Ukaguzi Wa Albam: Genetically Emancipated Musical Soul (G.E.M.S)
Msanii: MC Sharon (aka Decibelle aka Alshaverb)
Tarehe iliyotoka: 24/09/2018
Nyimbo: 20
Ma producer/Wapiga Midundo: Fred Fisher (Omnibeats LLC), Donovan Jarvis & Co (Exclusive Rap Beats, 20dollar beats (USA), Rudeboy Cabana aka Outspoken (USA), Mohjay Mohteaching (Kenya/Germany)
Mchanganya Sauti na Midudo: Michael Miheso Itebete
Studio: Alshaverb Music Group

Mc Sharon (aka Decibelle aka Alshaverb)

Japokua kihistoria mziki wa Hip Hop una mashabiki wengi, ukweli ni kuwa mashabiki wa kike asilimia yao ni ndogo ukilinganisha na mashabiki wa kiume. Hivyo hivyo kwa upande wa uchanaji ma emcee wa kike wapo ila kusema kweli ki asilimia pia ni wachache ukilinganisha na ma emcee wa kiume.

Ukija nchi zetu za Africa Mashariki ma emcee wa kike wanao fahamika idadi yao ni ndogo ila ukibahatika kuwasikia hao wachache ni jambo la kushukuru kwani unakuta ki uwezo wanajitahidi kama ma emcee wa kiume. Mmoja ya ma emcee hawa wa kike ni MC Sharon. Kitu ninachompendea MC Sharon nikua yeye anajiamini ki uwezo hadi hua hapendi kutambulika kama emcee wa kike (Femcee) bali tu kama Emcee kwani anaamini anauweza kama vile emcee yoyote yule wa kiume unae mjua.

MC Sharon ambaye alizaliwa kule Muhoroni, Kenya ana karama kibao kama vile kughani, kuimba, kundikia vitabu pamoja na kuchora pia. Yeye ni msomi mwenye shahada ya uzamili (Masters) na pia amesomea Muziki na Mawasiliano Ya Umma. Kando na hayo yote MC Sharon ni mwalimu; darasani na kwenye kinasa.

Kwa mtu ambaye alianza uimbaji kwa kuimba kwenye kwaya ndani ya kanisa la wasabato toka utotoni na pia kucheza kinanda, emcee huyu ambaye pia ni mama wa vijana wawili hadi sasa ameonesha uwezo wake wa “kuekelea kazi” kama wanavyo sema wakenya hadi kufanikiwa albam tano. Albam yake ambayo nimebahatika sana kuiskia ni Genetically Emancipated Music Soul (G.E.M.S).

Gems kwa lugha ya Kiswahili ni kito/vito au aina flani ya madini ya thamani yanayopatikana Ardhini. Hivyo basi, mradi huu una madini kibao ambayo utayapata pale utatulia na kuanza kuchimbua mistari iliyoficha madini hayo yaliyopo ndani ya ngoma ishirini.

Singo rasmi iliyobeba mradi huu ni Kutupanga ambayo mdundo wake mzuka umeundwa na Fred Fisher wa Omni Beats, LLC ni wimbo ambao unaongelea hali ya kisiasa sio tu nchini Kenya hata kwenye nchi nyingi Africa na kote duniani ambapo wanasiasa wanapoona mda wao wa kuwa ofisini unakaribia kuisha, hurudi tena na kutuhadaa na ahadi nyingi ambazo huwa wanazisahau pindi wanaposhika madaraka. MC Sharon anatema nyongo kwenye kiitikio akisema.

“Miaka mi nne zimepita umerudi tena mtaa/ (umerudi kutupanga)
Umerudi kutupanga bila haya wee mang’aa/ (Tunacheki tuko rada)
Kutubeba kama mafala kila masaa/ (That same propaganda)
Sasa mbaya jiwekee roundi hii tumesema zii/(Hatubebi mapanga)…”

Kisha Sharon anawachapa wanasiasa viboko vya mistari ambavyo vinawaacha na makovu kibao.

MC Sharon ambaye pia anajulikana kama Decibelle au pia ukipenda Alshaverb ana uwezo wa kuchukua mada yoyote iwe ngumu vipi na kuichana kwa urahisi sana bila ya kupoteza maana. Kwa mfano kwenye nyimbo kama Finish Line na Kipaji Na Kipanga ambapo anaongelea vile maisha yake yalibadilishwa na kinasa. Mziki ndio ulimuwezesha yeye kuwa yeye na kujitambua. Kwenye Kipaji Na Kipaza kama vile Common kwenye I used to Love her anakiri mapenzi yake ya dhati kwa Mic toka jadi na jadi.

Kwa wale ambao hawamfahamu MC Sharon, da’ kaamua kukurudisha nyuma na kukueleza alipotokea hadi kuwa emcee aliye sasa kwenye wimbo wake 33. Wimbo huu mzuka sana ulioundwa ki boombap na Rudeboy Cabana aka Outspoken Beats pia unaonesha uwezo wa Sharon kutema kwa  lugha mbili; king’eng’e kwenye beti ya kwanza na Kiswahili kwa beti ya pili. Kwenye beti ya pili pia anaonesha vile mkongwe wa Hip Hop Wodhes alicheza sehemu kubwa kumuwezesha yeye kukuza kipaji chake akisema,

“Three suspensions followed by an expulsion/
Toka Alliance kajipata kule Tala na kina Wodhes/
Kidogo kidogo nikaanza chunga beti akigonga judo watu design ya drumset/
Jam sessions kila Jumapili ya likizo hapo F2 na NYNY/
Nisingekosa micharazo juu ya beat za magwiji kama Prodigy/
Quiet Storm ni kama ni Havoc ya maklasiki/
Black Pope, Wu-Tang, Big Pun bado mi shabiki/…”

Mada nyingine nzito ambazo MC Sharon amegusia ni kama changamoto wanazopitia dada zetu wanapokwenda kufanya kazi ughaibuni kwenye Take Me Home ambapo anaonesha uwezo wake wa kuimba na kughani kwa wakati mmoja kama Ms. Lauryn Hill kwenye wimbo wenye hisia kali sana pamoja na mada ya msongo wa mawazo(depression) kwenye wimbo mzuka sana Juu On Top akiwa na CLD. Kwenye wimbo huu ambao CLD anatubariki na sauti yake nzuri, kuna gita linapiga tofauti sana kwenye mdundo wa Five Star Beats LLC anapomwaga hisia Mc Sharon.

Uhodari wa Sharon wa kuweza kughani unaoneshwa kwa njia tofauti tofauti kama vile kughani ki lugha kwenye ngoma Wang’e Tek ambapo anachana kwa lugha ya Luo pamoja na uwezo wa kuua freshi kwenye mdundo wowote akitema nondo kwende midundo ya Reggae ambao ni mziki anaoupenda kufanya kama vile kwenye Som A Dem na Serious Times.

Mim binafsi ninapenda anavyo pita na midundo ya ki Boombap kama tunavyoona kwenye Nairobi Block ambapo anaiwakilisha mitaa yake kwenye mdundo mzuka sana pamoja na kwenye Inaweza pamoja na Collect akiwa na 6ix Foot kwenye mdundo wa OneTone ambaye yupo America.

Mapenzi kwako binafsi na kwa mpenzi wako ni mada zimeguswa ki ustadi sana na Sharon. Sharon kwenye wimbo Black Pride akiwa na Kev Mamba anawakumbusha dada zetu kuthamini ngozi yetu nyeusi. Kev Mamba naye analeta mtazamo wa mwanaume kwenye mada hii. Mapenzi kati ya wawili yanaimbwa freshi kwenye wimbo chanya ambapo MC Sharon na Kash Grindhauz kama wapenzi wanabadilishana kinasa vizuri sana kwenye Leo Loving ambao ni wimbo danceable sana na umeundwa ki HipHop Funk hivi.

Baraka moja nyingine inayopatikana kwenye mradi huu ni pale tunaona uwezo wa Sharon kama mama alivyokuza kipaji cha dogo lake Jabali Tulani wanapo shirikiana kwenye wimbo flani freshi wa kula bata Muziki Bien(Tufurahi).Nimefurahi mimi binafsi nikiona ma Sharon akikuza vizuri kizazi cha ma emcee pia kwani uandishi wa dogo na uchanaji uko vizuri pia ukilinganisha na umri wake.

Mradi huu pia uliwashirikisha ma emcee wageni kama vile Trabolee kwenye I Keep My pamoja na producer Hiram Kimani kwenye Not At All na wote waalitika vilivyo wito walioitiwa kutimiza kwenye mradi huu.

Mradi huu kusema kweli ni madini kiutunzi , kimashairi, ki mdundo, ki mada, ki quality ya production na pia ki mziki kwa ujumla. Binafsi naweza sema kwamba kama huu ni mradi wa tano wa mwanamama huyu na bado upo juu kama alivyo anza kuskika, basi game la Hip Hop Kenya na Africa Mashariki ki ujumla lipo kwenye mikono mizuri kama MC Sharon ataendelea kutupatia madini kama hatochakachua uwezo wake.

Kwangu mimi Genetically Emancipated Musical Soul (G.E.M.S) ndio mpango mzima achana na madini gushi ya (Genetically Modified Organisms) GMO’s.