Kayvo Kforce - "Kenya Ni Yetu"

Tuzo ya kumi ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards (October 2022) tumemkabidhi Kayvo Kforce (Kenya Ni Yetu)

Mapema mwezi jana Kayvo Kforce aliachia ngoma yake mpya Kenya Ni Yetu. Ngoma hii ilikuja mda muafaka baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 2022 na ambao ulipita bila ya mushkeli yoyote tofauti na miaka mingine. Emcee huyu kwa kuliona hili pengine akachukua kalamu yake na kutuandikia wimbo huu.

Kenya Ni Yetu ni kama sauti ya baragumu kwetu sisi wananchi ili tuweze kukumbuka kuwa Kenya ni nchi yetu sote bila kujali mielekeo yetu ya kisiasa, kwa hivyo tunapaswa kujifunza na kuishi pamoja kwa utangamano na tusiwaache wanasiasa na/au siasa mbaya zitugawanye. Amani na Upendo kwa Wakenya wote”, anasema kaka Kayvo Kfrorce kuhusu wimbo huu.

Inaonekana wa Kenya waliskia ujumbe huu kwani mwaka huu uchaguzi uliisha bila rabsha zozote na maisha yakaendelea kama kawaida ukizingatia chaguzi za hapo nyuma zilikumbwa na umwagikaji wa damu nyingi kutoka kwa wananchi wa kawaida na sio wanasiasa.

Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa ma emcee wetu wana angazia hoja muhimu kama hizi zinazogusa jamii zao na pia wanatumia vinasa vyao kuelimisha jamii. Hapa sasa ndio unapata maana halisi ya msanii kuwa kioo cha jamii kwani Kayvo baada ya kutupatia mradi wake miaka ya nyuma tena (The Mwananchi Initiative) amerudi tena kuongea na wananchi na kuwakumbusha kuwa “Kenya Ni Yetu”.

Hongera sana kwa Kayvo Kforce kwa kujinyakulia tuzo yetu ya kumi ya mwezi October 2022 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Awards.