Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards (March 2022): Watunza Misingi

Tuzo ya tatu ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards ya mwezi March 2022 tumewakabidhi kikosi cha Watunza Misingi kwa nyimbo zao Dada Wa Kazi, Tunatenda, Haki pamoja na Dhidi Ya Ubeberu.

Baada ya kuangusha album yao ya pili Si.Be (Silaha Begani) ma emcee hawa hawakulala. Wamekua mbioni kuachia video ya baadhi ya nyimbo zilizopo ndani ya album yao ili kuweza kunadi mradi wao ambao umebeba madini kibao.

Dada Wa Kazi ndio ngoma ya kwanza kuachiwa mapema mwaka huu tarehe Januari 3 kama “singo” ya utangulizi kabla ya album kutoka. Ngoma hii inadadavua changamoto wanazopitia dada zetu wanapokwenda kufanya kazi za ndani zikiwemo, ujira mdogo, unyanyasaji wa ngono, kebehi pamoja na kutukanwa (“Kuku wa kienyeji”, “Beki 3” na kadhalika.). Kwenye ngoma hii wapo ma jenerali Opobo, Kaa Feel, Funda na Kella B.

Mwezi huo Watunza Misingi waliachia video yao ya pili Tunatenda wakati huu wakiwashirikisha ma jenerali Gome Jero, Majanta pamoja na Oby Hard. Wimbo huu unahimiza utendaji wa wana Hip Hop kwenye maisha yao halisi.

Haki ni wimbo wa tatu ulioachiwa rasmi toka kwa album ya Si.Be. Kwenye ngoma hii iliyowashirikisha ma emcee Kella B, Kido Boma, mwimbaji/mtayarishaji Tinie Cousin pamoja na mwanaharakati/mshairi Ras Muhemsi wahusika  wanaongelea swala zima la haki; haki zetu ni zipi, changamoto tunapotaka kudai haki zetu pamoja nini kifanyike ili tuweze kupata haki zetu.

Wimbo wa nne na wa mwisho uliowawezesha Watunza Misingi kunyakua taji hili ni ngoma yao Dhidi Ya Ubeberu na wakati huu wakishirikisha ma emcee Plate Mdaijasho toka Ushirombo, Geita na Bad Ngundo toka Kahama, Shinyanga.

Ngoma hii inaangazia mabeberu waliotumiliki, njia wanazotumia kutumiliki na wanachonufaika kutoka kwetu wanapotumiliki. Wimbo unataja elimu binafsi kama njia moja ya kujihami dhidi ya mabeberu hawa.

Mradi wote wa Si.Be pamoja na ngoma hizi zote tulizozigusia hapa zimeundwa chini ya usimamizi wa mtayarishaji Black Ninja wa Boom Bap Clinic.

Hongera sana kwa kikosi kizima cha Watunza Misingi kwa kuchkua tuzo ya mwezi March 2022.