Miradi Bora Ya Hip Hop Kutoka Africa Mashariki 2023

Mwaka mpya na mambo mapya wanasema,  ila kabla hatujaanza kuongelea ya mwaka huu wacha tuanzie na tulipoishia, tuongee ya mwaka jana. Mwaka jana 2023 ulikuwa wa neema sana kwani tuliweza kushuhudia ma emcee kibao pamoja na watayarishaji wetu wakitubariki na ma EP, Kanda Mseto, Beat Tapes na Albums Kibao.

Zaida ya miradi mia mbili (200+) iliachiwa na wasanii wetu na leo nimeona ni vyema nipate muda wa kuorodhesha miradi ambayo mimi binafsi nilipata muda wa kuiskia na kuipenda. Kwa kuwa miradi ni mingi leo nitaanza na albums kwanza halafu In Sha Allah panapo majaliwa nitakuja orodhesha Eps na pengine mixtapes zangu bora za mwaka 2023.

Heri ya mwaka mpya kwa wasomaji na waskilizaji wetu. Wacha tulianzishe na album zetu bora za 2023.

One The Incredible - Achieving Greatness

 

Uno ndio anatufungulia orodha yetu ya album bora za mwaka 2023 na hii ni kutokana na yeye kuachia kazi yake classic Achieving Greatness mapema mwaka jana. Mradi huu kusema kweli ulikuwa top tier sio tu ki mashairi bali hata ki midundo, ki utayarishaji na pia ki maudhui. Pia nilichokipenda kwenye mradi huu ni pale kaka One alipoweza kunata na kila aina ya mdundo, sio Boom Bap sio Trap, sio Ragga. Oh, nisisahau chemistry yake na dada TK Nendeze, mzuka sana. Mradi huu ndio ulitoa ngoma zilizomuwezesha emcee One The Incredible kujinyakulia tuzo ya 15 ya Micshariki Africa Emcee Of The Month Mwezi March 2023.

Ngoma Pendwa: Vitendo Dhidi Ya Maneno, Msaada Kwao, Achieving Greatness, In My Heart, Easy Tiger

$£€K ni moja ya albums bora za Hip Hop kutoka Kenya zilizodondoka mwaka jana. Sudough Doss chini ya label yake ya Zozanation aliibeba Eastlands mgongoni mwake kwa kutupatia mradi huu ambao kusema kweli ulikuwa mzuka sana. Kazi hii ilikuwa na wasanii waalikwa kama Kitu Sewer na wana Zozanation Skillo, Scar (Mkadinali), Domani Munga (Mkadinali) na Sewersydaa uliburudisha si haba. Kama mlidhania Umoja na Eastlando walilalia maskio mwaka jana imekula kwenu. Bado mtambue Rende ni Rong!

Ngoma Pendwa: Si Kupenda Kwetu, Kalenda, No Cap, Message, Karibu Eastside, Juu Ya Nini,

Moja ya album kubwa kwa idadi ya nyimbo na nzuri sana kuwahi kutoka mwaka jana ni Escape ya emcee Experience au ukipenda XP au hata Triple Double. album hii japokua ilichukua muda kutoka tangu taarifa ziachiwe kuwa XP anadondosha kazi mpya mwaka jana haikutuangusha mashabiki kwani subra zetu zililipwa na riba.

Kazi iliundwa kwa viwango vya juu na kutoka ngoma ya kwanza hadi ya ishirini na sita hakuna ngoma unaruka hapo. Pia tukiongelea maswala ya maudhui ki ujumla, mada za kila wimbo na midundo, kaka XP alifanya kazi nzuri sana. Ili kufanikisha kazi hii emcee huyu alipata usaidizi kutoka kwa waimbaji na ma emcee wapya na wakongwe kama vile Neno wakwanza, Nikki Mbishi, TK Nendeze, Misoji Nkwabi, Dark Master, Nash MC, Songa, Mnyama Double, Tribe 53 kutoka Kenya, Mwendazake Salu T, Attu Medicine, Black Jesus, JCB Makalla, Nikki Maujanja, Stereo Singa Singa, Kay Wa Mapacha na veteran emcee Rass Kass kutoka Marekani. Uki press play hii album una Escape mambo kibao kwa kuingia ulimwengu wa Hip Hop.

Kwa upande wa ma producer waliohusika ni kama Pallah Mdundo, Abby MP, Sigger, Wise Genius, Black Ninja, Patrino na wengine wengi.

Ngoma Pendwa: Bongo Coast 2 West Coast, Escape, Kama Ningejua, Kijiji Changu, Hustle Zangu, Return

Rotka ni emcee anayetokea Ufaransa ila ameshafanya kazi kibao na wasanii kutoka Africa Mashariki. Hili ndio linamuwezesha emcee huyu kufanikisha album yake kuwepo kwenye orodho hii. Kazi yake We Are One imenuia kuleta umoja na mshikamano sio tu kwa wana Hip Hop pekee bali hata kwa watu wa mashariki ya Africa kwa kutaka kutukumbusha kuwa sisi sote ni wamoja.

Kazi hii ambayo ni nzuri sana ina midundo ya Boombap wazimu sana na imeleta wasanii kutoka Kenya, Tanzania na Ufaransa. Wasanii walioshirikishwa kwenye album hii ni kama ZigiDigi Cultural Troupe, MC 255, Moroko Kalahari, Jay MauMau, Sight More, JCB, Emma Maasai, Wiseman Wizo, Mex Cortez, Dwee, Elisha James, Blak Odhiambo, Domokaya na wengine wengi!

Ngoma Pendwa: Karibu, Unity, Free Your Mind, Hope, We Are One, Pour le Hip Hop, Light Of Love, Soldiers Of Peace, Unapo Tema Sumu

Tukiwa bado kwenye roho ya umoja naileta kwenu album ambayo Micshariki Africa ilihusika kwa asilimia 100 uundaji wake. Tukishirikiana na Truce Label ambao waliunda midundo yote tuliweza kuwaleta ma emcee wawili chipukizi kutoka Kenya (Msito) na Tanzania (Fedoo) na kuwapatia wana Hip Hop mradi kwa jina Mashariki Ya Fikra.

Kwenye mradi huu ambao uligusia mada mbali mbali zinazowagusa wana mashariki Africa pia kulikuwa na ma emcee waalikwa kibao na waimbaji kama vile LNess, Jimwat, P Mawenge, Kayvo Kforce, Kaa la Moto, Nikki Mbishi, Killa Loop, Fivara, Shazzy B, Dizasta Vina, Elijah Moz, Tori Mugureness na wengine wengi.

Ngoma Pendwa: MauMaji, Hakuna Network, Kwetu Kwanza, E.A.S.T (Every Artist Should Teach), Tumeuzwa

Bad Ngundo - Nudhumu

 

Bad Ngundo ni nusu (½) ya kundi la Hip Hop kutoka kule Kahama Tanzania linaloitwa Wabeti pamoja na Papaa Frege. Baada ya kazi yao ya pamoja Ukubwa EP iliyotoka miaka miwili iliyopita, ma emcee hawa walikuwa wakiachia singles aidha wakiwa pamoja au kila mmoja kivyake emcee Bad Ngundo aliamua kujaribu kina cha maji ili kujipima uwezo akiwa peke yake. Matokeo yake ni Nudhumu, album iliyofadhiliwa na S.I.N.A.H.I (Sisi Na Hip Hop)

Album hii imeundwa chini ya usimamizi wa mtayarishaji Black Ninja kutoka BBC, Dar Es Salaam hivyo unajua kwamba midundo ni Boom Bap mwanzo mwisho. Elimu burudani hii hapa

Ngoma Pendwa: Hirizi Ya Shilingi Mia, Kufikirika, Maalim Shaaban Robert, Mashairi Ya Bad, Masomo Yenye Adili

Studio za Budhouse kutoka kule Nairobi mwaka jana zilikua busy sana kuachia miradi ya wasanii wake. Moja ya miradi mizuri kutoka kule ni Endorphins ya emcee Outlaw. Endorphin ni homoni zinazochochea furaha na kusema kweli mradi huu unaleta sio tu furaha hata pia shangwe, nderemo na vifijo pia

Kazi hii kutoka mtu mzima Outlaw ni mradi wa kukufanya ukae na utafakari kwa kina kinachosemwa kwenye ngoma ambazo zimeundwa freshi sana. Lugha zinazotumika kwenye mradi huu ni Kiswahili, Kiingereza, Sheng na Kigiriama. Kazi nzuri sana.

Ngoma Pendwa: Jam (Pt 1), Jam (Part 2), Is All Good, Time Froze, Better, Pleasure Pain, Say To You, Chill Tumedi,

Fivara – Tegemeo

 

Fivara baada ya album yake ya kwanza Fikra Ni Vazi La Rap iliyodondoka miaka kadhaa hapo nyuma aliamua kutukumbushia uwezo wake inapokuja kuandaa album bora kwa kutupatia kazi yake mpya Tegemeo. Kama kutoka zamani kinachokuvutia kwa emcee huyu ni pen game yake basi mcheki upate nakala yako kisha kaa kwa kutulia uskie mistari. Kazi hii ukiiskia mwanzo mwisho imejaa mafunzo, burudani, hekima, heshima, story na uwasilishaji mzuri pamoja midundo ya nguvu. Hii album ni classic and a half.

Ngoma Pendwa: Mtoto, Tabula Rasa, Mboni, Barua 2, Wakala, Wake Up Call,

Afrocentric ni kundi la Hip Hop lililoundwa na mtu nne, Hassano, Chumba, Katapilla pamoja na John More. Mwaka jana kundi hili lilidondosha album yao ya pamoja kwa jina Mass Hypnosis. Mradi huu ambao umeundwa chini ya watayarishaji wakiwemo Biko Beats, Vinc On The Beat, Fulami, KD, Visita pamoja na Luigi (On The Beat).

Nilichokipenda kwenye mradi huu ni vile vijana hawa hawakuwa waoga kujaribu vitu tofauti tofauti ili kuhakikisha wanatupa mradi wenye ladha nzuri, sio kuimba sio kuwakaribisha wasanii wengi wenye uwezo na talanta tofauti na wao, lengo likiwa kuunda kazi itakayofanya waskilizaji waduwae na ndumba ya mziki wao.

Ngoma Pendwa: Eh Eh, Work Hard, Day & Night, Burudani, Get Paid, Majigambo, Gonga Ndipo

Since 1990 ni debut album ya Kabinova ambaye ni robo ya kundi la UKonga Hoodz linalopatikana kule Ukonga, Dar Es Salaam, Tanzania. Album hii ni mzuka sana sio tu ki mashairi bali hata ki midundo ambayo mingine kapiga kaka Kabinova mwenyewe. Mwana sio emcee tu bali pia mtayarishaji na pengine hili ndio limempa sikio la kujipendelea midundo na mradi bomba sana. Cheki kwa mfano kwenye ngoma Afrika akiwa na mwimbaji/mtayarishaji Minor Tone ndio utanielewa vizuri.

Ngoma Pendwa: Rafiki, Afrika, Plama, Money, No Fear

Elisha Elai - A Man On A Mission

Elisha Elai sasa ndio kawasili na album yake ya kwanza inayonuia kuonesha kuwa yeye sio tu mchenguaji bali ni A Man On A Mission. Kazi hii ambayo mtayarishaji mtendaji ni producer Ares 66 ambaye wamefanya kazi pamoja toka kitambo inatuonesha ukuaji wa emcee huyu tangu alivyotuambia yeye ni Bazenga kwenye EP yake.

Album hii imejaa stori za kitaa, majigambo, kujiamini na pia imewashirikisha ma emcee kadhaa kama vile Motra The Future kutoka Tanzania, muimbaji Wyre, Dyna Cods, Magaa na Jasper. Dandora bado inaendelea kutoa vipaji na Elisha Elai ni mmoja wa kizazi kipya cha wasanii wanaoendelea kuwakilisha kitaa hichi ambacho ni muhimu kwenye historia ya Hip Hop, Kenya.

Ngoma Pendwa: Hii Rap, Thug Life, Icon, Wenyeji, Tongue Twisting, Mavichwa, Karma, Money Talks

Moja ya album zangu pendwa nilizozipiga sana ni Trust God ya emcee Izzo Bizness. Japokua kaka yupo mamtoni America, impact yake kwenye Utamaduni wa Hip Hop sio tu Bongo bali hata Mashariki ya Africa bado ni kubwa tu (skia Nilipotoka ambapo amewashirikisha ma emcee kutoka Tanzania pamoja na Kaa La Moto kutoka +254, both mainstream na underground emcees). Mwamba huyu ambaye enzi hizo alibobea na kibao chake Tumogele kilichotayarishwa na Duppy Beats kama ilivyokuwa kwenye mradi huu alitubariki na mradi mzuka sana ambao ulituhimiza tu Trust God.

Album hii ilikuwa a star studded project ambapo humu walishirikishwa wasanii kama Ray Vanny, Nikki Mbishi, Lugombo MaKaNTa, Banana Zorro, Salmin Swaggz, Mwasiti, Kaniba, Hance, Shapsin, Joe Makini, Chabba, P The MC, Kassim Mganga, Baddest 47, Barnabas, Lody Music, Linex, Damian Soul, One The Incredible, Zaiid na Dizasta Vina.

Ngoma Pendwa: Walimwengu, Dada, I Need You, Rushwa, Mboga, Nilipotoka, It’s Ok, Trust God, Kanunu, Put In, Siku Yetu, Huoni, Unanitosha, Scary Days

Sijui DJ Khaled ndio alituinspire sisi waandishi wa muziki kuanza kuunda hizi album au ni Motivation ya tunachokipenda kama inavyoitwa hii album kutoka kwa mwandishi mwenzangu Musiq Jared. Kazi hii iliwashirikisha wasanii na watayarishaji wa muziki kutoka sehemu tofauti duniani kama vile Kenya, Tanzania, South Africa na America pia.

Kazi hii iliangazia maswala kama umoja, kujithamini, Imani, historia ya mtu mweusi, utafutaji, kula bata na pia msuba.

Ngoma Pendwa: Awesome God, Grind, Boss Up, Memories, UNITY, Life Lessons, Furahia Maisha

Ilikuwa inakaribia mwaka kutoka emcee Bill Balaa atuoneshe uwezo wake wa kuunda mradi mkubwa baada ya mwaka jana kuachia EP yake Broken Way. Hivyo basi A.L.A.B.A ndio album yake ya kwanza rasmi na mimi naweza sema kuna ukuaji unaonekana kutoka kwa hatua ya kuachia EP hadi debut album hii.

Ukishaona album ina watayarishaji kama Black Ninja, Odilla Beatz, Killo Pound na 10th Wonder ujue hapo ni midundo ya Boombap na hili linampa Bill Balaa msingi mzuri wa kuweza kujieleza. Jamaa anaandika sio mchezo na ana uwezo wa kucheza na maneno aidha kuweka kitu bayana au kuficha ili mskilizaji aweze kufumbua fumbo mwenyewe.

Ngoma Pendwa: Wanazingua,Yokai, Broken Barz 2, School Drop Out, Alaba, Siwezi Lea Ujinga, Online Bitch, Tumejipata, Demu Wack

Mauru Unit kutoka kwa Sewersydaa ambaye ni theluthi moja (⅓) ya kundi la Wakadinali kwangu ulizidi kunionesha kwa nini huwa namuheshimu huyu emcee. Akiwa amesimama peke yake nahisi ubaya wake ndio unaonekana vizuri na ndio maana ya Mauru yaani mwenye ubaya mwenye ujeuri.

Ujeuri kwenye kinasa ndio unauona kwenye mradi huu kutoka ngoma ya kwanza mpaka ya 24. Yes 24, kwa Kenya nadhani Sewersydaa ndio mwenye mradi mkubwa mwaka jana. Watayarishaji kwenye mradi huu ni Aress 66 kama kawa, HR The Messenger, Asam April, Eyuh Chino pamoja na Keith Wamz. Zozanation tena kwenye album bora zetu, Rende bado Rong!

Ngoma Pendwa: Eastlands, C-4, Seasaw, Ki Di’ng, Kijana Good Job, Sema No, Tena Sitaki, Chief Gwetheist,

ChindoMan na Mo plus Chanya ni veterans kwenye hii game wanaotokea kule Arusha, A-Town Chuga. Mwaka jana walijivisha magwanda ya wanajeshi wa Hip Hop kwa ajili ya kutupatia usalama kwenye tasnia ya Hip Hop kupitia album yao Lindo The Album.

Album hii ambayo ni Boom Bap mwanzo mwisho imewashirikisha wasanii kama Fredro Starr na Fid Q kwenye Legacy, Rahma, Adam Mchomvu, Stereo Singa Singa, One The Incredible, Alexer, Kevin Tiba, J Deal pamoja na Noelle.

Ma veteran hawa ni kumbusho kwa ma emcee wa hivi sasa kuwa ni vizuri kusimama kwenye unachokifanya na kuwa consistent kwani kwenye u emcee hakuna maswala ya umri bali maswala ya nini unachokileta mezani kwa ajili ya mashabiki zako. Album yote kali!

Ngoma Pendwa: Legacy, Lindo, Street Gospel, Ndoto, Represse, Tindikali, Kibubu, Tuna Score, Tell Me, Furaha, Fungua Kitabao

Katapilla ndio emcee ambaye ana miradi miwili kwenye orodha yangu hii. Alisomeka hapo awali kwenye mradi wa pamoja na wenzake wa Afrocentric, Mass Hypnosis na sasa anasomeka hapa akiwa na mradi wake binafsi akipigana na nafsi yake mwenyewe Me Against Me.

Baada ya kujijengea jina kwa kudondosha singles kadhaa, kutokea kwenye cypher ya Khali Kartel, kuwa mshindi wa OdiNare Challenge na pia kudondosha album na Afrocentric Katapilla aliona ni vyema sasa aoneshe uwezo wake akiwa mwenyewe.

Mradi huu ambao ulitoka chini ya label ya Zozanation iliyowasajili akina Sudough Doss pamoja na Wakadinali ni mzuri kusema kweli. Kuanzia ngoma za kwanza, zilizoundwa na watayarishaji Luidgi, World War 3, Hatubahatishi, Unabonga Aje?, Zoza Na Rende, pamoja na Ndechu, HR The Messenger, Mwanaume Ni Bidii, Asum April kwenye Where They At?, AyoTrackNiYaLeo kwenye Belinda, ItsACollectible kwenye Different Energy, Eazy, Pressure, K9 kwenye Bumpin’ na wengine wengi! Album nzuri.

Ngoma Pendwa: World War 3, Mwanaume Ni Bidii, Where They At? , Me Against Me, Hatubahatishi, Pressure, Ndechu, Unabonga Aje?, Excuse Madam, Belinda,

Frost ni veteran emcee ambaye chimbuko lake ni Chuga ila kwa sasa makazi yake ni kule Marseille, Ufaransa, hivyo basi ndio maana unaona jina la album yake inaitwa Controversial Diaspora yaani ughaibuni kwenye utata. Album hii japokua imeundwa kule mamtoni lugha iliyotumia sana ni Kiswahili japokua utaskia uchanaji kwa lugha ya Kingereza na Kifaransa pia. Album mzuka sana hii ya Boom Bap Hip Hop heads.

Ngoma Pendwa: Nafanya, 115, Ya Leo Kali, Controversial Diaspora, I Put It Down, Wenyeji, The Truth, Shadow Of Success,

Japokua Boox KcK naye amekula chumvi kwenye hili game la Hip Hop, binafsi mimi mwenyewe naweza sema ameanza kuja kwa anga zangu miaka miwili hivi iliyopita. Ma emcee wapo wengi na wengine hufika kwa mtu kwenye muda muafaka na muda muafaka ndio huu kwani tumemsubiria Boox KcK Tangu Tumboni.

Aisee hii album kali, noma na nusu, ya Hip Hop heads na imesimamiwa na watayarishaji mahiri kutoka Chuga kama DX (Noizemekah), Dr. Luis, Licky Touchez na wengine. Nilipenda sana ubunifu kwenye ngoma za msela kama kwenye singo iliyobeba jina la album Tangu Tumboni. Jamaa anachana balaa, art of emceeing!

Ngoma Pendwa: Tangu Tumboni, Usikosee Kitasa, Mitaa Inalia, Habari Ya Miaka Yangu, Watu Adimu, Mwamwi, Derby, Haina Mambo Mob, Break The Limit, Peace In The World, It’s Math, Hainga Daz,

Shaulin Seneta - Zama Zijazo

Sela Ninja mwaka jana alikuwa busy kama msanii na mtayarishajii vile vile. Kigambonino’s own aliachia ngoma kibao pamoja na beat tapes na pia alihusika kuunda miradi ya wana kibao. Moja ya kazi zake binafsi ni Hatuwalambi Miguu akishirikiana na emcee Subtex kutoka Marekani.

Japokua miradi ya mdundo huu kwa asilimia kubwa ilisimamiwa na Sela Ninja mwenyewe kuna mingine iliundwa na watayarishaji kama Kunta Official Beats kutoka Kenya, Kwenu The Nigerian, Sanjo, Nomad Beatsggi pamoja na Niko Beats. Mataifa yaliyohusika kuunda mradi huu ni 11 ikiwemo Kenya, Israel, America, Uingereza, Canada na Greece.

Ngoma Pendwa: B.I.B.L.E, Dear Hip Hop, Hasira, Hatuwalambi Miguu, Kubwa La Maadui, Misingini, OG Wayback, Shukran, Disturb The Peace, Inabidi Tu Unielewe, Massnondo, Shit Finish,

Zama Zijazo ni debut album moja mzuka sana kutoka kwa Mwanazuoni, Shaulin Seneta. Album hii ambayo imeundwa mwanzo mwisho na Wise Genius ni moja ya album bora za mwaka 2023 kutoka Tanzania. Shaulin Seneta kwenye mradi amesimama kinabii na kuanza kuongea na hadhira kama fanani mwenye uzoefu japokua ndio kwanza kabisa anaanza safari inapokuja kwenye kuunda catalogue yake ya muziki. Nilichokipenda kwenye mradi huu ni mashairi ya mwana, uwasilishaji na midundo.

Ngoma Pendwa: Maisha Na Kifo, Simu Ya Dada, Chanzo, Sikio La Tatu, Duniani, Battle Rhymes, Sitakufa, Msafiri, Tusionane, Upendo Na Amani, Baba Halaumiwi, Mlalamikaji,

Hawa jamaa Oxide Music siwajui ni akina nani, nadhani wanatokea Mwanza, ila ninachojua wanajua kuchana na kuunda album nzuri, Arise & Ruin. Huu ndio uzuri wa Hip Hop heads sisi hapantambua majina tu, weka kazi tuskie, tuihifadhi au tuiweke kwenye jalala, Arise & Ruin tunaiweka kwenye kapu ya album bora za mwaka 2023. Boom Bap ndio nguzo ya album hii, mashairi ndio nondo zilizotumika kwenye kazi hii. Kudos Oxide Music.

Ngoma Pendwa: Vijimambo, Ndani Ya Club, Run The Show, Kina Kirefu, Happy Day, Tuma Na Ya Kutolea, Tega Sikio, Against All,

Sela Ninja mwaka jana alikuwa busy kama msanii na mtayarishajii vile vile. Kigambonino’s own aliachia ngoma kibao pamoja na beat tapes na pia alihusika kuunda miradi ya wana kibao. Moja ya kazi zake binafsi ni Hatuwalambi Miguu akishirikiana na emcee Subtex kutoka Marekani.

Japokua miradi ya mdundo huu kwa asilimia kubwa ilisimamiwa na Sela Ninja mwenyewe kuna mingine iliundwa na watayarishaji kama Kunta Official Beats kutoka Kenya, Kwenu The Nigerian, Sanjo, Nomad Beatsggi pamoja na Niko Beats. Mataifa yaliyohusika kuunda mradi huu ni 11 ikiwemo Kenya, Israel, America, Uingereza, Canada na Greece.

Ngoma Pendwa: B.I.B.L.E, Dear Hip Hop, Hasira, Hatuwalambi Miguu, Kubwa La Maadui, Misingini, OG Wayback, Shukran, Disturb The Peace, Inabidi Tu Unielewe, Massnondo, Shit Finish,

Wakazi alikuja kwa radar yangu kutokana na album yake Kisimani ambayo ilidondoka mwaka 2018. Baada ya kuachia miradi tofauti hapa na pale, singles, EP, Wakazi Live at Sauti Za Busara – The Live Tape jamaa akaona askie wito wa mashabiki na aje albums 3 ambayo mojawapo ni Beberu Declaration ambayo ilidondoka mwaka jana.

Album imegusa mada za majigambo, mapenzi, feel good vibes, urithi wa muziki, kutia watu moyo na mapenzi kwa ajili ya Utamaduni wa Hip Hop. Watayarishaji waliohusika humu ni watu wazima Black In This, Pallah Midundo, Ommy Pah na Black Ninja.

Ngoma Pendwa: Addict, Twaha Kiduku, The Legacy, Clouded Judgment (Nawaza), Warrior, Kabila Letu, Messi, Set It Off,

Opobo - Kontena

Opobo ni mmoja wa wana familia kutoka Watunza Misingi. Watu wengi siku hizi wakiskia tu jina Opobo wanaongeza Pub kwani wanajua ukifika kule Mbezi Mwisho Kwa Yusuph ndio bar hii inapatikana kwa ajili ya kujiburudisha na ukapata moja baridi.

Ila wasichokijua wengi ni kuwa Opobo pia ni mwana Hip Hop na mchenguaji mzuri tu ambaye kando na kuletea mashabiki na wateja wake pombe tu aliwaletea Kontena, ambayo ilikua solo album yake. Album hii ni balaa na imejaa Mazaga kibao kutoka kwake na watayarishaji kama Issam. Album nzuri hii, Issam popote ulipo chukua maua yako, midundo yako imerembesha mradi huu na Boom Bap Beats mzuka sana.

Ngoma Pendwa: Mazaga, Vita Kuu, Siri Za Msiri, Ukweli Mchungu, Usiombe Yakukute, Toka, Tusipindishe, Wakubwa Tu, Rhymes, Furaha, Sio Mbaya, Usawa, Black Woman,  Kitu Kizito

Black Ninja - Ilolo Confirmed 2

 

Ilolo Confirmed 2 pia isingekosa kwenye orodha ya album zangu bora mwaka 2023. Kama unamfahamu Black Ninja, huyu mwalimu ni Boom Bap head mwanzo mwisho kwenye miradi yake na mradi huu wa pili kwenye msururu ya miradi inayotoka chini ya jina Ilolo Confirmed sio tofauti.

Kama ilivyo kawaida ya Ninja kuna wachenguaji wa aina flani anaofanya nao kazi kila mara kama vile akina Cado Kitengo, Bad Ngundo, Plate Mdaijasho, Bill Balaa, Saru Clan, Nikki Mbishi, Ghetto Ambassador na wengine wengi. Kama ulikuwa unatafuta mradi mzuri wa Boom Bap, Ilolo Confirmed 2 hii hapa. Album ina ngoma pamoja na skits jumla 30.

Ngoma Pendwa: Pesa Na Michano, Demu Whack, Fimbo, Mbangaizaji, Mtemi Bad, Nai Nai, Ni Life Tu, Nukuu, Ilolo Confirmed, Ilolo Dojo, Pesa Yetu, Ilolo Hii Hapa, Kitengoni

Nikki Mbishi – Katiba Mpya

Nikki Mbishi nae akaona kama maandamano kufanya kitaani ni tatizo basi isiwe kesi akazama studio ili kutoa maoni yake kuhusu umuhimu wa kuja na Katiba Mpya. Katiba Mpya ilisimamiwa kwa asilimia kubwa na mtayarishaji Black Ninja kutoka Boom Bap Clinic akisaidiwa na watayarishaji kama Pallah Midundo, Black Beats, Nikki Mbishi mwenyewe, Kita The Pro na hata Ghetto Ambassador na Kalumanatics.

Kazi pia ilikuwa na ma emcee wa nguvu kama Kaa La Moto kutoka Kenya, JCB, One The Incredible, Mkoloni, P Mawenge, Mex Cortez na wengine wengi kwenye F.U.B.U  Cypher. Mashairi ya kufikiria kutoka kwa Baba Malcom.

Ngoma Pendwa: Watanganyika Wadanganyika, Kopareti, Resolution, Bara Zuri/Baradhuli, Muziki Haramu, Legend In The Making (LITM), Mashairi, Kazi Mbovu, GAG Wa Mtaa, Katiba Mpya, Nani Aliyeturoga

Mo Plus X D Wa Maujanja - Noma Na Nusu

 

Wana Arusha tena hawa. Veteran emcee Mo Plus (Chanya) ambaye yupo kwenye orodha ya miradi bora 2023 hapo juu akiwa na ChindoMan wakiwa na mradi wao Lindo The Album aliungana na D Wa maujanja ambaye ni nusu ya crew ya Mapacha (Maujanja Saplayaz. akiwa na Kay kutupatia album yao Noma Na Nusu.

Aisee amini nikikwambia huu mradi ni Noma Na Nusu kwani ni kazi ya ki utu uzima mwanzo mwisho. Ni mradi ambao ma old school heads pamoja na ma new school wanaojua kitu kizuri watapenda. Mtayarishaji Justin Cuckaz (Iko Sawa) ndio kahusika pakubwa hapa japokua amesaidiwa na Maco Chali, Q The Don na DJ Azz.

Ngoma Pendwa: Alright, On Fire, Put Your Hands In The Air, Potea, In Life (Wingu), Ghetto, Nipishe Nipite, Hii

Baadhi ya album zingine nilizoziskiza na kuzipenda ni:

Kay Wa Mapacha – 0I 0I
Adam Shule Kongwe – Dr. Shule
EMSA – L.I.D
Jakk Quill – Searching For Utopia
MC Sharon – Jambetre Ngolo
Mnabey – Mnabasics
Game Boi – Victims In Sadness
Duke Tachez - Father X-Mass
Bokonya – Star Wa Kitaa
Fikra Kweli – Late Bloomers
BBoy Blackfire - Macho Kuona
Songa - Mitaa Flani