
Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards (June 2022): Monaja
“Mgala muuwe ila haki mpe.” Ndivyo wanavyosema waswahili. Leo kutokana na ubunifu pamoja na kujituma kwake tumetambua uwezo wa emcee anayetokea kule Kenya, kaka Monaja na tumemtuza tuzo ya Micshariki Africa Emcee Of the Month Awards ya mwezi June, 2022.
Emcee huyu mwaka huu amefanikisha kutupatia miradi mi nne ya Hip Hop ambayo ipo ki mapinduzi kimidundo, ki mada na ki video. Pia emcee huyu ameweza kuchanganya utamaduni wetu wa kiafrika pamoja na utamaduni wa Hip Hop na kutupatia midundo mizuri sana mwana huu.
Kwanza kabisa mapema mwaka huu emcee huyu aliachia ngoma yake ya kwanza mwezi January, Ntamburukia Nkoro akiwashirikisha Ameru Crew. Ngoma hii ambayo kutoka kwa maelezo ya Monaja pale YouTube ni wimbo wa kiroho mtu anapoumizwa pamoja kuongelea siasa na pia kukumbushia historia ya wapiganaji wetu waliopoteza maisha yao wakati wa vita dhidi ya mkoloni ambapo wanatajwa Ntai wa Nkuraru na General Baimunga ambao walipoteza maisha yao kikatili. Wimbo mzuka sana.
Miezi mitatu baadaye emcee huyu akarudi tena na ngoma mpya tena Miankene akiwa na Ameru Crew pamoja na Chuka Drummers. Wimbo huu ambao uliimbwa na kuchanwa kwa lugha za Sheng na Kimeru (ambayo ni lugha ya mama ya Monaja na wasanii wenzake) na nia ya kuunganisha mambo ya kale na ya sasa kwa kuhimiza roho ya kuthamini utu.
Mwishoni mwa mwezi May kabla hata hatujapoa freshi, Monaja akaangusha bonge la chupa tena. Round hii akishirikiana na mtayarishaji Aloyo wa Mandugu emcee huyu aliachia Kanyaga Kubwa Kubwa.
Ngoma hii kama wewe ulikua enzi ya miaka ya tisini imechukua sampuli toka kwa wimbo wa Busta Rhymes kutoka America uitwao Put Your Hands Where My Eyes Could See. Watayarishaji hawa wawili walitumia sampuli hii vizuri na kuupatia mdundo wenye ngoma ya asili lakini walihakikisha bado ule mzuka wa Hip Hop unaskika vilivyo.
Kanyaga Kubwa Kubwa ndio jina la wimbo wao. Hongera sana Monaja kwa kazi hizi za kimapinduzi. Wimbo huu ambao ujumbe mkuu ulikuwa ni kutuonya dhidi ya marafiki wanafiki, pamoja na wanasiasa wanafiki ambao wanalolisema ni tofauti na wanalolifanya unakuhimiza uwe makini na watu wa aina hii na pindi unapowatia machoni waambie wakanyage kubwa yaani wapotee mbele yako. Kichupa kilikua kizuri sana.
Kabla ya mwezi June kuisha Mojana akarudi tena na kichupa kingine tena Tuchapiane. Neno hili ambalo linamaanisha tuongee kwa njia ya simu limetumika kuonesha vile emcee huyu ametekwa na hisia za mapenzi na pengine lile zumari linalopiga juu ya wimbo huu ni kama ishara ya mapenzi yalivyokolea moyoni mwake kwani linatia manukato wimbo mzima.
Monaja kwa juhudi hizi ambazo tumeziona tokea mwaka uanze hadi ulipofikia tumeona anastahili kutambulika kwa mchango wake mkubwa kwa utamaduni wa Hip Hop kwa kupitia ngoma tajwa hapo juu ambazo zina malengo ya kufunza, kuburudisha na kudumisha sio utamaduni wa Hip Hop bali pia utamaduni wetu halisia.
Hongera sana kwa Monaja kwa kujinyakulia tuzo yetu ya sita ya mwezi June 2022 la Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards.