kuanzia popote na kumalizika popote. Fani hii inaweza nipeleka safari ya kwenda hata Nairobi hata kama sikuwa na mpango au taarifa kuhusu safari yenyewe, siku haitabiriki. Pia uchoraji ni chemsha bongo inayo amsha ubunifu wangu nikisaka njia yakufanikisha kazi zangu zitoke vizuri zaidi.

Je kuna mchoro uliochora au ulio buni ambao unajivunia zaidi?

Mchoro wa Fela Kuti. Mchoro huu ndio ulinipa tuzo ya mchoraji bora kwenye tuzo za sanaa Sondeka Awards nchini Kenya.

Kazi ya Fela Kuti ya iliyo undwa kwa kutumia uzi na misumari.

Unavipaji gani vingine?

Mimi pia ni mshairi na seremala. Wakati huu wa Corona kazi ya useremala iliniwezesha nijikimu wakati kazi hizi zingine zilikua hazina soko.

Una ushauri gani kwa mchoraji anayeanza?

Ni muhimu kua mvumilivu na ujitahidi kujifunza kila siku na kuondoa dhana kua umekamilika. Kila mtu ni mwanafunzi na mwalimu kila wakati na kinachohitajika ni kujifunza na kufunza wenzio wakati kila wakati.

Kipi kingine ambacho ungependa kusema ambacho sikukuuliza?

Kazi yangu kubwa ambayo nilifanikiwa kuifanya hivi karibuni mwisho wa mwaka jana na mwanzo wa mwaka huu ni kua Jimbo la Mombasa lilitupa fursa wasanii kadhaa ili kuweza kupamba mji wetu wa Mombasa. Tulichora michoro kadhaa ambayo inaoneka mjini Mombasa ikiwemo michoro ya murals pamoja na graffiti. Nashkuru sana kwa serikali ya Jimbo la Mombasa kwa kutuaminikwa hili. Pia tunaomba serikali kuu ya Kenya iweze kutupatia fursa kama hizi.

Michoro ya Yonah Mudibo inapatika kwenye soko kuu la Markiti Mombasa

Mpate Yonah Mudibo kwenye mitandao ya kijamii:
Twitter: @mudiboyonah | Instagram: @yonna_mudibo_arts | Facebook: Yonah Mudibo The-artist