Uchambuzi Wa Album: Uhuru Wa Nafsi
Emcee: Nafsi Huru
Tarehe iliyotoka: 10.10.2022
Nyimbo: 10 (+ Intro)
Watayarishaji: Ananda A World, Akishpro, Addi Beats,
Mixing & Mastering: Chzn Brain
Studios: Wanene Studios, Shaash Studios, BigChase Studios

Nyimbo Nilizozipenda: Nafasi Yako, Mahaba, Lost, Hema Hema, I Wish, Zoza, Africa Simama, Simba Wa Magongo, Raha, Trust Nobody

Nafsi Huru

Baada ya miaka kumi tangu alipoingia kwenye game, Nafsi Huru ama ukipenda Rais Bila Ikulu aliamua kuadhimisha hatua hii kubwa kwa kuachia album yake Uhuru Wa Nafsi. Hapo awali emcee huyu alikuwa ashawachia mixtape kadhaa ambazo zilipokelewa  vizuri na mashabiki wake.

Kwa wale ambao pengine hawamfahamu Nafsi Huru ni mtaalamu wa sanaa ya ubunifu, mwanamuziki, Dj, mbunifu na mtaalamu wa kibinadamu anayeishi Nairobi Kenya lakini asili yake ni Magongo huko Mombasa.

Na kusema kweli mradi huu ulikuja na matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki wake wakitaka kujua, je Nafsi atawaweka Huru inapokuja kwa muziki watakaoupokea kutoka kwake? Nafsi naye hakuwaangusha. Mpishi mkuu wa mradi akiwa Chizzen Brain, mwenyeji wa Mombasa aliyejikita Dar Es Salaam basi moja kwa moja unajua viwango vya mradi vitakua vya hali ya juu.

Rais Bila Ikulu

Mradi unafunguliwa na Intro kutoka kwa Nafsi Huru akiwa mazingira flani ya porini kabla ya Nafsi kuweka gia ya kwanza kwenye Nafasi Yako juu ya mdundo wa Akishpro na moja kwa moja anaanza kukuonesha umahiri wake inapokuja kwenye swala la uandikaji mashairi, uchanaji, unataji kwa mdundo pamoja na uwezo wake wa kuimba pia. Wimbo huu unatambua na unasheherekea umuhimu wa watu wetu wa karibu; baba, mama, mke na watoto pia. Nafsi anawaambia hivi wapendwa wake kwenye beti ya pili,

“Undugu haununuliwi/
Undugu hauchaguliwi/
Undugu haubaguliwi/
Undugu huwa haukimbiwi/
Undugu hausingiziwi/
Undugu ni urafiki sugu usiokosa mavurugu/
Na ndugu sio ndugu wa damu pekee/
Kuna marafiki wanaohitim/
Inanilazim niwape shukrani/
Maana naona umuhim wenu maishani/
Tubakieni one visirani visije ingia asilani/
Kutengana iwe abadan katan ama namna gani/
Nguvu yetu iwe kwa umoja sio kuonyeshana vioja/
Kwa dhiki ama faraja siku zote tuwe pamoja/
Sioni haja kujenga ukuta tushikane kuunda daraja sote tupate faraja/”

Baada ya hapa emcee huyu anazama kwenye mambo ya mapenzi na Mahaba kabla ya emcee huyu kutuambia tusimuamini mtu yoyote kwenye Trust Nobody ambao unapiga chini ya dakika 2 na unatupa angalizo kuwa sio wote wa kuaminika. Wimbo huu ndio uliachiwa rasmi kama singo ya pili toka kwa album hii.

Kisha emcee huyu anashirikiana freshi sana na gwiji wa saxophone toka Mombasa Tutu kwenye Lost, wimbo flani mzuka sana unakupatia nostalgia.

Kwenye Hema Hema akishirikiana na Kev Mamba kutoka kundi la Washamba Wenza wanawakejeli ma emcee kanjanja ambao wanategemea ma back plays ili kuweza kuburudisha mashabiki wao kwenye matamasha ilhali huwa wanajisifia kuwa wao ni noma. Ngoma flani yenye ucheshi sana.

Nafsi anaendelea kuachia nondo zake kwenye I Wish ambao unapiga tarumbeta flani mzuka sana kwenye mdundo flani mzuri ambao utakufanya kama sio kucheza basi utikise kichwa chako ilhali mashairi yakimiminika toka kwa kinywa chake kuja kwetu kupitia kinasa.

Emcee huyu anaungana na mwenzake kutoka Mombasa, Kaa La Moto kwenye Africa Simama wakituhamasisha tuongee pale tunapoona hali sio nzuri. Kwenye kiitikio kuna dada kaimba freshi sana ilhali wawili hawa wanakuonesha kuwa Rap ya Mombasa ipo kwenye mikono salama.

Kwenye Simba Wa Magongo ambao uliachiwa kama singo ya kwanza emcee huyu anaiwakilisha mitaa anayotoka na anatumia mda kujigamba kuhusu uwezo wake pia. Baada ya hapa tuna Zoza na kisha kwenda moja kwenda kwa ngoma flani mzuka sana ambapo magwiji wa Ukoo Flani Mau Mau, Chzn Brain akiwa kwenye mdundo anasaidiana na Mchizi Gaza kwenye kiitikio kutupatia Raha.

Nafsi Huru ametumia ujuzi wake wa miaka kumi kutupatia album ya ki utu uzima sana. Kiswahili safi, mashairi mazuri, uchanaji na uwasilishaji wa kipekee, midundo imechaguliwa kwa umakini na ubora wa sauti wa mradi wote ni wa hali ya juu, Uhuru Wa Nafsi.

Instagram: nafsihuru
Facebook: Nafsi Huru
Twitter: @NafsiHuru