Ukaguzi wa EP: Mbingu Zatazama
Msanii: Muki Rai
Tarehe iliyotoka: 24.04.2021
Nyimbo: 5
Ma Producer/Wapiga midundo: Luwibeatz, Difrebeatsworldwide, CrocoMusic, NG
Mchanganyaji sauti na midundo: Arcane Krisphah (Ndovu Kuu)
Studio: Utopian Music
Baada ya miaka miwili kamili ya kuangusha tape yake ya kwanza Taswira Ya Fanaka (2019) emcee Muki Rai alirudi tena na kutupatia EP nyingine tena tarehe 25 April 2021 iendayo kwa jina Mbingu Zatazama.
Muki Rai ambae anajulika rasmi kama Daniel Mukirai ni emcee anayepatikana kule Kikuyu iliyopo Kiambu County, Kenya. Muki Rai ni emcee aliyehitimu toka chuo cha sanaa nchini Kenya. Kijana huyu ambaye amekuwa akichana tangu 2011 aliweza kufanikisha ndoto zake za kurekodi mziki wake 2015 na kuanza kuachia singo kadhaa kutokea hapo.
Mara ya kwanza mimi kumsikia Muki alinikumbusha emcee wa mamtoni E-40. Sauti ya Muki na utunzi wa mashairi yake yanayoandikwa kwa umakini ndio yalinifanya mie nimfananishe na E-40
EP hii ambayo imesimamiwa asilimia 100 na producer Arcane Krispah almaarufu Ndovu Kuu inaanza na Kitendawili ambacho tunatakiwa tukitegue kwenye mdundo flani wa Drill ambao amemshirikisha Malie. Mradi huu ambao uliundwa wakati wa janga la Corona ambalo limetuathiri sote pia limemuathiri Muki naye anatudhihirishia hivyo kwenye wimbo akitema mistari hii,
“Kuji distance hukuaga ni instantly/ (Mi kukanyaga kubwa nikiskia wakikoroma)
Si ati nini ama nini, ku quarantine/ (Ni habit nili adopt before Corona)”
Mali Ya Polisi ambao ndio wimbo wa pili kwenye EP hii ya nyimbo tano ni moja ya wimbo uliosimama sana na unaonesha vile kalamu ya Muki ina uwezo wa kuandika mashairi kuhusu maisha ya mwananchi wa kawaida (Wanjiku) na changamoto anazopitia toka kwa polisi ambao badala ya kumlinda, wanamnyanyasa, wanamdhalilisha na wakati mwingine hata kumuua.
Akiwa na Oksyde pamoja na Ndovu Kuu kwenye mdundo na kiitikio, ma emcee hawa kwa pamoja wanatema nyongo dhidi ya polisi. Muki haogopi kusema wazi changamoto ambazo amezipitia yeye binafsi kwenye mikono ya polisi akisema,
“Katika ile hali ya kusaka maziwa, Mtaani tumezoea ni kawa ni kudandiwa/
Me si wa Mungiki ila me ni mzaliwa, so usidhani hiyo bunduki inantishia/
Ni wazi ya kuwa, yako kuniua ndio nia, bila hata hatia/
Nikiwa tu kwa njia me sio kiruka njia, mimi tu ni raia sivunji sheria/
Hapa ndio home sa siezi kula vako? Hapa ndio home kwani siezi piga rao?/
Aih mkubwa, heshima si utumwa usinidharau, ni how?/”
Wimbo wa tatu kwenye EP hii ni Girimba. Neno Girimba lina maana ya ulafi au mtu mlafi ila hapa emcee huyu analigeuza na kulitumia kuonesha vile yeye ana tamaa na vitu vizuri maishani mwake ila kwa kupitia jasho lake. Mistari yake imesukwa makini sana kama rasta za maasai, hivyo lazma uchukue mda kuelewa mashairi yake pamoja na sheng inayotumika hapa.
Utakavyo ni wimbo ulioundwa na CrocoMusic ambao unaongelea changamoto za mihadarati na pombe mtaani na ni wimbo wa nne kwenye EP hii. Mbali na kutajiwa mihadarati kwa lugha ya sheng, mistari inatoka ambayo yenye ucheshi toka Muki na Oksyde ambae kashirikishwa tena. Muki anakueleza madhara ya kutumia vilevi kwenye kiitikio akisema,
“Huku maisha si London ipasavyo/
Lakini huku stimu utapata utakavyo/
Zita rundo hata utashindwa hata kuraukia wera/”
Hapa anamaanisha japokuwa maisha ya kitaa chao sio kama yanayopatikana mji mkuu wa Britain, utapata kila aina ya kilevi chenye uwezo wa kukusahaulisha majukumu yako kama vile kurauka kwenda kazini. Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu Julius Nyerere hakukosea aliposema Nairobi ni half-London. Jiandae kutafuta kamusi ya sheng kwa ajili ya kuongeza misamiati ya aina ya mihadarati inayotajwa kwenye wimbo huu; mavele, vela, veve, mushroom, mataptap, shuksha, kishashola, na kadhalika!
Producer NG naye anashika doria kwenye mdundo wa Mabadiliko ambao ndio tamati ya mradi huu. Wimbo huu ni wimbo wa kutupatia matumaini na kututia moyo kuwa mazuri yanakuja kama tutafanya subra. Dada Truphie kwenye kiitio anaimba kwa sauti nzuri inayotutia moyo akisema,
“Ni matatizo ya jana yalinipa masikitiko/
Hata sikudhani ya kwamba ningefika mahali nipo/
Mwenda pole hajikwai natarajia mabadiliko/
Moja kwa moja taratibu nikingoja mabadiliko/”
Mbingu Zatazama ni mradi mzuri toka kwa emcee huyu ambaye ameonesha uwezo wake kimashairi na kimada kwani kila wimbo ndani ya EP ulikuwa na lengo flani ambao ulichangia mada nzima ya mradi. Mradi ni mzuri ila nilipenda kuskia ma Boombap pia kwani mie ni shabiki wa hizi lakini Muki alinishawishi kuwa hata kwa mdundo wa Drill madini pia yapo kwa wingi.