Uchambuzi Wa Album: Mimi Na Taifa Langu
Msanii: Nala Mzalendo
Tarehe Iliyotoka: 25.05.2020
Nyimbo: 21
Watayarishaji: Ben Beats, Black Ninja, Wise Genius
Recording Na Mixing: Burnbob Wa Kitaa (R.I.P)
Studio: MaKaNTa House Jr.

Nyimbo nilizozipenda: Mimi Na Taifa Langu, Dole Gumba, Umri, Katalina, Sauti Zilizopotea, Diego Naladona, Ukiona Kimya, Jirani, Hisia, Siku, Mama Nala,

Nala Mzalendo - Mtu Mfupi Mistari Mirefu

Nala Mzalendo nilimfahamu kwanza kupitia EP yake Ishi ambayo aliiachia kama miaka miwili iliyopita. Kutokea hapo ikabidi nianze kuchimba zaidi ili niweze kumfahamu emcee huyu ambaye kwangu niliona ana kipaji sio tu cha kuchana bali hata cha uandishi. Hapa ndipo nilipoweza kupata nakala halisi ya album yake ya kwanza Mimi Na Taifa Langu.

Kutokana na jina la album, moja kwa moja nilianza kuwaza uzito wa kazi hii. Je kwa kuwa Nala ni Mzalendo je hapa atakuwa anaongelea nchi yake pendwa ya Tanzania?  Nilijitosa moja kwa moja kuuskiliza mradi huu ambao unaanza kwa Intro toka kwa emcee Nala ambaye anajitambulisha kwetu akitueleza kuhusu chimbuko lake.

Mradi huu ambao midundo imesimamiwa na Dr. Black Ninja pamoja na Ben Beats toka Njombe unaonesha uwezo wa uandishi alionao nao Nala; uwezo wa kuandika kwa ucheshi, kuandika kuhusu mada ngumu na tata, uwezo wake wa kuandika hadithi. Pia uwezo wake wa kuchana, uwasilishaji na unataji wa midundo unaonekana vizuri kwenye mradi huu.

Mradi huu unaanza freshi na ngoma flani yenye ucheshi Dole Gumba kabla ya Nala kubadili gia na kuanza kuzama kwenye hoja nzito kwenye Umri, Katalina, Sauti Zilizopotea akiwa na Jadah MakaNTa na kisha Mama Nala. Kwenye Umri wenye mdundo mzuka sana wa boombap toka kwa Black Ninja ndipo unaaanza kuona uwezo wa Nala wa kuandika na kuchana akisema,

“Najiona nimekua ki umri/
Mtaani pata shika nimekua shughuli/
Nimekua kiburi/
Sometime najiuliza au labda sijakua vizuri/
Nimeshavunja mila nimevunja desturi/
Dada alivunja ungo nikataka kuvunja bakuli/
Nipo gizani na nimevunja chemli/
Kichwa maji kila ninachojifunza sifuri/
Naiona mitihani ikinizonga/
Siongei na mama, baba sisalimiani na mjomba/…”

Kwenye Katalina akiwa na Black Ninja unaona uwezo wa Nala wa kusimulia hadithi wakati akitueleza masaibu yaliyomkuta dada Katalina ambae alikuwa ni punguani wa akili. Dada huyu  ananajisiwa analea mimba na kisha kufariki dunia wakati anapojifungua mtoto wake wa kiume. Mwisho wa hadithi hii mzuka sana.

Nala Mzalendo anaonesha uwezo huu wa kutupigia hadithi tena wakati anapotusimulia kuhusu maisha magumu aliyoyapitia yeye na mamae baada ya baba yake kuaga kwenye Mama Nala na kwenye mdundo mzuri toka kwa Black Ninja.

Wimbo Mimi Na Taifa Langu ndio umebeba jina la album hii na hapa ndipo unapoona bayana taifa analoliongelea Nala ni lipi. Taifa la Nala ni,

“Ni Mimi Na Taifa Langu/
Ukitoa Hip Hop kuna mimi na maisha yangu/
Taifa la rap ni zaidi ya chuo/
Kizazi cha trap mtabaki taifa la sup/
Hip Hop ndo mchongo/
Na hakuna wa kunitisha najua wote watu wa udongo/
Ninae jithamini kabla sijathaminiwa/
Amini nilijiamini kabla sijaaminiwa/
Namuona Mlafanyombo kwa mbali akila miwa/
Tupo chini handakini bado hatujafukiwa/
Taifa langu lina vikosi vya kutosha/
Usishangae hatuogopi tunaogopwa/
Chimbuka Na Hip Hop Watunza Misingi MAT DDC/
Kivipi tukose ushindi/
Haki ya Mungu mtapatwa na maafa/
Huku Wasadikaya huku Nash na Kinasa/
Adamoe waamshe MaKaNTa wapige jalamba/
Lugombo waambie Mapacha waje na magwanda/
Chem Chem Sana Rado wa Viraka na imani/
Mshtue Salu T na Empire ya Yunani/
Huu sio mda wa amani tupige goti tuombe/
Nikifia vitani nitarudisha medani Njombe/
JCB mshtue Adili tukachape kazi/
Kuna watoto wanaleta udwanzi/
Wapo chini wapo hoi hatujapiga risasi/
Sisi tunawaua kwa Bars/”

Nyimbo nyingine mzuka sana nilizozipenda ni kama Jirani ambao sio tu mzuri kiushairi bali hata mdundo na kiitikio. Kisha kuna Siku, Mke Wangu pamoja na Diego Naladona  ambao emcee huyu anaonesha vile kando na chenga za uchanaji yeye pia yupo vizuri kwenye chenga za mpira wa miguu kama vile gwiji  mwendazake Diego Maradona. Hadithi mzuka sana. Pia kuna Ukiona Kimya pamoja na Bado Haitoshi.

Mradi ni baraka sana kwa wana Hip Hop na ni mradi chanya kwa ajili ya wana Hip Hop wote, wachanaji, watayarishaji, wadundishaji, wachora majalada ya album, ma DJ, na mashabiki. Mradi huu ni kwa ajili ya Mimi Na Taifa Langu la Hip Hop.

Kupata nakala yako ya mradi huu mcheki nala kupitia;

Facebook: Nala Mzalendo
Instagram: nala_mzalendo
Twitter: Diego Naladona
WhatsApp: +255719568535