Msito

Msito ni mmoja wa wachanajii chipukizi kutoka handakini wanaoinuka kwa kasi zaidi wakitokea Mecca ya Hip Hop Kulture nchini Kenya, Dandora. Baada ya kuanza maisha yake ya muziki tangu utotoni, chipukizi huyu ameweza kunoa ustadi wake wa kuandika, wakuchana na wa mtindo huru na hivyo kuzua gumzo katika anga za Hip Hop sio tu nchini Kenya pekee bali hata Afrika Mashariki pia.

Njoo usome hadithi yake anapokupeleka kwenye safari yake ya muziki iliyoanzia ndani kabisa ya mitaa ya Dandora na inaendelea sasa kwenye kwenye studio za muziki.

Karibu Micshariki Africa kaka Msito. Mara ya mwisho tulikutana huko Dandora ambapo bila kupanga tulifaulu kufanya podikasti ya video ambayo ndio ilikua podikasti yangu ya kwanza ya video ambayo ilisababisha podikasti nyingi zaidi kama hizo. Umekuwaje tangu tulipokutana mara ya mwisho na unaendeleaje?

Nimekuwa sawa na tangu mara ya mwisho tulipokutana, nimekuwa nikifanya kazi kwenye miradi kadhaa. Nilishirikishwa kwenye KiswaHealing 2 ambayo ni albamu inayokuja ya Maovete. Pia nilipata kufanya kazi na Icon Radio ambapo tulitoa nyimbo nne ambazo kwa sasa tupo katika mchakato wakuziandalia video.

Pia nilifanya kazi kwenye na jamaa za Umoja Sounds ambapo nilipata nafasi ya kufanya kazi na baadhi ya wachanaji kundi la Ukooflani MauMau .

Kwa wale wasiokufahamu jitambulishe, Msito ni nani , majina ya serikali na unajihusisha na nini?

Msito ni msanii wa Hip Hop anayeishi Dandora, Nairobi Kenya. Jina langu rasmi ni Dennis Kimatu Mueni . Kando na muziki mimi pia hufanya ukusanyaji wa takataka kama harakati za maisha yangu ya kila siku.

Tuambie kwa ufupi kuhusu msingi wako wa muziki, safari hii ilianzaje kwako?

Safari yangu ya muziki ilianza nikiwa mdogo. Nilijiunga na MauMau mara ya kwanza nilipokuwa na umri wa miaka saba na nikapata fursa ya kufunzwa na wakuu wa Hip Hop. Katika kambi ya MauMau nilikutana na watoto wengine wadogo ambao pia walikuwa wanarap na tukaanzisha kikundi kilichoitwa Wafalme. Ni miaka 17 tangu nianze kufanya muziki.

Jina lako Msito lilikujaje na lina maana gani?

MSITO ni ufupisho unaotokana na neno la Kiswahili mzito lenye maana ya Mzito. Tangu niamue kuchana nikiwa peke yangu baada ya kundi kusambaratika watu wengi walikuwa wakiniambia kuwa nina nondo nzito. Neno MSITO pia nililipa maana ifuatayo;

Music (Mzuiki)

Soothes (Hutuliza)

Inside (Ndani)

Truth (Ukweli)

Only (Pekee)

Ndivyo jina MSITO ilivyokuja pamoja na maana yake.

Nilishangaa kugundua kuwa umekuwa ukiimba, ukirekodi na kutengeneza video za muziki tangu ulipokuwa una miaka 8? Je, uzoefu wako wa kufanya kazi na Dandora Music ulikuwaje na uliathiri vipi ukuaji wako kama msanii?

Kufanya kazi na Dandora Music kulikua na athari chanya sana kwa ukuaji wangu kama msanii tangu nilipopata nafasi ya kutumbuiza kwenye majukwaa makubwa na kuangaza uwezo wangu kwenye televisheni na magazeti nikiwa na umri mdogo. Wakati huo muziki ulilipia elimu yangu na mahitaji mengine ya kimsingi. Nilianza kuelewa muziki zaidi na mapenzi yangu kwa muziki wa Hip Hop yaliongezeka na hii ilinipa heshima kubwa sana. Niliweza kujifunza mengi zaidi kuhusu muziki nikiwa mdogo.

Kuwa katika tasnia ya muziki tangu umri mdogo hadi sasa lazima huja na changamoto zake. Je, umewezaje kuendelea na kasi ile ile ya mwanzo na kuendelea kufuata ndoto hii ya kua emcee wa Hip Hop?

Mimi maisha yangu yalikua ya hali duni sana wakati kule vitongoji vya Dandora na nimeona vijana wadogo wakipigwa risasi kutokana na uhalifu huku wengine wakiishia gerezani. Eneo letu lina sehemu kubwa zaidi la kutupa taka barani Afrika ambalo ni takriban ekari 30,000 za ardhi na eneo hili linalisha zaidi ya vijana 1,000. Kila aina ya utumiaji wa dawa za kulevya na vitendo vya uhalifu hufanyika huko. Changamoto na mambo niliyoyapitia humu ndio yananisukumu mimi kuendelea na hii ndoto ya kua mwana muziki na kamwe sitoacha kuifukuzia ndoto hii.

2022 ulikuwa mwaka ambao ulikua busy sana kwako. Ulifanikiwa kua katika kipindi cha pili cha Door Knockers Cyphers. Je, ulijiskiaje kufanya kazi na waandamizi wenzako kutoka ukanda wa Afrika Mashariki?

Kutokea kwenye Door Knockers Cypher (DKC 3) ilikuwa hatua kwangu. Ninawashukuru washirika wote waliokuja na jukwaa na kuunganisha wasanii kutoka Afrika Mashariki. Kwa kweli nilijisikia vizuri kupata fursa na kufanya kazi na watu kutoka kanda hhi, pia nilijifunza mengi kuhusu tamaduni za watu wengine kutoka kwa mashairi ya wasanii wenzangu na pia video ya kule wanapotokea washiriki wenzangu wa (DKC3). Kwa kweli nilijiskia fahari kushiriki kwenye cypher.

Pia ulitoa mradi wako wa kwanza kamili EP inayoitwa Gorilla. Je mchakato mzima ulikuwaje wakati ukiandaa mradi huu, ni nani walikuwa watayarishaji na wasanii uliofanya nao kazi? Kwa ujumla mradi mzima ulikuwa unahusu nini?

Ndiyo nilitoa mradi wangu wa kwanza, Extended Play list (EP) iliyopewa jina la Gorilla EP mwaka wa 2022. Singo ya kwanza niliyoiachia kutoka kwa EP hii ulikuwa Street Life ambao ulirekodiwa pale Dandora Hip Hop City Record's (DHC) mnamo 2021. Ulirekodiwa na kutayarishwa na Andare James. Niliunda wimbo huu baada ya kuwa kimya kwa miaka michache tangu kundi letu lisambaratike. Wimbo huo ulitokana na mambo niliyokua nayapitia maishani mwangu.

Baada ya kusikiliza wimbo huo nilihamasishwa kufanya nyimbo nyingine kutokana na mapokezi mazuri kutoka kwa waskilizaji. Niliingia studio tena na kuamua kurekodi Gorilla 1&2 ambazo zote zilirekodiwa katika 32 Records na James Elshado mnamo 2022. Pia ni sadfa kua Andare na Elshado ni wajina (wote wanaitwa James). Brima Maovete alipata nafasi ya kusikiliza nyimbo hizo katika Studio ya 32Records na akanishauri niunde mradi mzima. Alijitolea kulipia mradi huo na akafanya video yangu ya kwanza bila malipo kwani alijua ninachopitia. Brima aliokoa ndoto yangu (ya muziki). Pia alinitambulisha kwenye Studio ya Truce Label na huko nilipata nafasi ya kurekodi nyimbo zingine kwa ajili ya EP yangu. Nyimbo hizo zilirekodiwa na kusimamiwa vyema na mtayarishaji Kunta Official Beats .

Niliwashirikisha wasanii wanne kwenye mradi huu kwenye nyimbo zifuatazo;

Sura Punda ft. Brima Maovete na Snaidah Don dada

Each One Teach One ft. Brima Maovete na Shazzy B

Rada Ni Safi ft. Mc Lyrics

Mradi mzima ulilenga uzoefu wangu na mambo niliyokua nayaona kwa jamii yangu.

Ulikuwa makini sana katika kutangaza mradi wako ambao uliutolea video mbili. Maoni kutoka kwa mashabiki wako kuhusu mradi huo yalikuwa gani?

Nilipata maoni mazuri kutoka kwa mashabiki wangu. Jina langu pia lilikua kwa kiwango cha juu kwani watu wengi walihusiana na video za ngoma zangu. Video hizo pia zilinisaidia kutangaza EP yangu vizuri na kuniwezesha kuuza nakala (CD) za EP yangu.

Changamoto zozote ulizokabiliana nazo katika safari yako kama chipukizi na pia ulipokuwa ukitengeneza EP yako ya kwanza?

Nilikumbana na changamoto nyingi kama chipukizi kwa kuwa vikundi vyote ambavyo nilifanya kazi navyo vilianguka hadi nikaamua kufanya kazi peke yangu. Wakati natengeneza EP yangu sikuwa na pesa za kulipia studio na sikuwa na matarajio mengi ingawa kila kitu kilienda sawa

Mashabiki wako watarajie nini kutoka kwako mwaka huu wa 2023, una mpango gani nao?

Mashabiki wangu watarajie nyimbo kubwa na video 4 kutoka kwa EP yangu, pia nimeshirikishwa kwenye albamu ya Maovete na nina EP ya nyimbo tano kutoka kwa Icon Radio nikiwashirikisha Elijah Moz, Snaidah Don Dada, Nem R na Shazzy B. Singo kibao zinawajieni mwaka huu.

Micshariki Africa na K Dawg (Truce Label) wamekualika ufanye nao kazi katika mradi wao shirikishi pamoja na Fedoo kutoka Tanzania. Una maoni gani kuhusu hili na mashabiki wanapaswa kutarajia nini kuhusu mradi huu?

Kwa unyenyekevu naishukuru Micshariki Africa kwa kunialika kwenye mradi huu na kuniunganisha na Fedoo ambaye anaiwakilisha Tanzania. Kwa kweli najisikia kuhamasishwa na kuthaminiwa 🙏🏿 . Mashabiki wote wategemee muziki mzuri utakaoelimisha na kuburudisha. (Tazamia kinachotarajiwa!)

Je, ilikuwaje kufanya kazi kwenye mradi huu na umefurahia kwa kiasi gani kufanya kazi na mwenzako kutoka Tanzania, Fedoo ?

Kufanya kazi na Fedoo (Tanzania) imekuwa moja ki kitu kizu sana kuwai kutokea kwangu kwani nimejufunza mambo kadhaa kutoka kwake. Mradi wetu utakuwa kitu ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo awali na ndicho ninachofurahia zaidi.

Asante kwa wakati wako, neno la mwisho?

Afrika itahisi nguvu katika muziki na mradi wa Micshariki Africa. Harakati mpya ya Hip Hop ya Kizazi kipya kinayofanya kazi ni ishara kwamba muziki wa Hip Hop utaunganishwa 💯.

Unapatikana wapi kwenye mitandao ya kijamii?

Instagram: dennis_msito_32
Facebook: Dennis Msito (Gorilla)