Subtex

Subtex ni Hip Hop emcee anayepatikana kwenye handaki kule Marekani. Yeye ni baba, emcee, mfanyakazi wa afya ya akili na mwanaharakati pia. Subtex amejenga ufuasi mkubwa kutokana na orodha yake nzuri ya muziki ikiwa ni pamoja na kazi yake ya ushirikiano na Sela Ninja kutoka Tanzania, "Hatuwalambi Miguu".

Karibu sana Micshariki Africa kaka Subtex. Mafunzo yako ya lugha ya Kiswahili yanaendeleaje? Natumai Sela Nnja anajitahidi kukufundisha vizuri lugha yetu ya kiswahili..

Nimejifunza maneno kadhaa kwa sasa ila naamini naweza kujifunza zaidi ya hapa kusema kweli. Ninaweza kurudia mengi yale ambayo Sela anachana katika mistari yake na matamshi yangu ni mazuri, lakini ningependa kujifunza zaidi. Nitamwomba Sela aendelee kunipa mafunzo zaidi.

Kwa mradi unaofuata tunaofanya, ningependa kufanya wimbo ambapo nitarap kwa Kiswahili na yeye atarap kwa Kiingereza. Nadhani hiyo itakuwa nzuri.

Utangulizi kwanza, Subtex ni nani, unatoka wapi na unafanya nini?

Jina langu la serikali ni Zeke Kreitzer na ninatoka Amerika. Ninatoka Long Island, New York na nilikulia katika jimbo la Vermont. Niliishi miaka 10 huko Boston Massachusetts na miaka 10 huko Brooklyn, New York kama sehemu ya kikundi cha Hip Hop cha Gray Sky Appeal. Nilianza kufanya muziki kama solo artist mwaka wa 2017 na nikaanza kuachilia matoleo ya “The Book Of Ezekiel”. Tangu wakati huo nimetoa awamu tatu za “Book Of Ezekiel” na ninaishi tena Vermont kwa sasa, ambapo namlea binti yangu wa miaka 3.

Ulisomeka kwenye rada zangu nilipokuwa nikisikiliza miradi mingi ya Sela Ninja aliyo fanya kazi na wachanaji kutoka nje ya Tanzania. Ilikuwaje hadi mkakutana na kuanza kufanya kazi pamoja?

Naamini alinifikia kwa kupitia maswasiliano ya mtandaoni. Nilianza kutafiti kuhusu muziki wake na nilivutiwa sana na nilicho kisikia. Nadhani 'Mazabe' ndio wimbo wa kwanza tuliofanya pamoja. Tunaweza kusema mara moja kwamba kulikuwa na kemia kati yetu na ilikuwa ya kipekee. Tuliendelea kutengeneza wimbo baada ya wimbo, kila mmoja akisikika vizuri na vizuri zaidi, hatimaye tukaachia mradi  wetu wa kwanza, 'Hatuwalambi Miguu.'

Kabla ya kuangazia miradi uliyofanya na Sela Ninja, hebu turudi nyuma ambapo ulipoanza safari yako ya muziki. Tafadhali wajulishe wasomaji ulizaliwa lini na wapi. Mlikuwa wangapi katika familia yenu na utoto wako ulikuaje?

Nilizaliwa Manhasset, New York mwaka wa 1980. Familia yangu ilihamia Vermont mwaka wa 1981 na nililelewa huko mimi na mdogo wangu wa kiume  ambaye ni mdogo kwa miaka 3. Niliishi na mama, baba na ndugu yangu ambapo muziki ulikuwa sehemu kubwa ya familia yetu, kwani maisha ya baba yangu yalitokana na muziki. Baba yangu alikuwa ni sehemu kubwa ya kuchangia upendo wangu kwenye muziki tangu awali.

Nikiwa na umri wa miaka 21 nilihamia Boston MA, nikakaa miaka 10 huko, kisha nikahamia Brooklyn kwa miaka mingine 10, ambapo tulipiga kazi sana na kundi la Hip Hop la Gray Sky Appeal.

Nilianza kufanya kazi kama solo artist mnamo 2017 hadi leo.

Je, jambo hili la muziki lilianzaje kwako? Umegunduaje na kukuza talanta uliyokuwa nayo hadi wakati huu? Je, familia yako ilikuunga mkono?

Familia yangu iliniunga mkono tangu siku za meanzo na bado wanaendelea. Baba yangu alinipa msukumo  mkubwa wa kukomaa na  muziki na nilianza kucheza gitaa (bezi) na kujiunga na bendi nikiwa kijana. Nimekuwa jukwaani katika mazingira tofauti kwa muda sasa. Kitu cha pili na ninachopenda ni kuigiza. Hip Hop ilinivutia na nikaanza kuandika mashairi. Nilikomaa na kukuza ufundi wangu, na ninaendelea kufanya hivyo hadi leo.

Ni nini kilikuvutia kwenye Utamaduni wa Hip Hop na imeathiri vipi maisha yako?

Mashairi na kujieleza kupitia maneno.

Huu ukiwa ni mwaka wa 50 wa Hip Hop, je, ni nini baadhi ya matukio muhimu kwako binafsi ambayo yanakufanya ujivunie kuwa sehemu ya Utamaduni huu?

Kuachia sehemu ya tatu ya “Book Of Ezekiel 3” mwaka jana, ilikuwa mafanikio makubwa kwangu. Niliweka moyo na roho yangu kwenye rekodi hizo na ninaona kuwa nambari 3 ndio kazi yangu bora zaidi.

Turudishe nyuma kwa mara yako ya kwanza kuingia na kurekodi studio, uzoefu ulikuwaje ukiangalia vile ulikuwa mdogo na je ulirekodi wimbo gani na uliupokewaje na mashabiki zako?

Nilikuwa katika studio nyingi za nyumbani nikiwa kijana na marafiki ambao nao pia walikuwa wakifanya muziki. Wimbo wa kwanza kabisa uliokamilika niliorekodi uliitwa 'I Love Wrestling', hahaha. Labda nilikuwa na umri wa miaka 12 na ila ninachokijua nilipenda mieleka. Nazungumza WWF ya kitambo ya akina, Jake The Snake, Andre...na watu kama hao.

Nakumbuka kiitikio ikisema, “I love wrestling, I know it's fake, I love wrestling, Jake The Snake” ("Ninapenda mieleka, najua ni bandia, napenda mieleka, Jake The Snake.")

Nilijivunia wimbo huo, hahaha.

Kadiri muda ulivyosonga nilianza kurekodi nyimbo kali zaidi na kuziweka katika mfumo wa rekodi. Mnamo 2003, niliachia track inayoitwa "Nerve Vital" ambayo ilionesha vile maisha yangu ya ujana yalivyokuwa. Baada ya hapo safari yote imekuwa ni ya kupanda kuelekea juu tangu wakati huo.

Je, wewe pia unajishughulisha na utayarishaji wa muziki na ikiwa ni hivyo unafanyaje vyote viwili kati ya kuwa emcee na mtayarishaji wa muziki?

Kwa kweli mimi si mtayarishaji. Nimetengeneza midundo kadhaa kwa miaka mingi, lakini hiyo ilikuwa kwa kujifurahisha tu. Napendelea kuzingatia uandishi wa mashairi pekee.

Je vipi masuala ya muziki huko America? Je  Hip Hop ya handaki bado iko hai au inasuasua?

Hip Hop ya handaki huku Amerika bado iko hai na inasikika si mchezo. Japokua kuna panda shuka za muziki na pia mara kwa mara kunakubadilika kwa sauti ndani ya Hip Hop, lakini kwa ujumla Hip Hop ya handaki huku ipo vizuri na ina nguvu muda wote.

Kuna kuheshimiana ndani ya jumuiya ya Hip Hop ya Handaki ya huku. Kwa mfano, nilikutana na Freddie Black na Tash (wa kundi la Alkoholiks) wiki iliyopita huko Vermont kwenye onesho. Waliniruhusu nijiunge nao kwenye onyesho lao lililofuata huko Boston siku chache baadaye kwa seti nyingine. Mambo kama haya yananithibitishia kuwa Hip Hop haitawahi kupasuka kwa sababu ya aina ya wasanii inayowavutia ndani ya mizunguko ninayoijua.

Hebu tuzame kwenye katalogi yako, ni miradi gani kamili ambayo umeachia kufikia sasa iwe EP, kandamseto au albamu? Jina la mradi na mwaka mradi ulitoka?

Kuhusiana na kazi yangu nikikiwa peke yangu, nimetoa Book Of Ezekiel 1, 2 na 3. (2017, 2020 na 2023)

Hatuwalambi Miguu nikiwa na Sela Ninja (2023)

Kabla ya 2017 katalogi yangu ina rekodi zilizo na Grey Sky Appeal.

Moon Balloon na Esh (2016)
Occams Razor na Qwel (2014)
Hunt And Gather (2012)
Grey Sky Appeal (2011)
Du Er Smuk (GOTM054) na Zatoichi's Ears (2024)

Sawa wacha nirudi kwako na Sela Ninja. "Hatuwalambi Miguu", mradi huu ulikujaje? Je mada kwa ujumla, dhana au ujumbe kutoka kwa mradi ulikuwa upi?

Mimi na Sela tulikutana mtandaoni na tukaanza kurekodi nyimbo chache pamoja. Ngoma hizo zilitoka vizuri sana na tuliendelea kuboresha tulichokua tunakifanya. Tulikuwa tunaunda sauti ya kipekee na hatukutaka kuacha. Hatimaye tulileta mradi wa nyimbo 20 na tukautoa mwaka wa 2023.

Nimefurahishwa sana na jinsi mradi huu ulivyoungana na kuwa na nia moja kati ya Sela na mimi. Tulifanya kazi vizuri sana pamoja na tukawa tunarudisha mawazo na kuunda hadi nyimbo 3 kwa siku. Tulizidi kuunda kazi na tunazidi kufanya kazi nzuri kwa ajili ya rekodi yetu ya pili pamoja.

Hatuwalambi Miguu anajieleza kwa ubichi wake. Iliwaleta wasanii pamoja kutoka pande zote za dunia. Ikiunganishwa na tamaduni na lugha tofauti inawakilisha upendo wa Hip Hop, haijalishi unatoka wapi.

Nani alikuja na jina la albamu na jina la albamu linaendana vipi na jalada la albamu linapokuja suala la kufikisha mawazo yenu kwa msikilizaji? Nani alikuja na jalada la albamu?

Sela alikuja na jina la albamu na msanii ninayemfahamu kutoka Ugiriki alichora mchoro uliotumika kwa mradi huo. Jina la rekodi lingetafsiriwa kuwa "hatuinami" au "hatubusu miguu yao".

Kusema kweli, Vivi alisema ningeweza kutumia sanaa hiyo miaka mingi kabla sijakutana na Sela, lakini sikuwahi kuwa na mradi unaofaa.

Ilionekana kuwa sawa kwa rekodi hii na taswira kwenye jalada kwangu iliwakilisha machafuko ya maisha na kitendo cha mauzauza cha kuokoka. Kwenye jalada la nyuma, kuna ndege na magamba yaliyovunjika juu ya kasa. Kwangu mimi hili linawakilisha usawa wa mwanadamu.

Je, mradi uliofanya na Sela Ninja ulikuwa muhimu kwa kiasi gani linapokuja suala la kuvunja vizuizi vya kitamaduni na lugha katika Hip Hop?

Ni rekodi yenye nguvu. Siwezi kufikiria rekodi nyingine ambayo ilikuwa na wachanaji wa Kiingereza na Kiswahili ndani yake. Sela na mimi huunda timu nzuri na kufanya kazi pamoja kwa uzuri sana. Tuna mchakato kama huo linapokuja suala la kutengeneza muziki. Inatokea kwa kawaida sana.

Wimbo wa kwanza kutoka kwa "Hatuwalambi Miguu" ulikuwa B.I.B.L.E ambayo uliwashirikisha washikaji kutoka Kenya na Tanzania... je, tutegemee ziara ya Afrika Mashariki hivi karibuni?

Ningependa kuja Afrika kutumbuiza na kukutana na kila mtu ambaye nimekuwa nikifanya naye kazi ana kwa ana. Hiyo hakika inahitaji kutokea.

Wapi kutoka hapa...naona umedondosha EP, "Book Of Ezekiel 3", Msururu huu wa EP unahusu nini?

Msururu wa ‘Book Of Ezekiel’ ulianza mwaka wa 2017 na ulikuwa mradi wangu wa kwanza nikiwa peke yangu. Awamu ya kwanza ilifanikiwa sana na ilikubaliwa sana wana hip hop wa handaki.

Mnamo 2020, baada ya kuzaliwa kwa binti yangu, nilitoa toleo la pili, ambalo pia lilikuwa na matokeo makubwa. Muziki uliendelea kuwa bora. Mwishoni mwa mwaka jana nilitoa awamu ya tatu na ninaiona kama kazi yangu bado bora. Hiyo ndiyo trilogy au utatu, jinsi nilivyoifikiria. Kuna rekodi 3 ndio msingi wa kazi ya maisha yangu ... lakini kutakuwa na zaidi ...

Pamoja na ujio wa DSPs hii imeathiri vipi jinsi unavyowasilisha muziki kwa wasikilizaji wako na unanufaika kifedha kutokana na muziki huo?

Ilibadilisha mambo kwa hakika na imefanya muziki kabla ya umri wa mtandao. Ilidhoofisha tasnia nyingi na kurahisisha watu wenye ujuzi sifuri kufanikiwa.

Kwa maoni chanya zaidi, ilifanya muziki kuwa rahisi kusambaza kwa wasanii wa handaki na kuifanya iwezekane zaidi kufanikiwa kama rapa wa kujitegemea. Muziki unaweza kufikia umati kwa urahisi zaidi.

Ili kufaidika kifedha unahitaji kuwa mbunifu. Jaribu kuwa na aina tofauti za bidhaa na kutembelea miji mipya, kitaifa na kimataifa.

Je, unajishughulisha na muziki muda wote au una kazi nyingine inayokusaidia kujiendeleza?

Ninasawazisha muziki wangu na kufanya kazi katika tasnia ya afya ya akili. Ninafanya kazi na wagonjwa wa kiwewe ambao wanaishi katika nyumba ya makazi.

Tunapomalizia ni nini ungependa tujue kuhusu Subtex ambacho huenda hatukukuuliza?

Kwamba tu nimepata nyimbo nyingi mpya zinazokuja. Sela na mimi tunatayarisha rekodi mpya ya itakayotoka mwaka 2024. Zaidi ya hayo, nina rekodi nyingine tatu zilizokamilika. Toleo langu lijalo litakuwa Julai 2024 na linaitwa 'Du Er Smuk.' Imetayarishwa na Zatoichi’s Ears (London) na itatolewa na lebo ya rekodi ya Uingereza, Gold On The Mixer.

Zaidi ya hayo, nina albamu na UKs Ill information na albamu ya pia na mtayarishaji Rico James wa Man Bites Dog Records. Nimefurahi kuachia muziki huu wote.

Wasomaji wetu wanaweza kuwasiliana nawe wapi kwenye mitandao ya kijamii na wanaweza kupata wapi muziki wako?

Ninapatikana zaidi hapa,

Instagram: @_subtex

Unaweza kupata muziki wangu kwenye;

Bandcamp: https://thebookwaswritten.bandcamp.com/music

na majukwaa yote ya kidigitali

Boomplay: https://www.boomplay.com/albums/80217689?from=search&srModel=COPYLINK&srList=WEB

Spotify: https://open.spotify.com/artist/4DtFulxlK1vJEwMLtz1pp3?si=-VPjbM_2Shu4B8VSxlj4EQ

Asante sana kwa wakati wako kaka Subtex. Kila la kheri.

Asante, ninathamini sana wakati wako na maswali yako. Asante sana kwa support yako.