Albam: The Seed EP
Msanii: Mbize Poem Kid
Nyimbo: 5
Tarehe Iliyotoka: 30.01.2021
Ma Producer na wapiga midundo: Black Ninja
Studio: Boom Bap Clinic (B.B.C)
Mbegu inahitaji vitu vitano ili iweze kuota na kuchipuka kutoka ardhini ambavyo ni; maji, mwanga na madini, hewa na mda. Mbize Poem Kid ambae ni mkufunzi wa chuo kikuu cha Sokoine University of Agriculture (SUA) kama mhandisi wa Kilimo cha Umwagiliaji na Rasilimali Maji (Irrigation and Water Resources Engineering) kwa kulijua hili aliachia mradi wake rasmi wa kwanza The Seed EP.
Seed ni jina la kimombo limaanishalo mbegu. Hivyo basi Mbize akizangatia kanuni za upandaji mbegu zilizo ainishwa hapo juu ameweza kupanda mbegu ya kipaji chake na kutupa EP hii ya kwanza. Hivyo basi kama vile ukipanda mchicha unapata mchicha, Mbize kwa kupitia EP alitaka kuonyesha mashabiki wake kile anacho nuia kuwapa sasa na kule mbeleni. Hata pia ukitazama picha ya jalada ya EP hii mikono inayo toka chini ikielekea juu ikiashiria mbegu inayo pandwa chini na kuchipuka kuelekea juu na kutoa kile kile kilicho pandwa.
Georfrey Charles Malaja Mbize kama anavyo julikana rasmi msanii huyu alizaliwa miaka ya tisini kule Iyunga, Mbeya.Mbize alikulia kwenye mazingira ya ma emcee Mbeya ambao walimpa hamasa nae kujaribu kuandika mistari yake mwenyewe na kuchana na kutonaka na uwezo alioonesha kaka zake akambatiza jina la Mbize Poem Kid kuonesha kua yeye ni dogo alie na uwezo wakuandika mashairi. Pia kando na uchanaji Mbize pia ni mwanasarakasi.
Black Ninja toka B.B.C ndie alieshika doria ki midundo kwenye EP hii mwanzo mwisho na hakumuangusha Mbize kwa hili. Album hii fupi ina mbegu tano zinazo onesha vile penseli ya Mbize inauwezo wa kupanua wigo ki maudhu. Ana mistari inayo fanya utafakari kwa kina kama anavyosema,
“Huwezi amini, watu wanajinyonga kisa dini/
Hadi mpaka wachungaji hawaendi juu kisa chini/”
Kwenye Bangi na Chuo emcee huyu anatupa mitazamo miwili ya matumizi ya konde la bondeni au kama wanavyoiitwa waongea lugha ya mtaani ya sheng toka Kenya kindukulu, ngae au hata pia ndom. Ni nyimbo ambayo inamkuta Mbize anaongea ana kwa ana na bangi kama marehemu Mr. Ebbo alivyo longa na pombe. Wimbo huu umejaa mafunzo kwa wanavyuo na unapigwa kwenye mdundo mzuri sana.
Umri wa Mapenzi ni nyimbo wa ucheshi kidogo unaomkuta dogo Mbize kazama ndani ya mapenzi na mwanamke ambaye ni sawia na umri wa mamake. Black Ninja pia kaonesha kipaji chake na kumpa Poem Kid mdundo mzuka sana. Pengine kwa kutaka kutuonesha vile madogo wa siku hizi wanapenda urahisi wa maisha Mbize ana fall in love na Kikongwe kama msanii Picco enzi hizo.
Anaseme hivi Mbize,
“Mzee kijana mi namuita mama Chibu Dangote/
Kitandani anajipinda utadhani anapiga Yope/
Cha kwanza huyu mama ana hela/
Na ndio mana si mshangai kula raha na msela/
Kama kua nae kiukweli sina shaka/
Kama wazazi home mbona washanipa baraka/”
Anaendelea kwa kusema,
“Si utani, maza kanipita age flani/
Ila kusema haiwezekani ni mambo ya ki zamani/
So kinyonge alivyo, bi mdash, high class, sio Kikongwe wa Picco/”
Kweli umri namba.
Wimbo wa mwisho Abiria na Makonda unamkuta Mbize akiongelea usafiri wa uma na changamoto zake hususan kwa mtazamo wa abiria na makonda. Mbize anatupa uhalisia na hapa ndio unaona zaidi kwanini anaintwa Poem Kid. Mistari inachora picha hivi,
Mtazamo wa Abiria:
“Acha mwendo wa dereva unaeza hisi hatujali/
Tuko kwenye basi ila spidi ya Ferrari/
Nabaki kumuomba Yesu/
Sa ni vipi tumuelewe sababu safari yetu anataka kuwai yeye/”
Mtazamo wa Konda:
“Japo kuna vitu havija pigwa marufuku/
Lakini ni uzamani kwenye basi abiria eti unapanda na kuku/
Mara bata kuna mambo yana kwaza/
Unatapikia siti alafu Konda akiula ati Rambo zimekatazwa/”
The Seed EP ni mbegu ya mashairi iliochipuka na japo kua ni fupi imebeba matumaini ya Mbize na yetu kua vijavyo toka kwake vitakua vikubwa. Hata mbuyu ukianza kuchipuka huchomoza kama mchicha ila yale mahitaji tuliyo yataja awali kuwezesha mbegu yakiwepo basi ndoto iliyo bebwa na mbegu tutakuja iona. Mbize akiendelea hivi atawabadili mashabiki wake kua masela wake.
Kupata album ya hii ya The Seed EP wasiliana na Mbize Poem Kid kwenye namba ya simu/WhatsApp +255 658 525 766