Miradi 12 Bora Hip Hop Ya Mwaka 2021 Kutoka Africa Mashariki

Heri ya mwaka mpya 2023. Ni miaka miwili sasa tangu tuanzishe tovuti yenu pendwa inapokuja kwa maswala ya Utamaduni wa Hip Hop na sanaa kutoka Africa Mashariki. Kama ulivyo utaratibu wetu Micshariki Africa tunakuletea orodha ya album bora za mwaka huu ambazo zilitufikia na tuliziskia pia.

Mwaka huu tuliweza kunasa zaidi ya miradi mia mbili na kitu ya Hip Hop kutoka Kenya, Tanzania na mmoja kutoka Sudani Kusini. Kwenye mjumuisho wa miradi yote zipo EPs, Mixtapes, Albums na Beat Tapes ila sisi tutajikita kuonesha album zetu bora kwani hapa ndio tunaweza kuona ujuzi wa msanii husika.

Kazi hizi zote nimeziorodhesha hapa na unaweza kuziskia kupitia njia za kisasa za kutiririsha muziki au ukipenda streaming apps au kwa kuzinunua moja kwa moja kutoka kwa wasanii wenyewe kupitia namba zao tulizoziweka kwenye jedwali.

Karibuni mcheki album zetu bora za mwaka huu wa 2022

Watunza Misingi – Silaha Begani (Si.Be)

Mapema mwaka huu wana familia Watunza Misingi walipania kuingia vitani kulitetea bara lao la Africa ila cha kwanza walichokifanya ni kuhakikisha wameweka Silaha Begani (Si.Be). Mradi huu ambao uliundwa mwanzo mwisho na mtayarishaji mkuu wa Boom Bap Clinic (B.B.C), Black Ninja ulikuwa na mishale 22 ikiwemo intro na outro pia. Jopo zima la Watunza Misingi lilihakikisha kuwa mradi huu unakuelimisha wakati ukiburudika pia kwa kuachia vichupa vinne kwa ajili ya ngoma kadhaa kutoka kwa mradi huu.

Ngoma zangu pendwa:  Haki, Tunatenda, Tunatenda,

NuffSed - GUERILLA: Dynasties vs the PEOPLE

GUERILLA: Dynasties vs the PEOPLE ni albam mzuka sana kutoka kwa mwana 1183 NuffSed anapatikana anga za Nakuru kule nchini Kenya. Mradi huu ambao ulisimamiwa na mtayarishaji  Echo Chambers ni boombap mwanzo mwisho na haukuchoshi. Emcee huyu anaongelea mada muhimu zinazo gusa jamii yake na amesimama peke yake kwenye ngoma karibu zote isipokua pale aliposhirikiana na emcee Romi Swahili kwenye Don’t You Ever Learn na Fire alipomshirikisha muimbaji Ash. Emcee huyu kavamia ki Guerilla kwenye hii vita kati ya mabwenyenye na walala hoi, NuffSed!

Ngoma zangu pendwa:  Mzuka, Fire, Don’t You Ever Learn, Raw, Score, Nazidi, Real All The Way, Mware, State Capture + Hidden Track

Nikki Mbishi – Welcome To Gamboshi

Nikki nae hakuachwa nyuma na safari hii hakuwa Mbishi ila alikualika kwake kistaarabu kwa kukwambia Welcome To Gamboshi. Wana Micshariki Africa tulikubali wito wake na tukaanza kupiga misele taratibu ndani ya album yake ambayo kusema kweli ilituacha vinywa wazi. Kazi hii ilisimamiwa na watayarishaji kadhaa kama vile Black Ninja, Black Beats, Ringle Beats, Kise P, Paul Loops, Hunter, Chzn Brain, 10th Wonder, Gonchar/Wanene, Kita The Pro na rapper/producer SlimSal. Kama umjuavyo Nikki yeye anadondosha nondo juu ya nondo kwa kila mdundo aliopewa na watayarishaji hawa.

Ngoma zangu pendwa: Wazee Wabishi, Sinza, Nataka Kutoka, Nitumie Link, Uswazi Kishua, Straight Outta Gamboshi, Vita Ya Bengazi, Da Vinci Codes, Haijaeleweka, Adimu II, Jojo (Diss Track), Nyegere, Wanyonge, Nenda,

Trabolee x Akili Blaq – Ma Li Za Ro Ho (1NE)

Trabolee au ukipenda Tra alishirikiana na mtayarishaji Akili Blaq mapema mwaka huu na wakatupatia mradi wa kimapinduzi sana ki midundo na kimashairi. Kama hukuwahi kumskia Tra hapo awali kanda hii itakushawishi ukachimbe zaidi ili uweze kuskia kazi zake alizotoa kabla hii. TRA ni ART na hili halina ubishi; mashairi ya kijanja, ya kukufanya ujikune kichwa ukijaribu kuwaza alichokisema kama vile unavyocheza draft au chess na ukiwaza jinsi gani utafumbua njia ya kumpiku mwenzako. Akili Blaq nae kadondosha midundo si haba; si jazz, si boombap, ubunifu na uthubutu mtupu.

Ngoma zangu pendwa: We 1Ne, Rangi Zingine, Ma Li Za Ro Ho, Radiate, Sahau Shida, Hertz, Si Kioo La Tatu, Rafiki Pesa, The Healing, My Time, Born 2 Fight, Hii Spark

Maujanja Saplayaz – Ni Saa Ya Pesa

Mapacha mwaka huu nao hawakuachwa nyuma na kwa sababu time is money wakatuletea mradi Ni Saa Ya Pesa. Mradi mzuka sana huu ambao unawakuta Kulwa (K Wa Mapacha) pamoja na Dotto (D Wa Mapacha aka Nusu Trillion Dinero) wakituhamasisha twende tukatafute senti za kujikimu. Mradi una huu ambao umesimamiwa na Issam, Sigger na wengineo unaonesha maturity ya majamaa hawa toka Maujanja Saplayaz na ni Boombap mwanzo mwisho.

Ngoma zangu pendwa: Wahuni Wakubwa, Imetulia, Jioni Ya Leo, Mbugi, Chekeraa, Napo Flow, Dope

MC Sharon – The Last Will And Testament (TLWAT)

MC Sharon nae akaja na wosia na agano lake la mwisho yaani The Last Will And Testament (TLWAT). Ungedhania pengine utakuwa ni mradi wa kutuaga pengine anataka kuwaachia wadogo zake kinasa hivyo mradi utakuwa wa tafakuri na simanzi ila wapi. Mradi ndio kama unatangaza ujio wake tena baada ya ukimya wa mda mrefu toka alipoachia kazi yake ya mwisho. Mradi unaonesha uwezo wa MC Sharon kama mwandishi, mwalimu, mwana sanaa, mchanaji, muimbaji, mbeba maono, mzazi, mwanafunzi, mama, dada, mwanaharakati na pia mtu anayejivunia lugha yake ya Dhuluo. Inapokuja kwa midundo emcee huyu haogopi kutamba na mdundo wotote ule iwe umesukwa ki Boombap au ki Reggae au lugha yoyote ile iwe Kiswahili, Kiingereza na ki Luo.

Ngoma zangu pendwa: Onge Wichkuot, Tangazo Maalum, Why The Caged Bird Sings, Say My Name, Kwisha, Aliwara, Otek Small, Msafiri, So Special, Calm Down, A Page A Day, Shida Iko Wapi, Usikimye

Khaligraph Jones – Invisible Currency

Omollo amekua kwa game ya Hip Hop zaidi ya muongo mmoja. Kabla hata hajaanza kuchezwa kwenye radio zenu Omollo alikuwa ashajijengea jina mitaani na kukubalika kwa uwezo wake wa mitindo huru (freestlyes). Hivyo basi Invisible Currency kwangu imekuwa kama kitabu kinachokuletea kumbukumbu ya maisha ya emcee huyu kutoka utotoni mwake, wakati akijitafuta kama msanii hadi hivi sasa anatafutwa kama mmoja wa wachanaji bora waliowahi kutokea Kenya. Mradi ulisimamiwa chini ya lebo yake ya Blu Ink na midundo ilipigwa na Vinc On The Beat akisaidiwa kuchanganya sauti na mtayarishaji wake wa karibu Aress 66. Mradi huu ni ushuhuda tosha kuwa kila hatua anayoweka msanii kwenye sanaa yake ni dua inajibiwa pia.

Ngoma zangu pendwa: Rada Safi, Ikechukwu, Ateri Dala, Maombi Ya Mama, Wanguvu, Tsunami, How We Do, Bad Dreams, Flee, Hiroshima, The Khali Chronicles, All I Need

Adili Chapakazi – Peke Yangu

Mwanahisabati nae pia alichangamsha game na mradi wake mpya Peke Yangu. Akiwakilisha kutoka The Green City, Tanzania emcee huyu anatuletea mradi uliojaa rutuba kama mashamba ya viazi mviringo Mbeya. Kazi hii ambayo imesimamiwa na watayarishaji kama Wise Genius na Ndula B unakuonesha vile Adili bado kalamu yake ina mashairi kibao ya kuandika na mistari yenyewe imeshiba madini kama yote. Kama unataka elimu na burudani kwa wakati mmoja huu ndio mradi wako mie nimeuskia nikiwa Peke Yangu ila nimeona ni vyema niwashtue muweze kuucheki pia kwani hamtajutia.

Ngoma zangu pendwa: Nikikumbuka, Tofauti, Wanataka, Mipango Ya kiume,

Budder Manolo – Love Story

Budder Manolo alidondosha debut album ya Love Story mwaka huu. Album hii ya ki utu uzima kutoka kwa chipukizi huyu ulikuwa tofauti sana kwani jamaa aliamua kutoa elimu kuhusu swala la penzi au mapenzi na matokeo yake yalikuwa chanya sana. Mradi huu uliosimamiwa na wana Tongwe Records chini ya manahodha Tunchy Master na Wiser On The Beat ulikuwa na midundo mizuri sana iliyomuwezesha Budder kufanya yake. Dogo anaandika na kuchana vilivyo, debut na nusu.

Ngoma zangu pendwa: Mwanamke (Intro), Give Me A Hook, Mapenzi Gani, Doctor Love, Futa Machozi, Usinipe Moyo, Christmas Girl, Tunapendana, Hupati Mchumba, I Love You, Bora Tuachane, I Miss You, Dear Ex, Utanikumbuka, Kwa Nini, Sitokuacha,

Rama Wise – Mimi Ni Huyu

Rama Wise alichupikia kutoka handakini kama uyoga mazingira yalipokua sawa. Emcee huyu aliachia album yake ya kwanza mwaka huu na kusema kweli mradi ni mzuri kinoma. Kuonesha kujiamini kwake emcee huyu alipiga kazi na watayarishaji wazoefu kama ishara ya kuonesha kuwa yeye pia si haba inapokuja kwenye maswala ya kuandika na kuchana mashairi yake. Abby MP, Kise P, Mock Beatz, Gs, Duppy ni watayarishaji waliobariki mradi huu na midundo freshi ambayo emcee huyu aliitendea haki. Kosa kupata nakala yako uchekwe. Mimi Ni Huyu ni mzima wa kujipima kwa chipukizi yoyoye mwenye nia ya kutoa album.

Ngoma zangu pendwa: Ushauri Sio Amri (USA), Majaribu, Wana, Jipe Muda, Nimejirudi, Iko Hivyo…

Black Ninja – Ilolo Confirmed

Boom Bap Clinic wakiwa chini ya uongozi wa Black Ninja wamekua kila pahala inapokuja kwa maswala ya uandaaji wa sio tu singles na bali hata albums, beat tapes, eps na mixtapes zao binafsi na ma emcee kibao. Ila ilifika muda Ninja akaona ni vyema BBC wachangamshe game na album yao wenyewe. Hapa ndipo Ilolo Confirmed ikawasili. Kazi hii midundo yote mixing and mastering imesimamiwa na Black Ninja na imewashirikisha ma emcee wengi kutoka Tanzania na mmoja kutoka Kenya ambaye ni Veryl Mkali Wao.  Pia mradi ulikuwa na ma emcee wakongwe na chipukizi ambao wote kusema kweli walitendea haki mwaliko wako kwenye Ilolo Confirmed.

Ngoma zangu pendwa: Mama Ake, Hey Girl, Nitarudi, Your Love, Pole Mama, Maarifa, This Game,  10 vs 16, Maturity. Mbibi, Allah

Nala Mzalendo – Iambie Dunia

Mtu mfupi mwaka huu hakuja tu na mistari mirefu bali alikuja na moja ya album ndefu zilizoachiwa mwaka huu Iambie Dunia. Album hii yenye ngoma zaidi ya 30 ambayo ni ya pili rasmi kutoka kwa Nala inazidi kuonesha kwa nini yeye ni mmoja wa ma emcee wakali waliowahi kutokea kwenye kizazi chake. Mradi umejaa story, ushauri, mawaidha, hisia za furaha, hisia za huzuni, mapenzi, imani na ubunifu mwanzo mwisho. Watayarisha Mdachi The Funky, Wise Genius, Ben Beats, Y Soo Midundo, Catcher Beats, Patrino, 10th Wonder na wengine kibao. Diego Naladona kashinda na bao la Hand Of God kupitia mradi huu.

Ngoma zangu pendwa: Iambie Dunia, Fanya, Mabibi Na Mabwana, Malezi, Mchizi Wa Machizi, Mwambie Mama, Nakupenda Wewe, Ndugu Na Jamaa, Ng’ombe Wa Maskini, Ni Hivi, Shukrani, Sijui Mapenzi, Sio Msaada, Uhasama, Noma, Mrs Nala,

Nafsi Huru – Uhuru Wa Nafsi

Nafsi Huru aliweka sheng kando na kurudi Mombasa ili kutupatia mradi uliojaa mashamsham ya mashairi na Kiswahili cha pwani na Mombasa. Matokeo yake ni Uhuru Wa Nafsi ambao ni mradi ulioleta uzoefu wake wa miaka kumi wa kuandika mashairi, kuchana, kuimba, kupiga shoo na kurekodi akitumia vyombo “live”. Mradi huu ambao pia umeshiriki waimbaji, wachanaji na watayarishaji wenye ujuzi kama vile Ananda A World, Tutu juu ya saxophone, Chzn Brain ili kutuandalia Swahili Pop. Uhuru wa kubuni ndani ya Uhuru Wa Nafsi.

Ngoma zangu pendwa: Africa Simama, Raha, Hema Hema, I Wish, Nafasi Yako, Lost,

ChindoMan – Kijenge Juu

Veteran emcee kutoka kundi la Watengwa akifahamika kama ChindoMan aliweka rekodi kwa kutupatia mradi wa kwanza mrefu mwaka (ngoma 41) huu na kupiku ile ya Nala Mzalendo (ngoma 34). Akiwakilisha Kijenge Juu, kule Chuga emcee huyu alishirikiana na watayarishaji kadhaa wakiwemo Dully Sykes, Double, T-Touch, Palla Midundo na wengine wengi. Mradi chanya saana ambao jamaa kapiga kazi na wasanii old school na new school pamoja na waliopo handaki na mkondo mkuu, wa nyumbani na nje ya Tanzania na kutupa mradi ambao niliupiga sana.

Ngoma zangu pendwa: Mori, Furaha Yangu (Africa), Chaukucha, Dakika 90, Jah Reruu, Tumbonii, Nisamehee, Laleyo.

Ngala & MastaQuest - Nakala

Disemba nayo ilikuja na baraka zake. Baada ya kutuonjesha ngoma moja Camaraderie wakiwa na Rawkey na Akoth Jumadi kwanza jamaa walitupatia mradi mzima Nakala Disemba mosi. Mradi huu ambao uliwashirikisha ma emcee na waimbaji kumi na nne ki ujumla ulinishangaza sana kutoka na viwango vya juu vya midundo na sauti pamoja na mada za ngoma zote. Kuna ngoma flani pale chorus imeaimbwa kisonjo (kisomali) inaitwa Naagnool nom asana. Pia Kitu Sewer, Jemedari, Kaa La Moto wanakuja na kalamu zenye ncha kali kwenye mradi huu na kuhakikisha kuwa maskio na mioyo yetu wanaiwacha na ngeu ya mistari yao ilhali wenyeji wao Ngala na MastaQuest wanaenda sambamba nao inapokuja kwa mistari yao pia. Pata Nakala yako utanielewa kwanini nimeweke kazi hii hapa.

Ngoma zangu pendwa: Naagnool, Fanya, Wasanii, Nairobi, Duru, Nakala,

Young Killer – Msodoki Super Nyota

Young Killer aliongeza discography ya kazi zake kwa kuachia albamu yake ya mpya Msodoki Super Nyota. Kutoka enzi za Dear Gambe Msodoki kajitahidi bado kuwa relevant kwa game na kupitia mradi huu kaonesha bado yupo ngangari. Mradi umesimamiwa na watayishaji wazuri kama vile Dapro, na quality ya production ipo juu. Inapokuja kwa collaborations waalikwa wamefanya yao freshi sana.

Ngoma zangu pendwa: Msodokii Super Nyota (Intro), Changes, Yeah, Respect, Mrs Me, Ngosha, Blessing, Dada Jambazi Na Mdogo Wake

Buff G – The Colonial Child

Buff G ni mtayarishaji, mwanaharakati wa mazingira ila pia ni mchanaji mzuri pia. Jamaa kabla mwaka haujaanza nae akaamua kutumia vipaji vyake hivi na kutumia mradi wake mzuka sana Colonial Child uliosimamiwa chini ya Nawiri Records ambapo watayarishaji waliohusika kwenye mradi huu ni Ananda Edward, Dez 32, Freddy na Buff Beats mwenye. Buff G pia anawishirikisha ma emcee kadhaa kama vile Jomba Uncally, Smallz Lethal na Sela Ninja ili kutuletea mtazamo wake kuhusu maisha baada ya wakoloni kusema na kumuacha kama mtoto aliekuja baada ya ukoloni huu. Anatufungua macho kuhusu changamoto zinazotusibu sisi tunaoishi kwenye hizi zama za ukoloni mamboleo.

Ngoma zangu pendwa: Mother Nature, Podi, Sunshine, Table Of Contents, Mama Africa, Politics, Trust The Process (T.T.P), Democracy

Kaa La Moto – Mkanda Mweusi

Baada ya kuachia album yake Leso Ya Mekatilili mwaka huu mimi binafsi nikajua mwana keshatekwa na mkondo mkuu maana mradi ulikuwa tofauti na matarajio sio yangu tu bali ya wana Hip Hop wengi hasa hasa wa handaki. Sijui mwana manungu’niko yetu yalimfikia kwani jamaa kabla mwaka haujaisha akatubariki na kazi yetu sisi wana Hip Hop kindakindaki Mkanda Mweusi. Kazi hii ambayo imesimamiwa na Grandmaster Teknixx kutoka kule Kubwa Studios Mombasa haukutuangusha kusema kweli. Jamaa kapiga kazi na wasanii kutoka Kenya na Tanzania na pia ma emcee chipukizi na wakongwe.

Ngoma zangu pendwa: Addiction, Hoi, Darasa, Kijana Mwafrika, Prime Time, Salama, Shadi,

Dr. Lukuwi x Momumo – Afya [Health & Wellness]

Mradi huu ulidondoka siku ya mwisho ya mwaka wa 2022 na kusema kweli ni baraka ya kufungulia mwaka 2023 kwani unakukumbusha na kuhimiza kuhusu umuhimu wa kujali yako Afya (Health & Wellness). Dr. Lukuwi ni daktari rasmi ki taaluma na ameshirikiana na mzee wa Hisia Momumo kutupatia mradi wa burudani na elimu uliosimamiwa na watayarishaji kama vile Patrino (On The Beat), Issam, D Beats, Geezy, Sela Ninja na Ngoi Kazi. Shule bila ada hii.

Ngoma zangu pendwa: Ajali, Chakula Tiba, Jina, Furaha Yako, Mama Na Mtoto, Mazoezi, Mtindo Wa Maisha,

Kama ndio tumefunga/kufungua mwaka kwa style hii basi nina imani 2023 ma emcee watatuletea miradi mizuri. Ila tukiisubiria nirushie comment kuhusu album gani kwa upande gani zilivunja woofer yako.

Kitu ningewarai ma emcee wa Hip Hop ni kuhusu album cover za miradi yao, wajitahidi wazisuke vizuri zaidi kwani ukiangalia cover za miradi hapo juu na baadhi zilizopo hapo chini unakuta nyingi zimeweka sura za wasanii husika. 2023 tokeni ndani ya comfort zone na muwe wabunifu zaidi ili pia tuseme album cover flani ndio top manyota. Msisahau graffiti ni moja ya elements za Hip Hop.

Tukutane tena mwishoni mwa mwaka 2023 ili tuweze kuwapatia album zetu bora. Nimesepa!

Baadhi ya album zingine nilizo ziskiza nakuzipenda ni:

Killo Pound x Hechi – No More Discussions
Tdx Wangex – Kitalama
Kid Rucha – Head In The Sky
Octopizzo – Lamu Nights
Rapkemboi – Saints To Cents
Oksyde – Strictly For My Hoodlums
Trabolee x Akili Blaq – 2wo
Wanaboma – Milipuo Haisitishwi
Kella B – Kuhusu Maadili
Ukokola+ - Upande Chanya