Msanii: Miracle Noma
Mixtape: Fundikira
Tarehe iliyotoka: 26.11.2019
Nyimbo: 15
Wapiga midundo na ma producer: SlimSal, Qwitch, Ringle Beats, Kibabu Wapoteen, 10th Wonder, Bin Laden
Mixing & Mastering: Rama Genius
Studio: AJ Records
Baada ya kutoa wimbo wake wa kwanza akiwa na Bello Bin Laden uitwao Fire na kuchana humo ndani kuwa yeye ni emcee wa maajabu, rafiki yake wa karibu aliweza kumbatiza yanki flani toka Dodoma jina Miracle. Hapa ndipo lilipozaliwa rasmi juba la emcee Miracle Noma kisanii.
Miracle Noma alizaliwa miaka ya tisini kule Dodoma na anatambulika rasmi kama Said Yahaya Hussein. Miracle alianza kupenda mziki wa Hip Hop akiwa mdogo na alijikuta akipata inspiration na kuanza kuandika mistari yake mwenyewe 2010 na 2012 alifanikiwa kujiunga na kundi la Hip Hop toka Dodoma, Dom Down Click (D.D.C).
Baada ya kurekodi wimbo wa Naelekea Ikulu 2013 na kuuachia 2014 chini ya Duke Tachez aliendelea kuachia singles kadhaa. Akishirikiana na crew nzima ya D.D.C walifanikisha kuachia mixtape yao pamoja na Duke Tachez The Element Vol 2. Ilipofika mwaka wa 2019 Miracle Noma alifanikisha ndoto yake ya kuachia mradi wa kwanza, mixtape aliyoiita Fundikira.
Fundikira alikuwa Mtemi (chief) maarufu katika nchi ya Tanganyika (enzi hizo) na majina yake kamili yalikuwa ni Mtemi Said Fundikira (Sultan Said). Japokuwa Miracle Noma ni mzaliwa wa Dodoma asili yake ni Mnyamwezi, mtu wa Tabora alipokuwa anaishi Mtemi wa kinyamwezi Said Fundikira. Hivyo basi Said Yahaya aliamua kumuenzi mtemi wa Unyamwezini ambaye ni wajina wake (namesake) kwa kuuita mradi wake Fundikira.
Miracle Noma
Baada ya Intro albam hii inaanza na wimbo unaobeba jina la albam hii Fundikira ambao kwenye kiitikio ameshirikishwa producer Rama Genius wenye mdundo hard-hitting na vinanda mzuka sana. Kwenye vesi ya pili Miracle anaonesha ujasiri wake akirusha dongo kwenda kwa Young Dee akisema,
“Naona mnafoka hamna focus/
Bongo Bahati Mbaya ngoma nzima naona four bars/
Hiyo sio ngoma ni chorus/
Ambayo mtangazaji wenu anasema ni conscious/
Mnadhani Hip Hop ni game la ki Nokia/
Mje mcheze kama game la ki nyoka/”
Mpate fame na madem wa Kitonga/
Mskike kila sehemu na show za laki moja/”
Mashairi yanaendelea freshi kwenye Pingu akiwa na Eddy Mc na wimbo ni mzuri uliotumia sampuli toka kwa Willie Hutch, Hospital Prelude of Love Theme ambayo pia ishawahi tumika na ma emcee kibao kama vile Masta Ace – Good Old Love, Prodigy – Still Shinning na Nipsey Hussle – Blue Laces.
Team work nzuri ya Miracle na Eddy Mc inaonekana kwenye wimbo unaoelezea matokeo hasi ya utumiaji wa tungi kwenye Mua ulozamisha meli wenye mdundo mzuri. Mistari ya ucheshi inasikika pale wawili hawa wanapokwenda kupiga tungi.
Uwezo wa kuandika hadithi unazidi kuonekana vizuri zaidi kwenye wimbo ambao upo personal zaidi kwa Miracle, Dear Mama. Beat ni gitaa tu linapopiga freshi kwenye wimbo ambao Miracle anafungua moyo wake na kuweka hadharani mapenzi yake juu ya mama yake kwani hadi Miracle anajizuia kulia anapotema vesi moja la nguvu kwenye wimbo huu. Jela pia akiwa na Bin Laden ni story ya tahadhari kwa yoyote anayedhani kuwa ukienda kule ni hotelini.
Kwa ma emcee waliopo handakini huwa wanapitia vishawishi vingi kam watu wakijaribu kuwaambia waache kukaa underground na kwenda kuishi maisha ya ki mainstream. Wimbo Wanaongea akiwa na Rama Genius unaongelea changamoto hizi akisema Miracle kwenye mdundo moto sana kuwa,
“Yeah, wanasema Miracle acha hizo ngumu/
Rap kama Izo Bizzness, mwachie hizo Unju/
Waachie MaKaNTa, Watunza Misingi/
Fanya kama Bill Nass hapa utavunja kichizi/
Komesha ngoma kama Young Dee chupa kali/
Tutakubali uwezo unao, Tatizo misingi/
Piga picha na mademu wapo na chupi hizo ndio kiki/
Maana utaskika hadi kwa Suddy ShiLaWaDu/”
Kwenye kiitikio Rama Genius anawaua na kuwakejeli walio na fikra potofu dhidi ya Miracle akiimba freshi kwenye kiitikio.
Mada ya mahusiano ya mapenzi imegusiwa kwenye wimbo wa Mimi Na Wewe uliondwa na Ringle Beats
Ugumu wa maisha umesikika kwenye wimbo wa Shida . Shida ni story inayosikitisha sana kuhusu maisha ya binti flani anayepitia maisha magumu.
Uwezo wa Miracle kuchagua mdundo unaoendana na mada anayochana unaonekana na pia uwezo wake kuweka hisia kwenye nyimbo hizo. Hisia zake unaziona dhahiri kwenye wimbo wa Walimu Wetu ambapo Miracle anaskika akilia ndani ya booth! Wimbo unaoelezea unafiki wa watu tunaoishi nao akitema madini kibao hapa kama vile,
“Sometimes asubuhi napiganga chai kavu/
Haya maisha ni mafupi na hatukai babu/
Usione mtu amekufa ukadhani amedai sub/
Marafiki wanafiki uko hai wana snitch/
Ukifa wanakulilia sana Insta, “Mwana I miss you”/”
Miracle Noma anatuonesha uwezo wake wa kujigamba kwenye wimbo kama Ninja Assassin pamoja na Maangamizi. Maangamizi ni nondo tupu kwenye wimbo wa dakika tano ambao yupo Miracle, Javan, Eddy Mc, Meddy Samurai, Dod Gang, Megsan,Ben na kwenye doria ya mdundo ni producer Qwitch.
Muacha mila ni mtumwa, na Miracle kwa kulifahamu hili ameamua kuenzi vya nyumbani na japokuwa kazaliwa Dodoma, Mnyanyembe huyu kaamua kuwa lazma jina la mtemi wao wa kitambo litaendelea kuishi na kukumbukwa. Hakuna njia nzuri ya kumfanya chief huyu kuishi kama kumuenzi kwa kupatia mradi jina lake. Mradi huu umetupa fursa ya kuzidi kufanya utafiti kuhusu mtemi huyu na kuthamini historia yetu.
Mradi huu ulikuwa ni mzuri sana; ki midundo na ki mashairi. Pia ma emcee waalikwa walijitahidi kutendea haki mialiko yao kwenye mradi huu. Kama vile wajina wake Said amehakikisha kuwa ameacha historia ya mradi ambao utakumbukwa na vizazi vya baadae. Said Yahaya kama vile Mtemi Said ni Fundikira.
Kupata nakala yako ya Fundikira wasiliana na Miracle Noma kupitia:
Facebook: Miracle Noma
Instagram: miracle_noma
Twitter: miracle_noma