Uchambuzi Wa Album: The Last Will And Testament
Emcee: MC Sharon
Tarehe iliyotoka: 15.01.2022
Nyimbo: 21
Mtayarishaji Mtendaji: Sharon Alai (MC Sharon)
Mtayarishaji Mwenza, Mixing & Mastering: Michael Itebete
Studio: Alshaverb Music Group/Miheso Music

Nyimbo Nilizozipenda: Onge Wichkuot, Tangazo Maalum, Why The Caged Bird Sings, Say My Name, Kwisha, Aliwara, Otek Small, Msafiri, So Special, Calm Down, A Page A Day, Shida Iko Wapi, Usikimye

Baada ya kimya cha mda mrefu mchanaji kutoka Kenya mwenye a.k.a kama zote, Alshaverb Mama Yao, The Oracle Of Muhoroni, The Goddess Of Sound, Decibelle anae fahamika rasmi kisanii kama MC Sharon alifanikiwa kutupatia mradi wake mpya The Last Will And Testament mapema mwaka huu.

Mradi huu ambao ulianza kuundwa rasmi wakati janga la Uviko 19 akiwa amejifungia studio, umechukua muda kuandaliwa ila ninachoweza kusema kwa sasa ni kuwa subira huvuta heri kama anavyotuambia kwenye wimbo wa kwanza unaotufungulia mradi huu Sound Sage Kinda Vibe.

Kwenye mradi huu ambao MC Sharon alikuwa peke yake kwenye ngoma zote isipokua kwenye Brother’s Keeper alipowashirikisha wanawe Jabali na Sulwe emcee huyu amejaribu kututibu kwa njia tofauti kadri ya uwezo wa talanta zake ambazo zipo kibao kama a.k.a zake. Kwa kutumia mtindo unaoitwa Tema Imba ambao mimi binafsi niliufahamu kupitia mradi wa Monaja uendao kwa jina hilo hilo emcee huyu anatusafirisha kwenye dunia yake anayoishi. Mtindo huu unatumika kwa ngoma kadhaa kama vile Wozaa, Kwisha, Msafiri, World Newz, Shida Iko Wapi, Self Love pamoja na Usikimye. 

Kwenye mradi huu emcee huyu anaonesha ubaya wake kimada na kiuchanaji kwenye ngoma kadhaa kama vile kwenye Tangazo akitangaza uwezo wake wa uchanaji, uimbaji wake na ujio wake mpya akisema,

“SI Unit Alshaverb na nilianza mapema/
Na kama ni lyrics niko nazo ka simiti na tema/
Na hata bila airplay anga ni zangu na kema/
Mbogi ni bigi kama zile za Julius wa Malema/”

Kwenye Why The Caged Birds Sings ni wimbo uliotumia kichwa cha kitabu cha muandishi Maya Angelou ambapo Sharon anachana kuhusu kazi yake akieleza vile ngoma zake zina maono kuhusu siku za usoni ilihali kwenye kiitikio MC Sharon anatumia sauti vizuri kubariki wimbo huu mzuka sana.

Kama alivyotumia jina la kitabu cha Maya Angelou emcee huyu pia ametumia sampuli kadhaa kwenye nyimbo kadhaa zikiwemo Say My Name ambapo ametumia sampuli toka kwa wimbo wa Destiny Child’s akiwataja sio tu wale watu weusi waliouawa kule nchini Marekani kutokana na ubaguzi wa rangi bali hata Wakenya waliopoteza maisha kwenye hali ya kutatanisha nchini mwao pia. Wimbo mzuka sana. Hivyo hivyo wimbo Stop What You Doing unaotumia vizuri sampuli ya wimbo wa 2 Live & Die wa Whyte Foxx kuongelea unyanyasaji wa kijinsia.

Ngoma nyingine ambazo nilizipenda kwenye mradi huu ni Aliwara ambao Sharon anachana kwa lugha ya Kiswahili, Kingereza na Luo unaomkuta akiwatia moyo akina dada ambao kutokana changamoto moja au nyingine wanajikuta wao ndio baba na mama kwa watoto wao. Wimbo flani mzuka sana wa kucheza ambao unapiga vinanda wazimu sana unapoanza kufikia tamati. Utayarishaji mzuka.

Ma boombap kama tulivyomzoea nayo emcee huyu nayo si haba na unayapata kwenye ngoma kama Otek Small ambao anachana kwa kijaluo mwanzo mwisho. Uwasilishaji wa mashairi tu pamoja na uimbaji tu unakufanya umuelewe emcee huyu vizuri. Pia kuna So Special ambao pia ni chanya sana kama vile Calm Down ambao unamkuta MC Sharon akiongea na a.k.a zake Alshaverb na Decibelle ni kama ni watu wengine tofauti na yeye. Sharon hadi anabadili sauti kuweza kuchukua nafsi hizi.

Wimbo mwingine ambao niliupenda pia sio tu kwa boombap beats zake tu bali kwa mada tu ni A Page a Day ambapo Sharon anakutia moyo kujizoesha kusoma angalau kurasa kadhaa za vitabu ili kuweza kulisha na kushibisha ubongo kwani siku hizi mitandao ya kijamii ndio inachukua mda wetu mwingi.

Ooh na MC Sharon pia katupeleka batani kidogo kwenye wimbo flani unakuuliza Shida Iko Wapi mara moja tukijiachia baada ya mihangaiko ya dunia.

The Last Will And Testament ni mradi ambao emcee huyu amepania kutuachia wosia wa mwisho kupitia agano hili la albamu hii ila kama unatarajia uchanaji mwanzo mwisho pengine pale kwenye ngoma anazoimba unaweza jikuta unaziruka ila kama wewe ni shabiki wa Sharon basi pengine utamsamehe kwa hili na kuusikia mradi wote mwanzo mwisho bila tatizo.

Nunua mradi huu hapa - www.mcsharon.com

Pia mfuate MC Sharon kwenye mitandao ya kijamii;

Facebook: MC Sharon
Instagram: mcsharonke
Twiiter: MC Sharon
YouTube: MC Sharon