Katika kipindi hiki cha pili cha Micshariki Africa Mamtoni tulisafiri kwa ndege hadi Carolina Kusini, America kukutana na kaka Mowa ambaye ni mtu anae vaa kapelo nyingi. Mbali na kuwa mume wa mtu na baba wa familia, Mowa Olodumare ni mwanafalsafa, mkutubi, kiongozi wa jamii, mshairi na mchenguaji pia.
Tuliungana naye ili kuzungumzia maisha yake kama mtaalamu wa elimu kwa jamii yake na jamii ya Hip Hop na pia kujua zaidi kuhusu albamu yake iliyotolewa hivi majuzi Griot .
Karibu Micshariki Africa kaka/brother Mowa . Mambo ya kwanza kwanza, kwa fadhili jitambulishe.
Salamu, mimi ni Mowa Bioluwafe Olodumare. Mimi ni mume wa mtu na baba, kimsingi kila kitu kingine ni mapambo, lakini baadhi ya hayo ni pamoja na kuwa mwanafalsafa, mkutubi, kiongozi wa jamii, mshairi na mchanaji.
Mowa Olodumare, nilianza kukusikia kutokana na baadhi ya nyimbo ulizofanya na Kunta Official Beats na Romi Swahili. Jina hilo lilinivutia. Jina hili lilikujaje na linamaanisha nini?
Mowa linatokana na Kiyoruba Mo Wa linalomaanisha "MIMI NIKO" jina langu la kati Bioluwafe linalomaanisha "Kazi za" na Olodumare likiwa jina la Mungu katika utamaduni wa Kiyoruba. Hata hivyo, tumejenga utamaduni hapa Amerika unaoitwa "Hekalu la Mowa " ambapo falsafa yetu inapatana na dhana ya kujiumba na uthibitisho. Kwa hivyo, tunawafundisha watu jinsi ya kujifikiria wenyewe na kujifafanua wenyewe katika mazingira ambayo yataamua thamani yao ikiwa wataachiwa kufanya hivyo. Minyororo ya kwanza iliyoanguka kutoka kwa mababu zangu ilikuwa akilini mwao, chini ya ufafanuzi na maoni ya wazungu. Kuamua sisi ni nani ndio msingi wa uhuru.
Pia unajiita Mkutubi wa Watu, tufafanulie zaidi kuhusu hili…
Mimi ni mfanyakazi wa maktaba na ninazingatia viwango vya kusoma na kuandika vya jamii yangu. Ninaungana na shule, waandaaji wa jumuiya, wazazi na wengine ili kubuni njia bunifu za kufanya usomaji kufikia na kupendeza kwa watoto wetu. Kwa bahati mbaya, vijana wa Kiafrika wanashika nafasi ya mwisho linapokuja suala la kusoma na kuandika katika kusoma, hisabati na sayansi. Kwa hivyo, kuwa mtu mweusi katika nafasi ya kuendesha maktaba kunawapa vijana (na jamii) mtazamo tofauti wa jinsi mtu mweusi alivyo na tunatumai kupitia uhamasishaji wetu wa jamii wanaweza kujiona ndani yangu na kuitumia kama kichocheo cha mabadiliko. .
Uliunganaje na kufanya kazi na hawa ndugu kutoka Kenya?
Ilianza na kaka yangu MC Spook takriban muongo mmoja uliopita na kaka yangu Ill Flow kutoka Afrika Kusini ambaye alinitambulisha kwenye anga ya Hip Hop ya Kiafrika. Kisha kupitia taarifa zangu kuwafikia wengina na pia kuwa tayari kufanya kazi na karibu kila mtu. Nimeweza kukutana na kushirikiana na wasanii kama Kunta (Official Beats), Shazzy B, Drunken, Kayvo Kforce na wengineo. Hii ndiyo nguvu ya mitandao ya kijamii; inaifanya dunia kuwa ndogo sana.
Mowa, tueleze kwa kifupi historia fupi ya maisha yako; ulizaliwa wapi, mpo wangapi katika familia yenu, malezi na jinsi utoto wako ulivyokuwa ...
Nilizaliwa huko Columbia, Carolina Kusini. Mimi ndiye mdogo wa watatu. Nina dada mkubwa na kaka. Nililelewa na mama na baba wenye upendo katika mtaa wa watu wa tabaka la kati. Nilibarikiwa sana. Hata hivyo, mambo yalibadilika baba yangu alipofariki nilipokuwa na umri wa miaka 11 hivi. Unyogovu ulikuwa mzigo hadi miaka 23 hivi. Hata hivyo, kulikuwa na masomo ambayo baba yangu aliniachia kabla hajafa ambayo yalinisaidia kuniongoza. Ujumbe wake wa mwisho ulikuwa "Kuwa mtu anayenifanya nijivunie na hakikisha una SOMA pia" ambao uliniongoza kuwa mwanafalsafa.
Alipokufa, nilisoma kila dini na kila falsafa niliyoweza kupata ili kuelewa maumivu niliyokuwa nikikabiliana nayo. Kutoka Ukristo hadi Uhindu hadi Ifa. Kwa kufanya hivyo, ilinisaidia pia kuwa Raia Wa Ulimwengu kwa maana ya kwamba ningeweza kuelewa mitazamo mingine ya jinsi watu walivyoona ulimwengu na kusudi la hali ya kiroho.
Uliingiaje kwenye muziki?
Kuandika kumeokoa maisha yangu kwa njia nyingi. Ni mazoezi ya yanayo nitibu mimi. Nilianza na mashairi na kisha kukariri mashari haya inapokuja suala la kuelezea hisia zangu. Siku zote nilikuwa mfuasi wa uchanaji, lakini nilianza kuitumia kwa kupigana(ki michano). Nilipoamua kuchanganya wawili hawa, nikawa mchenguaji mwenye ufahamu...ambaye hubeba shoka la vita endapo vita vitatokea.
Safari yako ya muziki ikoje hadi sasa? Je, umetoa miradi mingapi iwe eps, mixtapes au albamu?
Albamu yangu ya kwanza inakwenda kwa jina The Lyrical Alchemist hii ilikuwa kabla ya mambo ya kutiririsha muziki (streaming) kuwa maarufu kama ilivyo sasa, kwa hivyo nilikuwa na nakala halisi za albamu hiyo. Hapana, ngoja, nilikuwa na nyingine kabla hiyo inaitwa The Heart Of The Poet ambayo ilikuwa albamu iliyochanganyika sana ambapo nilichomeka tu maikrofoni yangu, nikatumia loops chache kutoka kwa bendi ya gereji na kubonyeza rekodi, lakini bado ni albamu yangu ya hisia zaidi.
Kisha nikadondosha A Brief History Of Rhyme nadhani mwaka wa 2015, na nyimbo kadhaa za hapa na pale kama vile Black Kiss: An Ode To Black Women chini ya jina langu la Saymo wakati huo na nyingine ambazo siwezi kukumbuka. Ilikuwa kwenye tovuti ya mixtape asilia DatPiff , lakini sidhani kama tovuti hiyo ipo tena.
Pia nilisikia kuwa wewe ni mshairi na mwandishi wa baadhi ya vitabu. Tungependa kujua zaidi kuhusu hili...
Nimeandika vitabu 3. Cha kwanza ni The 3 Degrees of Knowledge: An Introduction to the Mowa Temple ambacho kilikuwa darasa letu la utangulizi juu ya Falsafa ya Hekalu la Mowa . Cha pili kinaitwa The Purpose and Power Of Prayer ambacho kilikuwa ni ufuatiliaji wa kitabu cha kwanza na cha tatu kinaitwa Nazareth ambacho ni kitabu cha mashairi kilichoshindana katika shindano la Tuzo la Pulitzer.
Hali ya Utamaduni wa Hip Hop huko Amerika ipoje?
Utamaduni upo vizuri kila wakati. Muziki wa rap kwa upande mwingine katika kiwango cha kawaida uko katika enzi ya wanakili jambo ambalo linaufanya kuwa wa kuchosha, lakini hilo halitadumu milele.
Unaweza kuwashauri nini watu ambao wako kwenye Utamaduni katika nyakati hizi za biashara ya kila kitu cha Hip Hop?
Ukishikilia Utamaduni, biashara itakuja kwako. Usidanganywe na maigizo unayo yaona kwenye runinga. wengi wao wamevunjika na hawawezi kuandika yale yatokayo katika nafsi zao. Kwa kuongeza, kuna njia nyingine za kuwakilisha Utamaduni nje ya matendo yake ya utendaji. Kuna vipengele 9 vya Hip Hop: Breakin (Break Dancing), Emceein , Deejaying, Graffiti Art, Street Knowledge, Street Fashion, Street Language, na Street Entrepreneurship.
Ukijua yote tisa, hiyo ni mikondo tisa ya mapato. Ukifaulu moja, tuseme sanaa ya grafiti, tumia ujuzi huo, uugeuze kuwa shule, na ufundishe jamii jinsi ya kuchora. Iuze kwa zaidi kwa wale walio nje ya Utamaduni ambao wanataka kuwa chini.
Ikiwa unaweza kuchora, unaweza kubuni graphic au kuchora nguo kwa wabunifu wa mitindo, kuunda mabango, uwezekano hauna mwisho!
Ikiwa wewe ni Deejay, tafuta klabu mpya iliyo funguliwa hivi karibuni ambayo inahitaji la deejay, toa huduma zako bila malipo na kisha kwa ada utakapo pata umati.
Ikiwa wewe ni emcee, tumia ujuzi huo huo kuandika jingles kwa ajili ya makampuni, kuandika nyimbo kwa watu wanaohitaji kujieleza kwa ajili ya mtu anayempenda.
Ikiwa ni break/break dancin, kuwa mwalimu wa kufunza hili na pia tengeneza video za kuonesha talanta zako.
Tena, kuna vipengele 9 , lakini njia nyingi za kufaidika kutoka kwao.
Hebu tuzame kwenye albamu yako mpya ya Griot . Eleza kuhusu mradi, dhana na mandhari nyuma yake, waliohusiki kwenye uandaaji wake na pamoja na wasanii uliowashirikisha.
Griot ni msimuliaji wa hadithi, ninasimulia tu hadithi za jinsi nilivyohisi wakati huo nikitumai kwamba kama vile kutoka kwa Wagiriki wa zamani utapata ujumbe kutoka kwa hadithi hizi. Nilifanya sehemu kubwa ya utayarishaji isipokuwa kwenye ngoma kama Uliza na South Carolina To Kenya ambazo ziliundwa na Kunta Official Beats. Wasanii waalikwa walitokea Kenya; Drunken, Kunta Official Beats, Shazzy B, na Kayvo Kforce .
Kwanini albamu yako ukaamua kuiita Griot ? Je story ya nyuma kuhusu jalada la album ni ipi?
Ni jambo la kuchekesha, nimekuwa nikifanya kazi kwenye albamu hii kwa muda mrefu sana hivi hadi nilisahau kile ambacho kilinipelekea kuiita Griot. Hata hivyo, Griot ni maktaba ya kibinadamu ya jumuiya, na niliutumia mchoro huo kutoa heshima kwa Griot, Wakutubi, Mtunzi wa Nyaraka, Walinzi wa Maarifa na Siri za Kimungu.
Katika mradi huu, ulifanya kazi na baadhi ya wasanii kutoka Kenya. Je, miunganisho hii ina umuhimu gani kwenye Utamaduni wa Hip Hop?
Ni muhimu sana kwa sababu Kulture ya Hip Hop inaweza kuwa chombo cha Muungano Wa Waafrika! Kupitia ustadi wetu, tunaweza kuhusiana sisi kwa sisi na kuvunja mila potofu hasi ambayo tunaweza kuwa tumeshikilia kuhusu sisi kwa sisi. Vizuizi vimevunjwa kwa sababu unaweza kurap na mimi pia naweza, halafu unajua, nakuambia nina mtoto njiani kwa sababu nyinyi ni familia.
Mowa wewe ni mtu wa kiroho pia. Je, kuna uhusiano gani kati ya muziki wako na muziki kwa ujumla na hali ya kiroho?
Swali zuri sana. Kitendo cha kuandika chenyewe ni tafakari. Hii ndiyo sababu mimi mara chache sana, hutumia simu yangu kuandika mashairi yangu. Kuna mshikamano kati ya akili, kalamu, na daftari, ambayo hutengeneza mashairi haya kutoka "mahali pasipojuikana" ili kujidhihirisha yenyewe mwilini kama wimbo. Mchakato huo ni jambo la kiroho ambalo sichukulii poa.
Je, kuna umuhimu gani kwetu kujua historia ya muziki na Utamaduni ambao tuko ndani yake, Hip Hop?
Inapaswa kuwa sharti kwa yeyote anayeshiriki katika kipengele chochote kujua historia ya Utamaduni. Wakati hatufanyi hivyo, hapo ndipo unapoona watu wanaabudu mashirika na kuwadharau wazee wa utamaduni. Leo mnawaita watu ma-DJ watu ambao hujawahi kuona wakitengeneza rekodi hata moja! Hayo ni matokeo ya kutokuwa na heshima kwa Utamaduni .
Je, unaifahamu vyema hali ya Utamaduni wa Hip Hop wa Afrika Mashariki? Je, ni wachanaji gani unaowafahamu, unawasikiliza na ungependa kufanya kazi nao?
Naam, nimekuja kugundua kua kushirikiana na Kayvo Kforce ni jambo kubwa na ni heshima kufanya kazi naye. Aidha, nimesikiliza baadhi ya nyimbo zake na hakika yeye ni emcee. Lakini, nimesema hapo awali ila nitasema tena...Nyie mmepata mchenguaji mzuru kwa jina Shazzy B! Niliuliza ma emcees wote walioshiriki kwenye wimbo wa South Cack To Kenya waoneshe ukali wao wa mashairi na kwa maoni yangu Shazzy B alikuwa na aya bora zaidi kwenye rekodi hiyo, bora zaidi kuliko yangu! Endelea kunoa pensel i yako dada...Lakini, hautonishinda kamwe kwenye kolabo zozote zijazo! 😁
Lakini heshima kubwa kwa MC Spook, Kunta Official Beats, Johnny Span-One, Musiq Jared, Drunken, Romi Swahili, Plate Mdaijasho na wengine wengi kutoka Kenya na Tanzania ambao nimepata fursa ya kufanya nao kazi.
Muziki sasa unapatikana kwa urahisi zaidi kwa wasikilizaji kupitia Dsps, swali ni je hili linawanufaisha wasanii? Nini uzoefu wako binafsi na ushauri juu ya hili?
Ni vizuri kwa maana kwamba ni rahisi kufikisha muziki wako kwa hadhira pana, haraka zaidi. Hata hivyo, kiasi unachopata kutokana na dsps hizi ni kidogo kuliko mikataba ya rekodi potofu ambayo wasanii hulazimika kushughulikia kwa kawaida. Nilisita kuweka albamu yangu kwenye dsps hizi za utiririshaji kwa sababu hiyo, lakini niliamua kuweka mradi huo pake dakika za mwisho.
Changamoto moja wanayokumbana nayo wasanii wa Hip Hop kutoka Afrika Mashariki ni kutochezwa kwenye vyombo vya habari vilivyopo mkondo mkuu. Je, hali ikoje huko na nyinyi mnakabiliana vipi na hili?
Ni jambo lile lile hapa. Mtandao ndio usawazishaji bora ingawa ikiwa unaweza kuigiza na kufanya muziki wako uwe soundtrack, basi una njia ambazo unaweza kukwepa mfumo.
Je, una kazi ya kando au umewekeza nguvu zako zote kwenye muziki?
Mimi nimeajiriwa kama mkutubi. Ninasimamia moja ya maktaba za kaunti. Mimi ni mwanafalsafa kwa wito na Mshairi/Mchenguaji kwa mapenzi.
Je, tutarajie nini kutoka kwa Mowa ijayo?
Kweli, sasa hivi niko shuleni kwa ajili ya Shahada yangu ya Uzamili katika Maktaba Na Sayansi ya Habari. Ninapaswa kuhitimu mwaka wa 2024. Nje ya hapo, ninaweza kuandika kitabu au kuanza utendakazi wa albamu nyingine.
Wasomaji wetu wanawezaje kuwasiliana nawe na kupata muziki wako?
Facebook: Moma Olodumare
Instagram: The People's Librarian
Spotify: Mowa Olodumare
Mawazo ya mwisho kaka?
Kamwe usidharau nguvu zako kwa sababu unahisi dhaifu kwa sasa. Ukweli ni kwamba kufikwa kwako hapa ulipo kwa sasa wakati huu ni ushuhuda wa nguvu zako.
Asante kwa wakati wako kaka Mowa, ilikuwa furaha kuwa nawe hapa Micshariki Africa.
Asante. Amani na upendo.