Mwaka huu wa 2021 ndio ulikuwa mwaka ambao tulianzisha rasmi tovuti yetu ya Micshariki Africa baada ya kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kuendeshea harakati zetu. Jambo hili lilituwezesha kwa mara ya kwanza kuanza kuorodhesha rasmi ngoma za wana Hip Hop zinazotoka pamoja na miradi(EP, Mixtape na Album) yao ambayo hapo awali haikuwa na sehemu rasmi inapopatikana.
Kutoka kwenye jedwali hili nimeamua kuandaa orodha ya album 12 bora za mwaka huu zilizo toka Africa Mashariki kwa mpangilio wa tarehe zilivyotoka.
1.Kitu Sewer x Maovete - KiswaHealing

KiswaHealing toka kwa Maovete wakishirikiana na Kitu Sewer kwangu mimi ndio mradi nilioupiga sana mwezi wa January. Mradi huu wa kimapinduzi uliundwa ki ustadi sana ukitumia sampuli nzuri pamoja mashairi mazuri toka kwa Brima na Kitu Sewer. Mradi kwa ajili ya kizazi. Mradi huu uliniburudisha sana kando na kunielimisha na mistari ya kijanja, ya kiucheshi na ya kuchangamsha bongo. Ngoma zilizotikisa spika zangu ni Kun Fay Kun, Utakwenda Wapi, Endelezi, Committee Ya Maovete, Drunken Master (Barua), Pandemic (Remix), Haina Makelele, Checki Number pamoja na Nayo Nayo.
2. Watunza Misingi – Misingi Na Hip Hop 2

Watunza Misingi hapo mwanzoni mwa mwaka huu waliamua kutukumbushia kuhusu nguzo za Hip Hop kwa kutupatia mradi wao wa pili Misingi Na Hip Hop. Mradi huu ambao kando na kua Boombap mwanzo mwisho umejaa mashairi toka kwa ma emcee wanaojiita Watunza Misingi kama vile Kaa Feel, Rado Kiraka, Adam Shule Kongwe, Kiraka Tosh(From Kwembe), Miracle Noma, Jesus Rebirth, Kella B, Jedikouga(R.I.P), Momumo, Opobo na wengine wengi. Mradi ulikuwa na nyimbo nyingi sana nilizozipenda kama nilioupenda binafsi sana Chem Chem Na Wana, Roho Ya Kwanini, Amsha Mizimu,Hauhusiki, Matusi na kadhalika.
3. Mantiki Barz – Uzito Wa Juu

Mantiki Barz mwaka huu alikuja tena na mradi wake Uzito Wa Juu ambao kama ilivyo kawaida yake uliundwa kwenye msingi wa mashairi mzuri, midundo mizuri na mada tofauti tofauti alizoweza kuziongezea kama vile kifo kwenye Nitakufa na changamoto za kuishi ughaibuni kwenye Mbali Na Nyumbani.
4. Shahidi The X – Calibur – X-Files

Niliposkia Shahidi The X-Calibur anatoa album yake ya kwanza nilisaka mawasiliano iliniweze pata nakala. Kwa mtu ambaye tulikuwa tunafahamu uwezo wake kwenye vilinge(rap battles) nilitaka ona je ikija kwa upande wa mradi ataweza kutupatia kitu cha nguvu? X-Files ndio matokeo ya juhudi zake za kutupatia mradi na japokua ulikua ni mfupi wenye nyimbo 11. Mradi huu ambao ulisimamiwa asilimia mia na producer Musyoka ni mzuri sana na nyimbo ambazo nilizipenda ni kama Keep Going On Part 1 na 2, Addicted, Where Am From, Victory na Live Life.
5. Adam Shule Kongwe – Uwanja Wa Fujo

Baada ya ukimya wa takriban miaka miwili Adam Shule Kongwe alirudi tena na mradi wake Uwanja Wa Fujo. Mradi huu ulizidi kuonesha uwezo wa emcee huyo toka Singida x Dodoma kwani ulikuwa wenye hadithi, mafunzo, madini, nondo pamoja na midundo mizuka sana toka kwa Sigga, Abby Bangladesh, Pallah Midundo, Patrino, Duke Tachez pamoja na SlimSal. Ngoma zilizokuwa zinapasua spika zangu ni kama Jumlisha, Shida, Sio Sawa, Hawa Viumbe, Subira, Wa Ngau, Lucky Me na Staki. Album moto sana
6. Kevin Catalyst x Muki Mala - Refraction

Mwezi wa sita ma emcee kibao waliingia studio na kutubariki na zaidi ya miradi 10 toka Africa Mashariki ikiwemo mmoja toka Uganda tuliofanikiwa kuunasa wa Roma Maenu – Ekituufu Bakimanya. Hata hivyo mradi uliokua tofauti mwezi huu wa sita ni wa Kevin Catalyst na Muki Mala - Refractions. Mradi huu wa boombap mwanzo mwisho ni mzuka sana na ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kuwaskia Catalyst na mwenzake Muki Mala na hawakuniangusha baada ya kuununua mradi huu siku waliyokuwa wana launch mradi wake kule Dar na mie nipo Geita kama kilomita 1200 kati ya miji hii. Ngoma zilizopiga vizuri kwenye mradi huu, Mistari-Barz, Free Wheel/Free Will, Idea/Dear, Idle, Idol, Imagination/Image Nation, Mtaa, Perscreativity pamoja na Kanabo Character . Mradi ulikua na ngoma 29 pamoja na skits, mzuka sana.
7. Kamusi – Kaka Kuona Mengi

Mwezi wa July ulikuwa mwendelezo wa mwezi wa 6 kwani ma emcee waliekelea kazi kama wanavyosema kule Kenya. Ila mradi ambao kwangu ulikua wa kimapinduzi sana mwezi huu ulitoka kwa Kamusi(Scavenger/Ndege Tai) – Kaka Kuona Mengi. Aisee handaki kuna vipaji, chimba utajionea. Mradi huu ambao umesimamiwa na Abby MP toka Digg Down Records unaonesha anaweza kutamba kwenye mdundo wowote na kuchana kuhusu mada yoyote. Ngoma zake zipo tofauti sana kama vile F.B.O (Full Battle Order), Conversation, Njozi, Ghorofa La Mawimbi, Deep, Home Africa, Who Are You?! na wimbo mzuka sana Kitendawili.
8. Fikrah Teule – Wazalendo Raia

Wazalendo Raia ni album ya tatu toka kwa emcee Fikrah Teule toka Mombasa, Kenya. Kwenye mradi Fikrah ameendelea kutupatia mashairi yenye elimu juu ya midundo mzuka sana. Akitumia sauti yake nzito Fikrah ameweza kuongelea changamoto raia wa kawaida wanazozipitia maishani mwao kisiasa, kibiashara, kidini, ki elimu.
Kwenye mradi huu Fikrah amepiga kazi kadhaa na producer wake mpendwa HR The Messenger kwenye kazi mbili tu All Day na Same Language tofauti na mradi wake Azania Na Wanawe ambao ulisimamiwa asilimia mia na producer HR The Messenger.
9. Rasta Michael – Nje Ya Dunia

Mwezi wa nane ulikuwa wa emcee Rasta Michael ambaye ufanyaji kazi wake upo Nje Ya Dunia hii kama inavyoitwa album yake ya nane! Mradi huu ambao umesimamiwa na Tinie Cousin toka Cosmic Sounds ni mradi wa kishairi sana. Mradi huu ni wa uthubutu, sauti tofauti, midundo tofauti, uimbaji tofauti, Nje Ya Dunia mambo ni tofauti. Nyimbo zilizosimama ni kama Shairi,Kazi Iendelee, Fanikisha, Chagua,Cheza Unapochezaga, Juu Ya Piramid,Kiumbe Kipya, Unaweza, Huu sio Muda,Nipe Dakika kwa ufupi mradi wote!
10. Lugombo MaKaNTa – Dreams

Dreams ni album mzuka sana toka kwa mwana MaKaNTa, Lugombo. Mradi huu uliosimamiwa na magwiji wa Boombap 10th Wonder na Wise Genius kwa asilimia kubwa ni mradi wa kukutia moyo na kukuskuma kuendelea kufanyia kazi ndoto zako uwe mdogo, mkubwa, wa kike, wa kiume, tajiri, maskini, umeajiriwa au umejiajiri. Mradi huu ni mzuka sana mwanzo mwisho ukitupatia vibao kama, Kwa Mama, Hip Hop Na Wana, Dreams, Mimi Ni Nani, Dibaji, Imba, Asante Mother Nature, Hutoishi Milele, Yanatimia Part 1 & 2, Hamjui Bifu, Hawatusikilizi, Endelea Kuchukulia Poa. Si wa kukosa huu.
11. Mex Cortez – Monsoon Winds

Hatimaye Mex akatubariki na mradi mwaka huu, Monsoon Winds. Uwezo wa Mex kuchana sio tu kwa lugha mbili bali juu ya mdundo wotote na kuchana kuhusu mada yoyote inafahamika. Hivyo basi mradi huu ambao uliundwa kwa mbinu zinazofanya kazi vizuri kwa emcee huyu zinatumika vizuri tena pia. Ngoma nilizozipenda kwenye mradi huu ni kama Transformation, My Name, Esco Bars, Bilingual, African Love, Kings, Do It na wimbo wangu bora pale Raw Uncut.
12. Veryl Mkali Wao - Shadow Of Death

Mwaka huu ulikua mwaka wa baraka kwa wachanaji wa kike pia kwani baadhi yao walitoa miradi yao kama vile Vodca, Nemmy Kim na Silverstone Barz. Ila kati ya wote hawa aliefanikisha kutupatia album kamili ni Very Mkali Wao toka Nakuru, Kenya akitupatia Shadow Of Death. Shadow of Death ni mradi mzuka sana ambao unaona ukuaji wa Veryl kama mchanaji, mshairi na mtumbuizaji. Mradi huu uliosimamiwa asilimia 100 chini ya uongozi wa producer Level Next ni boombap mwanzo mwisho na una nyimbo nyingi mzuka sana kama sio zote. Miongoni ya nyimbo zilizonivutia kwenye mradi huu ni kama True Love, Boogie, Audio Biography, Triggers, Enough Is Enough, Blame Game, Precious Love, Shadow Of Death na Can’t Keep A Woman Down.
Veryl Mkali Wao kawasili.
Tupe maoni yako kuhusu album tulizoorodhesha hapo na utuambie kama unakubaliana nasi na pia kama kuna album, EP au Mixtape inawezekana haikutufikia tuambie ili tuweze kuiweka kwa orodha ya miradi hapa Micshariki Africa.
Baadhi ya album zingine nilizo ziskiza nakuzipenda ni:
Sichangi – Soundtrack To A Heart Break
Jakk Quill – Lost In Motion
Tony Kings - Black N Blue
Rabbi James – Nyuma Ya Kitabu Cha Historia
Fredrick Mulla – Moro Jazz
Hafee Mauwezo– Mwanangu
SlimSal – Blind
Ponera – DemeCrasia
Abudabi Tembekali – Chapters
Liquid Flows – Boy Wa Daggo
Miracle Noma - Straight Outta Mars(S.O.M)