Kwa sababu ya kuwepo kwa miradi mingi mwaka huu niliamua kuandaa makala itakayoorodhesha album, mixtapes na eps zangu za mwaka jana 2022. Tulishamalizana na mambo ya album na sasa ni zamu ya EP. Twendeni moja kwa moja ili muweze kujua hapa Micshariki Africa ni EP gani nilizozipenda na kuziskiliza kwa sana.
Asum Garvey - Citrine

Asum Garvey amekuwa busy mwaka huu. Jamaa kafanikisha kuachia miradi mitatu; album mbili The Asum Cut pamoja na Shrapin’ Rage alioshirikiana na Groovy Jo na EP moja Citrine. Kama unavyojionea kwa jalada la album kuna aina flani ya dini ambalo Asum amesema linawakilisha “uponyaji, hali ya joto, fanaka na kujiamini kutokana na kung’aa kwa dini hili kama jua”. Mradi unaosheherekea maisha.
Ngoma zangu pendwa: Mambo Shwaa, Authentic, Crash (Asum’s Anthem)
Sniper Flowz – Ya Moto

Sniper Flowz kutoka Dar Es Salaam Tanzania aliachia EP yake mapema mwaka jana ambayo kusema kweli ni Ya Moto. Akiwa chini ya mtayarishaji Cjamoker toka Dreambooth Studios mwana anatupatia mradi mzuri ambao midundo ya kibunifu inamuwezesha mwana kutupatia mistari ya kibunifu pia. Mradi umegusia mada zinazogusa maisha yetu ya kila siku. Puliza, Ya Moto hio.
Ngoma zangu pendwa: Bounce, Wamberu, I Don’t Know, Chana,
Jemedari – Suits & Mics

Mzee wa Kaya naye baada ya muda mrefu pia alitubariki na EP yake Suits & Mics na kama jina la mradi na mchoro kwenye jalada linavyoashiria unatarajia mradi wa ki utu uzima. Kuanzia midundo ambayo ipo ki Hip Hop – Jazz fusion flani amazing, mashairi na uwasilishaji wake pamoja na uinmbaji mradi wote unagonga ndipo.
Ngoma zangu pendwa: Easy, Grown & Sexy, Bedroom, Taratibu
Chiku K – Woman

Chiku K amekuwepo kwenye game kwa muda sasa na baada ya kimya cha mda mrefu alirudi tena kwa game na mradi wake Woman. Cjamoker kutoka Dreambooth Dar Es Salaam ndio yupo nyuma ya vyombo kumpatia mwanadada midundo ya hadhi yake na hajamuangusha. Kutoka wimbo uliobeba jina na album Woman ambayo imejaa mapenzi yake kwa ajili ya mamake mzazi (ambaye ndie yupo kwenye jalada la album ila kaaga dunia mwaka huu wa 2023), hadi kuonesha uwezo wake kwenye Naleta Noma hadi kutuhamasisha tukasake Mapene, Chiku K katuonesha kuwa kwenye game hili bado yupo yupo sana. Mradi huu pia utamuenzi milele mama yetu alietutangulia mbele za haki.
Ngoma zangu pendwa: Woman, Noma, Mapene, Bwesa
HR The Messenger na Sewersydaa – Nocturnals

HR The Messenger ni mtayarishaji na vile vile emcee ilhali Sewersydaa ni tuluthi moja toka kundi la Wakadinali. Wawili hawa walishashirikiana kwenye miradi tofauti hapo awali ila wakaona itakua freshi zaidi wakituandalia mradi mmoja wa pamoja Nocturnals. Sasa jamaa walifanya unyama humu, sio wa kitoto. HR alionesha uwezo wake wa kuandaa miradi mzuka ilhali wote walinoa penseli zao ili wahakikishe hakuna mtu anampiku mwenzake kwenye mashairi yake. Kwenye kupimana nguvu hapa anayeshinda ni shabiki kwani anapokea mradi uliokwenda shule.
Ngoma zangu pendwa: Degree, Reuters, Mind, DOD, Haters
P Mawenge – Simu Na Matukio

P The MC au ukipenda P Mawenge mwaka huu alikuwa busy nae pia. Jamaa alitoka booth na kazi yake mpya Simu Na Matukio ambayo kusema kweli ilikuwa inazungumzia maisha yetu ya sasa inapokuja kwa mambo ya simu na changamoto zake. P Mawenge ana uwezo wa kuchukua mada muhimu na kuziandikia mashairi mazuri na ya kiujanja na anapowasilisha unanasa kila neno analochana. Mradi huu umetumia njia ya simulizi za hadithi kutufunza mambo mengi kuhusu athari za simu, hasi na chanya, kwa ucheshi sana.
Ngoma zangu pendwa: Tukutane Gesti, Customer Care, Call Za Minuso, Ujumbe Muhimu
Msito - Gorilla

Msito ni mmoja wa ma emcee chipukizi wakali wa kizazi chake ambaye mwaka huu aliamua kuanza kutuonesha unyama wake kupitia mradi wake Gorilla. Emcee huyu amekuja kuchafua hali ya hewa ya Hip Hop Kenya na hasemi samahani. Anachana, anaandika na anawasilisha nondo zake kwa wepesi flani ambao unaonesha ukomavu wake. Jamaa akiendelea hivi sio muda mrefu watu wengi watakaa na kumskia na kuwa wafuasi wake.
Ngoma zangu pendwa: Sura Punda, Each 1 Teach 1, Kinaga Ubaga, Taratibu, Gorilla 2,
Motra The Future – Baba Ako EP

Binafsi Motra nimeanza kumpa skio mwaka huu. Baada ya vuta nikuvute na ma emcee kadhaa kuhusu nani zaidi jamaa akaamua aingie studio ili kuweza kumaliza mjadala na kuweza kutambulika kama Baba Ako. Quality ya kazi hii ipo juu si mchezo, midundo ikisimamiwa na Davy Machody na Old Paper na inamuwezesha Motra kuiwasilisha vizuri mistari yake ya kijanja, uchokozi na ucheshi.
Ngoma zangu pendwa: How We Do, A Town, Wauwe, On Fire,
P-Tah – On My Case (OMC) 2

Jamaa alianza kuchana wakati wa janga la Uviko 2019 chumbani kwake wakati wa zile lockdown za lazima kule Uingereza anapofanya kazi. Jamaa kapiga hatua na OMC2 ni moja ya zao zuri la ukuaji wake. Jamaa kama kawa kasimamiwa mixing and mastering na Aress 66 wa Big Beats Afriq. Baadhi ya midundo imepigwa na watu kama vile Aress, Kunta Official Beats, Afrvka. Jamaa anaongelea mada tofauti akitumia Sheng, Kiswahili na Kingereza.
Ngoma zangu pendwa: Freedom Of Expression, Generational Wealth, Turn Off The Lights, Vices
Pido Mox - Ukarakihima

Wakati mwingine hauhitaji maneno mengi ili kuweza kujitambulisha kwa watu wanaokuskia. Na hili ndilo utakaloliona pale utakapo bofya play Kuskiliza Ukarakihima toka kwa Pido Mox kwani chini ya dakika 18 utaona uwezo wa huyu jamaa. Sio mashairi, sio uchanaji, sio unataji na midundo, sio mada yanki anapita freshi tu. Black Ninja kama ilivyo kawaida yake ni midundo ya Boombap na kwenye kazi hii aliyoisimamia hakuna utofauti. One for the future, msibanduke hapa.
Ngoma zangu pendwa: Uchawi, Karma, Rap Version, Kikwazo, Hip Hop Saved My Life
Big Yasa – BIGGS

Japokua mimi sio shabiki mkubwa wa Drill music Big Yasa aliweza kunifanya nikae chini niskilize kwani kupitia mradi wake BIGGS niliona kuwa kama mchanaji ni mzuri anaweza kunata na mdundo wowote ule. Na hapa ndipo Big Yasa alipopatia kwani hakuwachi kichwa kiduwae na midundo ya drill bali na mistari yake pia.
Ngoma zangu pendwa: Crystal Clear, Lil Bro, Halal Haram, Wasp
Duga Mawe – Kiu Ya Ukombozi

Duga Mawe akawasili na EP yake Kiu Ya Ukombozi, ambayo imesimamiwa na watayarishaji kama Salii Tecnic, Future Beats na Mock Beats. Mzee wa nginja nginja. Mradi mzuka sana ambao una madini kibao, mashairi mazuri na mafunzo pia.
Ngoma zangu pendwa: Omba, Yamenikuta,
Careem - Talent Ipo

Careem kutoka Mombasa naye alikuja na mradi wake wa kwanza rasmi ili aweze kukuonesha kuwa kule Mombasani pia Talent Ipo inapokuja maswala ya uchanaji. Akituwasilishia mashairi yake na lafudhi yake ya pwani emcee Careem anaonesha uwezo wake juu ya midundo ya B Recordz.
Ngoma zangu pendwa: Nane Kumi Na Sita, R.A.M.O.P (Wanafki), Nikubaya
Fedoo - Mangi Sabas

Fedoo ni kijana flani ambaye nilianza kumskia kwa kazi flani ya Adam Shule Kongwe. Baada ya kutoa singles kadhaa jamaa akaona ni vyema aanze kujenga catalogue yake na kwenye msingi kaweka tofali la jiwe Mangi Sabas. Mradi huu ambao umesimamiwa na Luis wa North Block Records kule Arusha ni bars on bars kutoka kwa emcee huyu chipukizi.
Ngoma zangu pendwa: Mapichapicha, Nicheki, Vichwavichwa, Money
Bigg – The Come Up

Bigg alianza kuja rada zangu na single flani tuliyoitangaza hapa Micshariki Africa. Kutoka hapa nilianza kufuatilia kazi zake na mda si mda jamaa aliachia EP yake The Come Up. Mradi huu wenye nyimbo 4 unamkuta mwana anajaribu kuchana juu ya midundo tofauti ila hapotezi uhalisia wake.
Ngoma zangu pendwa: Goodtime, Haileti,
Hechi – Come Back

Hechi amekuwa busy sana mwaka huu, EP tatu; Love City, Hewani na Come Back pamoja na album moja No More Discussion akiwa na mtayarishaji Killo Pound. Hechi huwa ana style flani ya kuchana ambayo ukiizoea ina stick na wewe. Hili unaliona bayana kwenye Come Back ambapo jamaa anaongelea mapenzi na mpenzi wake aliyemuacha na anataka arudi. Mradi mzuri.
Ngoma zangu pendwa: Intro, Amesepa, Come Back, Ni Wewe,
Brian Muok – Made In Nairobi

Nakuru imeweza kutupatia wachanaji kibao sana na hii ratiba sioni kama itabadilika hivi karibuni. Anaewania kupeperusha bendera ya Nakuru japokua yupo Made In Nairobi si mwingine bali ni Brian Muok. Jamaa anachana freshi juu ya midundo flani taratibu na kazi inatoka fiti sana. Jamaa anagusia mada tofauti kama mapenzi na siasa na kadhalika. Mchekini mwana ambaye pia alishinda tuzo mbili za muziki mwaka 2022. Brian ame muok (amekuja).
Ngoma zangu pendwa: Tumecheki, Makosa, When I’m Gone, Black Cat Plight, Elections
Sami Black – Maisha Utata

Sami Black ni emcee ambaye amerudi tena baada ya kutoweka kwa muda na alirudi na nia ya kutuonesha vile Maisha Utata. Mradi mzuri sana huu na niliufurahia sana na umesimamiwa na watayarishaji kama Double na Zenji Boy ambaye anatupatia beat flani ki West Coast kwa ajili ya ngoma iliyobeba jina la mradi huu Maisha Utata.
Ngoma zangu pendwa: Maisha Utata, Macho, Bora, Watu
The Vedette – Who Am I?

The Vedette amekuwa kwenye ulingo wa Hip Hop kwa mda hadi alikuwa na tovuti yake kwa ajili ya habari za Hip Hop. Ila mwaka 2022 aliamua kurudi na mradi wake wa kwanza ambao nia yake ni kututambulisha kuwa kuna jamaa anaitwa The Vedette ambaye kwa kuwa anavaa kofia nyingi akaona isiwe kesi Who Am I? ili ajitambulishe kwenu. Mradi mzuri sana, midundo, uchanaji na uimbaji mzuri wa Viquee Ofula na Eric Mbala.
Ngoma zangu pendwa: Crush, L’amour Va Me Tuer, Lord Forgive Me.
Adam Shule Kongwe – Kutoka Kwangu Kuja Kwenu (K.K.K.K)

Mwanangu Shule pia alituletea EP ya KKKK ambayo nayo pia ilikuwa chanya sana. Watayarishaji waliohusika humu ni kama Tenth Wonder na Qwitch kama kawa jamaa anaendelea kwa kile kinachomfanya awe bora kila siku; mashairi ya kina na uwasilishaji wa viwango. Mradi ulikuwa na Maujanja Sapplayaz kama wageni waalikwa pekee kwenye Wahuni Wakubwa. Kwa wale wanaotaka kujifunza kuhusu jinsi gani ya kuundaa muziki wao na beti zao, cheki wimbo Shule Yako, ndio shule yako.
Ngoma zangu pendwa: Wahuni Wakubwa, Game Itachafuka, Shule Yako.
The MC (Mukimala + Catalyst) - Brown Sense Outta Scratches/Hisia za Kahawia kutoka Kwenye Mikwaruzo Ep

Mukimala na Catalyst wakaona haitokuwa freshi 2022 ikipita bila wao kutupatia kazi ndio wakatu bless na Brown Sense Outta Scratches/Hisia za Kahawia kutoka Kwenye Mikwaruzo EP ambayo imesimamiwa na Black Ninja kutoka Boom Bap Clinic, Dar. Chemistry ya hawa ‘mapacha’ ki michano ni nzuri sana kwani hawajawahi kuniangusha. Skia ngoma kama vile Art Ya Booth, Why ndio utanielewa ninacho maanisha. Silly Ass/Serious inatukumbusha tulipotokea kwa Refractions.
Ngoma zangu pendwa: Silly Ass/Serious, Art Ya Booth, Why, Engolo
Dambwe La Hip Hop – Risasi Nane Za Moto

Wana Dambwe walitumiminia Risasi Nane Za Moto ambazo kusema kweli zilikuwa konki sana. Boombap mwanzo mwisho na mashairi yanatiririka sio mchezo na wanapopokezana mic wana Dambwe wako flawless. Yaani kazi inatiririka freshi mwanzo mwisho na huruki ngoma hapa. Jamaa wana skio flani la kuchagua midundo maana inagusa hisia sana. Kongole kwa hili na kazi ni murua sana, aisee!
Ngoma zangu pendwa: Mihemko Binafsi, Walikuja Na Risasi, Uwanja Wa Vita, Uvamizi, Nashina, Maiti Za Mateka, Nishani, Nitazame Tena,
EP za ziada nilizozipenda ni;
Fredrick Mulla – Master Manondo
EMC - Mchekula
Rino X – MAPEMA (Mapenzi Maisha)
Stamina – Love Bite
Jakk Quill – Finding Flows
Shilinde – Afya Ya Akili
Sela Ninja – Street King
Gamba Junior – Street Motivation
Rapcha – To The Top
Trump MC - Ndumbuli EP