Innocent Paul Gama almaarufu Mikono Ya Kazi

Kitu ninachopenda kuhusu sauti za mziki wa Hip Hop uliopo handaki ni kuwa utaweza kuskia midundo tofauti iliyoundwa kwa ustadi mkubwa sana. Kitu kizuri zaidi unakuta aliyeunda mdundo huo nae humjui.

Mara nyingi hili hunipa hamasa sana kutaka kumtafuta na kumfahamu mtayarishaji huyu.  Baada ya kuskia kazi kadhaa zilizokuwa na signature tune inayosema “Mikonooo” kwa sauti ya kuvuta niliamua kutafuta sio tu kazi nyingine za producer huyo bali hata yeye mwenyewe ili kuweza kumfahamu na kufahamu zaidi ubunifu wake kwenye kazi za wana Hip Hop.

Karibuni tupige gumzo na mtayarishaji mzuri sio tu wa mziki wa Hip Hop bali hata kiepe!

Karibu sana Mikono kwenye jukwaa la Hip Hop, Micshariki Africa. Tuanze kwa kufahamu majina yako rasmi,unatokea wapi na unapatikana wapi?

Mi naitwa Innocent Paul Gama

Mikono Ya Kazi, jina hili lilikujaje?

Jina la Mikono Ya Kazi alilitunga rafiki yangu anaitwa Sele kipindi tunaishi South Africa tumeenda kwa further knowledge kidogo ya mambo yetu ya production. Kabla ya Mikono Ya Kazi nilikua nafahamika kama Inno C.

Kwa nini aliamua kuniita Mikono Ya Kazi?

Mimi nina shughuli tofauti tofauti ninazofanya na mikono yangu, nashkuru mwenyezi Mungu amenibariki. Cha kwanza nafanya production, cha pili mimi ni kinyozi mzuri tu, cha tatu mimi ni dereva, cha nne pia mimi pia nafanya shughuli tofauti za upishi. Nina ofisi tofauti na mziki, nauza chakula, nauza chips, popcorn, crisps as long as inaniwezesha kupambana na hali ya maisha.

Mimi nafanya mziki ila kwa sasa bado mziki haujaanza kunilipa ili kuweza kufanya mambo yangu mengine au nikamudu mambo yangu ya kifamilia kwa njia ya mziki kwa hiyo lazima nijishughulishe na vitu vingine tofauti tofauti ili niweze kupata nguvu na utulivu wa kufanya mziki.

Mikono Ya Kazi unajihusisha na shughuli gani? Pia kando na mziki unajishughulisha ni nini kingine ili kuweza kujikimu kimaisha?

Mimi ni producer wa mziki na kama nilivyosema hapo awali nafanya vitu tofauti ili kuweza kujikimu ki maisha.  Kando na nilivyovitaja hapo juu pia nina piga rangi, nina skim kuta na pia ni mjasiriamali, hivo.

Tueleze historia yako kidogo kuhusu kuwa producer?

Mimi nilianza kwa kuimba, kuchana, yeah nilitokea huko. Nimekaa mda mrefu nikifanya hivyo vitu lakini tamaa na hamu yangu kubwa ilikuwa ni kufanya production.

Je Mikono unafanya chini ya studio zipi na pia unaimiliki au umeajiriwa?

Kwa sasa nafanya kazi pale The African Dream, maeneo ya Pembe, Buguruni, Dar.  Hii studio sio yangu, bali nafanya kazi pale na project zangu binafsi hua nazifanyia pale tofauti na za ofisi.

Ila Mungu ni mwema, siku si nyingi nitafungua studio yangu kwani nishaanza kuwekeza kwa ajili ya studio yangu binafsi.

Vitendea kazi vyako vikuu vya production ni vipi? Pia ni software aina ipi unayoitumia kwa shughuli zako?

Software ninayopenda kutumia katika mziki ni FL au Fruity Loops kwa urefu. Naipenda kwa ajili ya kuandalia beats, kurekodi, kufanyia mixing and mastering.

Pia kuna Cubase ambayo naitumia kufanyia production. Pia kuna uwezekano wa kuzitumia zote kwa pamoja.

Mikono, unapiga vyombo vipi vya mziki?

Kwa kweli katika vyombo vya live sio vyombo vingi naweza kuvitumia, napenda kutumia tu keyboard. Najua kupiga hizi percussions kama vile tumba.

Unapopata kazi, huwa unaanza vipi kuunda mdundo, kuingiza vocal hadi kuukamilisha? 

Ninapopata kazi kwa kupitia msanii au hata producer mwenzangu cha kwanza ninacho kiangalia ni kichwa changu kimekaaje? Hapa namaanisha kuwa nahakikisha kua kwa mda huo sina stress, sina jambo linalonisumbua kichwani au kunipa mawazo. Kama naona au nahisi kuna kitu kinanisumbua kichwani huwa sipendi kufanya mziki.

Mziki unahitaji utulivu, kichwa kitulie.

Unapounda mdundo ambao mteja hajaukubali huwa unajiskiaje kuona kazi yako imekataliwa?

Ninapounda mdundo na kisha kuumpa msanii na akaukataa cha kwanza ninachokifanya ni kufurahi kwanza, kwani naona kuna kitu kipya nitakipata kutoka kwa huyu mtu. Ila sijawahi kuona mtu akikataa beat yangu ila mara nyingi wanashauri cha kuboresha, cha kuongeza au hata kutoa au hata kusema nitoe melody iliyopo na kuweka nyingine.

Kwangu mimi mtu anapokataa tulichokifanya sio ishu sana kwani ili muweze kupata kitu kizuri lazima ku share idea kwa mziki mzuri haufanywi na producer peke yake bali kwa kushirikiana na watu tofauti. Kwa hiyo mtu mwenye mawazo tofauti siwezi mchukia kwani ili upate kitu chochote kizuri lazima upate ushauri.

Nimeona ulihusika pakubwa kwenye mradi murua wa Fivara, Fikra Ni Vazi La Rap. Mlipataje kufanya kazi pamoja kwani naona mli blend vizuri sana?

Fivara mimi napenda kumuita Nyati. Alikuja studio, Kibamba(Touch Music) na akatukuta mimi(Mikono) Professor Ludigo, Producer Biggy aka Mbanje Mbanje. Biggy namkubali sana, tutamzungumzia siku nyingine kwani amechangia pakubwa kwa maswala ya Hip Hop.

Fivara alikuja studio kwa ajili ya akina Ludigo na Biggy ila alipokua pale aliskia midundo ninayofanya akaniambia ameipenda sana. Akaniambia kuwa anataka kuandaa mradi wake na angependa tupige kazi pamoja. Kisha nikampa mdundo flani pale akachana pale ila nikampa aende nao akaandalie nao wimbo. Kwa wakati ule Fivara alikua ni mwanafunzi St. Joseph na mimi nilikua najua jamaa yupo shule anasoma, hana kazi hivyo ningesema anilipe kila kazi laki mbili au tatu hatoweza. Kwa hiyo nikaamua kufanya kile kinachowezekana.

Kando na Fivara ni mradi wa emcee gani ulipohusika pakubwa?

Wasanii ni wengi nimepiga nao kazi ni wengi sana. Nimefanya kazi na kaka Saigon, Damian Soul, Juma Nature, Dully Sykes, Rado(Kiraka) na tunafanya nae mradi kwa sasa. Wasanii ni wengi na kuwataja hata nashindwa.

Hivi karibuni nikiskia kazi yako na Kinya Mistari, Muda. Kando na wimbo huu kuna kazi zako nyingine ulizofanikisha ni zipi ambazo kuna uwezekano zimetupita?

Kinya Mistari au Kinya Wa Ambassador ni wa miaka mingi kabla mimi sijasafiri kwenye South Africa tulikua na group lilikuwa linaitwa Ambassadors. Kwa kundi hili kuna mimi mwenyewe , Kinya, Super, Justine, Vista, Pete(R.I.P), na Sule Ghost alieniita mimi Mikono Ya Kazi. Wote tulikua kundi moja.

Kinya aliaanda wimbo unaoitwa Kaka Zako ambao ulifanya vizuri kwenye radio lakini kama unavyojua unaweza ukawa na ngoma kali ila usifike kokote. Pia hivi karibuni tunatarajia kuachia ngoma yake mpya kali sana inaitwa Vikwazo pamoja na ngoma nyingine kibao ambazo zipo studio tunaziandaa. Hivyo mtegemee mengi toka kwa Kinya na wengine wengi.

Changamoto unazokabiliana nazo kwenye kazi yako ya production ni zipi?

Changamoto kubwa ninayo kutana nayo kwenye maswala mazima ya production ambayo hunikwaza ni pale unapoweka mda wako kufanya kazi na mtu halafu mwisho wa siku mtu anabadilika, ni kitu ambacho kinaumiza sana.

Wacha niwe muwazi, wasanii wengi si wakweli wawe ni ma star, sio ma star, underground au mkondo mkuu, yaani asilimia kubwa sio wakweli.

Ninapozungumzia kuwa sio wakweli kwasababu msanii anapokuja kwako anakuja mikono nyuma kama mtu alieenda kuomba kazi, waona? Mtapanga mipango mizuri, mnaelewana, kisha mnaanza kazi ila anachukua midundo yako, anaenda kwa producer mwingine, wana sample beat zako, kwa idea zako bila idhini.

Changamoto nyingine ni kuwa nilishawahi kufanya kazi na msanii flani; kwanza tulitoa singles kadhaa kabla ya kutoa albam. Tulifanya video kazi ikafika mbali. Kuna msaniii anaitwa Ishi yuko Philadelphia, America. Msanii yule aliskia kazi yangu kwa njia ya mitandao ya kijamii na akaomba nimtumie midundo tufanye nae kitu. Huyu dogo Ishi alikuja studio na kuhamisha albam nzima na kuipeleka studio nyingine, kitu ambacho kiliniumiza sana na sitoweza kusahau.

Pia kuna mwingine naye nili play part kubwa kwa albam yake ila mwisho wa siku hakuna nilicho kipata. Changamoto ni kua kwenye kazi watu wanakuwa wa binafsi, waongo. Wakati mwingine msanii mwenyewe hana nauli au unagharamia kula ila mwisho wa siku akiona kazi imepokelewa vizuri anasaliti makubaliano.

Viwango vya production Tanzania na Africa Mashariki unavionaje, tuna uwezo wa ku produce kazi nzuri kama wenzetu walio mamtoni?

Kwa upande wa viwango vipo vizuri ila wacha kwanza nizungumzie hapa hapa nyumbani(Tanzania) kwani nina uzalendo mazee. Kazi zipo, nzuri na kubwa sana. Ma producer tunajitahidi kufanya vitu vizuri ila utofauti tunaouona ni kuwa studio nyingi tunazozitumia sisi tunatumia software ilhali wenzetu wanatumia hardware.

Quality ya mziki wetu huwezi kuulinganisha kwa mfano na mziki anaofanya Dr. Dre kwa sababu viwango vya studio zetu hazipo vizuri kama za wenzetu waliopo mamtoni.

Ndoto zako ni kufanya kazi na ma emcee gani hapo mbeleni?

Napenda kufanya kazi na mtu yoyote ambaye anaweza ku deliver na jamii ikamuelewa, ikajifunza na kupata burudani toka kwake. Mimi huwa siangalii majina au hela au umbo la, ninacho angalia je huyu ni mtu sahihi wa kufanya nae kazi? Ninachoangalia ni je watakaomskia watajifunza toka kwake, taifa litanufaika na kazi zake?

Ila mtu ambaye napenda kufanya nae kazi ni kaka mkubwa Rado ambaye tushapiga nae kazi, Azma pia ambae nishafanya nae. Fid Q ningependa kufanya nae kazi, kuna Young Lunya, Nash Emcee, Nikki Mbishi, Mr. Blue(Byser) ni miongoni wa wasanii ningependa kufanya nao kazi.

Pia kuna mtu anaitwa Khaligraph Jones huyu hata iwe kesho au lini ningependa kufanya nae kazi, namkubali sana jamaa.

Mtazamo wa watu wengi kuhusu Hip Hop ni kua ni mziki wa kihuni, unalizungumziaje swala hili?

Bro, Hip Hop sio mziki wa kihuni. Hakunaga mziki wa kihuni duniani kwa sababu ukiangalia hiyo Hip Hop imesaidia vitu vingi sana kwenye jamii. Hip Hop ni maisha ila kuna baadhi ya wasanii Wana tabia za kihuni.

Hip Hop kweli. Wapinga kweli ndio wanaopenda kusema Hip Hop ni mziki wa kihuni. Ila sijawaskia watu wakisema bongo flava mziki wa kihuni wakati bongofleva watu wanaimba kila siku matusi. Hip Hop ni mziki naweza kukaa na familia yangu iwe ni mke, mtoto, baba, mama au hata jirani na tukaskia wote vizuri bila tatizo tofauti na bongo flava.

Hip Hop inaonekana mziki wa kihuni kwasababu unasema kweli!

Je kazi hii inakulipa? Na kando na kuwa producer je unajihusisha na shughuli gani zingine?

Kiukweli hii kazi bado haijanilipa. Ukiangalia muda na pesa niliotumia kutengeneza kazi mpaka kufikia hapa nilipo bado haijanilipa ila inanisaidia kwa sababu inanipa connection, nakutana na watu tofauti, wafanya biashara, wengine wakulima, ma doctor, ma engineer, wanapenda ninachokifanya.

Mwisho wa siku hawa watu wanakupa mchongo ambao unawezesha kuongeza kipato ila mziki kama mziki bado haujanilipa.

Ungeshauri nini wana Hip Hop na mashabiki wa Hip Hop kiujumla kuhusu mziki huu?

Ushauri wangu kwa yoyote anaefanya Hip Hop kama vile msanii, producer na kadhalika ni kuwa ili kuweza kufikia pale tunapowaza kufikia tuache ubinafsi. Mimi napenda kuzungumza ukweli na mimi sipendi unafiki.

Kwa mfano unakuta kuna msanii umemtangulia mwenzako kwa jina au umejulikana na kisha anapo kuomba featuring unamvimbia. Pia mashabiki wa Hip Hop pia tuwache unafiki, tukikaa mtaani tunaongelea Hip Hop ila tukienda YouTube tunaenda kuangalia vitu vingine tofauti na Hip Hop japokuwa sio mbaya kufuatilia mambo mengine kwani lazima tujifunze. Lakini ushirikiano ndio kila kitu, bila ushirikiano hakuna kitu.

Unaposkia kwa mfano Fivara kaachia kazi basi wote tumsupport ila tukileta ubinafsi basi hatutoweza na ndio zinaanza kejeli kuwa mziki wa kihuni kwani hatuelewani. Ukiangalia bongo flava kila kunapokucha utaona kua huyu kamshirikisha huyu ili kazi ziende ila kwenye Hip Hop hicho kitu hakuna, wachache sana kwa sababu ya ubinafsi.

Tuache ubinafsi, tushikamane, tushirikiane, tusogee..

Kumalizia, ungependa kusema nini kingine ambacho sijakuuliza?

Cha kwanza Mungu akubariki wewe unayenihoji kwa sababu kuna watu wengi sana wanazitafuta hizi nafasi. Kwa hiyo kama wewe umeweza kuskia kazi zangu na kunitafuta na kunihoji ili watu waniskie na wanifahamu kuwa mikono anajihusisha na nini na anapatikana wapi na anafanya nini, hilo hujaniuliza kwanza, naomba niliongelee hili Mungu akubariki sana.

Hiyo nguvu isiishie hapa, isiishie kesho, ifike mbali na nakutakia kila la heri kwa kitu unachokifanya na naamini kwa nguvu za Mungu tutafika mbali. Watajulikana watu wengine kupitia hicho unachokifanya.

Kingine, kwa ma producer kwanza kabla sijaenda kwa wasanii; ma producer tuache kuvimba. Ma producer tunavimba sana. Pia ma producer tuwe wa kweli, msanii kama mbovu mchane tu, “Babu we mbovu”, na kama ni mtu mzima mwenye akili timamu ataelewa na atajirekebisha. Mimi binafsi sina tabia ya kumsifia mtu. Pia tuache ubinafsi na tushirikiane hata kama tunafanya mziki tofauti.

Wasanii wengine wa Hip Hop tofauti na wa bongo flava ni kua wanapokuja studio anajiamini kupitiliza hadi hataki kushaurika kabisa kuhusu anachokifanya. Wasanii wa bongo flava unakuta waskivu sana tofauti na baadhi ya hawa wasanii wa Hip Hop, daah, kaka, changamoto.

Mikono anapatikana vipi kwa yoyote ambaye angetaka kukutafuta pengine mfanye nae kazi?

Mimi napatikana kwa namba za simu +255 742 364 945 au +255 710 647 220. Hizo ndio namba zangu zinapatikana.

Instagram: Pro_Mikono
Facebook: Mikono Ya Kazi
YouTube: Pro_Mikono
Email: mikonomusic002@gmail.com

Na kingine ni kuwa mimi ni producer huru ambae nipo mwenyewe na kama msanii yuko mkoani na studio iko mkoani tunaweza kuwasiliana tukafanya makubaliano, tukakutana tukafanya jambo.

Shukran.