The Vedette

Ian Kafuna anayejulikana kwa jina la kisanii kama The Vedette, ni rapper wa Kenya anayeishi Mombasa. Ameachia EP ya nyimbo 4 inayoitwa Who Am I? na kwa sasa inafanya vizuri sana katika majukwaa ya upigaji muziki (DSPs). Iwapo ukuwahi jua, The Vedette ndiye mwanzilishi wa jukwaa la Hip Hop linalojulikana kama Rap Knights. Jukwaa lilianza kwa kusaidia wasanii wa Pwani pekee lakini baadaye likapanuka na kuangazia Hip Hop kutoka nchi nzima ya Kenya.

Micshariki Africa ilikutana na The Vedette ili aweze kutufahamisha kuhusu mradi wake wa hivi majuzi wa Who Am I? Pamoja na kutupatia mtazamo wake kuhusu hali ya sasa ya Hip Hop ya Kenya . Soma mahojiano haya aliyofanya na Musiq Jared.

Tupe historia fupi kuhusu The Vedette , majina yako halisi na ulianzaje kama msanii wa Hip Hop na mwanaharakati?

Jina langu ni Ian Kafuna . Sikumbuki ni lini nilianza kurap. Ni jambo ambalo nimekuwa nikifanya kwa muda mrefu sana. Nikiwa shule ya msingi, nilikuwa sehemu ya kikundi cha watu watatu wa kurap, tulijiita Mission Boys. Katika shule ya upili, nikiwa pale Thika High Way, nilikuwa sehemu ya kikundi kingine cha rap. Tulijitengenezea jina wakati huo.

Lakini ili kujibu swali lako vizuri naweza sema kua nilirekodi rasmi wimbo wangu wa kwanza mnamo 2013 nikiwa Chuo. Miaka miwili baadaye nilitoka kwenye game. Nadhani ndiyo sababu unaweza kusema "harakati" ilianza, ingawa sijawahi kujiona kama mwanaharakati. Nilikuwa na msukumo wa kufanya mambo, na kusema mawazo yangu na nadhani hivyo ndivyo imekuwa.

Kabla hatujazungumza kuhusu EP yako ‘Who Am I?', una mradi wowote wa pamoja ambao ulifanya hapo awali kabla ya kupumzika kutoka kwa muziki?

Ndio, nilifanya single kadhaa. Nimefanya kazi na mtayarishaji Emmy Dee, alirekodi kama nyimbo 4 za kwanza nilizowahi kufanya. Nimefanya kazi na Teknixx, na rafiki yangu wa muda mrefu Petrooz, ambaye alitayarisha EP yangu mpya. Nyimbo nyingi zilipotea kwa wakati, lakini zingine ziko  Spotify na Apple Music.

Ni sababu gani kuu iliyokufanya upumzike, ulikuwa uamuzi wa kibinafsi au ni kwa sababu ya watu (wanaokuzunguka)?

Kusema kweli, kuna mambo mengi. Tunaweza kufanya mahojiano yote kulingana na hilo swali lako. Lakini nitaweka kwa ufupi. Kwanza, sikuwa na pesa. Nilikuwa bado chuoni, nikipata usaidizi kutoka kwa wazazi wangu. Sikuweza kumudu muda wa studio, achilia mbali utangazaji na uuzaji. Lakini hii ina uhusiano mkubwa na muundo wa mfumo wetu wa muziki nchini Kenya.

Kuiangalia kutoka kwa pembe ya biashara, ilikuwa uwekezaji mbaya. Muda na rasilimali nilizoweka hazikunipa matokeo niliyotaka. Kwa hiyo nilichukua jukumu la kuisoma tasnia hiyo na kujua jinsi inavyofanya kazi na hapo ndipo nilipokodolea macho kuibua mambo yaliyokuwa yananirudisha nyuma, na si mimi tu, wasanii wengi wa nchi hii. Jambo la pili lililonifanya nirudi nyuma, nililigusia katika ubeti wangu wa pili wa wimbo wango Who Am I? Inabidi usikilize ili kujua.

Wewe ndiye mwanzilishi wa Rap Knights, blogu inayoangazia Hip Hop ya Kenya. Hivi majuzi ilitoweka kwenye tovuti, ni nini kilitokea ukizingatia kuwa ilikuwa moja ya jukwaa linalokua kwa kasi nchini Kenya?

Rap Knights ilianza kama blogu ndogo inayoangazia msanii wa Pwani (ya Kenya), lakini haraka niligundua kuwa kulikuwa na mahitaji ya makala na hadithi halali za Hip Hop kote nchini. Na ninamaanisha habari halisi, makala za kujenga, sio porojo za kawaida tunazopata kutoka kwa blogu zingine. Picha niliyokuwa nayo kwa Rap Knights ilikuwa kubwa kuliko blogu tu, nilitaka iwe na athari, na kuinua taaluma za watu.

Ilikua ngumu sana kuiendesha, ukizingatia ratiba yangu ngumu sana. Nilijua nilihitaji msaada. Baadhi ya watu waliingia ndani na kusaidia sana kusukuma ajenda, kama vile Musiq Jared na Kev The Deejay. Lakini nilijua kwamba kutimiza ndoto zangu kikamilifu, nilihitaji kuacha kuifanya kama uraibu wangu. Nilivuta wavuti chini ili niweze kuirekebisha, na kuifanya ifanye kazi kama nilivyotaka. Wakati huo huo ninataka kila mtu anayechangia alipwe fidia kwa kujitolea wakati wake kwenye shughuli hii. Kumekuwa na vikwazo vingi, lakini nimekuwa nikipiga hatua nyuma ya pazia na hivi karibuni tutakuwa hewani tena. Nilitarajia mwaka huu ungekuwa mwaka wakurudisha tena Rap Knights, lakini mazingira yamenilazimu kuahirisha tarehe za uzinduzi hadi mapema mwaka ujao.

Hebu tuzungumze kuhusu mradi wako wa hivi karibuni 'Who Am I?' Tupe mchakato wa kuandaa mrafi huu, msukumo nyuma yake na wale wote walio nyuma ya pazia walioiwezesha.

EP ilikuwa zawadi ya siku ya kuzaliwa kusherehekea miaka 30 ya kuwepo. Katika miaka yangu yote 20, nilifanya mambo mengi sana, nilivaa kofia nyingi sana. Nimekuwa mwanablogu, mratibu wa hafla, MC, mpangaji wa safari, mtaalamu wa mikakati ya uuzaji, na mpiga picha mtaalamu. Nimekuwa na vitambulisho vingi sana lakini moja ambayo sikuwahi kupata kujitambulisha nayo ilikuwa utambulisho wangu wakua mchanaji.

Watu wengi walishtuka nilipoachia EP kwa sababu hawakujua ninaweza kurap. Jina la EP, Who Am I? kwa kweli ni mradi wenye nia ya kujibu swala la utambulisho wangu. Nilitaka watu waone upande wangu ambao hawakuwahi kuuona. Wakati huohuo, nilitaka kuwakumbusha wale walionijua tangu zamani  kua mimi ni nani. Nilitaka kueleza ukuaji wangu kupitia mistari yangu, ingawa nilikuwa nimekaa pembeni. Tena, zaidi ya haya utayaskia kwenye wimbo wa kwanza wa EP Who Am I?

Kati ya nyimbo nne, ni ipi unayoipenda zaidi, na kwa nini?

Hiyo inabidi kuwa Lord Forgive Me . Inazungumza juu ya tukio la kutisha maishani mwangu ambalo lilibadilisha maoni yangu juu ya dini na Mungu.

'Lord Forgive Me' ni ngoma ninayoipenda kutoka kwa hii EP yako . Ninapenda kemia uliyo nayo na Viquee Ofula , yote yalianzaje? Je mlishawai kufanya kazi pamoja hapo awali?

Viquee ni mtu ambaye nimemfahamu kwa muda mrefu. Nilishakutana naye mara kadhaa hapo awali, na bendi yake, Juukua Band. Ni mwimbaji mwenye kipawa kikubwa na mtu ninayemheshimu sana. Kuwa mkweli, sikujua kuwa atakuwa kwenye EP. Nilikuwa nikipambana na kiitikio cha wimbo huo, na Crush pia (wimbo wa pili kwenye EP). Producer wangu aliniambia nisiwe na wasiwasi, atalitatua. Sikujua kama Viquee ndio angebariki nyimbo zangu .

Niliposikia toleo la mwisho, nilivutiwa zaidi. Ni kama alijua kile nilichotaka. Kama nilivyosema, hatukuzungumza chochote kuhusu wimbo huo. Kweli EP nzima nilikuwa nairekodi kwa siri. Sikuwa na uhakika nitaiachia. Kwa hiyo niliposikia wimbo huo, nilimpigia simu. Ilikuwa ni usiku sana, sikuwa na uhakika kuwa alikuwa macho, ila mimi nilitaka tu kumjulisha jinsi nilivyokuwa na shukrani.

Umeamua kusukuma mradi huu kwenye DSP, ni nini siri ya hili kwamba wasanii wengine wanapaswa kujifunza kuhusu DSP na labda kuacha kutegemea YouTube sana?

Kwa nini utumie jukwaa moja tu wakati kuna chaguzi zingine kadhaa? Pia, nilikuja kugundua, watu wanaotumia majukwaa kama Spotify, Boomplay, hawa ni wasikilizaji sugu. Asilimia yao ni kubwa kuliko watu wanaotumia YouTube. Hao ndio watumiaji wa muziki ninaowalenga. Pia, YouTube ni kwa ajili ya video. Bado sina video.

Neno la ushauri kwa wasanii wajao wanaojitahidi sana ila wanakaribia kufikia hatua ya kukata tamaa?

Muziki huchukua muda na pesa nyingi kabla ya kuanza kurudisha mapato yako. Inaweza kukuchukua miaka kabla ya wewe kuanza kupata marejesho. Usiamini unachokiskia. Ushauri wangu bora ni kuwa na angalau chanzo cha mapato ambacho kitakusaidia kufadhili miradi yako.

Baada ya 'Who AM i?' nini kinafuata kwa The Vedette ?

Kusema kweli sijui. Ninahisi kama bado sijazama ndani ya kima cha ubunifu wangu. Nina mengi zaidi ya kutoa. Na kama ninavyosema katika wimbo wa kwanza wa EP, sikuwahi kutaka tasnia iamuru kile ninachofanya au kusema, nitafanya tu ikiwa ninahisi.

Neno kwa mashabiki wako?

Hahaha, nina mashabiki sasa? Naam, MASHABIKI WANGU, hahaha , asante kwa support yenu. Kwa kweli sikutarajia mapokezi makubwa kama haya, ukizingatia nimekuwa nje kwa muda mrefu. Wasanii wachache sana wameweza kufanikisha hili. Kwa hivyo asante kwa kunifanya nijisikie kama Nyashinski, hahaha.

Je, una maoni gani kuhusu hali ya sasa ya Hip Hop ya Kenya?

Kuna kazi nyingi zinazohitaji kufanywa. Wapo watu wengi ambao wamejizatiti kuusukuma na kuutangaza utamaduni huo bila kupata chochote. Tunahitaji kuwaunga mkono zaidi watu hawa.

Unapatikana wapi kweny mitandao yako ya kijamii rasmi?

Facebook: The Vedette
Twitter: The_Vedette
Instagram: The.vedette

Neno lako la mwisho?

Tena, asante sana kwa kuskia muziki wangu kwenye DSPs zenu pendwa. Haya ndiyo yote niliyotaka. Ninawashukuru sana.