Nala Mzalendo

Japokua Tanzania haijahalalisha mtu kuwa na uraia wa nchi mbili, leo nimefanikiwa kumpata emcee flani toka Njombe ambaye ana pasipoti mbili na kazimiliki kihalali kabisa bila kuvunja sheria.

Emcee huyu pia amebarikiwa na vipaji kibao vikiwemo uandishi wa mashairi, kughani, ucheza mpira wa miguu pamoja na uigizaji. Kijana huyu ameweza kukuza vipaji hivi vyote wakati akiwa chuo akisomea Shahada Ya Rasilimali Watu (Bachelor in Human Resources).

Hapa simzunguzii mwingine bali namzungumzia Nala Mzalendo. Karibu umfahamu yeye na uweze kujua kando na Tanzania ana uraia wa nchi gani nyingine!

Karibuni.

Karibu sana Micshariki Africa, jukwaa la Hip Hop. Kwanza kabisa tuanze kwa kumfahamu Nala. Jina lako rasmi ni nani na unajishughulisha na nini?

Kwa majina naitwa Sudi Ally Mwakilachile au Sudi Aidan Andrew Mtewele Kalonga. Ally Mwakilachile ni jina la Babu kizaa mama. Nimelelewa na familia ya mama na ndipo nilipokulia na ndo maana nilitumia jina la babu. Baba yangu alifariki kitambo kipindi naanzishwa shule hadi namaliza shule yeye hakuwepo. Hivyo basi mchongo mzima alisimamia babu. Ila huyo Aidan Andrew Mtewele Kalonga ndio jina la baba rasmi.

Nala tueleze story yako ya nyuma ya mziki?

Mziki tulianza shule miaka ya 2005 kipindi akina Professor Jay wameachia ule wimbo wao Nikusaidieje , nilikua napenda kuimba zile nyimbo zao hadi 2008 nikawa napenda ngoma za Z-Anto nilipenda nyimbo zake kama Binti Kiziwi hadi 2010 tukawa tunaimba nyimbo za Tip Top Na TMK.

Pia tulikua tunashiriki kwenye vikundi vya ngoma kama ngonjera, kuaga madarasa kwa wanafunzi wanaohitimu darasa la Saba, na wenzangu tulipenda kuiga nyimbo za wenzetu kama vile Chidi Benz, Tunda Man. Kwa hiyo tulikua tunaimba nyimbo za watu kabla hatujaanza kuimba za kwetu.

Tulianza kuandika nyimbo zetu mwaka 2009, nilikuwa likizo  kati ya darasa la sita nikitaka kwenda la saba. Nilipofika kidato cha kwanza nikiwa shule ya Kilombero-Morogoro ndipo nilipoanza rasmi kushika maiki studio 2011 hadi nilivyoenda kurekodi rasmi mwaka 2016, nilirekodi wimbo wangu wa kwanza nikiwa Morogoro Uptown Records unaitwa Ng’ombe Wa Masikini au John tarehe 5/02/2016  na badae nikaachia ngoma tatu nyingine.

Mnamo tarehe 20/1/2017 nilitoa wimbo unaoitwa Kibosi,  na mnamo tarehe 20/7/2017 nikatoa wimbo wa  sanaa kwa jina Nyapara.  Kisha nikaenda Mbeya kwa ajili ya masomo mnamo 2016 mwezi wa 8 katika Chuo cha Utumishi Wa Uma (cheti) na 2019 nikawa nimemaliza Diploma na kisha nikaunga Degree Mzumbe.

Nje ya mziki najihusisha na Shule  na nipo Chuo cha Human Resources na hivi sasa niko ngazi ya Degree.

Jina Nala Mzalendo lilikujaje pamoja na a.k.a yako Diego Naladona?

Tukianza na jina Nala, jina lilikuja kwenye Aidan Andrea Mtelele Kaonga, na Mzalendo lilikuja wakati nilikuwa nasafiri safiri sana na nilikuwa na enjoy. Nakumbuka nilikuwa natoka Tanga naenda Njombe na safari ndefu na njiani ilikuwa burudani sana kwani nilisafiri nikiwa mdogo nikienda kutambulishwa kwa upande wa baba kule Njombe. Hapo ndio nikaona kumbe ninaipenda nchi yangu na ndio nikagundua kuwa mimi Nala ni Mzalendo. Pia ni Mzalendo kwenye Hip Hop yani nina mapenzi ya kweli.

Na Diego Naladona limetokana na Diego Maradona (R.I.P). Huyu ni mchezaji wa mpira ya miguu ninaempenda sana na ninapenda kucheza mchezo wa Play Station Pro Evolution Soccer kwa hiyo ni mchezaji ninayependa kumtumia kwenye mchezo huo kwa hiyo nilivutiwa naye nikabadilisha jina kidogo na nikajiweka hivyo.

Nala Mzalendo aka Diego Naladona

Nala Mzalendo, kando na mziki naona pia ni muigizaji? Je vipaji vingine unavyomiliki ni vipi? Unawezaje kukuza vipaji vyote hivi?

Nje ya mziki ni kweli ni muigizaji lakini pia kipaji kingine ninachomiliki ni kucheza mpira wa miguu.

Kuweza kuvikuza vipaji vyote hivyo kinachohitajika ni mda; mziki unaweza ukautengea mda, masomo ukayatengea mda, uigizaji ukautengea mda, na mpira ukautengea mda. Kufanya vyote kwa pamoja ni uongo.

Mpaka sasa una miradi mingapi, iwe ni albam, Ep au mixtapes na zilitoka lini?

Mpaka sasa kuna albam moja ya kwangu binafsi (Mimi Na Taifa Langu) na ya pili nimeshirikiana na wenzangu Wise Geniuz na Sajo Mc (Loyal To The Truth). Kuhusu Ep ni kama ifuatavyo:-

Nina Ep inaitwa Nalation ali produce Catcher

Kuna Ep inaitwa Njia Sahihi ali produce Wise Genius

Kuna Ep  Nala Mzalendo wali produce ma producer mbali mbali
Kuna EP inaitwa Ishi aliproduce NaChB

Kuna Ep inaitwa Akili Kichwani nimefanya na Trickson Knowledge.
Hivyo basi mpaka sasa kuna Ep tano (5) na mbili (2).

Albam yako Mimi Na Taifa Langu ilitoka lini? Nani aliunda midundo kwenye mradi huu? Mixing and Mastering alifanya nani na mradi uliundwa studio zipi? Mada ya albam hii ni nini?

Albamu Mimi Na Taifa Langu niliachia tarehe 25/05/2020. Midundo walipiga Black Ninja na Ben Beats kutoka Njombe. Recording na mixing alifanya Burn Bob Wa Kitaa ambaye ni marehemu sasa hivi katika Studio za MaKaNTa. Ujumbe katika albam hii lengo langu wale underground Hip Hop na nilitaka kuwapa hamasa zaidi. Ukiskia wimbo wangu wa Mimi Na Taifa Langu unalenga tusonge mbele bado na harakati inaendelea.

Nala mzalendo unaona kama wana Hip Hop wanakupa heshima unayostahili kwa mchango wako kwa Hip Hop bongo?

Mimi naona wananipa heshima ninayostahili. Wananipa heshima.

Nala tueleze vizuri siri ya Hip Hop ya Mbeya. Nini kinachofanya Mbeya kutoa vipaji vipya na siyo tu wachanaji bali hata na ma producer?

Mbeya kama mbeya naona kwamba wanajitahidi siyo tu kwa wachanaji na hata ma producer wanaendelea. Vipaji vipya vinaibuka katika Nyanja mbalimbali

Nimeona unajihusisha na vilinge na matukio ya Hip Hop ndani na nje ya Mbeya. Kuna manufaa gani yanayopatikana kwa emcee na shabiki kuhudhuria kwenye matukio kama haya ? 

Kuhusiana na vilinge manufaa yake ni kuwa unajuana na watu wengi na kukutana na ma emcee wanaochana katika style tofauti, na watu pia mnaonana ana kwa ana na kando na kuwa washawahi  kukusikiliza kwa audio wanapata fursa ya kuona vipi unavyo perform inakuaje ukiwa kwenye tamasha au tukio. Unaweza kuwa upo vizuri ukiwa studio kumbe kwenye jukwaa uwasilishaji haupo vizuri, hivyo ni fursa ya kujipima na kuona uwezo wako. Vilinge vinasaidia sana na vina faida kubwa na ndo maana huwa siachi kwenda.

SAWINA, nieleze kidogo kuhusu kundi ambalo pia upo ndani.  Jina lina maana gani? Albam yenu ya Loyalty To The Truth ilitoka lini, mwezi na mwaka? Waunda midundo waliohusika hapa ni akina nani? Albam iliundwa studio gani? Mixing and mastering pia nani kahusika? 

SAWINA inatokana kwenye majina yafuatayo;

  • SA- Sajo (Mc)
  • WI – Wise (Genius)
  • NA – Nala (Mzalendo)

Hili kundi ni kama familia ambalo tuliliunda na tukawa tunafanya shughuli zetu na tulikubaliana kurekodi albam moja na tulirekodi na baada ya hapo hatukutoa albamu nyingine maana lengo lilikamilika, hatukuwa tena na ishu nyingine ya kuendeleza.

Katika swala la midundo aliyegonga ni Wise Genius kwenye studio yake inaitwa (AMG) ni studio ya hapohapo ambapo kila kitu alifanya mwenyewe.

Naona una chata lako linaitwa Nala Mzalendo. Lilianzaje na lini na mapokezi toka kwa mashabiki yakoje?

Chata lilianza mda mrefu sana.  kuna idea ambayo alitoa mshikaji wangu, aliwahi kuitoa wakati tukiwa tupo sekondari. Kwa sasa nikaja kupunguza tu, lakini idea ya chata imekuja kupewa nguvu na kampeni ya TMT (Tunavaa Machata Tu) ambayo iliyo anzishwa na akina  Lugombo MaKaNTa. Pia mashabiki wanayapokea, wana support na maisha yanazidi kwenda.

Ushawahi kuwa ghost writer? Wewe mwenyewe ushawahi kuandikiwa mashairi yako yoyote ?Emcee anayeandikiwa je ni emcee?

Sijawahi kuandikiwa lakini sijui kama emcee kama anayeandikiwa ni emcee au siyo emcee nadhani anaweza kuwa ni rapa kwa sababu atachukua mashairi na kazi yake kubwa inakuwa ni ku rap, lakini mawazo yakawa siyo yake. Ila sijajua kama kuandikiwa ni dhambi au vipi. Nadhani mtu anaweza akaandikiwa wimbo na akafanya kwani inawezekana ikawa ni biashara na kuna makubaliano kati yao.

Je midundo ni muhimu kwa mziki wa Hip Hop au haijalishi kama mdundo ni mzuri au mbovu bora uchanaji tu?

Mdundo katika Hip Hop ni muhimu na unatakiwa uwe mzuri  kwani mdundo unakuwa na hisia zaidi wakati mwingine alafu ndio mashairi ndio yanafuata. Mdundo ukiwa mkali we unadonoa donoa tu wimbo umeisha. Mdundo ndio kila kitu.

Ukiwa na mdundo mbovu  kufanya kazi nzuri ni changamoto sana.

Mziki umekunufaisha vipi kando na kukupa salari?

Mziki wa hip hop umeninufaisha sana nje ya kipato umenipatia watu, familia kubwa sana. Yani kuna wakati ninaishi kwa sababu nina watu kwenye familia ya Hip Hop.

Ili emcee aweze kuboresha kipaji chake anatakiwa kufanya vitu gani vya msingi ili afanikishe hili?

Ili emcee aweze kuboreshe kipaji chake anatakiwa ajue watu wake wanataka nini au katika huo u emcee awasilishe kitu gani. Akijua kwamba mimi ni emcee na akishalitambua hili anatakiwa aishi kwa hadhi ya emcee na kwenye Hip Hop atakuwa amefanikiwa.

Kipi ambacho sijakuuliza ungependa kutuambia? 

Mimi nimezaliwa Morogoro, nimekulia Tanga, kwa sasa naishi Mbeya na nyumbani kabisa ni Njombe.

Shukran sana Nala Mzalendo kwa mda wako.

Shukran sana Micshariki Africa.

Mcheki Nala Mzalendo kupitia mitandao ya kijamii:

Facebook: Nala Mzalendo
Instagram: nala_mzalendo