
Jaykah Mtengwa
Tuzo ya nane ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards (August 2022) tumemkabidhi Jaykah Mtengwa (Conjestina)
Jaykah Mtengwa ni mmoja wa ma emcee ambao wamekua kwa game kwa muda ila afahamiki kivile. Emcee huyu ambaye mashairi yake yamejikita kwenye kuelimisha jamii, amebobea handakini mwa Kenya kwa kuachia kazi ambazo ni za kimapinduzi ila kama wanavyosema “Mapinduzi hayataoneshwa kwenye runinga zenu”.
Emcee huyu mwezi jana aliachia nyimbo kadhaa ikiwemo Conjestina ambao kwa wasiofahamu uliundwa kwa ajili ya kutukumbusha kuhusu gwiji wa ndondi toka Kenya dada Conjestina Achieng (Hands Of Stone/Mikono Ya Mawe).
Ngoma hii ambayo mdundo wake uliandaliwa na mtayarishaji Hii Beat Ni X ambaye wameshirikiana nae kwenye miradi kibao japokua inamuongelea Conjestina kama gwiji wa ndondi na vile tunavyowatelekeza mashujaa wetu wanaopeperusha bendera yetu, binafsi naona inaongelea changamoto ya yeyote yule ambaye akitumia kipaji chake anaipa nchi sifa ila mwisho wa siku mambo yanapomwendea mrama nchi yake haimthamini tena.
Conjestina baada ya kupigana ndondi muda mrefu alipata changamoto za kimaisha hadi kupata msongo wa mawazo na kurukwa na akili na kubaki kivuli cha alivyokuwa hapo awali.
Nilichokipendea kuhusu ngoma hii ni kuona vile emcee huyu kajitwika jukumu la kumuenzi mwanamasumbwi Conjestina juu ya mdundo mzuri unaotumia sampuli toka kwa lugha ya Luo ambayo ni lugha mama ya mwanamichezo huyu. Ni jambo jema kuona ma emcee wakiangazia mambo ambayo yanagusa maisha yetu ya kila siku kwenye sanaa zao.
Hongera sana kwa Jaykah Mtengwa kwa kujinyakulia tuzo yetu ya nane ya mwezi August 2022 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards.