Neno WaKwanza

Neno WaKwanza ni emcee ambaye amekuwa kwa game la Hip Hop hususan handakini kwa mda mrefu. Kama vile “Hapo mwanzoni kulikuwa na Neno” basi Neno huyu ameaminia hili na kuongozwa na Neno ambalo linamuwezesha yeye kutema Neno muafaka kwa mda muafaka.

Neno WaKwanza kwa kutumia mashairi yake na kinasa anaonya, anabomoa, anajenga, anaweka bayana maovu, ana burudisha wakati huo huo akielimisha.

Leo tumepata fursa ya kuongea live na Neno WaKwanza ambaye uwezo wake wa kumiliki neno ulimuwezesha yeye kuunda albam ya kwanza Tanzania kwa njia ya Mitindo Huru au kwa kimombo Freestyle. Karibuni mpate Neno.

Karibu sana kaka Neno WaKwanza. Kama utangulizi kwanza tunaomba ututajie majina yako halisi.

Utambulisho: Fredy Emanuel

Unapatikana wapi kwa maana ya makazi.

Arusha

Jina lako Neno Wakwanza lilikujaje? Historia ya jina hili niipi?

Naamini  kupitia nguvu ya  kinywa, neno ni roho, neno ni sauti ya Mungu kwa watu. Kupitia jina Neno nimejikuta kwamba jina la kitabu sasa linafanana na kilicho ndani, kwani mwanzo nilikuwa najiita Black P au Black Wa Hisabati lakini katika movement zangu nilikutana na Adili Hisabati katika maskani moja ya Mapacha (PKP) ikaonekana kuna dalili za ku share jina hivyo tangia hapo nikaanza kujitafuta kwa upya kwamba mimi ni nani.

Kumbe mimi ni Neno na Neno sio maneno mengi ila ni kuwa na neno lenye nguvu. Nilipokuwa Black Wa Hisabati nilikuwa na tungo nyingi zinazochochea jeuri, kujisifu lakini tangia roho anibatize jina la Neno nimejikuta na mabadiliko makubwa.

Sasa nimekuwa nachunga mdomo kila ninapotaka kutema neno. Nimegundua neno linaumba, na sasa limekuwa kiini cha ujumbe wangu ni kutaja tabia za Mungu. Kumbe neno ni Mungu, nafikiri ni kwa kuwa niliumbwa kwa mfano wake. Ndio maana mimi ni Neno, Mungu  ndani  ya mimi.

Je ulianza lini kujihusisha na game ya Hip Hop na ilikuwaje mpaka ukajikuta unajihusisha na Hip Hop?

Kinasa cha kwanza nilikishika mwaka 1999 nikawakilisha misingi ambayo mpaka sasa sijaivunja. Siku ya kwanza nashika mic ilikuwa siku ya mashindano ya rap na nikashinda nikiwa na wanajeshi wenzangu kama Fred Luu, Mr Tix, Mlost (R.I.P).

Ilikuwaje mpaka ukahamasika kushika kinasa au nani alikuhamasisha?

 Nafikiri ni roho wa rap aliniingia baada ya kusikiliza kwa mara ya kwanza mziki wa rap wa nje ambao kwa wakati huo sikujua wana rap nini wala ni akina nani wana rap na baadaeye nikaja kuisikia rap ya Kiswahili kupitia Mr Two, Kwanza Unit na freestyle za Dogo Hashimu. Tangia hapo mambo yangu yakaanza.

 Kwanini uliamua kufanya album ya freestyle tu?

Kwanza ni kuonesha kukomaa katika uandishi, ngazi ya pili baada ya kuandika, ukisha staafu kuandika inabidi uteme tu hapo kwa hapo na bado ilete maana. Pili ni makaratasi ya mistari yaliyotapakaa ghetto na mengine yaliyopotea bila kurekodiwa yalinipelekea ku stop kuandika kwa muda.

Unaweza kuongezea katika hili swali kwa upana zaidi kuwa idea ulipata wapi, na ni producer gani aliyepiga midundo kwenye hii album na je imekupa mafanikio gani?

Niliamua kufanya album ya mitindo huru (freestyle) kwa sababu nilitamani kuonesha ukomavu kwa sababu hatua inayofuata kwangu baada ya kuandika ni kutokuandika, ni kutema ana kwa ana na bado ikaleta maana. Pia makaratasi mengi ya mistari yalikuwa kama kero na mengine kupotea yakiwa na mawazo mazuri. Ikafanya nisiandike bali ni freestyle kwa kuwa niliamini naweza ku freestyle wazo moja au tofauti lenye kuleta maana. Track namba 10,7,4,6 na 11 inathibitisha hili.

Studio ni Mcs Records zilizopo Arusha na producer ni Flux Kichwaa.

Una albam nyingine tofauti na hiyo uliyofanya ki freestyle?

Ninazo album mbili na nyimbo nyingine ambazo bado sijachukua uamuzi wa kuziweka katika albums

Kwa nini bei ya Tshs 10,000.00 kwa album ya freestyles?

Kwa sababu thamani ya kilicho ndani ni zaidi ya Tshs 10,000.00.

Neno Wakwanza - Jalada la albam yake ya kwanza Staafu Kuandika

Mziki unaoufanya una uhusiano gani na jamii yako?

Uhusiano ni mkubwa kwa sababu naongelea maisha, nakanya, naonya, naonesha wasichoona, naongoza, nasema na kila nafsi itakayoonja mauti. Mziki wangu ni sauti ya Mungu kwa watu.

Watu wengi hatujui kama mziki ni sehemu ya elimu muhimu na inaweza kuleta mabadiliko chanya katika mitaa yetu. Unawasaidia vipi wa Tanzania wa kizazi cha leo kuweza kuona ama kutambua umuhimu wa mziki kama chanzo cha elimu ilhali kazi uzifanyazo huzitoi bure?

Kinachotakiwa kwangu ni kusema kweli, kweli haina promo, wachache watanunua wengi watajifunza bure kwa hiyo wale walioandaliwa kufunzwa, kuonywa na kuponywa kupitia neno langu, hao ndio kizazi cha leo na cha kesho ambacho nategemea kitapata mabadiliko chanya.  Pia itambulike kuwa neno ni mbegu na mioyo ya watanzania wa kizazi cha leo ni shamba hivyo kazi yangu ni kupanda mbegu chanya juu ya shamba lenye udongo mzuri na hata lisilo lenye udongo mzuri.

Hapa umenikumbusha track yako ya Jeraha unaweza kutuambia kuhusu hii ilivyofanyika, je Ipo kwenye hiyo album ambayo iko chimbo au iko katika project nyingine? Je wimbo huu Jeraha unapatikana mtandaoni?

La, Wimbo huu bado haupatikani mtandaoni.

Wimbo huu upo katika project nyingine kabisa. Hii ni hisia ya kweli ya superstars  waliopoteza u superstar au walioshindwa kuifikia ndoto ya kuwa superstars japo walistahili, aidha kwa sababu zao wenyewe za mfumo wa maisha yao au mfumo mzima wa muziki wa Tanzania.

Mtu anayeamini anaweza na mitaa pia hukubali nakuamini anaweza ila mfumo mbaya wa mziki wetu na maisha binafsi ya mhusika  yanachangia  kumfelisha na kumuachia jeraha. Naamini mnayo mifano ya ma emcees wakali waliotoka na media zinazoamini mziki wa Tanzania uko chini yao zikawafelisha majamaa na majamaa wakafeli. Wimbo mkali sio unao hit ila wimbo uliofanyiwa promo. Kwa hiyo kama hauna uongozi na hauna kipato cha promo ni rahisi kufeli pia.

‘Tuna hope life japo life inatupa scars. Hofu life japo life haihofu kumtupa star. “

 Je mziki unaofanya una reflect real political and social situations iliyopo Afrika, Tanzania ikiwemo? Nini maoni yako katika mfumo mzima wa siasa za afrika?

Upendo na umoja ni kitu kilichokosekana kwenye siasa za Africa ikiwemo Tanzania. Najaribu kupenyesha mawazo ya upendo sio tu kwenye sikio la siasa ila hata sikio la dini na makabila ya Africa. Upendo pekee ndo huweza kuifanya Africa moja. Mungu mmoja.

Kuna kazi zako zipo YouTube kule mfano Rangi Ya Afrika, je zina album zile?

Haziko kwenye album ila nafikiria kuziandalia packages.

Je unauzungumziaje muziki wa handaki kwa hapa kwetu?

Ukweli usiopingika ni kwamba wanamuziki wakali na wa kipekee wako kwenye mahandaki na hawa ndio vioo vya wasanii ili wasanii waweze kuwa vioo kwa jamii.

Na pia nimegundua kuwa wasanii wengi waliopo mainstream Bongo huwa wanawasikiliza sana wanamuziki wa handaki na huku ndipo wanapopata idea zao.

Nimeshawahi kukusikia kwenye track za Sosa kadhaa mfano Where Is The Peace na pia kwenye mixtape ya Ado ile ya SwastickMuzic je uko vipi na hawa jamaa?

Hawa jamaa ni ndugu zangu rafiki pia.

Unazungumziaje technolojia mpya ya kusambaza mziki, yaani streaming apps?

Ni nzuri japo hakuna elimu ya kutosha kuhusu faida tunazoweza kupata.

Je wewe miradi yako ushawaza kuiweka huko?

 Nishawaza na wakati ukifika nitaweka huko.

Pia miziki yako kando na YouTube siioni Mdundo au hata Audiomack. Hili unalizungumziaje?

Elimu ya kutosha itolewe tu.

Unazungumziaje mchango wa wana Hip Hop toka Arusha? Je wanazidi kuiwakilisha fani au wamefifia? Ni ma emcee gani wapya toka A-town ambao ungependa wafuatiliaji wa Hip Hop wahakikishe wanawafuatilia na kuwaskia?

Kaka zao wameweza kuwaambukiza wadogo zao utamaduni, nafikiri huu ni mchango japo unahitajika kuchochewa zaidi. Kuna uhaba wa ma emcee wapya wakali kutokana na mfumo wa mziki unavyobadilika ila kuna wingi wa ma emcee wa zamanii wakali. Embu watu wajaribu kufwatilia watu hawa (Uhuru, Nguzo, na Fred Luu na Donii)

Kando na kuwa mwanamziki, je Neno Wakwanza anajishughulisha na kipi kingine?

Neno ni graphic designer, Neno ni director wa video na huduma nyingine za kijamii. Ukifuatilia hizi accounts tutaendelea ku connect pamoja.

Instagram: nenografix  
Instagram: nenowa_kwanza
Instagram: ourkids_ourvision

Pia kando na kinasa Neno Wakwanza ashawahi kujaribu kua producer au hata muunda midundo?

Ndio nilishajaribu hadi kumuambukiza mdogo wangu mmoja ambaye kwa sasa ndio mmiliki wa studio za Mcs Record ambapo kuna baadhi ya kazi zangu zimefanyika hapo, lakini kutokana na majukumu mengi ya kuhudumia vipaji vingi kwa wakati mmoja nikajikuta nafifia kwenye kuunda midundo.

Je Neno Wakwanza ni Hip Hop Gospel emcee au Hip Hop underground emcee?

Hip Hop Gospel Emcee! Hip Hop Gospel Emcee!

Je kuna vipaji vyovyote ambavyo wewe binafsi umehusika au umevisaidia kuvikuza vya Hip Hop?

Nimeambukiza watu wengi jinsi ya kuchana ambao kwa sasa wao wanafahamika kuliko mimi.

Kando nakuwa emcee ni mchango gani tofauti na kushika kinasa umeweka kwenye Hip Hop ya bongo ambao pengine sisi kama mashabiki hatufahamu?

Nimefanikiwa kuwa na production ya video na mdogo mdogo na wapiga vichupa wadogo zangu pamoja na marafiki.

Tupe Neno la mwisho ambalo linaweza kuwa akilini mwako na pengine sijakuuliza.

Mimi ndio msanii wa kwanza ambaye Duke (Tachez) alitaka na akashindwa kuni sign MLab!

Shukran..