Uchambuzi Wa Album: Compilation CD
Msanii: Nafsi Huru
Tarehe iliyotoka: 2017
Nyimbo: 10
Watayarishaji: Chizan Brain, Nje Producer Msanii-Ufuoni Records, Ananda Edward, MG, Mosee, Mansachusa

Ulimwenguni kuna ma Rais tofauti tofauti; kuna ma Rais wa Nchi, ma Rais Wa vilabu vya michezo na pia ma Rais kwenye sanaa ya mziki kama vile rais wa Manzese, rais wa WCB na pia rais bila Ikulu ambaye ni mheshimiwa Nafsi Huru toka Mombasa, Kenya na anajulikana rasmi kama Musa Adam. Rais bila Ikulu linamtambulisha Nafsi Huru kama kiongozi aliye nje ya mamlaka ya kiserikali na siasa.

Nafsi Huru ni Emcee toka Mombasa aliyezaliwa miaka 34 iliyopita kule Mombasa na anatokea mitaa ya Magongo. Nafsi Huru anajitambulisha rasmi pia kama Swahili Hip Hop Ambassador na kando na kuwa Emcee ni mwanaharakati na mtu mwenye talanta nyingi kama, mwandishi wa gazeti moja nchini Kenya,mjasiriamali, graphics designer na Disc Jockey (DJ).

Nafsi Huru alianza muziki utotoni na kwa bahati nzuri alibahatika kuwa mtaa mmoja na jeshi la wasanii wa hip hop Ukoo Flani toka Mombasa mitaa ya Magongo. Msanii kama Nguchi P na wengineo toka Ukoo Flani walimpa Nafsi Huru hamasa sana Ya kujaribu uchanaji. Baada ya kuingia Chuo Kikuu Cha Nairobi (University of Nairobi) akisomea Shahada yake(Bachelors of Commerce – Marketing option) 2007 alibahatika tena kuishi na kundi hili kule Nairobi wakati walipokuwa wakiandaa mradi wao uitwao “Kaya HipHop”. Hapo alipewa beat na super producer Chizan Brain na kuunda wimbo wake wa kwanza Tunasonga ambao upo kwenye Compilation CD hii iliyoachiwa 2017.

Mbali na Compilation CD hii kutoka 2017, Nafsi Huru hapo awali alikuwa ameshatoa nyimbo kadhaa na kanda mseto (mixtape) moja 2012.

Kwenye compilation CD hii aliwashirikisha wasanii wengine kama Juma Tutu, King Bilari, Emcee/Producer Chizan Brain,Kaktus, Man Op wa Skani Flani, E Mc, Ananda Pamoja na Fikra Teule.

Compilation CD ina Ukweli mwingi kama unavyosema wimbo wa kwanza kwenye mradi huu. Nafsi anachana mistari kadhaa ya kukufanya utafakari kwa kina anachomaanisha  akisema,

“Sio lazima utege skio ndio uiskie radi/
Pia viziwi hushtuka inapo tetemeka ardhi/
Walimwengu ni baadhi ndio waadilifu/
Wengine wote waliosalia sio waaminifu/”

Pia album hii ina nyimbo kama Gozigozi inayoonesha changamoto za maisha yetu, Haja Gani akimshirikisha King Bilari inayohoji vile tunavyovipatia thamani vitu visivyo na thamani yoyote. M.U.S.A iliyotoka kwenye ile mixtape iliotoka 2012 ipo kwenye Compilation CD hii na imeundwa ki ustadi na Chizan Brain pia. Kwenye wimbo huu Nafsi Huru anadeka vile yee emcee tofauti, matawi ya juu.

Sitachoka ni wimbo mzuri sana ambao beat yake imeundwa kwa kifaa cha muziki kiitwacho Xylophone na wimbo unatuhimiza kutochoka kuota, kiitikio kilicho imbwa na Kwame Rigi kikisema,

“Sitachoka kungoja/
Na sigomi kuota/
Ninapaa, ninang’aa/
Nipe time nita pepea/”

Nafsi Huru pia hajasahau nyumbani anapochana juu ya wimbo ambao beat imeundwa kwa ki Bango-Salsa uitwao Uzalendo. Saxaphone kama ya Mzee Ngala wa Freetown, Mombasa inaanza kwenye wimbo huu unaohimiza upendo, uwiano na umoja kwenye jamii, “Upendo ndio ukithiri/Chuki isituathiri/Nchi ndio inawiri/Mambo yawe shwari/" anasema Nafsi Huru.

Nyimbo zilizopo kwenye album hii ni nzuri, zinaburudisha, zinaelimisha na zinagusa uhalisia wa maisha yetu ya kila siku.Compilation CD hii ni msingi mzuri uliojengwa thabiti kwa ajili ya miradi mingine ya baadaye atakayoachia Nafsi Huru.

Kupata nakala yako ya mradi huu wasiliana na Nafsi Huru kupitia;

Facebook: Nafsi Huru
Instagram: nafsihuru

Yela Yela!