Uchambuzi Wa EP: Utu Na Watu
Msanii: Mentality
Tarehe iliyotoka: 20.01.2021
Nyimbo: 6
Muunda Midundo/Producer: Wise Geniuz
Mchanganya Sauti na Midundo: Wise Geniuz
Studio: AMG Studioz
Mwaka 2021 japokua ulikuwa mwaka tulioutegemea uje kitofauti bado ulikuja na mizigo ya majanga yaliyoikumba 2020 kama vile majanga ya Uviko 19. Ila japokua kulikua na viporo ila mwaka huu ulikuja na baraka kibao kama vile ma emcee chipukizi, wakongwe na wapya wakitoa miradi mipya. Mmoja wa ma emcee hawa ni Mentality ambaye alitupatia mradi wake Utu Na Watu.
Mradi huu unaanza na utangulizi mzuri Intro ambapo anashirikishwa nahodha wa midundo kwenye safari hii ya kuwaelewa kwenye mdundo ambao unajua tu moja kwa moja ni WG wakati Mentality akitueleza
“Watu hawa ukiwa mwema wanakuona goigoi/
Wakizingua ukiwatema wanakuona haufai/
Unaweza uzungukwe na watu na bado ukawa mpweke/
Kutokana na aina ya utu walionao pekee/
Kuna watu wachache sana mfano wa malaika/
Kwenye vazi kuukuu wao huwa kama kiraka/
Hawachoki kusitiri bila dhihaka/
Wamejaliwa kuzikosa hofu na mashaka/
Je umejifunza nini kuhusiana na Utu/
Umechagua roho gani je ni safi au ya kutu/
Kuboresha utu wako yakupasa uthubutu/
Utu bora ni silaha kali sana zaidi ya mtutu/”
Sajo Mc anashirikiana na Mentality kwenye wimbo wa pili uitwao Sanaa ambao unaongelea sanaa kiujumla na mziki wa Hip Hop akishauri hadhira imfuate wakati anatumia sanaa yake kwa manufaa ya jamii yake.
Naanza Na Wewe akiwa na Sammy anayeimba taratibu wakati mdundo wa kinanda unapiga taratibu juu ya kinanda cha WG ni wimbo mzuka sana unaotushauri kutojisahau tulipotoka baada ya kupata riziki.
Kwenye Watu ambapo unapiga tarumbeta taratibu, Mentality anakupa tahadhari kuhusu watu, uzuri wao, ubaya wao, unafiki wao, kejeli zao ila cha msingi usiwafuatilie sana. Basi gita la mdundo huu unapiga freshi na tofauti sana.
Wimbo ambao umenigusa sana na niliopiga on repeat ni Unaona Nini akiwa na Nala Mzalendo. Wise Genius aliwapatia mdundo wenye mzuka sana ambao unaanza na vinanda matata sana, kicks na snare pamoja na kiitikio kizuri toka kwa Nala akisema,
“Unaona nini ukitazama juu na chini/
Unaona vingi venye ualakini/
Unaona utamaduni unaona dini/
Vijana wahuni na mabinti wenye vi mini/
Unaona nini kwa wanadamu/
Ukiwa unalia wanatabasamu/
Unaona nini uliona kaburi/
Au huwa hauoni vizuri/”
Maishani utaona vingi hadi mwishoni ni mavumbini unarudi.
Wimbo wa mwisho wa mradi huu ni Msamaha ambao unapiga mdogo mdogo ambapo Mentality anachana kwa hisia akikumbushia kuhusu umuhimu wa msamaha ndani ya maisha yetu. Maana ya msamaha ni nini na nani anauhitaji? Mentality anasema hivi,
“Wasamehe walokosa moyo uwe huru na wote/
Waliokuumiza wote na yote usikumbuke/
Usiwakumbuke waliokujaza hasira na ujifunze kuwapa nafasi nyingine walokosa/
Wajifunze walipokosa wapunguze ujinga wa fikra/
Msamaha kwa waliokuvuta shati ulipokua ukiifuata riziki/
Msamaha kwa alovunja ahadi na akajikweza kwa ukaidi/
Msamaha kwa rafiki na mpenzi walo share penzi ulilolienzi kwa dhati/
Na wote waliokuumiza moyo ukakata tamaa/
Msamaha kwa niliowatenda vibaya wakabeba na chuki juu yangu/…”
Mentality amejitahidi kadri ya uwezo wake kutuonesha kuwa duniani humu japokua kuna watu kinachowaweka wawe watu kwa asilimia 100 ni utu. Mradi umejaa madini, tahadhari, wosia, maono na mtazamo mzuri kuhusu walimwengu. Kwa kila tunaloliona au kulipitia kwenye mahusiano yetu tusisahau cha muhimu ni kuwa na Utu Na Watu.
Wasiliana na Mentality kupitia mitandao ya kijamii;
Facebook: Mentality Asili
Instagram:goodmentaly