Ukaguzi wa album: Black Mwamba
Msanii: Mwamba Mgumu
Tarehe iliyotoka: 23.03.2021
Nyimbo: 13
Ma Producer na wapiga midundo: Black Mwamba (Sima on the map)
Uchanganyaji sauti na midundo: Mweusi Traveller, Flyder
Studio: Magix Sound Production

Koboko au kwa jina la kimombo Black Mamba anasemekana kuwa aina ya nyoka mwenye sumu kali zaidi duniani baada ya Swila Mfalme au King Cobra. Hivyo basi unapomchokoza Koboko ujue akikudonoa madhara yake ni kifo moja kwa moja kama utachelewa kupata dawa dhidi ya sumu ya nyoka huyu.

Mwamba Mgumu aliyezaliwa miaka ya mwanzo ya tisini anajulikana rasmi kama Lameck Sinika Tungu. Ni emcee ambaye amekuwa kwenye game la Hip Hop tokea 2016 na hadi sasa ameachia EP nne “Njia Yangu”, “Nira”, “Game Over” na “Beautiful Chaos” pamoja na album nne “Hali Halisi”, “8619”,”Ushindi” na hii ya mwaka huu “Black Mwamba”. Hili linakuonesha wazi kuwa penseli ya Lameck kila mara inazidi kunolewa ili kuweza kuandika mashairi kwenye daftari lake.

Kwenye mradi huu wa Black Mwamba, Lameck amejikuta ana hasira sana kama za Koboko hivyo basi album hii iliyopo chini ya dakika 30 ina lengo la kutema sumu iuayo fasta sawia na ile ya Koboko lengo likiwa kuua ma emcee chawa.

Baada ya utangulizi wa albam Mwamba Mgumu anaanza kutema mistari yenye sumu kali kwa wapinzani wake akiwaambia kuwa ana,

“Sumu aina mbili single bite 20mls/
20 minutes upo chini ushatutoka Rest In Peace/”

Na kama vile Koboko alivyo na tabia ya kurudia kugonga mara kadhaa, Mwamba anaendelea ki sitiari akionesha hata vile yeye mistari yake akikulenga hakuachii hadi roho ikate akisema kwenye kiitikio,

“Mchezo na mimi na wewe huku haipo/
Wenzako wananiogopa wananiita busu la kifo/
Kichwa juu mita mbili sitishiki utajutia/
Nikikugonga mara moja siridhiki narudia/”

Maadui wa Mwamba wawe makini na hili.

Uwezo wa Mwamba Mguu kuandika tamthilia ki mashairi unaonekana kwenye wimbo uitwao Changamoto ambao unamkuta emcee huyu kamdunga mimba denti wa shule na kwa kuhofia kuchukuliwa sheria na serikali na jamhuri anaamua kusepa baada ya kujilipa ki Belle 9. Ila kwa kuwa alikuwa na upendo wa dhati na binti huyu anajiweka hatarini kwa kumuandikia barua ya kumfariji.

Kwenye album hii pia emcee huyu amekaribisha ma emcee na waimbaji kadhaa kufanya naye kazi kama vile G Black, Ntuzu Boy, Bassnass,Dynamic Gos, Venture na Bc Bu. Kwenye wimbo wa Utata ulio na mdundo ambao gita linapiga mdogo mdogo wageni Venture na Bc Bu wanajitahidi kwenda sambamba na Mwamba Mgumu wakimwaga punchline za kijanja akisema Venture,

“Simiyu begani ndio yangu kauli mbiu/
Nawashangaa vichwa maji wakisema wanahisi kiu/”

Ilhali Bc Bu anasema,

“Ujue siku ukifa kwa vijembe utazikwa na madera/
Na ukifa na kiharusi basi shera/”

Kando na punchlines Mwamba Mgumu anazungumzia hoja muhimu kwenye nyimbo kama vile Utumwa na Habari Imesambaa ambazo zinamkuta emcee huyu akiongelea ukoloni mamboleo na gonjwa la Corona. Utumwa inamkuta Mwamba akitupa tahadhari kuhusu mambo yanayoletwa na watu weupe kuwa sio yote ni mazuri kwa mfano dawa za mpango wa uzazi na pia wanavyofanya majaribio ya dawa zao huku kwetu Africa.

Pia wimbo mwingine wenye hoja nzuri japokuwa nao ni mfupi ni wimbo uitwao Upuuzi Unaendelea unaomkuta Mwamba Mgumu akiongelea tasnia ya muziki kiujumla na changamoto wanazopitia wasanii wengi sio ma emcee tu zikiwemo ishu za rushwa za fedha na  ngono pamoja na mapungufu ya BaSaTa ili kufanikisha miziki yao kuchezwa maredioni na kuoneshwa kwenye runinga. Mwamba Mgumu anarusha dongo akisema,

“BaSaTa nao wamelala usingizi wa pono/
Video wanazoruhusu ni nusu ya picha za ngono/
Cheki ngoma kwenye chati/
Hakuna maudhui nishawasoma wawekezaji!”

Kwa upande wangu hii albam ilikua nzuri bali fupi. Mashairi ya nyimbo nyingi yalikua na vesi moja na pia fupi mmo chini ya dakika mbili. Kwa mfano kwenye wimbo kama Changamoto intro ningefurahia kama kungekuwa na sehemu ya pili bado kwenye album hii. Mwamba Mgumu amejitahidi ila naamini bado angetupa mengi zaidi kwenye album kimashairi na kwa ubora wa midundo kama angevuta pumzi na kupunguza hasira za koboko.

Kupata album ya hii ya Black Mwamba wasiliana na Mwamba Mgumu kwenye namba ya simu +255 742 097 950 au pia kupitia mitandao ya kijamii:

Instagram: @iam_namba_10

Facebook: Mwamba Mgumu