Ukaguzi wa album: Gold
Msanii: Monski
Tarehe iliyotoka: 20.12.2020
Nyimbo: 14
Ma Producer na wapiga midundo: Alex Vice,Kvpture,HR The Messenger,Jamie Rylo,Epistra,Dope Boyz Music, Mvnci Bevts,Klae Beats,Simba,Maze Music
Studio: Minic Studio

Hayati baba wa taifa la Tanzania alisema hivi kuhusu Nairobi,”Kama ungependa kwenda mji wa London na hauna uwezo, usiwe na shaka, fika hapa Nairobi tu kwani ni half-London! Kila kitu utakachokipata kule London kipo Nairobi tayari!”

Ni katika mazingira haya ya Nairobi ambapo mchanaji Monski  anaye julikana rasmi kama Sarah Mukethe Kiatine alizaliwa mwanzoni mwa miaka ya tisini ndani ya taxi iliyokuwa ikimsafirisha mamake kuelekea hospitali ya Pumwani. Changamoto ziliendelea kumuandama huyu binti na miaka kadhaa baadaye akiwa bado mdogo sana alijikuta yatima.

Sarah alipiga moyo konde na kuendelea kupambana na maisha na akafanikiwa kusoma hadi shule moja ya upili kule Machakos ambapo aligundua kipaji chake cha kughani. Aliendelea kukuza kipaji chake. Akiwa kule shuleni  rafiki yake mmoja akampa jina lake la usanii, Monski. Pia kama vile mkongwe wa Hip Hop Foxy Brown alivyo jiita The Ill Nana dada Monski pia anaonesha kua ananui kufikia viwango vya Foxy kwa kujiita The Ill Dada.

Baada ya kuachia miradi kadhaa iliyomtambulisha kwa mashabiki wake mwaka wa 2020 Monski aliona amekomaa tayari na mwenye uwezo wa kuachia mradi wake wa kwanza: GOLD.

Kama ilivyo kwa dhahabu ambayo hupitia mchakato tofauti toka ardhini hadi kufika sokoni, hivyo basi maisha haya magumu yalimnoa mwanadada huyu na kumfanya naye awe dhahabu ki ugumu na kiuthamani pia.Hivyo hivyo basi ndivyo mradi wa GOLD ulivyochukua muda toka 2014 alipoanza kuandika mashairi yake hadi kufika studio kurekodi kuukamilisha na kuufikisha sokoni.

Single ya kwanza kwa jina Gold ndio umebeba jina la mradi huu. Wimbo una mdundo mzuka  ulioundwa na producer Epistra akipiga vinanda, violin na chelo nzuri sana. Japo kua wimbo huu kama vile nyimbo nyingi kwenye mradi huu zinachanwa kingereza kwa asilimia kubwa, jumbe bado ni nzuri na chanya. Kiitikio cha wimbo huu unaoimbwa na muimbaji Xenia Manasseh unasema hivi,

“If you look into my eyes you will recognize my soul/
If you listen to my words you can recognize its gold/
We are only meant to go higher/
They can never put out this fire! /”

Kwenye wimbo huu Monski akiwa na Trabolee na Manif3sto wanatema madini ya dhahabu ambayo yanakuacha ukiamini kuwa chochote unachokipitia maishani mwako kitakufanya utoke mwenye thamani na ubora zaidi kuliko awali.

Kwenye nyimbo kadhaa Moski anaonesha ujasiri wake wa uchanaji kama vile kwenye Goat akimshirikisha producer HR The Messenger na ulioundwa ki ustadi na Maze Music. Mada ya majigambo inaskika pia kwenye nyimbo za John Cena pamoja na Atrocious akiwa na Okxyde. Out here pia unaendeleza mada hii ambapo Monski akiwa na Boutrous pamoja na Jovie Jov wanajigamba vile wao ni wakongwe kwenye mitaa hii ya rap kwenye wimbo ulio na mdundo mzuri sana.

Mada ya kula bata ni mada ambayo The Ill dada Monski ameigusa kwenye nyimbo kadhaa kama Steady Drippin akiwa na Tunji na Nairobi bounce unaomkuta Monski akitoa shoutout kwa mji wake aliokulia. Kwenye wimbo Kiasi Moski anatuambia vile ni muhimu mara moja moja kujiachia akiimba,

“Unaweza jump kiasi/
Pewa mbili leta top kwa glasi/
Shida nyingi lenga stress kiasi/
Keti chini skiza flow kiasi eeeh eee/”

Wakati watu tofauti duniani wakiendelea kuchangia maoni yao kuhusu mmea wa bangi dada Monski anatupa maoni yake kuhusu boza kwenye wimbo uitwao Hiyo Kitu. Wimbo unapiga taratibu na gita linaskika mdogo mdogo kama vile dada ameshakiwakisha tayari akiwa na kaka Lucid. Anasema Monski,

“Nimechizi kitu flani/
Ningechizi usingedhani/
Usiulize kitu gani/
Pedi nampigia leta kitu tafadhali/
Mapenzi hii ni kali/
Milele kuwa nami/
Sipendi ukiwa mbali/
Pedi nampigia leta kitu tafadhali”

Anaendelea kwa kuongea na bwana Cannabis akimwambia,

“Nimejiingiza box hiyo mi sibishi/
Hawataki tuwe close but sitishiki/
Bila wewe mi nahisi hivi hivi/
Nikubomoe kisha niku set kwa ziggy/
Nikupumue alafu kisha niskie fiti/
Wanifanya napepea hapa juu ya kiti/
Natabasamu kila saa kila wiki/
Hii safari bila wewe mi sifiki/”

Mahaba ya Monski juu ya Hiyo Kitu ni ya dhati.

Happy ni wimbo mzuri pia ulioundwa kiustadi sana anaomshirikisha mwimbaji Agolla. Saxaphone linapiga kwenye mdundo unaogonga taratibu akitukumbushia Monski kuwa kwa kila tunachokifanya kila siku kuwa na furaha ni maamuzi yetu binafsi. Anasema hivi Monski beti ya pili ya wimbo huu,

“Wanasema happy is a mindset/
Niko na mind set/”

Furaha ni mtazamo wako kwa hiyo fanya maamuzi uwe ni mtu wa furaha. Wimbo ni madini tupu.

Nyimbo nyingine zilizosimama toka kwenye mradi huu ni kama 4K, Midas touch na Run It Up ambazo zinatufungia mradi huu. Kwenye wimbo wa 4K, Moski anajadili changamoto za siasa nchini Kenya. Kiuhalisia 4K ni kauli mbiu ya klabu cha kilimo ya shule za Kenya ikiwa na maana “Kuungana, Kufanya, Kusaidia, Kenya” ila Monski kwa kuchoshwa na serikali yake ambayo anaona hawaajibiki kama wapaswavyo anabadilishia maana ya 4K kumaanisha “Kukula, Kukunywa, Kuvuta, Kuiba”.

Run It Up pia ni wimbo mzuka sana wenye vinanda kama soundtrack ya movie unapo anza anaowashirikisha ma emcee Katapilla pamoja na muimbaji Tesla anayetuimbia kiitikio na sauti yake murua sana. Monski anasema anajiamini kwa kile anachokifanya,

“They can’t get enough they know the flow is addictive/
We were putting work I was building up this biz/
Some suckers doubted they thought it was risky/”

GOLD ni mradi uliosimama ki production, kiuandishi na pia kiuchanaji. Wageni wote waalikwa walijituma kuhakikisha mradi huu utakuwa dhahabu ya grade ya juu pindi itakapofika sokoni. Kwa kuwa mradi huu ni wa Nairobi, Kenya jiandae kujifunza misamiati mipya ya Sheng kama vile kuchachisha na kadhalika. Midas touch ya Monski ipo bayana kwa kila atakayepata mda kusikia mradi huu. Mradi huu naweza sema una asilimia themanini ya dhahabu ambayo si mbaya sana ukilinganisha hii ndio mara ya kwanza dada huyu kuzamia machimboni kujaribu kutafuta na kutuletea madini ya GOLD.

Mfuate Monski kupitia mitandao ya kijamii:

Instagram: hail_monski
Facebook: Monski Fan Page
YouTube: Monski 254